NASAHA
Na. 067 Jumatano Septemba 27 - Oktoba 2, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
USHAURI NASAHA

‘Mama, hela hii inanunua nini?'

Na Khadija M. Idd

"Mama hela hii inanunua nini?" aliniuliza binti yangu mwenye umri wa miaka minne. Niligeuka na kuangalia, halafu baada ya kuona sarafu aliyoishika mkononi nilimjibu", hainunui kitu chochote". "Nataka nikanunue karanga", alisistiza. Mjadala huu ulikatizwa na kaka yake aliyemwambia kwa msisitizo, "hela hiyo ndogo hainunui karanga." Nilimshukuru kwa kunisaidia kumaliza hilo kasheshe lakini akili yangu ilisafiri kurudi miaka ya nyuma, zamani kidogo enzi hizo nikiwa shule ya msingi.

Niliangalia ile sarafu ya shilingi moja na kukumbuka jinsi nilivyokuwa mwingi wa furaha nikienda shuleni asubuhi nikiwa nimepewa Shs.1. Nakumbuka jinsi ambavyo niliweza kununua vitu vingi vya kula na rafiki zangu na bado nilibakisha senti 50/- kwa ajili ya matumizi ya shule kesho yake. Sasa hivi taswira ninayoiona kwenye Shs.1. hii inafanana na ile taswira niliyoiona enzi zile katika sarafu ya senti 1., ile yenye tundu katikati - pesa isiyo na thamani!

Hata hivyo mawazo yangu yanakatizwa mara kwa mara na kelele za hawa watoto wanaonyang’anyana pesa hii na huku wakizomeana "ooh! Hela yenyewe hainunui kitu hiyo!" Naamua kurudi kutoka zamani mpaka sasa na kujiuliza hali itakuwaje wakati watoto hawa nao watakapofikia umri kama wangu. Je, na wao watashuhudia haya maswali ya "mama hela hii inanunua nini?" Watakapokumbuka jinsi walivyokuwa wanazomeana juu ya Sh.1 ambayo hainunui kitu watajisikiaje? Je ni pesa yenye thamani gani sasa hivi ambayo wakati huo itakuwa kama hii Shs.1 ya wanangu na ile senti moja yangu? Ni shilingi ngapi za sasa zitakuwa na taswira hii ya magazigazi (mirage)? Ya kuitegemea kununulia kitu lakini mara tu unagundua kuwa haiwezi kukidhi haja yako.

Wakati haya yanaendelea nakumbuka kuwa mimi mwanauchumi, labda katika anga la nyumbani kwangu. Lakini najipa moyo kuwa naelewa kidogo kuwa thamani ya pesa ina uhusiano na hali ya uchumi wa nchi. Kwa namna gani? Nawachia wachumi wenyewe. Hata hivyo hili linakumbusha suala la umaskini wa nchi yangu na hususan katika ule mkutano wa kuondoa umaskini katika nchi za dunia ya tatu, Tanzania ikiwa mojawapo iliyochaguliwa kutokana na kuonyesha mikakati ya kufuta umaskini.

Hata hivyo, mambo ya kwenye mkutano huu naona kama vile hayanipi matumaini ya kuondoa umaskini na hatimaye kupanda kwa thamani ya pesa. Naona kuna ukungu mwingi hasa kutokana na uzoefu wa huko nyuma, kuwa mikataba ikishasainiwa, pesa za misaada mbalimbali zinafujwa na watu wachache. Na kwa vile wahusika hawakukanusha, nafikiri ni za kweli. Hata hivyo wakipenda wanaweza kujitetea kuwa misaada ni ya watu maskini, na wao ni maskini pia. Kwani kuna ubaya gani wakianza kuondoa umaskini wao ili waweze kuwasaidia maskini wenzao baadaye? Kwa kweli mikakati ya nchi kuondoa umaskini haiwasaidii maskini wengi, bali wachache tu walioko mjini.

Pamoja na haya yote ninayowaza, bado mwanangu anataka kwenda kununua karanga na ile Shs.1. Kwa nini asiweze kupata karanga dukani na ile ni hela? Labda niende kusikiliza kampeni na mwanangu huyu tunaweza kupata la kusaidia ili mwanangu huyu apate matumaini kidogo. Lakini, hawa wagombea kuna wale walio na madeni ya miaka mitano iliyopita. Ahadi zile hazijatimizwa watamsaidiaje mwanangu? Na hao wengine je wanaelewa tatizo la mwanangu?!

Ushauri NASAHA unaelewa fika juu ya kampeni na uchaguzi, na ningependa wagombea waelewe hili tatizo kwamba si suala la mtoto mtukutu, asiyeambilika la! Hili ni suala letu na kizazi kipya. Je watoto wetu warithi umaskini na thamani ndogo ya shilingi? Wapiga kura wanahitaji mgombea atakayeleta mabadiliko, atakayeondoa kero hii ya kuwa na pesa isiyo na thamani, pesa isiyoweza kununua kitu. Ambaye atawafanya watoto na kizazi kipya wasizomeane kwa kuwa mmoja wao ana pesa isiyoweza kununua karanga. Mgombea ambaye anajua namna ya kuwasaidia ipasavyo hawa "maskini" wanaosaini mikataba ya kuondoa umaskini wa nchi, lakini wakaamua, Ah hapana, ....wakasahau na kuishia kuondoa umaskini wao tu. Labda thamani ya pesa itabadilika angalau kidogo na labda baada ya miaka mitano wanangu hawa watauliza "mama hela hii inanunua vitu vingapi? Na si inanunua nini?

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Polisi ‘isiibebe’ CCM

Wapinzani kumuimarisha Prof. Lipumba

Ngangari kung’olewa Sokoni, Ilala

Polisi nchini hawajui mipaka ya kazi yao -OAU

MAKALA
BBC, CCM ndugu au tajiri na kibaraka?

HABARI
‘Walioshindwa kutawala wasikimbilie matusi’

ATV yatakiwa kuzingatia maadili

Wakazi wa Tabata walalamikia athari ya maji machafu

Maalim Seif akanusha madai ya kumwaga damu

USHAURI NASAHA
‘Mama, hela hii inanunua nini?'

MAKALA
Demokrasia ni kukubaliana kutokukubaliana

MIPASHO NASAHA
HEBU VUENI MIWANI ZENU!

KALAMU YA MWANDISHI
Juha haliambiliki!Juha haliambiliki!

MAKALA
Amani ya Tanzania itadumishwa na haki

MWENYE MACHO…
Hoja za uongo katika kampeni

MAKALA
Chonde Dk. Omari na Karume wahurumieni Wazanibari wenzenu

Habari za Kimataifa

LISHE
Kimfaacho  mtoto

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga kuwakosa Mahadhi, Mbuna
  • Idd Azzan lawamani
  • Kibadeni, Kayuni wanafaa Stars - Machuppa
  • Said Maulidi: Sihami Simba

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita