NASAHA
Na. 067 Jumatano Septemba 27 - Oktoba 2, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MWENYE MACHO

Hoja za uongo katika kampeni

Na Toroka Kanyika

LEO katika safu hii tutaona jinsi wananchi wenye usongo na maendeleo ya nchi yao walivyofanikiwa kuwaweka watawala roho juu.

Kilipoanza kipindi cha kampeni za uchaguzi Agosti 18, kauli iliyokuwa inasikika kutoka kwa viongozi wa chama tawala ilikuwa ni kusisitiza kwamba wao watanadi sera zao na kuwa wananchi watawachagua kwani vyama vya upinzani havina sera.

Kwa majigambo haya ilitegemewa kwamba hotuba zote za viongozi wa CCM zitakuwa zimejaa sera za chama hicho kwa lengo la kuwafanya wananchi kupima sera hizo na kuzilinganisha na zile za wapinzani ambazo tangu hapo CCM ilishadai kuwa wapinzani hawana sera mbadala ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Tunachokishuhudia sasa ni ama uongo au matusi kwa wapinzani. Uongo na matusi au kejeli zinazotolewa zinakilenga zaidi chama cha wananchi, CUF.

Viongozi wake wamekuwa wakiandamwa sana. Tumesikia ikidaiwa kuwa CUF inakusudia kumwaga damu endapo itashindwa katika uchaguzi MKUU UJAO. Lengo la uongo huu ni kuwatisha wananchi ili wasikichague chama hiki. Ama kwa upande mwingine kinachokusudiwa na kwa dhana kuwa upo wizi wa kura. Awali chama cha CUF kilitangaza na kimeendelea kushikilia msimamo wake kuwa endapo kitapokonywa ushindi kwa hila yoyote ile ikiwapo ya wizi wa kura wanachama wake hawatokubali;. Ikaelezwa bayana kuwa wakati itakapobainika kuwa CUF imepokonywa ushindi basi sera ya 'Jino kwa Jino' itatumika.

Chama kinachotuhumiwa kuhusika na wizi wa kura hakijajitolea kujibu tuhuma hizi kwa hoja za kueleweka bali zimebuniwa mbinu za kuonesha kuwa lengo la CUF ni kumwaga damu.

Jambo la kushukuru ni kuwa kila uchao wananchi kwa mamia wanakuwa ngangari. Wameshapania uchaguzi huu, wamejiandikisha kwa wingi na wanasubiri kupiga kura zao na kisha kuzilinda.

Umejengwa pia uongo mwingine kuwa CUF ni chama cha Waarabu chenye nia ya kurudisha usultani na utumwa. Uongo huu nao kwa mwenye macho hausaidii kumwepusha na CUF bali huwa kama barometa ya kujua ni kwa kiasi gani watawala wameingia hofu na woga juu ya kuzipoteza nafasi zao. Pili wengi wa watu waliopo leo masuala ya utumwa na usultani kwao ni mambo ya historia tu. Haingii akilini kuwa Prof. Lipumba anaweza kuacha kazi zake katika anga za kimataifa arudi nyumbani kuikabidhi nchi kwa wakoloni.

Kuhusu wagombea imekuwa ilidaiwa kuwa Prof. Lipumba hafai kuongoza nchi kwani hana mke. Japo haijawahi kuelezwa kuwa sifa ya mtu mgombea urais ni kuoa, lakini uzushi huu umekuwa ukienezwa na watu wenye hadhi upande wa chama tawala. Wananchi licha ya kufahamu kuwa mke siyo sifa ya kutawala, wanafahamu pia kuwa Prof. Lipumba anaye mke.

Ukweli huu umesaidia wenye macho kuthibitisha kuwa wale waliodai kuwa na sera hawanazo badala yake wana kejeli na uongo.

Hatua ya hivi karibuni ni ya chama tawala kuagiza polisi kuwa macho na CUF. Hatua hii kwa wengine imejenga hisia kuwa yanafanywa maandalizi ya kuwatisha wananchi. Hata hivyo CUF haikukawia kujibu. Imeripotiwa kuwa CUF wanadai kuwa sasa wao ni ngangari kinoma.Ifahamike kuwa uogo hautadumisha amani na utulivu unaodaiwa kuwepo....Tukutane wiki ijao.
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Polisi ‘isiibebe’ CCM

Wapinzani kumuimarisha Prof. Lipumba

Ngangari kung’olewa Sokoni, Ilala

Polisi nchini hawajui mipaka ya kazi yao -OAU

MAKALA
BBC, CCM ndugu au tajiri na kibaraka?

HABARI
‘Walioshindwa kutawala wasikimbilie matusi’

ATV yatakiwa kuzingatia maadili

Wakazi wa Tabata walalamikia athari ya maji machafu

Maalim Seif akanusha madai ya kumwaga damu

USHAURI NASAHA
‘Mama, hela hii inanunua nini?'

MAKALA
Demokrasia ni kukubaliana kutokukubaliana

MIPASHO NASAHA
HEBU VUENI MIWANI ZENU!

KALAMU YA MWANDISHI
Juha haliambiliki!Juha haliambiliki!

MAKALA
Amani ya Tanzania itadumishwa na haki

MWENYE MACHO…
Hoja za uongo katika kampeni

MAKALA
Chonde Dk. Omari na Karume wahurumieni Wazanibari wenzenu

Habari za Kimataifa

LISHE
Kimfaacho  mtoto

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga kuwakosa Mahadhi, Mbuna
  • Idd Azzan lawamani
  • Kibadeni, Kayuni wanafaa Stars - Machuppa
  • Said Maulidi: Sihami Simba

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita