NASAHA
Na. 067 Jumatano Septemba 27 - Oktoba 2, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA

Chonde Dk. Omari na Karume wahurumieni Wazanibari wenzenu

Na B.A. Maua

MWANZONI mwa miaka ya tisini dunia ilishuhudia maelfu ya raia wakiuliwa bila hatia nchini Irak. Mauaji hayo yalifanywa na majeshi ya Marekani na washirika wake. Kwa kisingizio cha kuikomboa Kuwait iliyovamiwa na majeshi ya Saddam Hussein. Wakati wananchi wa Irak na serikali yao wakihangaika na athari ya vita hivyo, Wamarekani wao kwa kuwa vita havikupiganwa katika ardhi yao wamekuwa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.

Kupelekwa kwa askari wengi Zanzibar wakiwa na magari ya Deraya kutoka Tanzania bara kunaashiria hatari inayoweza kutokea kama ilivyokuwa Irak. Hisia hizi zinapata uzito na kauli ya Dk. Omari na mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Mahita.

Kauli ya Dk. Omari kuwa majeshi yaliyopelekwa Zanzibar yamepelekwa kwa lengo la kuidhibiti CUF na vitisho vya IGP Mahita kuwa kama CUF ni ngangari basi polisi ni ngunguri ni kauli za kutisha zenye kubeba hisia za uhasama wa kisiasa zaidi, kuliko ulinzi wa raia na mali zao.

Hizi ni kauli za kutisha kutokana na ukweli kuwa zimetolewa na viongozi wakuu serikalini. Maneno ya Dk. Omari yangekuwa yametolewa na Mtopea tusingeyatia akilini hata kidogo. Dk. Omari ni kiongozi wa juu katika serikali ya Muungano. Kwa hiyo anayoyasema lazima yatakuwa yanatoka katika vikao maalum vya CCM na serikali yake.

Bwana Omari Mahita ni mkuu wa jeshi la Polisi nchini. Polisi kama walivyo maaskari wengine duniani wamekula kiapo cha kuitii serikali iliyokuwepo madarakani kwa hiyo aliyoyasema Dk. Omari ni amri ya serikali na aliyoyasema Bwana Mahita ni maneno ya utii kwa serikali na sasa ni utekelezaji wa amri ya serikali.

Ni vyema ieleweke kuwa madhara ya kuidhibiti CUF kwa majeshi na magari ya Deraya hayatowaathiri wananchama na wapenzi wa CUF peke yao. Popote pale inapotumika nguvu athari zake huwapata watu wote, waliokuwemo na wasiokuwemo uwe CCM uwe CUF cha moto utakiona. Deraya litakapofyatuliwa halitachagua mtu.

Kwa kuwa hicho kitimtim chake kitakuwa ndani ya Zanzibar wasio kuwa Wazanibari watashuhudia kupitia Runinga zao; kama ambavyo Wamarekani walivyo kuwa wakishuhudia majeshi yao yalivyokuwa yakiteremsha mabomu ndani ya ardhi ya Irak mwanzoni mwa miaka ya tisini.

Historia inaonyesha kwamba hakuna serikali ya nchi yoyoe duniani, iliyowahi kupambana na raia zake na kisha serikali hiyo ikaibuka kuwa mshindi.Wananchi wanahoji kwanini tufike huko kote? Wakati tunaambiwa kuwa CCM ndio baba wa amani? Hakuna watu ndani ya hiyo CCM wanaoweza kumshika masikio shetani anayeinyemelea Zanzibar na kumtuliza?

Waswahili wanasema:

Kila shetani na mbuyu wake. Mbuyu wa shetani anayeinyemelea Zanzibar uko wapi? Uko CCM au uko CUF?. Lakini ninalolijua ni kuwa Dk. Omari na Karume ni watu muhimu wanaoweza kumshika masikio na kumtuliza shetani mbaya anayetaka kuipatiliza nchi ya Zanzibar badala ya kuwa wapiga mikwara kama wanavyofanya hivi sasa.

Hii inatokana na ukweli kuwa Dk. Omari yeye ni kiongozi wa juu katika serikali ya muungano na isitosheni Mzanzibari. Na Bwana Karume yeye ni mgombea wa Urais Zanzibar na ni kipenzi wa Chama Cha CCM Bara. Vile vile Dk. Omari kwa kuwa baada ya awamu ya tatu kumaliza kipindi chake ana nafasi kubwa ya kupitishwa kuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, kuinusuru Zanzibar katika kipindi hiki ambapo nchi inachungulia shimo la vurugu kubwa kutamuongezea sifa na imani kwa wapiga kura siku za usoni. Kwa hiyo ushauri wake utakuwa ni wenye kusikilizwa sana ndani ya CCM.

Kwa hiyo hawa watu wawili kwa ushawishi walionao kwa viongozi wa CCM bara wanaweza kuishauri serikali ushauri huo. Kwa kufanya hivyo watakuwa wamewanusuru Wazanzibari wenzao wasiumizwe na majeshi ya ngunguri yenye magari ya deraya kutoka bara.

Kwa vile kwa maelezo ya Dk. Omari majeshi hayo na magari yao ya Deraya yamepelekwa Zanzibar kwa lengo la kudhibiti chama cha Wananchi (CUF) na kwa kuwa hiki ni kipindi cha uchaguzi inaweza kama pia nia ya ngunguri kudhibiti chama cha wananchi, ikawa ni moja njama za chama tawala kutaka kumrahisishia mgombea wake wa nafasi ya urais apite kwa urahisi na yeye pia anaweza kurekebisha dhahama inayoinyemelea Zanzibar kutoka Tanganyika, kwa visingizio vya kuilinda amani na kulinda muungano.

Siku chache kabla ya kuteuliwa kwake kuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM Mheshimiwa Karume alisema hataki "kubebwa" na kupewa ushindi wa wizi. Mheshimiwa Karume ni Muislamu japo huenda akawa hachanganyi dini na siasa kama chama chake cha CCM kinavyopenda ionekane, lakini tunaamini kwamba anafahamu kuwa ahadi ni deni na ni yenye kuulizwa kesho mbele ya Mungu. Hivyo basi napenda kumpa ushauri nasaha akumbuke Mheshimiwa Karume kwambaa anze kutimiza ahadi yake kuanzia sasa kwa kukataa matumizi mabaya ya majeshi dhidi ya raia kwa faida yake yeye kama mtaka urais Zanzibar na wananchi wa Zazibar kwa ujumla.

Muota moto haachi kunuka moshi. Mgombea urais wa Zanzibar (CUF) Maalim Seif aliwahi kusema kuwa pamoja na kuwa Karume ni kijana mzuri kwa kuwa yumo CCM si wa kumwamini hata kidogo. Kwahiyo sisi wananchi tunasema ili Karume asinuke moshi wa moto anao uota aanze sasa kuwatetea ndugu zake Wazanzibariw anaotaka kuangamizwa. Asipofanya hivyo, tutaendelea kumwamini Maalim Seif kuwa pamoja na uzuri wake Mheshimiwa Karume moto wa CCM umemfanya unuke moshi.

Tumefurahishwana kauli za Dk. Salmin kukataa Zanzibar kugeuzwa Rwanda. Na tunaungana na Maalim Seif kumpongeza Dk. Salmini kwa ujasiri wake huo wa kuwapinga watu walio nje ya Zazibar wanaotaka kuleta chokochoko na kuifanya Zanzibar kuwa uwanja wa mazoezi ya "majeshi" yao. Hapana shaka wenye nia zao watakuwa wamechukizwa na ujasiri wa Dk. Salmin.

Lakini sisi wapenda amani, haki na usawa tunatakiwa tumuunge mkono Dk. Salmini na kukataa kuwapa kura watu waliopandikizwa na wasio ionea huruma Zanzibar na raia wake.

Mwisho napenda kuchukua fursa hii kuwaomba waheshimiwa Karume na Dk. Omari waige mfano wa Dk. Salmin katika kuinusuru Zanzibar hasa katika kipindi hiki kigumu cha uchaguzi ambapo watu wenye chuki zao wamekusudia kuigeuza Zanzibar kuwa Rwanda. Nyinyi ni waumini wa dini moja na sifa mojawapo mliyopewa na Mwenyezi Mungu ni kuoneana huruma ninyi kwa ninyi. Kwa nini mnaweka maslahi ya vyama vyenu mbele, kuliko maslahi ya dini yenu.

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Polisi ‘isiibebe’ CCM

Wapinzani kumuimarisha Prof. Lipumba

Ngangari kung’olewa Sokoni, Ilala

Polisi nchini hawajui mipaka ya kazi yao -OAU

MAKALA
BBC, CCM ndugu au tajiri na kibaraka?

HABARI
‘Walioshindwa kutawala wasikimbilie matusi’

ATV yatakiwa kuzingatia maadili

Wakazi wa Tabata walalamikia athari ya maji machafu

Maalim Seif akanusha madai ya kumwaga damu

USHAURI NASAHA
‘Mama, hela hii inanunua nini?'

MAKALA
Demokrasia ni kukubaliana kutokukubaliana

MIPASHO NASAHA
HEBU VUENI MIWANI ZENU!

KALAMU YA MWANDISHI
Juha haliambiliki!Juha haliambiliki!

MAKALA
Amani ya Tanzania itadumishwa na haki

MWENYE MACHO…
Hoja za uongo katika kampeni

MAKALA
Chonde Dk. Omari na Karume wahurumieni Wazanibari wenzenu

Habari za Kimataifa

LISHE
Kimfaacho  mtoto

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga kuwakosa Mahadhi, Mbuna
  • Idd Azzan lawamani
  • Kibadeni, Kayuni wanafaa Stars - Machuppa
  • Said Maulidi: Sihami Simba

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita