NASAHA
Na. 067 Jumatano Septemba 27 - Oktoba 2, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA

BBC, CCM ndugu au tajiri na kibaraka?

Na Mariam Sudi

Tarehe 22/9/2000 asubuhi, katika kipindi cha BBC Network Africa kwenye jarida la BBC World Service for Africa,kulikuwa na mahojiano kati ya mtangazaji aliyejitambulisha kwa jina la Ben Dose Malo na Waziri wa Nishati naMadini Tanzania, Bw. Abdala Kigoda.

Mahojiano hayo yalihusu siasa na kampeni zinazoendelea nchini Tanzania, ambapo mtangazaji alianza na anuani ya "General election in Tanzania a foregoing conclusion for the ruling party", yaani,"Uchaguzi Mkuu Tanzania ni matokeo (ya ushindi?) ulio wazi kwa chama tawala."

Msikilizaji yeyote angelitarajia hoja za mahojiano zithibitishe dhana ya mtagazaji ambaye alikuwa akimhoji Waziri wa chama tawala.

Na zaidi ya hayo msikilizaji angelitegemea kuona mtangazaji huyo anazo takwimu za hali halisi ya siasa na matukio yanayotawala kampeni zinazoendelea kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Kinyume chake, mtaganzaji huyo ama alikuwa mbumbu wa hali halisi ya kampeni hizo ilivyo nchini au alikuwa akijifanya hivyo.

Maana alielekea kukubali mengi aliyoambiwa na Kigoda, pasipo kuhoji ukweli wake hata yale ambayo hayakuwa na ukweli.

Kwa mfano, Dr. Kigoda alimwambia mtangazaji huyo kwamba chama chake kimeweka wagombea wote waliopendekezwa na wananchi kwenye kura za maoni, jambo ambalo ni kinyume na ukweli kwamba chama hicho kiliwaengua wagombea zaidi ya 50 waliopendekezwa na wananchi.

Kama vile wanalindana, mtangazaji wala hakuhoji suala zito la kwa nini chama hicho tawala kilizuia wanawake wasigombee nafasi ya Urais, kinyume cha haki za kibinadamu, katiba ya nchi na misingi ya kidemokrasia.

Wala hakuhoji rekodi mbaya ya chama hicho na serikali yake kuhusu suala la rushwa ambapo Tanzania ni nchi ya tatu Afrika na ya saba duniani kwa kubobea katika rushwa.

Pamoja na hali hiyo mtaganzaji huyo wala asione habari muhimu kujua lawama zilizomuendea rais wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama tawala na mgombea Urais wa chama hicho katika uchaguzi ujao, kuhusu uwezo wa kuondoa rushwa.

Kwamba vipi alilaumiwa kumchukua mwenyekiti wa mkoa wa chama hicho na kusafiri nae nje ya nchi wakati mwenyekiti huyo alikuwa akihojiwa na maafisa wa kikosi cha kuzuia rushwa nchini. Kwamba baada ya kusafiri naye, inasemakana maafisa wale walihamishwa toka mkoa huo na hivyo mahojiano hayo kusitishwa kwa "hofu".

Pamoja na yote hayo, mtanganzaji huyo wa BBC, shirika lenye mtandao na uwezo wa kupata na kujua habari nyingi, asimhoji Dr. Kigoda kuhusu malalamiko ya rushwa kutumika katika kura za maoni ya kuteua wagombea udiwani na ubunge kwa tiketi ya chama hicho (CCM) jambo ambalo ni maarufu nchini na licha ya kutawala katika vyombo vya habari, lilitajwa pia katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM wakati wa kuwachuja wagombea waliopendekezwa na wananchi.

Kwa kuwa mahojiano hayo yalihusu muelekeo wa matokeo ya uchaguzi mkuu ujao, mtangazaji huyo alipaswa kujua na kumhoji Dr. Kigoda kuhusu Polisi wanavyotumika na kulalamikiwa na wapinzani kwamba wanavuruga kampeni zao ama kwa kuwanyima vibali vya mikutano au kuwazuilia wananchi kwa namna moja au nyingine kuhudhuria mikutano ya vya vya upinzani.

Mtangazaji huyo wa BBC kwa mfano angeliweza kuhoji kuhusu virungu vya polisi huko Zanzibar dhidi ya CUF, shutuma za CUF dhidi ya serikali na chama tawala kupeleka watu toka bara kwenda kujiandikisha kupiga kura Zanzibar kinyume cha sheria, na pia kupeleka askari wa jeshi, vifaru vya jeshi na vitisho kwamba majeshi hayo na silaha hizo ni kwa ajili ya CUF.

Mtangazaji huyo pia angeliweza kuuliza kuhusu matumizi ya lugha ya jazba, chuki na matusi dhidi ya wapinzani.

Ajabu ya mtangazaji huyo hakuona umuhimu wa swali kuhusu Zanzibar ambapo uchaguzi wa mwaka 1995 ulizua mgogoro na kazi kubwa na ya gharama kwa Jumuiya ya Madola ambayo kiongozi wake ni mlezi wa serikali ya Uingereza na BBC.

Wala asione umuhimu wa kumuuliza Dr. Kigoda kuhusu madai ya CUF,kwa Tume ya Uchaguzi na Taasisi ya Kuzuia Rushwa nchini kwamba alietakiwa na wananchi kwa tiketi ya CUF kugombea ubunge dhidi ya Dr. Kigoda, "aliingia mitini kiajabu-ajabu" siku ya kurudisha fomu za mgombea uchaguzi, katika nafasi ya ubunge.

Hatujui kuna uhusiano gani kati ya BBC na CCM, kiasi cha BBC kuonekana kutaka kuingilia siasa za nchi kwa kuchagua upande mmoja wa kupigia zumari chama kimojawapo kati ya vingi vinavyogombea nafasi ya kuchaguliwa na wananchi katika uchaguzi mkuu ujao.

Awali nilifikiria kuwaandikia BBC juu ya hilo kupitia kipindi chao cha Talk Back, lakini baada ya kuona baadhi ya wakereketwa wa CCM wanayatumia mahojiano hayo (kati ya BBC na Dr. Kigoda) kufanikishia ushabiki wao kwa CCM dhidi ya vyama vya upinzani katika mitaa kadhaa jijini Dares Salaam, nikaamua bora nami nipeleke makala haya gazetini ili ukweli wa mambo toka upande wa pili nao pia ueleweke mitaani. Na madhali BBC wana watu wao nchini,nina hakika kama si woga wa maoni ya upande wa pili, watawapelekea wenzao nakala ya makala haya yenye habari hizi.

Nina hakika vile vile kama mtangazaji huyo wa BBC angelikuwa mkweli katika wajibu wa kazi yake, na kuhoji mambo kadhaa pamoja na hayo niliyoyataja, angelitambua udhaifu wa chama tawala (CCM) katika umri wake wa miaka 40 kuanzia jina lake la zamani, TANU.

Angelijua jinsi kilivyoshindwa katika sera zake za ujamaa, jinsi kilivyoangusha uchumi wa nchi hadi kupelekea wananchi enzi za utawala wa Marehemu Nyerere kudhalilika kwa kutegemea msaada wa unga wa njano, kupitia mgao wa "posho" ya kilo mbili kwa wiki toka kwenye maduka ya kaya.

Angelijua jinsi utawala wa chama hicho ulivyoangusha viwanda na mashirika ya umma hadi kuuzwa kwa bei ya "kutupa". Angelijua CCM imeifanya Tanzania iwe nchi ya kwanza kwa umasikini barani Afrika ukiondoa nchi nne zilizokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambazo ni:Siera Leone, Ethiopia, Somalia na Msumbiji.

Angelijua jinsi utawala wa CCM ulivyopelekea nchi hii kuwa chini katika elimu kiasi kwamba kuna watoto milioni tatu wasioenda shule na kati ya wanaokwenda, ni asilimia 0.3 ndio wafikao chuo kikuu.

Mtangazaji huyo angelijua kuwa licha ya Watanzania wengi kufa kwa maradhi kutokana na ukosefu wa kupata uwezo wa kulipia matibabu, nchi hii pia ina tatizo kubwa la njaa, kiasi kwamba mwaka juzi chini ya utawala wa Serikali ya CCM,iliripotiwa watu zaidi ya 40 kufa kwa njaa Wilayani Ulanga, katika mkoa wa Morogoro.

Kwamba umasikini huo hautokani na hali ya nchi. Nchi hii, mtangazaji huyo angelitambua, ina mito, maziwa, bahari, mabonde na ardhi yenye rutuba na hali ya hewa nzuri kwa kilimo, uvuvi, ufugaji na uhifadhi wa wanyama pori.

Angelijua jinsi nchi hii ilivyo na maeneo mengi ya vivutio vya utalii. Na kwamba kuna akiba kubwa ya madini ya thamani na ya kila aina, pamoja na gesi,na petroli. Kwamba umasikini wa nchi hii ni matokeo ya utawala na sera mbovu za chama tawala ambacho kimeshindwa kuiendeleza nchi na hazina yake ya maliasili kwa manufaa ya wananchi wake.

Kwa kuyajua hayo, naamini mtangazaji huyo wa BBC, angelijua ni upi muelekeo wa wananchi kuhusu uchaguzi mkuu ujao. Angelijua kwa nini wananchi wameamua kuleta mabadiliko ya utawala katika uchaguzi ujao nchini. Angelijua kwa nini Profesa Lipumba anakubalika nchini kote mijini hadi vijijini.

Na kwa kuujua ukweli huo, mtangazaji huyo kama si mshabiki wa chama tawala basi asingeliweka anwani ile (au kichwa cha habari) kinachoashiria sifa kwa CCM. Au pengine tuseme anashuku kura zitakujaibiwa? 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Polisi ‘isiibebe’ CCM

Wapinzani kumuimarisha Prof. Lipumba

Ngangari kung’olewa Sokoni, Ilala

Polisi nchini hawajui mipaka ya kazi yao -OAU

MAKALA
BBC, CCM ndugu au tajiri na kibaraka?

HABARI
‘Walioshindwa kutawala wasikimbilie matusi’

ATV yatakiwa kuzingatia maadili

Wakazi wa Tabata walalamikia athari ya maji machafu

Maalim Seif akanusha madai ya kumwaga damu

USHAURI NASAHA
‘Mama, hela hii inanunua nini?'

MAKALA
Demokrasia ni kukubaliana kutokukubaliana

MIPASHO NASAHA
HEBU VUENI MIWANI ZENU!

KALAMU YA MWANDISHI
Juha haliambiliki!Juha haliambiliki!

MAKALA
Amani ya Tanzania itadumishwa na haki

MWENYE MACHO…
Hoja za uongo katika kampeni

MAKALA
Chonde Dk. Omari na Karume wahurumieni Wazanibari wenzenu

Habari za Kimataifa

LISHE
Kimfaacho  mtoto

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga kuwakosa Mahadhi, Mbuna
  • Idd Azzan lawamani
  • Kibadeni, Kayuni wanafaa Stars - Machuppa
  • Said Maulidi: Sihami Simba

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita