NASAHA
Na. 041 Jumatano Machi 29 - Aprili 4, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA 
 
 

Tatizo la ubakaji katika jamii yetu:
Mazingira katika shule zetu 



NA H. SULAYMAN 
 

TUKIJA katika mazingira ya shule zetu, ile kazi ya shule kama kituo cha malezi ya maadili, tunakuta haifanyiki tena. Suala la malezi katika shule zetu ameachiwa mtu mmoja au wawili aitwaye Mwalimu wa nidhamu, ambaye kutokana na mazingira mabaya ya shule zetu na makali ya maisha mbele ya pato dogo, kazi hii haipi muda wa kutosha. Wakati mwingine unakuta mwanafunzi ambaye ni mtovu wa nidhamu ni mwajiri wake katika masomo ya tuition. Sasa vipi atamkemea mwajiri wake? Hakika ni mtihani mkubwa.
 

NI taasisi hii ya elimu ambayo wasomi wote wanakubaliana (akina Durkheim, Brunei na Bernstein) kuwa inayo nafasi ya pekee katika kujenga maadili kwa vijana hata kuweza kumrekebisha tabia mtoto sugu, mtundu na mkorofi. Walichomaanisha wataalamu hawa ni kuwa kama itapatikana mitaala mizuri ya elimu basi shule itafanya maajabu hayo. 

Lakini ni mitaala/shule ya aina gani waliyoipa uwezo huo? Je ni mitaala kama ile ya kuwafundisha watoto elimu ya ngono? Tunashangaa kusikia kuwa bado nchi zetu zinaipigia debe elimu ya ngono ili iwekwe katika mitaala yetu, ingawa ipo chini ya pazia la mpango wa uzazi wa majira 'Family planning' na 'Family life education'' kwa mitaala ya Zanzibar (1992). 

Tunashangaa tena na kujiuliza ni familia ya nani mtoto wa washule atapangilia uzazi wake wakati yeye hajaoa au kuwa na familia? Au ni ruhsa kwa watoto wetu kutenda tendo la ngono lakini kwa mpangilio maalum! 

Jamii ya leo na kesho tunaipeleka wapi na ujinga huu? Wazungu walitutangulia kwa hili, lakini nini yalikuwa matokeo? Utoaji mimba, kutupa watoto na kuwaua wengine ndiyo yaliyokuwa matokeo ya mchezo huu hatari. 

Gazeti la The Times la 9 Desemba 1985 liliripoti kuwa katika mwaka huo, iligundulika kuwa katika kila wanafunzi 1000 (elfu moja) wasichana 300 (miatatu) walikutwa na mimba. Na hii ni katika shule moja tu ya Chicago D.U. High School, nchini Marekani. Sikuelezi vyuo maana huko ni rukhsa. 

Turudi hapa kwetu, tujiulize ni matukio mangapi ya kutoa mimba au kukutwa na mimba watoto wa darasa la tano, sita na la saba yameripotiwa!! Imefikia hatua ya kujadili uhalali wa sheria ya kumzuia mtoto wa shule aliyejifungua mtoto kuendelea na shule, na viongozi wetu, wabunge na wazazi! 

Kwa hakika hali ni mbaya inatisha. Sasa katika mazingira kama haya ni matukio yepi utayahesabu ni ubakaji na yepi utayahesabu ni kwa ridhaa? Au ukubaliwe ushahidi wa upande mmoja tu!. 
 
 

VYOMBO YA HABARI





Hivi navyo vinatoa mchango mkubwa katika kueneza tabia chafu kwa kiwango kikubwa, na huwa ni kichocheo kwa wabakaji. Mathalan suala la mtoto kuwa na 'boy au girl friend" kuonyesha vitendo vya aibu hadharani ambavyo vinaashria kufanyika tendo la ndoa. Magazeti kama ya KASHESHE, SANIFU na kadhalika yamekuwa ni hadithi za kuvutia kwa watoto wetu mashuleni na hata nyumbani. Maadui wa maadili mema hawakwishia hapa, bali mpaka ndani ya mtandao wa Internet wameweka sumu hii hatari. 

Tatizo ni kuwa nchi yetu imelifumbia macho suala la maadili, na pale linapozungumzwa basi huishia midomoni mwa wakubwa, bila ya kuweka taratibu za kuyalinda maadili yetu mazuri. Tunapenda kuwauliza Waheshimiwa hao; Nchi hii itaongozwa na watu wa aina gani baada yenu ikiwa hali hii hamkuirekebisha? Au mnadhani mtatawala milele? Uhai wa nchi na maendeleo yake vipo mikononi mwa vijana. Hivyo wahami vijana nchi ipate maendeleo. Wahurumieni vijana wanaochanganyikiwa wapatapo maelezo tofuati toka kwa wazazi wao na vyombo vya habari juu ya faida au madhara ya kitu fulani katika maisha yao. Mgongano huu unapamba moto zaidi pale anapohoji kuwa kama kilichooneshwa ndani ya TV au kanda ya video au kutangazwa na gazeti ni kibaya, kwa nini Serikali yetu ikiruhusu maana ndiyo inayotoa vibali vyote kwa vyombo hivi. Siku moja niliulizwa darasani; Kwa nini Serikali iruhusu utengenezaji wa sigara, pombe na kadhalika wakati ikijua madhara yake ya kiafya, kiuchumi na kimaadili kwa jamii yake kama unavyodai Mwalimu? Tumuamini nani wewe au serikali? Una maana wewe unatupenda zaidi kuliko Rais wetu? Sijui msomaji wangu ungejibu nini? 

Siku hizi pombe zimekuwa nyingi tena za kila aina mpaka zile ziitwazo 'Dhahabu'. Na limekuwa ni suala la kawaida kunywewa hata ndani ya basi la abiria! Zinauzwa sambamba na unga na mchele katika viduka hata vya uchochoroni! 

Yote hayo ni kutokana na kutangazwa kila dakika na vyombo vya habari, kiasi kwamba hata wale waliokuwa wakisikia kinyaa ikitajwa pombe hawana hisia hizo tena. Je katika mazingira ya walevi utatumia lugha gani kumzuia mlevi asibake au kunajisi? 

Sasa nini la kufanya ili kuiokoa jamii yetu na janga hili la ubakaji na kunajisi watoto? Watoto ni amana ya Mwenyezi Mungu kwetu. Na kila mzazi aliyesawasawa hupendelea mwanawe awe vile vile sawa sawa kiakili, kiroho na kiafya. Na haya hayawezi kupatikana mpaka uwepo mfumo madhubuti na maandalizi mazuri ya kumtayarisha mtoto ili ajali na kuyalinda maadili mema. 

Hivyo tunashauri yafuatayo:- 

(i) Itengenezwe programu ya kuelimisha jamii umuhimu na faida ya kulinda maadili mema. (ii) Ziundwe kamati ndogo kwa mfumo wa utaratibu wa nyumba kumi kumi au mtaa, na kazi yake iwe (a) kuelimisha jamii kama asemavyo Allah S.W.. "Hatukuwa ni wenye kuudhibu umma (Jamii) ila ni baada ya (kuelimishwa kwa) kumtuma mjumbe" (b) kumlazimisha anayeelekea kuwa mkorofi afuate maadili mema ya jamii ile - yaani jamii impige vita mpaka ake katika msitari (c) kumpeleka aliyeshindikana kwenye vyombo vya sheria. Huko ni lazima tuhakikishe kuweko kwa watekelezaji wa sheria kwa ukamilifu wake na haki "The rule-enforcers" kama alivyowaita mmoja wa wanamaadili Becker (1963). (iii) Taasisi zetu za dini zifanye kazi ya kuelimisha jamii umuhimu na faida ya mwanadamu kufuata amri ya Muumba wake hapa duniani naakhera. Yaenezwe mafhumu ya heshima kwa mkubwa na huruma kwa mdogo na kuwa mtoto ni wajamii nzima. Anasema mwanafalsafa Aristotle kuwa nidhamu kwa mtoto itakuwa ya juu kabisa pale kila mtoto atakapomuona kila mtu mzima kama baba yake. Bila shaka na mtu mzima atakapomuona kila mtoto ni mtoto wake. (iv) Taasisi zetu za elimu ziboreshwe kwa kuwekwa waalimu wenye maadili mema. Mitaala nayo itokane na mafundisho ya dini zetu zilizosahihi na mila zinazokubalika katika dini hizi, na kupiga vita maadili mabovu ya kigeni. 

(v) Wizara husika na vyombo vya habari ifanye kazi yake vizuri kwa kupambana na maadui wa maadili mema katika jamii yetu. Ifuate ushauri wa wataalamu wa taaluma ya malezi na washauri wa kidini. (vi) Na kubwa ya yote hayo ni kila mtu kujiona ni muhusika katika kulinda na kutetea maadili mema hapa duniani. Na kuwa anafanya hivyo kama sehemu ya ibada aliyotakiwa na Muumba wake aifanye. Hivyo akemee, achukie, na apambane ikibidi na wale wote wenye kueneza ufisadi katika ardhi. Aanze kazi hii tukufu kwa kuisafisha nyumba yake, ya nduguye kisha ya jirani. Kuna methali ya Kiingereza isemayo: "Kama kila mtu atasafisha mbele ya nyumba yake/barazani kwake, basi mtaa mzima utakuwa msafi." 
 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Tume ya Uchaguzi ipigwe msasa, sio wananchi

Mkapa awatahadharisha wanawake  CCM

Lipumba: Wananchi wana uwezo wa kuondoa utawala mbovu 

Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishitaki Serikali

Habari za ndani
Polisi hawana uwezo wa kuzuia mabadiliko’

Sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu kufanyika Dar

MPASHO NASAHA
Hawavumi lakini...

Ushauri Nasaha
Urafiki na makuzi ya mtoto

MAKALA
Toba ya ‘Pope' liwe somo kwa utawala wa Mkapa

WAZO  LA  WIKI
Viva Senegal

MAKALA
Tatizo la ubakaji katika jamii yetu:
Mazingira katika shule zetu

Kalamu ya Mwandishi
Tahadhari isipochukuliwa huenda damu ikamwagika Zanzibar

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (4)

Habari za Kimataifa

Barua

Riwaya
Kisasi cha mauti

Lishe
Baba kulea ujauzito

MICHEZO

  • Ndoa ya Mobitel na Yanga mashakani
  • Homa ya pambano la Ghana na Stars yapanda

  • Makoye: Fedha za Simba nimetafuna mwenyewe
     



     
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com



     
     
     
     
     
     
     
     

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita