NASAHA
Na. 067 Jumatano Septemba 27 - Oktoba 2, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
HABARI

‘Walioshindwa kutawala wasikimbilie matusi’

Na Mwandishi Wetu

WANANCHI wamelaumu tabia ya viongozi wa Chama tawala na serikali yake kukimbilia kutukana badala ya kujibu hoja za wapinzani.

Wakiongea na NASAHA mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, wananchi hao walionesha kusikitishwa na kauli ya Waziri Mkuu, Frederick Sumaye iliyonukuliwa na gazeti moja litolewalo kila siku akisema:

Wanaotaka kumwaga damu wakawachanje wake zao. Kauli hiyo ambayo ilidaiwa kujibu ile ya Maalim Seif Sharif Hamad kuhusu wezi wa kura, iliripotiwa kutolewa na Bw. Sumaye wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika uwanja wa Urafiki Jimbo la Ubungo jijini Alhamisi iliyopita.

Katika hotuba yake aliyoitoa huko Unguja kwenye kiwanja cha Kibandamaiti, Mhe. Seif Sharif Hamad, mgombea Urais (CUF) Zanzibar, alirudia msimamo wa chama chake kuwaonya wezi wa kura kwamba endapo hawataacha, basi wananchi hawatokubali tena kudhulumiwa ushindi wao, na hivyo vurugu zinaweza kutokea nchini na damu kumwagika.

Wananchi hao walisema, kauli ya Maalim Seif ni onyo sahihi. "Nani asiyeshuhudia wezi wakipigwa mitaani na kutolewa damu kutokana na vipigo hivyo?" alihoji mmoja wa wananchi hao na kuongeza, "na wezi wa kura wasipoacha wizi wao safari hii damu itawatoka kwa kipigo".

Wakionesha kusikitishwa na kauli ya Sumaye, wananchi hao walisema kuwa alichotakiwa kujibu Sumaye ni kwamba serikali yake itahakikisha kuwa kura hazitoibiwa badala ya kusema "damu itakayomwagika ni ya wake zao".

Akitoa maoni yake, mwananchi mwingine aliyeonesha kushangazwa na "kigugumizi" cha serikali inapohusu hofu ya upinzani kuibiwa kura zao.

Mwananchi huyo alisema kwamba kwa maoni yake, serikali au kiongozi wake kutoa kauli ya kuwahakikishia wananchi kwamba kura zao hazitoibiwa ni moja ya sifa za utawala bora na kinyume chake ni udhaifu.

"Hivyo kama viongozi hao wameshindwa kutoa majibu, ni vyema wakakaa kimya badala ya kutukana", alisema mwananchi huyo ambaye kama waliomtangulia, wote hawakupenda kutaja majina yao.



ATV yatakiwa kuzingatia maadili

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemtaka mmiliki wa kampuni ya mafuta na sabuni aina ya komoa ambayo pia inamiliki kituo cha televisheni cha ATV mjini hapa, aache kutumia televisheni hiyo kutangaza chuki binafsi badala yake azingatie miiko ya habari.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Kampeni wa chama hicho wilaya ya Morogoro Bw. Abeid Mlapakolo alipokuwa akiwanadi wagombea wa ubune na udiwani kupitia chama hicho katika viwanja vya nguzo kata ya Mazimbu - mjini hapa mwishoni mwa wiki hii.

Aliyasema hayo baada ya kituo hicho cha Luninga kuutangaza mkutano wa CUF uliokuwa ukihutubiwa na Profesa Ibrahimu Lipumba mjini hapa, mapema wiki hii kuwa ulitawaliwa na vurugu, habari hizo zilizokuwa na kichwa cha habari: vurugu kubwa za kutisha zatokea katika mkutano wa CUF zilizotangazwa na Karim Besta ambazo hazikuonyesha kipande chochote katika sehemu ya mkutano huo ambao ulifurika watu, kuonyesha fujo zilizotanda, amesema mwanakampeni huyo kuwa huo ni uchochezi.

"Mbona hakutoa picha ya fujo hizo, na kituo kipo kilomita chache kutoka katika uwanja wa mkutano, badala yake kwa ushabiki ameonesha mkutano wa CCM uliofanyika katika Kilabu cha Pombe za Kienyeji Manzese", akasema.

Aidha akamtaka mmiliki wa kituo hicho cha televisheni ambaye aliangushwa katika kura za maoni katika kinyang’anyiro cha ubunge kwa tiketi ya CCM jimbo la Morogoro mjini kama ameshindwa kutoa huduma ya habari aachane nayo badala yake ashughulike na bidhaa zake za mafuta na sabuni.

Kadhalika aliwaomba wananchi wa kata ya Mazimbu wamkopeshe kura zao za udiwani Bw. Bakari Mbaga na kura za ubunge wazipeleke kwa Bw. Athumani Maringo ambao utendaji wao utaboreka zaidi ukiwa chini ya Profesa Ibrahimu Lipumba kupitia chama cha CUF-CHADEMA. 



Wakazi wa Tabata walalamikia athari ya maji machafu
  • Maji machafu yamwagwa ovyo katika makazi ya watu
  • Wengi waugua matumbo na kutapika
Na Mwandishi Wetu

Wananchi wa maeneo ya Tabata na jirani yake wamelalamikia umwagaji ovyo wa maji taka unaofanywa na magari ya Mamlaka ya Maji-Safi na Maji-Taka (DAWASA) katika maeneo waishio watu na hivyo kuleta athari kubwa ya kiafya kwa wananchi.

Maeneo yaliyoathirika sana ni kuanzia Tabata Relini, Tabata Shuleni, Mtambani, High Bar, Vingunguti hadi Kota za TAZARA. Kwa mujibu wa maoni yaliyotolewa na wanachi mbalimbali waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi ni kwamba tayari watu kadhaa na hasa watoto wadogo wanaugua vifua, vichwa, kuharisha pamoja na kutapika hali ambayo inaashiria kwamba hewa hiyo huenda ina sumu.

Haya maji machafu ya vyooni yanayomwagwa na magari ya DAWASA yanatoa harufu mbaya sana katika "maeneo mbalimbali ya Tabata na hivyo kuhatarisha afya zetu," alisema Mwalimu Salehe (31) wa Shule ya Msingi Tabata. Maelezo kama hayo pia yaliungwa mkono na Mama Abdallah (35) ambaye ni mfanyabiashara wa samaki anayefanya shughuli zake katika eneo la TAZARA Kota.

Kwa mujibu wa maelezo mengine yaliyotolewa na Mama Lyimo (31) ambaye anafanya biashara eneo la Shule ya Msingi Tabata na Mzee Hamza (67) wa Mtambani ni kwamba athari za umwagaji huo wa maji machafu kiholela tayari zimeonekana katika familia kadhaa ambazo zinauguza watu wao na hasa watoto ambao sasa wanaugua matumbo, vifua pamoja na kutapika ovyo. Vilevile mwandishi wa habari hizi alibahatika kuongea na Bi Sharifa (25) ambaye ameathirika kwa kuugua kichwa ambacho anadai kimesababishwa na hewa chafu inayotokana na maji hayo.

Mwandishi wetu pia alijionea mwenyewe jinsi maji machafu ya choo yanavyomwagwa ovyo kati ya Vingunguti, Buguruni na sehemu ya Tabata inayojulikana kama SPENCO. "Ninashangazwa na tabia ya watu hawa kumwaga maji machafu katikati ya makazi ya wananchi," alisema Bwana Tony Shirima (25) wa eneo la Tabata Mtambani. Sambamba na kulalamikiwa kwa umwagaji holela wa maji machafu ya vyoo, vilevile wananchi kadhaa wa maeneo ya Vingunguti wamelalamikia umwagaji wa maji machafu ya viwandani katika maeneo ya kuishi watu na hivyo kuhatarisha afya zao. Kwa nyakati tofauti Mzee Mbegu (55) mkazi wa Tabata shuleni (SunBurst), Mzee Hamza wa Mtambani, mama Maria (30) wa eneo la Tabata Relini na Mwalimu Abdallah Ngatenda anayeishi eneo la Shule ya Msingi Tabata, wametoa malalamiko yanayofanana juu ya hali hiyo na kushauri kwamba ni bora maji machafu yamwagwe maeneo yasiyo makazi ya wananchi kama pwani ya Kunduchi, Ndege Beach, Boko na kadhalika. Vinginevyo, wanasema wananchi hao, kuna hatari ya kuzuka magonjwa ya mlipuko au hata magonjwa ya hatari zaidi kama kansa kutokana na maji machafu yenye kemikali yanayomwagwa toka viwandani na kuingia kwenye vijito vinavyotumiwa na wanachi kumwagilia bustani za mboga na matunda.

Hadi tunakwenda mitamboni mwandishi wa habari hizi hakufanikiwa kumuona mhusika yeyote wa DAWASA ili kutoa maoni yake kuhusiana na hali hii kwa maelezo kwamba alikuwa ametingwa na kazi.
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Polisi ‘isiibebe’ CCM

Wapinzani kumuimarisha Prof. Lipumba

Ngangari kung’olewa Sokoni, Ilala

Polisi nchini hawajui mipaka ya kazi yao -OAU

MAKALA
BBC, CCM ndugu au tajiri na kibaraka?

HABARI
‘Walioshindwa kutawala wasikimbilie matusi’

ATV yatakiwa kuzingatia maadili

Wakazi wa Tabata walalamikia athari ya maji machafu

Maalim Seif akanusha madai ya kumwaga damu

USHAURI NASAHA
‘Mama, hela hii inanunua nini?'

MAKALA
Demokrasia ni kukubaliana kutokukubaliana

MIPASHO NASAHA
HEBU VUENI MIWANI ZENU!

KALAMU YA MWANDISHI
Juha haliambiliki!Juha haliambiliki!

MAKALA
Amani ya Tanzania itadumishwa na haki

MWENYE MACHO…
Hoja za uongo katika kampeni

MAKALA
Chonde Dk. Omari na Karume wahurumieni Wazanibari wenzenu

Habari za Kimataifa

LISHE
Kimfaacho  mtoto

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga kuwakosa Mahadhi, Mbuna
  • Idd Azzan lawamani
  • Kibadeni, Kayuni wanafaa Stars - Machuppa
  • Said Maulidi: Sihami Simba

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita