|
Na. 067 Jumatano Septemba 27 - Oktoba 2, 2000 |
|
|
|
|
|
Amani ya Tanzania itadumishwa na haki Na Mwinjilisti Kamara Kusupa NENO la Mungu linasema "haki huinua Taifa".
Kwa ajili hiyo amani ya Tanzania haitadumishwa kwa ngonjera za kusema kila
mara kwamba tunataka amani. Wala amani ya Tanzania haitadumishwa kwa propaganda
za hadaa kwamba eti chama fulani kikitawala basi ndipo amani itaendelea.
Wala amani ya Tanzania haitadumishwa kwa sala, na maombi, na dua na mahubiri
ya kinafiki kwani sisi Watanzania hatuna Mungu wetu tofauti na Mungu aliyewaumba
Warundi, Wanyarwanda, Wasomali na Wakongo, hivyo mtu akisema amani yetu
imeletwa na Mungu atakuwa anamtukuza Mungu kwa fitina, kwasababu atazua
swali kwamba je, na hizo nchi zenye vita na machafuko ina maana watu hao
Mungu amewasusa? Jibu ni kwamba la hasha! Mungu hajawasusa bali anawapenda
watu wote, anasikia kuomba kwao, kulia kwao, ama kuimba kwao na kuabudu
kwao, kwahiyo, leo hii kama kuna nchi moja ina machafuko na nyingine haina,
ni wazi kwamba kuna sababu za machafuko na sababu za utulivu isipokuwa
wengine wanasita kuzinena hadharani sababu hizo kwakuwa wana ajenda zao
za siri.
MOJAWAPO ya maandiko yenye ajenda za siri ni hicho kitabu cha kampeni kilichotolewa hivi karibuni na halmashauri ya Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste yaani PCT au Pentecostal Council of Tanzania na kuratibiwa na Askofu Sylivester Gamanywa chenye kichwa cha habari "Amani katika Tanzania italindwa kwa kutenganisha dini na mamlaka ya nchi: Katika mada hii ya Amani kudumishwa na haki tu, nitaitoa katika mtiririko au "series" na sehemu kubwa nitamega kutoka katika kitabu ambacho nimekitunga kwa lugha ya Kiingereza kiitwacho Peace and Conflicts in Africa. Kitabu hiki kitazinduliwa siku za usoni, sasa kwakuwa imekuja mada inayohusu amani sina budi kuchota katika aya zake au "chapter" zake na kuzitafsiri katika Kiswahili na kuongezea maneno mengine katika kujenga hoja zenye nguvu kuhusu somo hili la amani kudumishwa na haki. Chapter ambazo nakusudia kuzitafsiri ni ile ya kwanza, ya tatu na ya tano:- (a) Peace through justice (b) Harmonizationof interest between rulers and the ruled (c) Poverty: an obstacle Kabla ya kuingia kwenye maelezo ya undani jinsi ukiukaji wa haki unavyopelekeza uvunjifu wa amani, na kusababisha nchi nyingi za Kiafrika kukumbwa na machafuko, nalazimika kusema kuhusu kitabu cha Gamanywa kwasababu kimetolewa kwa hila si kwa nia ya kudumisha amani na pia Gamanywa kama mtu binafsio ana ajenda yake ya siri. Ni jukumu la Wakristo kujitofautisha na ajenda ya Gamanywa na hila zake, pia ni vyema Watanzania kutoka makundi yote Wakristo, Waislamu, Wahindu, wenye dini nyinginezo, wazee kwa vijana, wake kwa waume wakaelewa kwamba Gamanywa hawakilishi Wakristo, yote anayoyasema kwenye kitabu chake ni maoni yake binafsi ambayo amekuwa akiyatoa mara kwa mara kwenye gazeti lake la MSEMAKWELI ambalo limetokea kuendesha upinzani dhidi ya Waislamu, Chama cha CUF, na papo hapo kushabikia sera za chama tawala (CCM). Pili, Gamanywa siyo msemaji wa serikali kwasababu serikali ya nchi hii siyo ya Wakristo wala siyo mali ya CCM bali serikali ni ya wote, hivyo yeye anapokuwa mstari wa mbele kutoa majibu juu ya lawama au madai yoyote yanayoelekezwa serikalini anafanya kazi ya kujiajiri mwenyewe, amejivika uwakili na kutetea hata yale asiyoyajua ili tu kukidhi malengo yake binafsi. Anachokifanya Gamanywa na PCT yake ni sawa tu na kile ambacho BALUKTA ilijaribu kikifanya miaka ya tisini enzi za utawala wa Alhaji Mwinyi. Tatu ,hicho chombo kinachoitwa PCT hakiwakilishi wala hakitokani na Makanisa ya Kipentekoste bali ni brain child yake Gamanywa, na kwamba aliunda kwa namna ya kuigiza lile baraza la CCT yaani Christian Council of Tanzania. Baadhi ya makanisa makubwa ya Kipentekoste na Maaskofu wakuu kama akina Ranwell Mwenisongole wa T.A.G., Zakaria Kakobe wa Full Gospel, Mosses Kulola wa EAGT, Tibananeson wa KLPT, Mark Mhina na Obedi Sichembe wa Redeemed Church, Swedish Free Mission, Deeper Life Church na mengineyo mengi ninayoyafahamu hawamo katika PCT, sasa Gamanywa aeleze ni Halmashauri ya Maaskofu gani ambao ananena kwa niaba yao? Ieleweke wazi kwamba katika dini ya Kikristo mtu anayeitwa Askofu, ni mtu mzito sana, kiakili inatazamiwa awe amepevuka, na kielimu inastahili awe na elimu ya kutosha kiroho, na elimu ya kidunia ili anenapo na jamii asinene mambo kwa namna ya ubabaishaji. haiyumkiniki wala haiwezekani Maaskofu wenye sifa zote za kuitwa Askofu, wakakutanika pamoja kisha wakatoa tafsiri finyu na potofu ya dini kama inavyoelezwa kwenye kitabu cha Gamanywa kwambaeti neno dini lina maana ya "itikadi" au "imani" inayohusiana na mambo ya kiroho baina ya binaadamu na Mungu. (Mwisho wa kunukuu). Huu ni uthibitisho wa wazi kwamba haya ni mawazo ya mtu mmoja tena asiyeelewa maana halisi ya neno itikadi. Itikadi kwa lugha nyingine ni "ideology" neno ambalo chimbuko lake ni "idea" yaani wazo au fikra. Sasa mtu anayeitafsiri dini kwa kiwango cha chini namna hiyo, kwamba iwe sawa na mawazo tu, au fikra kama zile za socialism, humanism, communism, racialism, globalisation, indegeounisation na nyinginezo, basi huyo hata elimu yake na uaskofu wake ni wa kutilia mashaka. Na mwisho nalazimika kuiweka wazi hila na ajenda yake ya siri kwa sababu ni vitu hatari sana endapo vitafanikiwa kama ilivyokusudiwa, kwani madhara yake hayatibiki. Ni vyema nitoe mfano hai wa Interehemwe ilivyoinuka huko Rwanda, ilianza na watu wachache wenye nia ovu lakini kwasababu ya uchache wao wasingeweza kutekeleza nia yao ovu ambayo ili kutimia ilihitaji nguvu ya watu wengi tena walio shikamana pamoja. Mshikamano wa aina hiyo nauita mshikamano wa "kishetani". Hivyo kwa ujanja wa hali ya juu na kwa kutumia mbinu ya kujiweka kimbele mbele, hao wachache walijipa jukumu la kuwa wasemaji kwa niaba ya wengi ili tu kushirikisha wengine mawazo yao na kushawishi nia yao, wakavamia vyombo vya habari ili kupata fursa ya kusambaza nia yao ya kishetani huku wakitumia vitisho kwa wae wasioafikiana na mawazo yao mwisho walio wengi wakajikuta wametekwa nyara na kuingizwa kwenye utekelezaji wa kazi mbovu ya kuuua. Sylvester Gamanywa anachokifanya hakina tofauti na kiongozi wa Interehamwe yaani kuamsha hisia za chuki na kujenga hali ya kutokuaminiana. Kwanza alianza kwa kujipa jukumu la kuwa msemaji wa Wakristo kupitia gazeti lake la MSEMAKWELI na mwisho anataka kumalizia kazi yake ya kupanda mbegu ya fitina, kama msemaji wa Maaskofu lakini haelezi kinagaubaga ni Wakristo gani hao na ni Maaskofu gani hao walioamua kuwavalia njuga au kusimama kidedea dhidi ya Waislamu. Katika Tanzania hatuna matatizo kati ya Waislamu na Wakristo na hali hiyo inajidhihirisha katika maisha ya siku kwa siku ya Mtanzania kama vile nyumba za kupanga, Wakristo wengi wamepanga kwenye nyumba za Waislamu, ndoa ambalo ni suala nyeti sana hasa inapokuwa mume ni dini nyingine na mke ni dini nyingine, lakini hilo katika nchi yetu si tatizo kwani Wakristo naWaislamu wameoleana. Kwa mantiki hiyo, hakuna udini katika maisha ya kawaida ya Mtanzania. Wala Waislamu katika madai yao yote, yale yenye maana na yale ambayo hayana maana, hakuna wakati wowote ambapo wamedai kutokutendewa haki na Wakristo bali wanadai kutokutendewa haki na serikali, sasa kuna mantiki gani kwa mtu anayejiita Askofu kuibuka na kwamba huko Serikalini hakuna watu wenye hekima wawezao kujibu madai yote ya Waislamu dhidi ya serikali? Gamanywa ana uhusiano gani na serikali!! Madai hayo inabidi yajibiwe kikatiba. Zaidi ya yote Gamanywa anajulikana kwamba ni mwenye asili ya Kitutsi, kanisa analoongoza ndani yake kuna chachu ya ukabila pale Technical College wanaokutanika hakuna hata Mhutu mmoja japokuwa hapa Dar es Salaam Wahutu waliookoka ni wengi. Gamanywa ameshindwa kuonyesha upendo anaouhubiri kwa matendo kama vile kushirikiana na Wahutu kama ndugu badala yake amebaki na upendo wa maneno na mahubiri ya kushutumu wengine kama alivyomshutumu hadharani Askofu Mkuu Kakobe, wakati aliposema anaichukia CCM kwasababu ya unafiki. Kwenye gazeti lake la MSEMAKWELI anayo sera ya kufukuza yeyote yule asiyekuwa Mtutsi, alianza gazeti hilo na wenzake Watanzania wa makabila mbali mbali lakini taratibu kila anapompata Mtutsi, anamfukuza kazi mtu wa kabila jingine mpaka sasa MSEMAKWELI ina Watutsi watupu. Je mtu wa namna hiyo anaweza kweli akawa na mbegu ya kulipenda taifa moyoni mwake au kuna kitu kingine zaidi anachokipenda anapotoa kitabu chake kuhusu amani? Kwenye Gazeti lake la MSEMAKWELI kwa namna moja au nyingine anajaribu kuchochea mgawanyiko, Waislamu anawaita wao pasipo kujali kwamba nao ni sehemu ya taifa hili. Mtu yeyote katika taifa anayeanza lugha ya kuwaita wengine ni wao, na wengine sisi ndani ya nchi moja huyo tayari anatengeneza ufa wa kuligawa taifa na haitakii mema nchi anayoishi. Kwenye gazeti lake la MSEMAKWELI amejaribu kutoa picha au taswira ya kwamba Waislamu ni watu hatari, au kuna hatari inayotaka kuletwa naWaislamu lakini hatoi hitimisho la wazi kwamba ili kuondokana na hatari hiyo kitu gani kifanyike. Je Waislamu waangamizwe na nchi ibaki pasipo Mwislamu ili iwe na amani? Au Gamanywa anataka nini hasa? Ni vyema pia watu kumwelewa Gamanywa katika uhalisi wake, mnamo 1995 alijionyesha wazi kwamba anamshabikia Augustine Mrema wa NCCR (labda kwa watumaini kuwa umati wa watu wanaomkusanyikia kwenye mikutano ya hadhara, wengemfikisha Ikulu) akafikia hatua ya kuandika unabii wa mtumishi mmoja wa Mungu katika South Africa kwamba Mrema angeshinda kiti cha Urais. Baada ya uchaguzi mkuu Mrema akawa hakushinda, kuanzia hapo Gamanywa alihisi huenda amewaudhi watawala sasa ili kujionyesha kwamba ametubu, ndipo safari ya kuishabikia CCM ilipoanza na papo hapo kuwa shapu kumjibu yeyote yule anayejitokeza hadharani kuikosoa CCM au kuilaumu serikali, amemjibu Kakobe, amewajibu Wasilamu, na pia ameandika makala nyingi tu za kujibu mada zangu kuhusu dini na siasa hii yote ni katika kujisafishia na kujitengenezea njia na watawala lakini funga kazi ni mwaka juzi ambapo alichukua baadhi ya maandiko ya kikundi fulani cha Waislamu kilichokuwa kinazungumiza fatwa na akataka kuombea ukimbizi na hifadhi (assylum) huko Marekani kwa kisingizio cha kwamba kutokana na sera yake ya kutetea Ukristo, basi Waislamu wanataka kumuua, hata hivyo juhudi zake ziligonga ukuta. Mtu ambaye mguu moja ndani mwingine uko hewa ni unatafuta nchi ya kutua je uzalendo wake uko wapi hasa asame AMANI? Katika kitabu chake kichwa cha habari Amani katika Tanzania italindwa kwa kutenganisha dini na mamlaka ya nchi, huu ni uwongo kwasababu hakuna mtu yeyote aliyetaka dini na serikali viwe kitu kimoja. Wala hawezi kututhibitishia kwamba machafuko yaliyozikumbwa Rwanda, Burundi na Somalia yanatokana na watu au mtu kuunganisha dini na mamlaka ya nchi. Wala hawezi kututhibitishia kwamba nchi zilizoamua kuwa na serikali za kidini zina machafuko badala yake kuna mfano hai wa nchi jirani ya Zambia, rafiki yangu rais Chiluba ametangaza rasmi kwamba Zambia ni taifa la Kikristo mbona Zambia isikumbwe na matatizo kama Burundi na Rwanda? Uingereza ni nchi ya Kikrsto tena ili kuiongoza ni lazima kiongozi awe Muanglicana. Ujerumani ni nchi ya Kilutheri, Marekani ni taifa la Kikristo tena Ulokole, mbona hizo hazijatenganisha dini na dola? Kwa kutoa mifano hiyo sikusudii kwamba nasi Tanzania tuige mfano wa Zambia, Uingereza au Marekani la hasha isipokuwa ninachotaka kusema Gamanywa kwenye kitabu chake hamaanishi kutenganisha dini na mamlaka yanchi, bali anamaanisha Waislamu watengwe na mamlaka ya nchi. Hii ni roho ya nyoka inabidi ipigwe vita kabla ya kuzaa matunda kama ya Interehamwe. Wiki ijayo amani kudumshwa na maendeleo.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Wapinzani kumuimarisha Prof. Lipumba Ngangari kung’olewa Sokoni, Ilala Polisi nchini hawajui mipaka ya kazi yao -OAU MAKALA
HABARI
ATV yatakiwa kuzingatia maadili Wakazi wa Tabata walalamikia athari ya maji machafu Maalim Seif akanusha madai ya kumwaga damu USHAURI NASAHA
MAKALA
MIPASHO NASAHA
KALAMU YA MWANDISHI
MAKALA
MWENYE MACHO…
MAKALA
LISHE
|
|
|
|
|