NASAHA
Na. 067 Jumatano Septemba 27 - Oktoba 2, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MIPASHO NASAHA 

HEBU VUENI MIWANI ZENU! 

Na Abu Halima Sa Changwa

WIKI mbili zilizopita nilikuwa na kazi na wasomaji wa Mpasho Nasaha niliokuwa nikikutana nao mtaani. Wengine waliniambia moja kwa moja kwamba wamechoka na Utatu Mtatanifu. Wangine waliniuliza kama nimeshanunuliwa. Sasa, msikonde, msikonde. I am back, I mean...yaani, nimerudi. Utatu ulikuwa utatu kweli, maana ulitoka kwenye matoleo matatu mfululizo.

Mambo mengi yamepita, leo nitazungumzia mambo kadhaa, na yote yanahusiana. Katika kampeni hizi kuna dini moja imepewa umuhimu wa pekee. Nayo ni dini ya Kiislamu. Nikiwa kama muumini wa dini hiyo, nashangaa imekuwa ni issue kubwa katika kampeni. Uislamu unatakiwa kwa namna fulani, na hautakiwi kwa namna nyingine. Kinachoudhi zaidi ni pale Uislamu unapotumika kama kigezo cha kampeni kuwafarakanisha watu. Kwa upande mmoja kuna watu wanaolaaniwa kuwa wanatumia Uislamu kwa maslahi ya Kisiasa. Lakini utakuta huyo huyo anayelaani kutumika kwa Uislamu ndiye huyo huyo tena anayeutumia kuwa stepping stone (kivuko). 

Kwanza kabisa ninashangazwa na Mashehe ambao wamejiingiza katika ushabiki wa vyama kiasi cha kusahau hadhi zao. Kama nilivyoelezea ule utatu mtatanifu, kuna wengine wameibuka, sijui wamepewa nini, kuwashambulia Waislamu. Kuna huyo mmoja, alwatan wa Mwembechai, maarufu. Baada ya baba, mwana na roho, yeye ameibuka kuwa Nabii (kama Paulo). Baada ya vurugu zote, kumuudhi baba, mwana na roho, sasa amejiunga nao, na yeye amekuwa akihubiri kinyume na yaliyomsweka jela. Kipindi cha kampeni kina mambo! 

Juzi juzi nilipita katika kampeni za chama kimoja sehemu moja inaitwa Sandali, kule Temeke, nikamkuta kada mmoja wa Chama ambaye ni mwanajeshi, mwenye cheo cha kaputeni, akisema kwamba katika Qur'an yoote, kuanzia Iqra mpaka 'amma hakuna sehemu inayozungumzia siasa kuchanganywa na dini. Eti anavyoelewa yeye watu wote wanatakiwa kuitii serikali. Huyu naye sijui ushehe wake kausomea wapi! Shehe wangu Mzee Mnenge aliwahi kusema kuna Waislamu wengi ambao ukiwauliza kila jambo atakwambia hajui. Lakini Uislamu, anaujua wote. Ndio hawa akina kapteni waliosoma mpaka Aana Auna wakahitimu. Lakini kwa nini hasa ujidai wewe ni shehe kwenye kampeni, huku ukuwakataza wenzako kwenda kwenye siasa wakiwa ni Waislamu? Maana watu wanadhani Uislamu ni kama koti, unaweza ukauvua ukautundika sehemu, ili usiende nao kwenye siasa. 

Kuna mwingine kule mkoani Kagera, nilisikia habari zake kutoka kwenye redio moja iliyoanzishwa hivi karibuni. Nakumbuka jina lake linaanzia na neno "Kichwa", kama sikosei ni "Kichwabutu". Yeye naye mada yake ilikuwa ni Waislamu hao hao. Alielezea mengi kuhusu alichokiita "madai" ya Waislamu. Alipewa kazi ya kurudisha imani ya Waislamu, kwa kuvunja hoja za waislamu kuwa nyuma, kwamba ni uzembe wao wenyewe tu, akasema pia kwamba East African Muslimu Welfare Society iliyovunjwa na Mwalimu Nyerere haikuwahusu Waislamu wote, bali wale wa Ismailia tu. Yaani ni mkanganyiko wa mambo. Mimi ninachouliza, hivi mbona Uislamu umeshupaliwa hivi katika kipindi hiki? Kuna nini hasa? Ukuienda huku, "Uislamu na waislamu", ukigeuka huku "Uislamu na Waislamu". Jamani. What's up? 

Kuna mjamaa mmoja naye, anaitwa Paskali, maarufu, aliuliza swali kwenye televisheni, (nasikia kwa Kiswahili yaitwa "runinga", sijui radio yaitwaje!) Akimuuliza Profesa Lipumba, kuhusu wasi wasi wake wa tuhuma kwamba CUF ni chama chenye muelekeo wa Kiislamu. Sababu za kudhania hivyo zilikuwa kama ifuatavyo. Kwanza, Wanaohudhuria mikutano ya CUF ni wafuga ndevu, wavaa vibalakashia, kanzu na mabuibui. Pili habari za Lipumba huandikwa mno kwenye magazeti ya mafundamentalist, n.k. 

Labda ni kweli kwamba hizo ni alama za dini fulani. Lakini mimi nimekuwa na imani kwamba mtu ambaye anauliza maswali akizingatia kwamba sehemu kubwa ya jamii inamuona na kumsikiliza inabidi awe makini sana, ili asije akatoa swali la kuchekesha. Pili, huwa naamini kwamba wanahabari ni wataalamu wasomi, waliobobea kwenye lojiki (logic), maarifa ya kupanga hoja. 

Pengine Bwana Paskali aliuliza maswali yale kumsaidia tu Lipumba, ili kuondoa dhana ile iliyojazwa kwenye mbongo za watu, kwamba CUF ni Uislamu. Lakini pengine pia alikuwa siriaz kwamba hiyo ndiyo dhana yake kwa vigezo alivyovitoa. Ikiwa hili la pili ndilo, basi nashangaa mno kwamba wako wana habari wa hii. 

Lipumba anabebwa na magazeti ya mafundamentalist. Sasa kama magazeti ya mapacifisti hayambebi, sasa abaki anagaragara chini tu? Wote tunasafiri. Madaladala mengine,yaliyoandikwa WAKORINTO, KWA YESU KILA GOTI LITAPIGWA n.k., yanawabeba wengine mimi yananipita, yamejaa, nimepata la kudandia niliache eti kwa sababu limeandikwa OSAMA BIN LADEN? Na hayo magazeti ya mafundamentalist yalisajiliwa yafanye kazi gani kama si uandishi? Na kila chombo cha habari kina sera zake ndogo ndogo. Hatusemi ni udini kwa Redio Tumaini kuacha kupiga Kaswida. 

Majibu yalitolewa siku ile ni ya kuridhisha, lakini naomba, kama Sa Changwa, niongeze chumvi kidogo kwenye chungu hiki kinachotokota. Watu huwa wanavaa miwani za sampuli mbali mbali. Kuna zile za rangi. Ukivaa miwani ya vioo vyekundu, basi kila kitu kinakuwa chekundu. Ukivaa sun goggles nyeusi basi unaona kama mvua itanyesha sasa hivi. Ukivaa ya vioo vya bluu, basi dunia nzima inakuwa bluu. Lakini ni kweli mambo yako kama unavyoona baada ya kuvaa miwani? Ni wazi kwamba mwenye rangi hizo ni wewe tu., maana kiukweli hazipo. 

Vile vile kuna wale akina sisi, tunaovaa miwani za macho. Kuna zile zinazokuza vitu, vidogo vikawa vikubwa. Sasa mtu anaweza kuvaa miwani hii ikawa kasheshe, maana anaweza kuona paka halafu akatoka mkuku. Ukimuuliza nini, anakwambaia "Nimeona simba". Khe! Sasa ni simba kweli au miwani yako tu? Basi watu wenye miwani za hivi kwa kukuza mambo!!! Kichuguu cha siafu kinakuwa bonge la mlima! 

Halafu kuna wale ambao miwani zao zina vioo vya kupunguza ukubwa wa kitu. Huyu aweza kukutana na simba akadhani ni nyau tu. Kumbe miwani yake. 

Ndiyo maana nawauliza akina Paskali. Hivi kuna Uislamu au ni miwani zenu. Maana miwani yako inakutuma kwamba mtu akivaa kanzu tu, Mwislamu, hata kama ni Papa John Paulo. Akifuga ndevu tu, mjahidina, hata kama ni Castro wa Cuba, au Samora Machel wa Msumbiji. Akivaa kibalakashia tu basi ni Mwislamu, hata kama ni Agostino Mrema? Mwisho Wamasai waliogundua kuvaa vikoi (misuli) nao pia wataambiwa wadini. Maana kuna mtaka madaraka mmoja kawabatiza watu kwa kuwaita wavaa vikoi. 

Tukijumlisha yote, tunakuta kwamba watu wanaonyesha chuki ya wazi kwa dini fulani, tena bila ya aibu. Hivi wanaovaa kanzu na balakashia hawafai kushiriki kwenye mikutano ya siasa, bali wavaa tai, wavaa sketi na wavaa vimini tu? Au siku hizi kuna nguo za mikutano ya siasa, kwamba Sa Changwa nikienda huko nivae tai kubwa kama ya rafiki yangu Muinjilisti Samson Mwaipyana? Hapo ndio sitaonyesha udini? Hawa akina Paskali wameona vibalakashia tu, na wengine wakianza kuangalia misalaba, na sketi zinazohudhuria kwa wingi kwenye mikutano mingine ya siasa wasemaje? Au tumuombe msajili wa vyama atuambie nguo za kuvaa tukienda kwenye mikutano. 

Tunafahamu kuwa kampeni ni vita, na vita haina macho, wala aibu, ndio maana hata Mzee MAHEATER akaona kwamba wenye fujo ni ngangari tu, lakini SISI, Mh! Ndio akasema kama wao ni ngangari, SISI (CC...) ni ngunguri, kwa hiyo MAHEATER katangaza kuwachemsha wafuasi wa CUF (kama maheater yanavyochemsha maji) kwa sababu miwani aliyopewa kuvaa inamuonyesha kwamba CUF tu ndio kuna fujo. Simlaumu kwa vile naye yuko kazini, na inabidi avae miwani anayopewa na wakuu wake. Nawalaumu wale wanaoona Uislamu mtamu pale wanapowahitaji akina Mtopea, Magezi na Yahaya Huseni tu. Nje ya hapo Uislamu unakuwa udini. Ukiangalia ni watu wenyewe ndio wamevaa au wamevalishwa miwani za udini, miwani za chuki, na wanaona rangi za udini na vurugu, ambazo pengine hazipo. Hebu vueni miwani zenu!!! 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Polisi ‘isiibebe’ CCM

Wapinzani kumuimarisha Prof. Lipumba

Ngangari kung’olewa Sokoni, Ilala

Polisi nchini hawajui mipaka ya kazi yao -OAU

MAKALA
BBC, CCM ndugu au tajiri na kibaraka?

HABARI
‘Walioshindwa kutawala wasikimbilie matusi’

ATV yatakiwa kuzingatia maadili

Wakazi wa Tabata walalamikia athari ya maji machafu

Maalim Seif akanusha madai ya kumwaga damu

USHAURI NASAHA
‘Mama, hela hii inanunua nini?'

MAKALA
Demokrasia ni kukubaliana kutokukubaliana

MIPASHO NASAHA
HEBU VUENI MIWANI ZENU!

KALAMU YA MWANDISHI
Juha haliambiliki!Juha haliambiliki!

MAKALA
Amani ya Tanzania itadumishwa na haki

MWENYE MACHO…
Hoja za uongo katika kampeni

MAKALA
Chonde Dk. Omari na Karume wahurumieni Wazanibari wenzenu

Habari za Kimataifa

LISHE
Kimfaacho  mtoto

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga kuwakosa Mahadhi, Mbuna
  • Idd Azzan lawamani
  • Kibadeni, Kayuni wanafaa Stars - Machuppa
  • Said Maulidi: Sihami Simba

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita