|
Na. 067 Jumatano Septemba 27 - Oktoba 2, 2000 |
|
|
|
|
|
Demokrasia ni kukubaliana kutokukubaliana
Na M.M. Mbogo
WAKATI tukielekea katika uchaguzi mkuu wa pili ndani ya mfumo wa vyama vingi, ambao mambo mengi yanafichua uchanga wetu katika demokrasia hii ya shindani yanazidi kudhihirika. Viongozi wa vyama vya siasa na wale wa serikali wanatoa picha halisi juu ya uchanga wa Tanzania katika mfumo huo. Picha hii pia inafichua siri kubwa ya kwamba pengine viongozi waliyopo madarakani hawapo tayari kuukubali upinzani katika namna ya kiistaarabu. Kimsingi, mfumo wa demokrasia y aushindani unayo asili yake toka katika ustaarabu wa kukubaliana kutokukubaliana. Ustaarabu huu unakiri tofauti mbalimbali zilizopo miongoni mwa wanadamu katika mitizamo, fikra na namna ya kukabiliana na matatizo mbalimbali. Historia ya mwanaadamu inashuhudia kwamba kadri mwanaadamu na dola yake katika vipindi mbalimbali alivyojaribu kupingana na ukweli huu wa kimaumbile, ndipo alipokumbana na matatizo makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ambayo hatima yake imekuwa ni migongano na misuguano yenye madhara. Ni kutokana na misuguano hiyo isiyoisha ndipo mwanaadamu akajifunza lugha ya kistaarabu ya kuzikubali na kuzitambua tofauti hizi kama sehemu ya maisha yake. Kwa kuwa tofauti huleta utengano na hatimaye migongano, kadri mwanaadamu alivyokuwa kimawazo na kisiasa ndivyo alivyogundua njia na utaratibu wa kuowanisha tofauti hizo na hatimaye akaibuka na msingi mkuu wa ushindani unaowataka washindani kukubaliana kutokubaliana. Miaka mingi imeshapita toka ustaarabu huu ulipoingia katika vitendo, japo kudhihiri kwake kumekuwa kukitofautiana toka sehemu moja kwenda nyingine. Hatuwezi kusema kwamba Tanzania iliingia katika ustaarabu huu mwaka 1992 bali hata ndani ya mfumo wa chama kimoja ustaarabu wa kukubaliana kutokubaliana ulikuwepo japo siyo katika rangi yake halisi. Tunakumbuka enzi za nyundo kwa jembe japo mtindo huu ulionekana katika sura ya mtu na kivuli kwa upande wa kiti cha urais. Tunachoweza kusema kuhusiana na kipindi hicho ni kwamba dhana ya kukubali kutokubaliana ilichukua sura finyu sana kuliko uhalisi wake. Kuingia kwa mfumo wa vyama vingi kulitarajiwa kuipa dhana ya demokrasia ya ushindani rangi sahihi. Baadhi ya dalili za kutaka kufanya hivyo zilionekana pale serikali ilipofanya marekebisho mbalimbali ya kisheria ambayo hatimaye yalihalalisha vyama vya upizani. Hata hivyo, kadri muda unavyozidi kwenda ndivyo siri moja kubwa inazidi kufichuka. Kwamba serikali ya chama tawala ilianzisha mfumo huu ikiwa na fikra kwamba usingeathiri kwa namna yeyote utawala wa chama tawala. Kinyume cha matarajio hayo, kasi ya kukubalika kwa vyama vya upinzani machoni kwa wapiga kura imekuwa kubwa kuzidi kiasi. Kutotekelezeka kwa sera za chama tawala, kukithiri kwa tatizo la rushwa, kukuwa kwa tatizo la ajira, kudumaa kusikoisha kwa uchumi wa nchi na hatimaye kukosekana kwa huduma bora za kijamii ni miongoni mwa masuala yanakofanya kuanguka kwa utawala wa CCM jambo lisiloepukika. Kwa mtu yeyote anayefuatilia kwa makini kampeni za uchaguzi, bila shaka atagundua ukweli kwamba viongoz iwa CCM wako katika kipindi kigumu cha kulazimisha kucheka katika matanga. Tofauti na vyama vingi vya upinzani ambavyo husherekea kampeni zake kwa kuwa na halaiki kubwa ya watu, mikutano ya kampeni ya CCM huambulia watoto wa shule, wakereketwa wachache wa CCM pamoja na makundi ya wacheza dansi na ngoma za kienyeji. Licha ya kutumia fedha nyingi na kugawa zawadi lukuki, bado wananchi wamekuwa wagumu kuhadaika. Ukweli huu unafupishwa na maneno ya hekima ya Mgombea ubunge wa Temeke kupitia chama cha CUF pale aliposema SISI TUNA WATU WAO WANA PICHA? Kuna uwezekano mkubwa kwamba maneno ya hivi karibuni ya Mheshimiwa Omari Juma kuwa hata wananchi wasipoipigia kura CCM lazima itashinda yalitokana na athari za ukweli huo. Hatujui kama CCM na serikali yake vimejiandaa vipi kuifanikisha azma hiyo. Hata hivyo, sheria zote za nchi ikiwemo katiba hazihalalishi kwa namna yoyote ushindi pasipo kura na hatutarajii kuwa na kikao cha bunge kwa ajili ya kurekebisha sheria kabla ya uchaguzi mkuu. Bila Bwana Omari Juma na chama chake kutoa tafsiri sahihi ya maneno yake, uchaguzi mkuu utabaki katika hali ya utata mkubwa na zoezi zima la kujiandikisha na kupiga kura litabaki kama KITENDAWILI ambacho hakuna awezae kutegua ila waliyo juu. Tunafahamu fika kuwa kauli hiyo ya bwana Juma ingekuwa na meno halali, kama ingehusiana na uchaguzi ndani ya chama chake. Kama kikao cha wakubwa wachache huko Dodoma kwa shinikizo la mtu mmoja, waliweza kuzifanya kura na maamuzi ya wengi pata potea ni kitu gani kingezuia maneno ya bwana Juma kuelezeka. Labda athari za maamuzi hayo ya wachache zinazoonekana sana? Japo tulitegemea kwamba athari za uamuzi huo wa kiimla zingetosha kuwa fundisho kwa chama hicho, lakini kinyume chake viongozi wa chama hicho wameonesha kutotishwa na maamuzi yoyote ya kidemokrasia. Wanaamini katika nguvu za kidola walizonazo na kusahau kwamba nguvu za kidola katika nchi kama Tanzania zinapaswa kupata uhalali wake katika nguvu za kidemoakrasia. Huwenda ni kutokana na ukweli huo ndiyo tunaona kushamiri kwa matumizi ya lugha ya nguvu dhidi ya raia. Kila kuchapo imekuwa nadra sana kutosikia watu kadhaa wamejeruhiwa na polisi katika kampeni za uchaguzi za vyama visivyo CCM. Matamshi ya hivi karibuni toka kwa Makamanda wakubwa kabisa wa jeshi la polisi yakiwaelekeza walinzi wa amani kutumia nguvu katika zoezi zima la kampeni za uchaguzi yanaweza kupewa tafsiri toka katika ukweli huo. Japo tunaamini kwamba sheria za nchi zinalitambua jeshi la polisi kama chombo huru kisicho na itikadi ama mtizamo wa kisiasa, mazingira mazima ya hali ya kisiasa ya Tanzania yanatulazimisha kuutilia shaka ukweli huu. Hata kama kuna ukweli juu ya shaka hii, bado siyo rahisi kutupia lawama katika jeshi la polisi. Yawezekana kwamba walio juu na ambao sheria za nchi zinawaruhusu kuwa na itikadi za kisiasa wanashindwa kutofautisha kofia mbili walizonazo. Kushindwa kwao kutofautisha kofia hizi mbili kunaweza kuwafanya makamanda wetu waaminifu naWATIIFU washindwe kujua kama amri ama maelekezo ya kazi yanatoka katika kofia ipi kati ya hizi mbili. Kwa wanaofuatilia vizuri zoezi zima la maandalizi ya uchaguzi mkuu wanajua ni kipi kilichoanza. Siyo rahisi kusahau maelekezo waliyopewa toka juu kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi kwamba kipindi cha uchaguzi kinakaribia mtakutana na kashi kashi nyingi hivyo msisite kutumia uwezo wenu. Yawezekana maneno hayo yakawa na tafsiri nzuri lakini maneno kama hayo walipaswa kuwa wameyapata katika mafunzo yao ya awali ya kijeshi au mafunzo mbali mbali wanayoyapata toka kwa makamanda wao. Kwa mtaji huo ni vigumu kuamini kama kweli Tanzania imeingia katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ama imeingia katika mfumo wa ukiritimba wa chama kimoja mamboleo. Kwani hali ya kisiasa Tanzania inaonyesha serikali na chama chake kuwa mbali zaidi na demokrasia kuliko ilivyokuwa awali na kuwa karibu sana na vyombo vya mabavu. Matokeo yake uhuru wa wananchi wa kuchagua chama wanachotaka na viongozi wanaowataka umebaki kuwa ukweli usiotekelezeka. Huo ni shahidi tosha kwamba serikali na chama chake iliingiza nchi yetu kama mfumo huu bila kuwa tayari KUKUBALIANA KUTOKUBALIANA. Liwe liwalo uhalisi wa ushindani katika mfumo wa vyama vingi hauwezi kuwepo bila ya waliyopo juu kukubali kukubaliana kutokubaliana. Kinyume chake mfumo wa vyama vingi katika mapungufu kama haya siku zote utabaki kuwa chanzo cha matatizo makubwa ya kisiasa. Picha kamili juu ya hili imeanza kuonekana Zanzibar toka uchaguzi wa 1995 na mpaka sasa hali inaashiria kuwa mbaya zaidi. Maoni na ushauri wa mwandishi kwa serikali ni kwamba maji ukisha yavulia nguo huna budi kuyaoga. Kama serikali imewafanya watu waamini kwamba wamo ndani ya mfumo wa vyama vingi lazima wakubali kutokubali. Ama ni kuacha kura za watu ziamue ni yupi aliye
sahihi.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Wapinzani kumuimarisha Prof. Lipumba Ngangari kung’olewa Sokoni, Ilala Polisi nchini hawajui mipaka ya kazi yao -OAU MAKALA
HABARI
ATV yatakiwa kuzingatia maadili Wakazi wa Tabata walalamikia athari ya maji machafu Maalim Seif akanusha madai ya kumwaga damu USHAURI NASAHA
MAKALA
MIPASHO NASAHA
KALAMU YA MWANDISHI
MAKALA
MWENYE MACHO…
MAKALA
LISHE
|
|
|
|
|