NASAHA
Na. 041 Jumatano Machi 29 - Aprili 4, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Riwaya 
 

Kisasi cha mauti 

MTUNZI: Juma S. Katanga (Jushaka) 

"LAZIMA afe! Lazima afe!" Komandoo Mlasi Kasanura Bamba alirudia tena kujiapiza. Damu ilikuwa imetapakaa sakafuni chumba kizima. Maiti kumi zisizo na vichwa zilikuwa mbele ya macho yake na nyingine zilikuwa zimetapakaa hovyo nje. Grand Kapakacha alikuwa bado kajificha nyuma ya mlango bunduki mkononi ,jambia kiunoni. Ni operesheni kabambe kweli kweli. Je, mambo haya yakoje? Ungana na mwandishi katika riwaya hii ya kusisimua.
 

GHAFLA Grand Kapakacha alishtuka kutoka usingizini. Mwenyewe alipenda kujiita kwa jina la "Grand K". Hivyo watu wengi walimzoea kwa jina hilo la Grand K. Baada ya kushtuka usingizini Grand K. alijiinua na kuketi kitandani huku akifikichafikicha macho yake kwa kiganja cha mkono ili kuondoa ukungu wa usingizi uliokuwa umetanda katika macho yake. 

Kana kwamba kuna kitu kimemuamsha vile Grand K. aliangaza huku na kule mle chumbani ili kujaribu kutafuta kitu hicho lakini hakubahatika kuona chochote chumbani humo zaidi ya mkewe aliyekuwa amelala fofofo pembeni yake, kabati refu la nguo pamoja na fenicha nyinginezo za ndani kadha wa kadha. 

Aliinua macho ukutani kuangalia saa na mshale ukamuonyesha kuwa hiyo ilikuwa ni saa moja kasorobo ya asubuhi. Alimwangalia tena mkewe pale pembeni yake na kumwona bado angali katika usingizi mzito akikoroma utadhani paka mwitu. Akainuka kitandani taratibu kuelekea bafuni kujitayarisha kwa ajili ya kwenda katika shughuli za miradi yake ya kila siku. 

Ni Mzee Mtanashati, mrefu wa wastani, mnene kidogo na mwenye siha nzuri sana. Falau ingalipasa kubashiri ningaliweza kusema kwamba alikuwa ameumbwa kwa dongo zuri sana. Dongo lile la mfinyanzi hasa ,si mchezo! Macho yake maang'avu yanayong'aa sana na nywele zilizochanganyikana na mvi ni baadhi tu ya vitu vinavyomfanya avutie mbele ya macho ya watu. Umri wake unakaribia kufikia miaka ipatayo hamsini na mbili hivi. 

Grand K. alizaliwa katika Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa. Yeye na mkewe aitwae Samara walihamia hapo Magomeni Kagera tangu mwaka 1984, mwaka alipofariki dunia yule Waziri Mkuu mashuhuri na jasiri kwelikweli wa Tanzania Bwana Edward Moringe Sokoine. Kijana wa kabila la Kimasai aliyekuwa akipendwa kweli kweli na wananchi wengi hapa nchini. Bwana Sokoine alifariki dunia katika ajali mbaya ya gari iliyotokea eneo la mkoa wa Morogoro katika msafara wake uliokuwa ukitokea Dodoma. Bwana Sokoine alifariki dunia papo hapo bila hata ya kuomba maji! 

Basi baada ya Grand K. kutoka bafuni aliingia moja kwa moja chumbani na kumkuta mkewe Bi.Samara bado amelala fofofo vilevile kama alivyokuwa amemuacha kabla na bado akikoroma tu. Grand K. alitungua nguo zake ukutani zilizokuwa zikining'inia juu ya msumari na kuanza kuzivaa upesi upesi huku akitazama tena ile saa iliyokuwa ukutani mle chumbani na sasa mshale ulimuonesha kuwa ilikuwa imefikia saa moja na dakika ishirini na tano asubuhi hiyo. 

Alipomaliza kuvaa alitoka na kuelekea sebuleni ili kupata kifungua kinywa. 

Alipokuwa akitoka kuelekea kule sebuleni mara akamwona mlinzi wa ndani nyumba amelala fofofo juu ya magunia ya mahindi yaliyokuwa yamepangwa vizuri ukumbini ,akiuchapa tu usingizi na kutoa mikoromo utadhani simba aliyekabwa na mfupa kooni. 

Grand K. alipiga hatua kumuekea yule mlinzi pale juu ya magunia ya mahindi. "Shenzi kabisa! Yaani anajisahau kabisa kama yuko kazini anachapa usingizi halafu mimi nimpe mshahara wa bure? Ngoja nimuoneshe cha mtema kuni leo!" ,alimaka Grand K. kichinichini huku akizidi kupiga hatua kumuendea yule mlinzi ambaye hadi sasa alikuwa akielea kwenye ndoto tu asijue nini kinachoendelea juu yake. 

Grand K. alipomfikia tu yule mlinzi , alimnasa kibao kikali sana cha usoni kiasi kwamba yule mlinzi usingizi wote ulimtoka ghafla akaporomoka kutoka juu ya yale magunia hadi chini akafikia kubamiza kichwa chake sakafuni akawa anaona nyota nyota tu zikipita mbele ya macho yake. Alipoinuka, kabla hajakaa sawaswa, akatandikwa konde la kichwa hadi chini akainuka tena upesi upesi kujitetea huku akiomba msamaha na akitetemeka kwa woga kweli kweli. 

"Nisamehe Mzee,shikamoo", aliamkia upesi upesi yule mlinzi kwa kurudiarudia kana kwamba amepagawa au amechanganyikiwa vile. 

Grand K. alimwangalia kwa jicho la dharau kuanzia miguuni hadi utosini kisha akafanya kama kujikohozakohoza vile halafu akamtemea makohozi mazito usoni yule mlinzi. "Bahati yako yamekupata sawaswa, ungejidai kukwepa ungekiona cha moto leo, pumbaf," alimaka Grand K. huku akiondoka na kumwacha yule mlinzi ameduwaa asijue cha kufanya. Maskini mlinzi wa watu hakuwa na la kufanya zaidi ya kuanza kujifuta yale makohozi usoni kwa kutumia magwanda yake baada ya kukosa makaratasi. 

"Hapana, Huu sasa ni utumwa kabisa! Hii siyo kazi tena, loh!! Kazi gani ya mateso namna hii?" alilalama yule mlinzi kwa huzuni huku machozi yakimdondoka. Akabakia sasa kufikiria mawili tu; asalimuamri na kubwanga manyanga aache kazi lakini watoto wake wafe njaa au ahimili zahama za Grand K. apate chakula cha wanawe. Kwa kweli hakuwa na la kufanya bali kuendelea kafiri tu na kazi kwa kujipa tumaini la kwamba "mtumikie kafiri upate mradi wako." 

***************** 

KAMA kawaida yake, mfanyakazi wa ndani, Hausigeli Grace alikuwa keshaandaa kila kitu mezani wakati Grand K. akimsulubu yule mlinzi kule varandani. Kuanzia mishikaki, chai ya maziwa, nyama ya kukaangwa, maini, chapati, mikate iliyopakwa siagi na matunda kadhaa wa kadha vyote vilikuwa tayari mezani kwa ajili ya kifungua kinywa cha Mzee, Grand K. mwenyewe. Basi akiishakaa hapo mezani hula kwa kudokoadokoa kimoja kimoja badi amalize mzunguko wa mafungu yote ndipo ashushie na maji baridi halafu huyo anatimka zake. 

Sasa ilikuwa yapata saa moja na dakika thelathini na tisa. Kila siku msichana Grace hutakiwa kuamka saa kumi na moja alfajiri na kuanza kufanya usafi wa nyuumba. Kwanza hupiga deki nyumba yote halafu asafishe vyoo vyote, kisha afagie uwani na uwanja wote unaozunguka nyumba kabla ya kusafisha mabanda ya kuku na ya ng'ombe. Halafu sasa baada ya hapo ndipo atayarishe chai ya Mzee kabla ya kutimu saa moja kamili. 

Ole wake siku moja avuruge ratiba hiyo, atakiona cha mtema kuni kwa kuchakazwa makofi na Grand K. hadi ajute kwa nini alikubali kutoka kwao Makambako kuja huku mjini kufanya kazi kwa Grand K. 

"Kama huwezi kazi rudi kwenu kijijini ukachunge ng'ombe na baba yako, pumbaf!", ungesikia Grand K. akimgombeza Grace. Halafu msichana Grace ambaye ana umri wa miaka kumi na miwili hubakia kunywea tu kwa huzuni moyoni kwa jinsi anavyohenyeshwa vibaya hapo nyumbani kwa Grand K. Siku nyingine huwa ni zamu ya mke wa Grand K. Bi.Samara kumchamba na kumchachafya Grace kwa matusi na masimango ya kila namna. Hiyo ndio hali halisi inayowakabili walinzi na mahausigeli wa Grand Kapakacha. 

Grand K. alipomaliza kupata kifungua kinywa alitoka sasa kuelekea kwenye gari lake analotembelea kila siku akiwa katika mizunguko yake mbalimbali. Ingawaje siku nyingine hubadilisha magari hata mara tatu kwa kutwa lakini ile Toyota LandCruiser yake nyekundu ndiyo huipendelea zaidi kuitumia. Mara zote wakati Grand K. akipata kifungua kinywa, dereva wa gari atakalotumia siku hiyo hutakiwa kuwamo ndani ya gari mapema ili yeye Grand K. atakapotoka nje tu tayari kwa safari basi dereva amfungulie milango kama wanavyofanyiwa Marais au viongozi mashuhuri vile. Basi Grand K. akaelekea katika gari lile alilokuwamo dereva huku kashikilia 'Briefcase' yake mkononi. Kulifikia gari, dereva hakutoka nje kumfungulia mlango kama ilivyokuwa desturi siku zote. 

Hili lilimshangaza sana Grand K. Kumbe yule dereva alikuwa kauchapa usingizi mle ndani ya gari juu ya sukani. "Shenzi kabisa!", Grand K. kite kilimtoka. "Yaani analala usingizi wakati anajua kabisa kwamba muda huu mimi nitatoka? Basi we wacha tu aendelee kukoroma asiamke mwenyewe, atakiona kilichomtoa kanga manyoya!", alifoka Grand K. pale nje ya gari huku kufura kama chatu aliyemwagiwa maji ya moto. Dereva yule wala hakuzinduka kabisa. Wale madereva wenzake na walinzi waliokuwa pale uwani walitamani malaika au jini atokee kwenda kumuamsha mwenzao mle garini kwani walijua nini kinachomkabili mwenzao mbele ya mwili uliofura wa Grand K. uliokuwa umesimama pale nje ya mlango wa gari. Kuona yule dereva haamki, Grand K. hasira zikazidi kumpanda, sura ikamwiva kweli kweli na macho yote yakabadilika rangi kuwa mekundu. Akabakia kufyonya tu kila baada ya sekunde. Mwishowe akaamua kufungua mlango yeye mwenyewe na kuingia mle ndani ya gari ambapo alimtandika yule dereza kwa "mbata" moja kali sana la kisogoni! Yule dereva akashtuka ghafla na kutoa ukelele mmoja tu mkali "eee!" kisha akadondoka chini hadi nje ya gari na kuzimia huku damu zikitiririka masikioni na kufanya vibwawa vidogo vidogo pale ardhini. "Kaua leo! Kaua! Kaua jamani!!", minong'ono iliwatoka wale walinzi na madereva wengine pale nje uwani. 

Itaendelea toleo lijalo
 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Tume ya Uchaguzi ipigwe msasa, sio wananchi

Mkapa awatahadharisha wanawake  CCM

Lipumba: Wananchi wana uwezo wa kuondoa utawala mbovu 

Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishitaki Serikali

Habari za ndani
Polisi hawana uwezo wa kuzuia mabadiliko’

Sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu kufanyika Dar

MPASHO NASAHA
Hawavumi lakini...

Ushauri Nasaha
Urafiki na makuzi ya mtoto

MAKALA
Toba ya ‘Pope' liwe somo kwa utawala wa Mkapa

WAZO  LA  WIKI
Viva Senegal

MAKALA
Tatizo la ubakaji katika jamii yetu:
Mazingira katika shule zetu

Kalamu ya Mwandishi
Tahadhari isipochukuliwa huenda damu ikamwagika Zanzibar

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (4)

Habari za Kimataifa

Barua

Riwaya
Kisasi cha mauti

Lishe
Baba kulea ujauzito

MICHEZO

  • Ndoa ya Mobitel na Yanga mashakani
  • Homa ya pambano la Ghana na Stars yapanda

  • Makoye: Fedha za Simba nimetafuna mwenyewe 



     
     



       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com



     
     
     
     
     
     
     
     
     
     
     
     

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita