NASAHA
Na. 067 Jumatano Septemba 27 - Oktoba 2, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
KALAMU YA MWANDISHI

Juha haliambiliki!Juha haliambiliki!

Na Maalim Bassaleh

SAFARI moja Juha alikaa mwisho wa tawi la mti, akilikata tawi hilo kwa kutumia msumeno. Akapita mtu mmoja akamtahadharisha kuwa kitendo alichokuwa akikifanya ni cha hatari. Alimwambia kuwa lile tawi likikatika naye ataanguka! Alimshauri akae kwenye shina la tawi atanusurika.

Juha hakutaka kabisa kusikiliza ule ushauri aliopewa. Alimgeukia yule mtu na kumwambia, "Wewe imekuhusu nini? Nikianguka, mimi ndiye nitakayeumia! Hebu achana na mimi, shika njia uende zako!"

Yule mtu, ingawa alikuwa ana hakika kuwa Juha ataanguka tu, lakini hakuwa na njia ya kumzuia. Akaona bora aende zake. Juha alipomwona anaondoka akaaanza kumpigia kelele, "Mtanzameni huyo. Hana analolijua isipokuwa kuwaombea wenziwe mabaya tu".

Yule bwana akajifanya kama hakuwa akiyasikia yale aliyokuwa akiambiwa. Lakini alikuwa akisema moyoni, "Asiyesikia la mkuu, huvunjika guu!"

Kabla hajafika mbali akasikia kishondo na mayowe yakipigwa. Alipogeuka akamwona Juha yuko chini na lile tawi la mti limwelemea juu yake. Anapiga kelele kuomba msaada. Basi yule mtu akawaita wapita njia, wasaidiane kumwokoa Juha. Walifanikiwa kumnusuru, lakini Juha alikuwa ameumia kiuno!

Yule mtu akamwuliza Juha, "unalia nini? Ungelisikiliza maneno yangu yangalikufika haya?" Juha akajibu, "kweli ningalikusikiliza uliyoniambia nisingalianguka! Lakini mimi sikuwa nikijua kuwa wewe una ujuzi wa kutabiri mambo yajayo, ndiyo maana niliudharau ushauri wako. Kwa vile sasa nimeelewa kuwa wewe ni bingwa wa kutabiri basi niambiye na siku yangu ya kufa!"

Yule mtu akastaajabu sana kwa swali hilo. Akamwuliza Juha, "Tokea lini mtu akaweza kuagua siku ya kifo cha mtu mwengine?" Juha akamjibu, "Mbona ulitabiri kuwa ningeanguka, na kweli nikaanguka? Basi hapana shaka, na siku yangu ya kufa unaijua!"

Yule mtu ilipombainikia kuwa yule hakuwa Juha wa jina tu, bali hata wa vitendo, aliamua kumwacha kama alivyo, na kuendelea na safari yake.

Kisa hiki si cha kweli. Ni katika zile hekaya za Abunuwasi. Ni hadithi za PAUKWA, PAKAWA! Lakini ni kisa chenye mazingatio makubwa kwa yule mwenye kutaka kuzingatia.

Jumanne iliyopita, Septemba 19, 2000, Mkurugenzi wa Idara ya Siasa ya OAU, Bwana Sam Ibok, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, katika ukumbi wa MAELEZO, Jijini Dar es Salaam, aliitahadharisha Tanzania isiichezee amani iliyo nayo. Alionya kuwa kama amani hiyo itaachwa ipotee, itahitaji gharama kubwa kuirejesha.

Bwana Ibok aliwataka viongozi wote wa vyama vya siasa, nchini, bila ya shaka ni pamoja na chama tawala, waelewe kuwa uchaguzi ni ushindani, kuna kushinda na pia, kushindwa! Aliwanasihi viongozi hao wasichukulie ushindani huo kama ni uadui.

Maalim Seif Shariff Hamadi, mgombea urais wa Zanzibar, kwa tiketi ya chama cha Wananchi, CUF, naye amkaririwa akisema DAMU ITAMWAGIKA!

Mradi mambo si shwari. Hofu imetanda kila pahali. Mradi, kila mwenye macho amekwisha iona hatari inayoikabili Tanzania, katika uchaguzi mkuu ujao. Kwa nini basi tujifanye JUHA? Hatari tunaiona, lakini tunaipuuza kwa makusudi? Na wale wanaotuonya tunawaambia kuwa wanatuombea shari!

Badala ya viongozi wetu waliopo madarakani kuyapa uzito unaostahiki maneno ya viongozi hao, ili kuinusuru nchi yetu isiingie katika janga, wao wanayageuza maneno hayo kuwa ni propaganda za kumtuhumia Maalim Seif kuwa akishindwa katika uchaguzi ujao atamwaga damu!

Jambo hilosi la kweli. Na hao wenye kutangaza hivyo wanajua kuwa hayo wanayoyasema si ya kweli. Aidha, wanaelewa kuwa Maalim Seif hakusema hivyo, na wala hathubutu kusema hivyo. Alichokisema Maalim Seif ni kuwa kama ATASHINDA NA AKAPOKONYWA USHINDI, DAMU ITAMWAGIKA!!!

Na hilo liko wazi! Kama uchaguzi utakuwa si huru na wa haki wapinzani hawataridhia. Na jambo hilo linaweza kusababisha kuvurugika kwa amani.

Maalim Seif hakusema kwamba yeye ndiye atakayemwaga damu. Na wala hakudai kuwa yeye atawachochea wafuasi wa chama chake wamwage damu. Hapana. Yeye ameangalia mazingira tunayoingia nayo katika uchaguzi, na ameaona kuwa, kwa mujibu wa mambo yanavyoendeshwa kuna uwezekano uchaguzi usiwe huru na wa haki, na kwa hivyo kusababisha damu kumwagika.

Tokea kuanza kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura, mpaka wakati huu wa kampeni, viongozi wa vyama vya upinzani, wamekuwa wakilalamika kuwa hawatendewi haki! Wanadai kuwa Polisi inawapa mkong'oto na inakishabikia chama tawala.

Na hata Mkurugenzi wa Idara ya siasa ya OAU, Bwana Ibok, amekiri kuwa ujumbe wake umepokea malaalamiko kutoka vyama vya upinzani, nchini, kuwa havitendewi haki.

Na ushahidi wa kimazingira, nao, unaelekea kuthibitisha madai ya wapinzani.

Kwa mfano, taarifa zilizoandikwa na gazeti moja, la kila siku, katika toleo lake Na. 1606, la Jumapili 24, 200, zimeeleza kuwa Polisi wa kikosi cha kutuliza fujo (FFU), siku ya Jumamosi, Septemba 23, 2000, huko Manzese, Darajani, waliwapiga mabomu ya machozi wafuasi wa Chama cha CUF, waliokuwa wakirudi kutoka katika mkutano wa kampeni wa chama chao, kwa madai kuwa walikuwa wakiandamana!

Lakini gazetihilo hilo likaeleza kuwa vijana wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa chama cha CCM walifanya vurugu katika mkutano wa kampeni wa chama cha NCCR-Mageuzi uliofanyika kwenye viwanja vya Ilala Boma, na hawakuchukuliwa hatua yo yote na Polisi.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, fujo hizo zilianza pale gari mojaa ina yaPajero, lilipopita karibu na eneo la mkutano huo, na kupiga kelele wakati mgombea ubunge wa jimbo la Ilala, kwa tiketi ya chama hicho, Bwana Joseph Selasini, alipokuwa akihutubia. Baadaye magari mengine matatu yakajiingiza kushiriki katika fujo hizo. Gazeti hilo limeeleza kuwa badala ya Polisi waliokuwapo pahali hapo kuyakamata magari huyo, wao, walimkamata Ndugu Mwanahawa Kombo, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Wilaya ya Ilala, na kudai kuwa ndiye aliyesababisha fujo hizo!

Gazeti jingine linalotoka kila jioni, katika toleo lake Namba 1189, la Jumatatu Septemba 25, 2000, limekionya chama tawala kwa kuandika katika TAHARIRI yake, "CCM isitumie kutawala ikatisha watu."

Maoni hayo ya Mhariri yametilia mashaka kauli ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, nchini, kuwataka Polisi wapambane wana-ngangari kwa madai kwamba wanafanya vurugu na kutishia kumwaga damu!

Kwa mujibu wa TAHARIRI hiyo wasiwasi huo umezidishwa na tamko la Kamati Kuu ya CCM, lililotolewa na Katibu wake Mkuu, Bwana Phillipo Mangula, kuziagiza serikali zote mbili, ile ya Muungano na ile ya Zanzibar, zichukue hatua madhubuti kukomesha vurugu zinazodaiwa kufanywa na chama cha CUF ili kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa wa amani, huru na wa haki.

Tahariri hiyo imesema chama tawala kuziagiza serikali zake, kutumia vyombo vyake vya dola kukomesha hizo vurugu zinazodaiwa kufanywa na CUF, ni kuzidisha kuwatia hofu wananchi, kwa sababu kinachoelekezwa hapo ni, "Nyie Polisi pigeni Wana-CUF!"

Hebu kila mmoja, ajaribu kuzipima kauli hizo, bila ushabiki, kisha aseme ni za kuomba amani au kuchochea huo umwagaji wa damu? Kwa vyo vyote vile hakuna njia ya kutuhakikishia amani isipokuwa uchaguzi ukubalike na washiriki wote, kuwa ni huru na wa haki.

Kama kauli ya Maalim Seif , DAMU ITAMWAGIKA inatishia amani jee, na tamko la Kamati Kuuya CCM la kuviagiza vyombo vya dola kuwakomesha Wana-CUF halihatarishi amani?

Chama cha CUF kimekuwa siku zote kikidai kuwa kinaamini na kina ushahidi kuwa kilishinda katika ichaguzi mkuuwa 1995; lakini kilipokonywa ushindi! Wafuasi wa chama hicho walikasirika na wakataka wadai haki yao, haidhuru lo lote liwe! Maalim Seif, kwa kutumia hekima na busara, aliweza kuwatuliza wafuasi wake wasipandwe na munkari. Aliwaahidi kutumia njia za kidiplomasia kudai haki yao.

Madai hayo yaCUF yakasababisha mgogoro mkubwa baina ya chama hicho na CCM, Zanzibar. Ndiyo maana ulipopatikana mwafaka CUF ikajitahidi kufanya kila iwezalo kuufanikisha mwafaka huo. Lakini chama chaCCM kikawa kinaweka ngumu. Mwafaka huo ukashindwa kutekelezeka.

Kwa hiyo, Maalim Seif anasema kama safari hii akishinda na akapokonywa ushindi wake kuna uwezekano wa kumwagika damu, kwa sababu ni dhahiri wafuasi wake hawatavumilia na yeye atakuwa hana uwezo wa kuwatuliza, kwa sababu hawatamsikiliza.

Lakini kama serikali inataka uchaguzi ufanyike kwa amani kwa nini haiziachii Tume za Uchaguzi zikashughulikia, moja kwa moja, mambo yote ya uchaguzi? Kwa nini lazima vyombo vya dola, serikali yenyewe, na chama tawala ambacho chenyewe nacho kinashiriki katika uchaguzi huo vizipiku Tume za Uchaguzi katika mas'ala hayo ya uchaguzi? Huku si kutaka kuvipunja vyama vya upinzani? Jee! Haki itapatikana hapo? Na kama haki haipo, amani itakuwapo?

Tusijigeuze Juha tukawa tunamtuhumu Maalim Seif kuwa eti anataka kumwaga damu; wakati tunazipuuzia ishara zinazoonyesha kuwa tunaelekea katika kumwaga damu hiyo! Ni wajibu wa viongozi wetu wa nchi watuhakikishie kuwa mazingira tunayoingia nayo katika uchaguzi mkuu yanaashiria katika kuufanya uchaguzi huo kuwa ni huru na na wa haki. Ni hapo tu ndipo tutakapokuwa na amani ya kweli!
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Polisi ‘isiibebe’ CCM

Wapinzani kumuimarisha Prof. Lipumba

Ngangari kung’olewa Sokoni, Ilala

Polisi nchini hawajui mipaka ya kazi yao -OAU

MAKALA
BBC, CCM ndugu au tajiri na kibaraka?

HABARI
‘Walioshindwa kutawala wasikimbilie matusi’

ATV yatakiwa kuzingatia maadili

Wakazi wa Tabata walalamikia athari ya maji machafu

Maalim Seif akanusha madai ya kumwaga damu

USHAURI NASAHA
‘Mama, hela hii inanunua nini?'

MAKALA
Demokrasia ni kukubaliana kutokukubaliana

MIPASHO NASAHA
HEBU VUENI MIWANI ZENU!

KALAMU YA MWANDISHI
Juha haliambiliki!Juha haliambiliki!

MAKALA
Amani ya Tanzania itadumishwa na haki

MWENYE MACHO…
Hoja za uongo katika kampeni

MAKALA
Chonde Dk. Omari na Karume wahurumieni Wazanibari wenzenu

Habari za Kimataifa

LISHE
Kimfaacho  mtoto

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga kuwakosa Mahadhi, Mbuna
  • Idd Azzan lawamani
  • Kibadeni, Kayuni wanafaa Stars - Machuppa
  • Said Maulidi: Sihami Simba

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita