NASAHA
Na. 067 Jumatano Septemba 27 - Oktoba 2, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Wiki tano kabla ya Uchaguzi Mkuu:

Wapinzani kumuimarisha Prof. Lipumba

  • Kamati kusambaza ujumbe wa mshikamano nchi nzima
  • Yaelezwa ndiye anayeelekea kushinda
Na Mwandishi Wetu

KAMBI ya upinzani dhidi ya chama tawala, sasa inafanya kazi kumuimarisha mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano, Profesa Ibrahim Lipumba anayegombea kiti hicho kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) na ridhaa ya Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA), imefahamika jijini.

Wakizungumza na NASAHA jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, wajumbe wawili wa kamati iliyoundwa kusambaza "ujumbe wa mshikamano" wameeleza kuwa wazo la kumuimarisha Prof. Lipumba lilitokana na wazee kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Mwanza, Shinyanga na Kagera, waliokutana mwanzo mwishoni mwa mwezi Agosti. Katika wajumbe hao wawili, mmoja ni mwanachama wa UDP na mwingine ni TLP.

Kwa mujibu wa wazungumzaji hao, kikao cha wazee kilichozaa wazo hilo, kiliwajumuisha wazee wanachama wa vyama vya UDP, TLP na NCCR ambao baada ya kujadiliana walibaini kwamba "kura za wapenzi wa UDP pekee haziwezi kumpelekea Bw. (John) Cheyo Ikulu"

"Na wale wa TLP waliona hivyo hivyo... kura zao pekee hazitoshi kumwingiza mgombea wao (Augustine Mrema)Ikulu", alieleza mjumbe mmoja.

"Baada ya kubaini hilo, wazee wetu wakaona badala ya kupoteza kura zetu bure, ni bora sisi sote tumpe kura mgombea anayeelekea kushinda....basi wakakubaliana tumpe Prof. Lipumba", alisema mjumbe huyo.

Walipoulizwa ni vipi maslahi ya vyama vyao yatalindwa katika serikali mpya hali ya kuwa vyama vya UDP na TLP havina makubaliano na CUF au CHADEMA, walisema jambo hilo hatuna shaka kwa vile Profesa Lipumba alipokutana na wazee mjini Mwanza alisema yeye hana ugomvi na Bw. Cheyo wala na Bw. Mrema.

"Profesa aliwambia wazee (kwamba) katiba ya nchi ya sasa inawawezesha wapinzani kushirikiana kuongoza nchi; yeye akiwa rais amepewa nafasi kumi za kuteua watu ambao si wabunge kuingia bungeni hivyo hawezi kushindwa kuwachukua Mrema na Cheyo", alisema mjumbe ambaye ni mwanachama wa TLP.

Wamesema Profesa Lipumba aliwaambia wazee hao kwamba watu wa upinzani hawana ugomvi baina yao bali wote wanapambana na CCM ambayo ndiyo sababu ya uduni wa maisha ya Watanzania.

Na akasema CCM haitaki mshikamano wa watanzania ndio maana ilikataa kuunda serikali ya mseto.

Ujumbe huo wa watu wawili ulifika Dar es Salaam ukitokea mikoa ya Mara, Arusha, Tanga na Kilimanjaro. Mjumbe wa tatu ambaye walieleza ni mwanachama wa NCCR hakuweza kufuatana nao baada ya kupata dharura ya kifamilia.

"Mwenzetu wa NCCR anamuuguza mkewe hospitali ya Bugando", alieleza mjumbe mmoja.

Wameeleza, baada ya wazee kukubaliana kumuimarisha Prof. Lipumba, waliunda kamati ambayo wajumbe wake walipewa kazi ya kuzunguka katika kanda zote nchini.

Kamati hiyo yenye wajumbe 11, iliunda timu tatu zenye wajumbe watatu kila moja kuzunguka kanda Kaskazini (Mara, Arusha, na Kilimanjaro ),Kanda ya Kati (Shinyanga, Tobora, Singida na Dodoma)na Kanda ya Magharibi (Kigoma, Rukwa na Mbeya).

Wamesema wajumbe wawili wa kamati hiyo waliopangwa kubaki mjini Mwanza ambako ndiko makao makuu ya kamati kwa ajili ya kupokea taarifa na kuratibu shughuli za uhamasishaji na uchangiaji fedha. Kamati hiyo imeanza kazi wiki mbili zilizopita, wakiwa jijini Dar es Salaam, wajumbe hao wamesema wamezungumza na "wapenda mageuzi" wa hapa na wamekubaliana kimsingi kuundwa kwa ujumbe utakaopeleka salaam za mshikamano katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma. Aidha wamesema Kanda ya Dar es Salaam itajumuisha mikao ya Tanga, Pwani na Dar es Salaam yenyewe.

"Plan (mpango) yetu ni kwamba kutakuwa na makao makuu ya kila kanda, na tumeteua mikoa ya Mwanza, Shinganya, Dar es Salaam, Mbeya na Ruvuma kuwa makao makuu ya kanda, alieleza mjumbe mwachama wa UDP.

Wakieleza mafanikio ya safari yao, wajumbe hao wa kamati hiyo toka vyama vya upinzani inayozunguka kumuimarisha Prof. Lipumba wamesema hawakupata tabu kueleweka kwa watu kwa vile "Profesa (Lipumba) ni mgombea anayekubalika sana nchini kote."

Hata hivyo wajumbe hao walitaka majina yao wala yale ya wanakamati wenzao yasitajwe kwa kile walichodai ni kuogopa hujuma dhidi yao. Hawakufafanua hujuma hiyo ni ipi na inaweza kufanywa na nani.



Ngangari kung’olewa Sokoni, Ilala
  • Vijana wasema wapo ngangari
  • Polisi kutumika
Na Mwandishi Wetu

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Bw.Yusuf Makamba, ameagiza kuondolewa mara moja kwa bendera ya chama cha wananchi (CUF) iliyopo mbele ya soko la Mitumba linalotazamana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wa Dar es Salaam eneo la Ilala-Boma, kwa madai kuwa "inamdhalilisha" Rais Benjamin Mkapa.

Agizo hilo limetolewa na huyo wa Mkuu wa Mkoa majira ya saa 5 asubuhi jana.Mhe. Makamba alisimamisha gari katika eneo hilo na kuwaita vijana wafanyao biashara ya mitumba na kuwaagiza waiondoe bendera hiyo ya CUF pamoja na ya TLP zinazopepea katika eneo hilo zikiwa zimeiweka kati bendera ya CCM.

Baada ya kutoa amri hiyo Mkuu huyo wa mkoa aliwaambia vijana hao kuwa hahitaji maswali na kwamba wasipotekeleza amri hiyo atalivunja eneo hilo lote chini ya usimamizi wa polisi.

Kufuatia hatua hiyo zogo kubwa lilizuka miongoni mwa vijana hao wauza mitumba huku wale wa CCM wakiwataka wale wa CUF na TLP waondoe bendera zao ili kuweza kuendelea kufanya biashara katika eneo hilo, jambo ambalo lilipingwa vikali na wanangangari.

Baadaye wanangangari wakaamua kumtuma mwenzao aitwaye Mohamed Athuman ofisi kuu ya CUF Buguruni kutoa taarifa, huku wakiapa kuwa hawatashusha bendera yao mpaka ile ya CCM nayo ishuke. Wakasema kuwa wao wako "ngangari kinoma." 

Mwandishi wa habari hizi alipowasiliana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa kujua msimamo wao kuhusu suala hilo alijibiwa na aliyepokea simu kuwa Mkuu huyo wa Mkoa alikuwa ametoka kuelekea nyumbani kwa kuwa anaumwa. 

Bw.Ernest Lyanga ambaye ni Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa CUF naye alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi kama wana taarifa zozote na hatua gani wangechukua alijibu kuwa wameshawasiliana na ofisi ya Mkuu wa polisi Mkoa wa Dar es Salaam ili kuwafahamisha juu ya walivyoviita vitisho dhidi ya wanachama wake.


Polisi nchini hawajui mipaka ya kazi yao -OAU

Na Mwandishi Wetu

Imeelezwa kuwa jeshi la Polisi nchini halijui mipaka ya kazi zake ,jambo ambalo linaweza kuathiri utulivu, amani na mwenendo mzima wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu. 

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa idara ya Mambo ya Siasa ya Umoja na Nchi Huru za Afrika (OAU) Sam Ibok alipozungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika ukumbi wa idara ya Habari (MAELEZO) Ibok alisema yeye na ujumbe wake wamebaini upungufu huo wa polisi baada ya kuzungumza na viongozi wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu Zanzibar.

Alisema: "Tumeambiwa badala ya Polisi kulinda amani wanawashambulia viongozi wa vyama vya siasa...."

Vyama vya upinzani nchini vimekuwa vikieleza malalamiko yao kwamba wafuasi wake wananyanyaswa na polisi wanapohudhuria mikutano ya kampeni za vyama vyao.

Viongozi wa vyama vya CUF na NCCR-Mageuzi wamelishutumu jeshi la polisi na Mkuu wa Jeshi hilo, Inspector Jenerali wa Polisi Omari Mahita kwa kuwaagiza polisi kuwakamata na kuwatesa wafuasi wa vyama vya upinzani.

Katibu Mkuu wa CUF, Bw. Seif Shariff Hamad mbali na kumwandikia barua mkuuw a Jeshi la Polisi nchini, amelituhujumu jeshi hilo kula njama za kuhujumu chama chake.

Mpaka sasa mikutano kadhaa ya kampeni ya chama hicho ambacho kwa tiketi zake Bw. Hamadi anagombea urais wa Zanzibar na Prof. Ibrahim Lipumba anawania Urais wa Jamhuri, imevurugwa na polisi ambao wafuasi kadhaa wa CUF wameripotiwa ‘kupata mkong’oto’, kuwekwa ndani na hata wengine kufunguliwa mashtaka ya kukusanyika au kuandamana bila kibali na kufanya fujo.

Wakati huo huo, IGP Mahita ameseme jeshi la Polisi nchini litawadhibiti wale wote wanaotaka kuleta fujo ili kuvuruga uchaguzi.

Kpt. Mahita aliyasema hayo Alhamisi iliyopita alipozungumza na askari polisi na maafisa wa jeshi hilo wapatao 4000 jijini Dares Salaam ambapo alisema jeshi hilo litahakikisha kila mtu anapiga kura kwa utulivu na amani.

Akionya dhidi ya wale waliodai wanaweza kusababisha vurugu Mahita alisema: "hakuna Kosovo —ngangari wala NATO."

Ingawa Mahita hakufafanua kauli yake hiyo, watu wengi wametafsiri kuwa waliolengwa hapo ni CUF na wafuasi wake.

Msimamo huo wa Inspekta Jenerali wa Polisi nchini, umelalamikiwa na wengi kwa madai "unawabana wapinzani na kuwaacha wafuasi wa CCM wafanye wapendavyo."

Mahita amekuwa akilaumiwa kwa kuwafumbia macho CCM kwa kauli zao zinazodaiwa kuashiria shari za "mtu kwa mtu."

Siku chache kufuatia tamko hilo la Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Kamati Kuu ya CCM iitoa agizo kwa serikali za Mungano na ile ya Zanzibar kuimarisha ulinzi dhidi ya madai ya vitisho vinavyotolewa na viongozi wa CUF.
 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Polisi ‘isiibebe’ CCM

Wapinzani kumuimarisha Prof. Lipumba

Ngangari kung’olewa Sokoni, Ilala

Polisi nchini hawajui mipaka ya kazi yao -OAU

MAKALA
BBC, CCM ndugu au tajiri na kibaraka?

HABARI
‘Walioshindwa kutawala wasikimbilie matusi’

ATV yatakiwa kuzingatia maadili

Wakazi wa Tabata walalamikia athari ya maji machafu

Maalim Seif akanusha madai ya kumwaga damu

USHAURI NASAHA
‘Mama, hela hii inanunua nini?'

MAKALA
Demokrasia ni kukubaliana kutokukubaliana

MIPASHO NASAHA
HEBU VUENI MIWANI ZENU!

KALAMU YA MWANDISHI
Juha haliambiliki!Juha haliambiliki!

MAKALA
Amani ya Tanzania itadumishwa na haki

MWENYE MACHO…
Hoja za uongo katika kampeni

MAKALA
Chonde Dk. Omari na Karume wahurumieni Wazanibari wenzenu

Habari za Kimataifa

LISHE
Kimfaacho  mtoto

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga kuwakosa Mahadhi, Mbuna
  • Idd Azzan lawamani
  • Kibadeni, Kayuni wanafaa Stars - Machuppa
  • Said Maulidi: Sihami Simba

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita