AN-NUUR
Na.163 Rabiul Thani 1419, Agosti 21 - 27, 1998
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
Hoja binafsi

Uhusiano na Marekani usituletee maafa


 


Na Said Rajab

SHAMBULIO la mabomu katika Balozi za Marekani nchini Kenya na hapa nyumbani ni baya mno na la kusikitisha. Mandhari ya tukio lile inatisha sana na Watanzania na Wakenya wasingependa kabisa kuona unyama kama huu ukifanyika katika ardhi zao. Usalama wetu na wa vizazi vyetu ni muhimu zaidi kwetu kuliko uhusiano au jambo lingine lolote.

Ingawa walengwa walikuwa Wamarekani, lakini wengi miongoni mwa waliopoteza maisha ni Watanzania wenzetu na ndugu zetu Wakenya. Wao wamekuwa majeruhi wa mazingira tu (victims of circumstances). Vifo vyao ni matokeo ya ugomvi wa Marekani na hao wanaoitwa magaidi.

Watanzania na Wakenya hatuna utamaduni, historia, wala kumbukumbu ya vitendo vya kinyama kama hivi. Ardhi zetu zimetumiwa na wapendwa wetu wameangamizwa kwa sababu ya uhusiano wetu na Marekani.

Wamarekani na Wayahudi wana historia na kumbukumbu nzuri tu ya matukio kama haya ndani na nje ya mipaka yao. Kwa hiyo, wana uzoefu, ujuzi na tahadhari ya kutosha kuhusiana na ugaidi wa kimataifa. Huenda hiyo ndiyo sababu ya wao kutopoteza raia wengi kama ilivyokuwa Tanzania.

Labda jambo la msingi, tujiulize kwanini vitendo vya kigaidi kama hivi vinaelekezwa kwa Marekani? Hawa Wamarekani wana ugomvi na hao wanaoitwa magaidi?

Hali hii inasababishwa na siasa za kibeberu za Marekani katika maeneo au nchi za hao wanaoitwa magaidi. Wamarekani wanalaani ugaidi wa kimataifa wakati wao wenyewe wanafanya ugaidi mbaya zaidi kuliko huo. 

Wamarekani wanaunga mkono ugaidi wa serikali (State terrorism) ya Israel dhidi ya Wapalestina. Ndiyo maana amani ya kudumu Mashariki ya Kati ni agenda isiyokwisha. Miaka nenda miaka rudi watu wanazungumza tu lakini muafaka haupatikani. Sababu Marekani inaunga mkono udhalimu wa Mayahudi dhidi ya watu wengine katika eneo hilo.

Wamarekani na washirika wao wamesaidia sana kuvuruga amani ya Algeria. Wamekinyima chama cha FIS haki ya kuunda serikali nchini humo wakati chama hicho kilishinda uchaguzi wa kidemokrasia kwa viwango vya Kimagharibi.

Badala yake wakashiriki kuiweka serikali haramu na kibaraka madarakani pasipo idhini ya Walgeria walio wengi. 

Vile vile Marekani inashirikiana vyema na serikali ya Misri dhidi ya wananchi wa nchi hiyo.

Tukirudi katika matukio ya Noriega, Grenada, Vietnam, Iraq, Libya na kwingineko, tutaona kwa nini Marekani iwe shabaha ya ugaidi wa kimataifa.

Marekani imethubutu hata kuziorodhesha nchi kama Iran, Iraq, Misri, Sudan, Libya, Algeria, Afghanistan kuwa zinaendesha na kudhamini ugaidi wa kimataifa. Lakini hii ni hofu tu ya Marekani inayotokana na uadui iliyojijengea na wananchi wa nchi hizo.

Wamarekani wanataka dunia nzima iungane dhidi ya mataifa hayo kwa lengo la kulinda maslahi ya Marekani au Magharibi kwa ujumla katika Mashariki ya Kati, eneo la Ghuba ya Uajemi, Kaskazini mwa Afrika na maeneo mengine ya dunia.

Ikumbukwe kuwa alipokuja Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Balozi wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi walisusia dhifa ya taifa aliyoandaliwa kiongozi wa nchi hiyo na Watanzania.

Na Mabalozi hao wameitahadharisha Tanzania juu ya uhusiano wake na Iran. Yaani adui wa Marekani ni adui wa dunia nzima. Hiyo ndiyo ndoto ya Marekani.

Vile vile kufuatia ziara ya Rais Bill Clinton katike eneo la Maziwa Makuu, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Bibi Madelaine Albright alinukuliwa na vyombo vya habari vya kimataifa akitamba: "We want to build a new democratic Sudan".

Kwa mtazamo wa Bi. Mkubwa huyu, Sudan siyo nchi inayoongozwa kidemokrasia. Sasa wao (Marekani) wanataka kujenga Sudan mpya itakayoongozwa kidemokrasia. Tafsiri ya kauli ya Bi. Albright ni kuangusha utawala halali uliowekwa na wananchi wa Sudan na kupachika vibaraka watakaokuwa watiifu kwa "White House" na Maghabiri kwa ujumla.

Nadhani hiyo ndiyo sababu Marekani kuvisaidia vikundi vinavyopingana na serikali halali ya Sudan kikiwemo cha gaidi John Garang (Wamarekani wanamwita mpigania haki na demokrasia).

Turudi katika maudhui kuu ya makala hii. Baada ya tukio la mabomu, viongozi wengi duniani wamelaani kitendo hicho na kutoa misimamo ya serikali zao kuhusu ugaidi wa kimataifa.

Rais Bill Clinton alisisitiza umuhimu wa jumuiya ya kimataifa kuungana dhidi ya ugaidi wa kimataifa. Nasi serikali yetu imeitikia wito wa Marekani moja kwa moja na kuahidi kutoa ushiriakiano unaohitajika kwa Marekani katika vita hii.

Swali: Huku kuungana kimataifa katika vita vya ugaidi ambako Marekani na washirika wake wanakopigia debe sisi kunatunufaishaje? Ni wazi vitendo vya kigaidi ni matokeo ya siasa za Marekani katika mataifa mengine. Vipi nguvu za kimataifa zitumike katika jambo ambalo halina manufaa ya kimataifa? 

Sisi ni ngao ya Marekani dhidi ya maadui zake? Hatuna ugomvi na mataifa yanayoitwa magaidi na Marekani. Marekani ni rafiki zetu, na mataifa hayo pia ni rafiki zetu. Lazima tuwe makini katika ushirikiano huu wa kuupiga vita ugaidi wa kimataifa. Sisi siyo shabaha ya magaidi. Tusije tukajiingiza katika shabaha bila wenyewe kujua.

Tuzingatie tu kwamba, tumepata msiba mkubwa na uharibifu wa mali kwa sababu tu ya uhusiano wetu na Marekani, na wala si kwa sababu ya ugaidi wa kimataifa kama vyombo vingi vya habari vinavyojaribu kupotosha ukweli huu.

Ulimwengu mzima unaelewa kwamba Tanzania na Kenya hazina sababu yoyote ya kuandamwa na magaidi. Balozi za Marekani zilizopo nchini mwetu ndizo zilizotuponza.

Kinyume chake, Marekani, Israel na washirika wao ndiyo wanaolengwa na magaidi wa dunia nzima.

Napenda kuvishauri vyombo vyetu vya usalama visitaharuki katika kulishughulikia tatizo hili. Vifanye kazi kama watalaamu. Kamata kamata hovyo kwa sababu tu mtu anatoka Sudan, Iraq au Somalia kunaweza kutugharimu jamani! Hii siyo kesi ya bangi au ugoni ambayo inaweza kusuluhishwa hata nje ya mahakama. Mustakabali wa taifa letu mbele ya jumuiya ya kimataifa inategemea jambo hili. Tusiwe na papara ambayo inaweza kutujengea uhasama na mataifa mengine.

Dawa ya ugaidi wa kimataifa dhidi ya Marekani si kuomba msaada wa nchi kama Tanzania kupambana na ugaidi huo, bali Marekani yenyewe kuacha ubabe na ugaidi. Inachowatesa watoto wa Iraq nini, inachowatesea watoto wa Libya ni nini? Kwa maslahi gani ya kimataifa inamuunga mkono na kumsaidia Garang.

Na huko Mashariki ya Kati ni Saddam tu mwenye silaha? Mbona Marekani haisemi juu ya zana na silaha za nyuklia ilizonazo Israel! Mbona hatuioni kuwa kali kuishutumu Israel inapowaua Waarabu na kukalia ardhi yao! Mbona na yenyewe iliwahi kuiangusha ndege ya Iran wakaua mamia ya watu?

Namalizia kwa kuwatahadharisha Watanzania wote kwamba iwapo matukio ya kigaidi kama haya yataendelea katika balozi za Marekani, taasisi na vituo vyake vilivyopo nchini, itatubidi tuurejee upya uhusiano wetu na Marekani. Hatuwezi kusamehe kuwaona ndugu zetu wakipukutika kama senene nasi tusiwe na la kufanya. Uhusiano au ushirikiano lazima utuletee manufaa na siyo misiba ya kutisha.
 

Juu

YALIYOMO



TAHARIRI

Milipuko ya mabomu Dar, Nairobi: Waislamu walaani vyombo vya habari
Na Mwandishi wetu

Wanawake Waislamu Tanga waazimia kupigania haki
Na Ibn Masoud, Tanga

Marekani yashambulia Sudan, Afghanistan

Maoni: Kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani:
Huu ni unazi au sehemu ya mtandao?

Nguruwe kuzua tafrani Kibamba
Na Mwandishi Wetu

Sheikh Mbukuzi ataka vijana wajihadhari  na utamaduni wa Magharibi
Na Said Shariff

TAMPRO kuzindua Tawi Iringa
Na Mwandishi Wetu

Tamasha la kusaidia wagonjwa laanza Moro
Rajab Rajab na Mussa Ally, Morogoro

Kambi ya matibabu ya Macho Tanga yaanza
Na Mwandishi Wetu

MAONI: Kanisa mshiriki wa ukandamizaji

Porojo za Ngatara
Na J. Hussein

Ubatizo kupitia TVZ?
Na Salahuddin Ahmad

Waislamu Kosovo waangamizwa

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA 
SHIRIKISHO LA TANZANIA -2

Hoja binafsi: Uhusiano na Marekani usituletee maafa
Na Said Rajab

Darasa la Muhammad (s.a.w)

Wanamume toeni haki  za wanawake kuepusha ufisadi
Na Halima Issa Ndabi,  Mwanza

MAKALA: Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu,  ni uzushi mtupu! - 2
Na Muhibu Said

Mwanaadamu alipofikia
Na Nineka B.N., Geita

Mafunzo ya Quran

Barua za wasomaji

Mashairi

Masomo ya dini ya Kiislam

Chakula na Lishe

Matangazo

 

 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita