NASAHA
Na. 067 Jumatano Septemba 27 - Oktoba 2, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
TAHARIRI

S.L.P. 72045, Dar es Salaam

Polisi ‘isiibebe’ CCM

Fujo ni fujo iwe imefanywa na wafuasi wa vyama vya upinzani au wale wa chama tawala. Madhara yake ni kuvunjika kwa amani katika jamii. Lakini, wakati mwingine fujo zinazofanywa na wafuasi wa chama tawala huenda zikawa kubwa na zenye madhara zaidi kwa vile wafanya fujo hao huwa na kiburi fulani wanajivuna "wao ndio wao", jeshi la polisi ni lao na hivyo hakuna atakayethubutu kuwagusa.

Alhamisi iliyopita Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Omar Mahita, alipokuwa akizungumza na makamanda wa jeshi hilo mkoani Dar es Salaam alitangaza kwamba jeshi la polisi litahakikisha kila mtu anapiga kura bila hofu na ulinzi madhubuti utakuwepo. Akifafanua kuwepo kwa ulinzi madhubuti alisema: "....hakutakuwepo na ngangari, NATO wala Kasovo".

Akaendelea kuwambia makamanda wa jeshi hilo kwamba kama watu wengine wanajifanya "ngangari, Polisi watakuwa "ngunguri".

Ingawa Mkuu huyu wa Jeshi la Polisi nchini hakutaja ni kundi gani la Watanzania au ni wafuasi wa chama kipi cha siasa katika vile vinavyoshiriki uchaguzi mkuu ndio wenye kuhofiwa kutaka kuleta fujo, maneno aliyoyatumia Bw. Mahita ya "ngangari", "NATO" na "KOSOVO" yanashiria kwamba wanaokusudiwa hapo ni wafuasi wa Chama Cha Wananchi (CUF).

Sisi hatuoni mantiki ya Bw. Mahita kuelekeza makemeo na vitisho vyake kwa Wana-CUF pekee. Tunachofahamu CUF wamekuwa wakitangaza kwamba iwapo wataibiwa kura zao, watapambana na dhalimu wao. Kwa kauli hii sisi hatuoni cha ajabu kwa sababu iweje mtu alalamike kwa kutahadharishwa asimwibie mwenzake? Kwani kuiba ni haki yake?

Lakini pia hatuoni mantiki ya IGP kutowataja wafuasi wa CCM ambao wamekuwa na rekodi ya matukio yenye kuashiria kutaka kuvunjika kwa amani.

Wakati wa upigaji wa kura za maoni kuwapata wana-CCM watakaogombea udiwani na ubunge taarifa za vurugu na vitendo vya rushwa zilisikika karibu nchi nzima. CCM walikuwa ‘wakifanyiziana’ wao kwa wao. Tunauliza:Mtu anayeweza kupanga hila kumdhulumu nduguye atashindwa vipi kupanga dhuluma dhidi ya mtu baki? CCM itashindwa vipi kupanga dhuluma dhidi ya CUF, NCCR, TLP, UDP na wengineo? Je Afande Mahita analionaje hili?

Vimbwanga vya CCM havikuishia kwenye kura za maoni tu:Maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM kutengua matokeo ya kura za maoni katika baadhi ya majimbo yamepelekea kuibuka kwa kambi za upinzani.

Zipo taarifa kwamba wapo Wana-CCM ambao wameamua kuwapigia debe wagombea wa upinzani na wakati huo huo CCM imewataka wanachama wale wanaofanya hivyo na wale wasiokubaliana na maamuzi ya Kamati Kuu wajiengua. Je mgogoro huu unaofukuta ndani ya CCM hauwezi kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani nchini wakati wa upigaji kura? Afande Mahita hili halimshughulishi?

Tuonavyo sisi ni muhimu sana Afande Mahita akabadili mtazamo wake haraka. Karipio lake liwalenge wote bila kujali huyu ni ‘kidumu’ na huyu ni ‘ngangari’; au huyu ni "Nambari Wani’ na yule ni ‘wa kujaza mapesa’. Fujo ni fujo, lakini fujo mbaya zaidi ni ile inayoanzishwa na wafuasi wa chama tawala.

Juu ya hilo tunapenda kutanabaisha kwamba tangazo hilo la IGP lisije likawa ndiyo ‘waranti’ ya kuwabugudhi wananchi kwa kisingizio cha "kudhibiti uwezekano wa kutokea fujo". Bali wananchi waachwe huru kuhudhuria mikutano ya kampeni na kujadili hatma ya nchi yao mahali popote wanapojaaliwa kukutana na kupata wasaa wa kufanya hivyo, bila kujali watu hao wanakiponda chama gani na wanakisifu chama gani cha siasa.

Pia tumewatanabaisha wananchi kwamba kauli ya Afande Mahita, ingawa ina walakini isipuuzwe. Ni muhimu wananchi msikubali kuchokozeka: msije mkavunja bilauri ya kioo ya shilingi 300, mkatakiwa kulipa gudulia la kioo la Shs. 300,000.


Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Polisi ‘isiibebe’ CCM

Wapinzani kumuimarisha Prof. Lipumba

Ngangari kung’olewa Sokoni, Ilala

Polisi nchini hawajui mipaka ya kazi yao -OAU

MAKALA
BBC, CCM ndugu au tajiri na kibaraka?

HABARI
‘Walioshindwa kutawala wasikimbilie matusi’

ATV yatakiwa kuzingatia maadili

Wakazi wa Tabata walalamikia athari ya maji machafu

Maalim Seif akanusha madai ya kumwaga damu

USHAURI NASAHA
‘Mama, hela hii inanunua nini?'

MAKALA
Demokrasia ni kukubaliana kutokukubaliana

MIPASHO NASAHA
HEBU VUENI MIWANI ZENU!

KALAMU YA MWANDISHI
Juha haliambiliki!Juha haliambiliki!

MAKALA
Amani ya Tanzania itadumishwa na haki

MWENYE MACHO…
Hoja za uongo katika kampeni

MAKALA
Chonde Dk. Omari na Karume wahurumieni Wazanibari wenzenu

Habari za Kimataifa

LISHE
Kimfaacho  mtoto

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga kuwakosa Mahadhi, Mbuna
  • Idd Azzan lawamani
  • Kibadeni, Kayuni wanafaa Stars - Machuppa
  • Said Maulidi: Sihami Simba

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita