NASAHA
Na. 041 Jumatano Machi 29 - Aprili 4, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Barua 

Tatizo ni ubinafsi na kipaumbele

Ndugu Mhariri,

HIVI karibuni iliyokuwa tume ya Jiji la Dar es Salaam ilimaliza muda wake uliopewa na serikali ya awamu ya tatu ya CCM, ya kuliendesha jiji huku likiandaa mazingira mazuri ya namna ya kuliendesha mara baada ya kukabidhiwa kwa halmashauri katika manispaa zake tatu.

Watu wengi wamesifia ujuzi, ubunifu na hata ujasiri wa viongozi hao wa Tume katika kutekeleza majukumu yake. Ilibidi nyakati fulani kuwe na kutoelewana kati ya tume na watendaji wa serikali mkoani ili kuweza kutekeleza majukumu yao. Hata baadhi ya wakereketwa wa CCM ambaohufungua mashina yao pasiporuhusiwa na kuyaendesha bila bughudha ya serikali au mgambo wa jiji, walikutana na makali ya waheshimiwa hawa wa jiji. 

Tukiacha huko, tuzungumzie kipaumbele. Moja ya sababu ya msingi kabisa iliyopelekea kuvunjwa kwa Halmashauri ya Jiji na kuundwa tume ni kushindwa kwa hiyo iliyokuwa Halmashauri ya Jiji kukusanya na kuzoa taka jijini. Leo tujiulize tatizo la mrundikano wa taka hapa jijini limekwisha? Utagundua kuwa limepungua tu. Maeneo mengi ya vichochoroni kama vile Kariakoo, Buguruni na kwingineko tatizo bado liko palepale. 

Eneo la kuzunguka soko la Kariakoo ilibidi lifanyiwe ubunifu wa kina wa namna ya kupambana na uchafuzi unaofanywa na wachuuzi. Angalau pangetengenezwa vijikabati vya waya (cadges) kama ilivyo kule kati kati ya jiji, ili vyakula viwe katika hali ya usafi badala kuwekwa chini viking'ong'wa na mainzi kwenye maji na tope la uchafu. Yale majani yote yangetakiwa yasifikishwe hapo eneo la soko, na kwamba pangekuwa na eneo maalum la kuoshea nyakula hivyo. 

Pili tuangalie tatizo sugu la kutuwama kwa maji machafu na maji ya mvua katika mitaro ya barabara nyingi hasa ile ya uhuru karibu na Mataa (Traffic lights) ya Mnazi Mmoja na karibu mzunguko wa shule ya Uhuru, pia barabara ya Msimbazi karibu na klabu ya Simba, ukiacha maeneo mengine mengi tu. 

Ndipo hapo ninaposema kuwa tatizo letu ni ubinafsi na kipaumbele. Kabla hatuja tatua tatizo muhimu kwetu, wamekimbilia kukarabati makao makuu ya jiji na kujenga shule katikati ya jiji ili tuweze kuona kwa haraka na kusema fulani bwana kafanya kadhaa na kadhaa wakati wa uongozi wake. 

Tatizo la msingi wameliacha palepale. Haya sasa kazi kwenu nyie Halmashauri/Manisapaa mufanyie ukarabati mitaro hiyo kwani mvua zimekwishaanza na maji yameanza kujaa na kuzifanya barabara kutopitika. Lakini napata mashaka kama kweli mtaweza, kwani tumeshasikia kuwa hamna fedha. Iliyokuwa tume ya jiji imekwisha komba zote. 

Justin Jacob, 
Buguruni, 
Dar es Salaam.



 

Hongereni RTD! 
 

Ndugu Mhariri,

Naomba angalau nafasi kidogo tu ndani ya gazeti lako hili ambalo sina shaka kwa hivi sasa ndio tegemeo pekee kati ya majarida mengi yaliyopo hapa nchini katika kupata habari za uhakika za ndani na nje ya mipaka yetu ili niweze kutoa pongezi zangu zisizo za dhati kwa watayarishaji wa kipindi cha Lugha yetu kinachorushwa hewani kila Jumatano saa nne na nusu usiku hadi saa 5.00 usiku au kwa ufupi niseme kwa uongozi mzima wa RTD.

Napenda kuushukuru uongozi wa Radio Tanzania Dar es Salaam kwa jitihada zao za kila siku za kuhakikisha Radio Tanzania, Radio ya Tifa wanaifanya kuwa ni sehemu ya propaganda za Chama Cha Mapinduzi ilihali radio hiyo ni haki ya kila mwananchi kuitumia bila kujali itikadi yake ya chama. 

Hali hiyo imedhihirika hivi karibuni pale walipoamua kwa makusudi kuacha kukiongolea Kiswahili kama lugha ya Taifa na badala yake kuchukua nafasi hiyo kuwaelezea watu binafsi waliowahi kushika nyadhifa za juu za uongozi wa chama tawala. Ni hapo tarehe 19-1-200 alipokaribishwa Bw. Said Nyoka katika kipindi hicho na kuanza 'porojo' zake juu ya Mwl. Julius Nyerere, na tarehe 26-1-200 yaani wiki moja baadaye alikaribishwa Mzee Hamisi Akida naye hakua na tofuati sana na Bw. Nyoka isipokuwa huyu Mzee yeye alizungumzia sana habari za Bw. Rashid Kawawa hali ambayo siyo siri imekuwa ikituudhi sana na hata kutuchosha sisi wasikilizaji na wapenzi wa kipindi hicho na RTD kwa ujumla. Ni matumaini yangu kuwa mtairekebisha hali hiyo mapema iwezekanavyo ili kuleta uhusiano mwema na wasikilizaji wenu. 

Mtagaluka Rashid, 
Dar es Salaam.


Uislam usichezewe katika Malumbano ya Hoja 
 

Ndugu Mhariri,

MIMI ni mmoja wa watu wanaofuatilia kwa karibu kipindi cha malumbano ya hoja kinachoendeshwa na ITV.

Mara kwa mara kumekuwa na juhudi za makusudi kuzuia neno Uislam lisitajwe ila pale tu linapotumiwa vibaya. Watangazaji wa kipindi hiki wamekuwa mara zote wakiwakabili washiriki wa kipindi na kuwanyang'anya 'Mike' mara tu wanapotoa hoja zenye muelekeo wa Kiislamu kwa kisingizio kuwa eti kipindi chao hakiruhusu mambo ya dini. Mifano safi imejitokeza kwenye kipindi kilichokuwa kinajadili suala la mahari iwapo limepitwa na wakati au la na hivi karibuni kwenye kipindi kilichojadili suala la wanawake kubadili majina wanapoolewa. 

Japo wachangiaji wengi walijadili kwa mtazamo wa Kikristo na kutoa mifano ya kutoa ahadi mbele ya mchungaji kuwa ndoa yao haitovunjika, hakuna hata mmoja aliyezuiliwa asiongee. Ila alipotokea kijana mmoja akatamka kuwa yeye angelitazama suala lile kama Uislamu unavyoliona alikemewa na kunyang'anywa 'mike' mara moja; kiasi kuwa hata baadhi ya watazamaji hawakumwona. Hawa watangazaji wametumwa na nani kudhalilisha Uislamu? 

Utaratibu huu wa chuki a kidini usipokomeshwa utaathiri mustakabali wa Television ya ITV na zingine zote zenye tabia hii chafu. 

Mwanaheri Ally, Dar es Salaam. 
 


Makonda acheni kunyanyasa wanafunzi wa Kiislam 
 

Ndugu Mhariri,

Mara nyingi nimeshuhudia makondakta wa daladala wakiwanyanyasa wanafunzi wa Kiislamu hasa wale wanaovaa hijab.

Bila shaka makondakta hawa sio Waislam na wanajifanya hivyo kwa chuki dhidi ya Uislam. 

Nataka niwaambie kwamba hata sisi wengine tusiovaa hijab udini huo unatuudhi. Ni vyema makonda hawa wakaiacha tabia hiyo mara moja. 

Sisi Waislamu tumekatazwa kuwaonea wasiokuwa Waislamu na tumekatazwa zaidi kuonewa kwa ajili ya dini yetu. Waislam tupo wengi nchini chuki hizo za kidini zinazofanywa na makonda hao zinaweza zikazua balaa kubwa nchini. 

Mwanaidi Seif, 
Dar es Salaam. 



 

Masheikh wa Bakwata jiepusheni na upande unaodhulumu 
 

Ndugu mhariri,

HISTORIA inatuonyesha kuwa maaskari walioamrishwa kuua na kutesa wananchi katika vita kuu ya pili ya dunia walifikishwa mahakamani. Utetezi wao kwamba walikuwa wakitekeleza amri za wakubwa haukusaidia.Hali hiyo inawakuta wale wa Bosnia na Rwanda.

Huko Rwanda uongoziwa dini, maaskofu na makasisi walioshika panga, walioshinikiza mauaji kwa maneno yao na waliojifanya majasusi wa kuwasaidia wauaji wote wako mahakamani. Nao wameshindwa kujitetea kwa hoja za kuwatumia wakubwa. 

Nyie masheikh, wengine maimamu wa misikiti mnajua kwamba nchi hii waislamu wamedhulumiwa na wengine wameuliwa lakini bado mnasimama kwenye semina na kutoa kauli za kujipendekeza kuwaa eti waislamu hawadhulumiwi, wana uadui tu na watu wengine. 

Hivyo, siku ya siku itakapofika na mkasimama mahakamani kama ilivyo Rwanda na Bosnia, utetezi wenu kwamba mlikuwa mnaifurahisha Bakwata au waziri fulani hautowasaidia. 

Hali yenu hakika itakuja kuwa mbaya zaidi siku mtakaposimama kwenye mahakama ya Allah. 

Bi. Sharifa M.
Mwananyamala,
Dar es Salaam.
 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Tume ya Uchaguzi ipigwe msasa, sio wananchi

Mkapa awatahadharisha wanawake  CCM

Lipumba: Wananchi wana uwezo wa kuondoa utawala mbovu 

Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishitaki Serikali

Habari za ndani
Polisi hawana uwezo wa kuzuia mabadiliko’

Sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu kufanyika Dar

MPASHO NASAHA
Hawavumi lakini...

Ushauri Nasaha
Urafiki na makuzi ya mtoto

MAKALA
Toba ya ‘Pope' liwe somo kwa utawala wa Mkapa

WAZO  LA  WIKI
Viva Senegal

MAKALA
Tatizo la ubakaji katika jamii yetu:
Mazingira katika shule zetu

Kalamu ya Mwandishi
Tahadhari isipochukuliwa huenda damu ikamwagika Zanzibar

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (4)

Habari za Kimataifa

Barua

Riwaya
Kisasi cha mauti

Lishe
Baba kulea ujauzito

MICHEZO

  • Ndoa ya Mobitel na Yanga mashakani
  • Homa ya pambano la Ghana na Stars yapanda

  • Makoye: Fedha za Simba nimetafuna mwenyewe



     
     



       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com



     
     
     
     
     
     
     
     
     
     
     
     

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita