NASAHA
Na. 041 Jumatano Machi 29 - Aprili 4, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Lipumba ahutubia Jangwani na kusema: 
Wananchi wana uwezo wa kuondoa utawala mbovu 
  • Chukueni mfano wa Senegal 
  • CCM imekiuka Ilani yake ya uchaguzi 


Mwandishi wetu 
 

KWA mara ya kwanza katika mwaka huu na pia katika historia ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa nchini, Jumapili iliyopita, maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam walifurika katika viwanja vya Jangwani jijini kuhudhuria mkutano wa hadhara ulioitishwa na Chama cha Wananchi (CUF) na kuhutubiwa na viongozi wa kitaifa wa chama hicho.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na vijana na watu wazima, viongozi hao wa CUF, mbali na kuwahimiza Watanzania kujiandaa kikamilifu kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao, waliainisha baadhi ya mambo kama ushahidi ambayo kwayo wamewaomba Watanzania wainyime CCM nafasi ya kuwaongoza tena Watanzania. 

Akiwahimiza Watanzania kutorudi nyuma katika kuleta mabadiliko, Mwenyekiti wa CUF Taifa, Prof. Ibrahim Lipumba alisema hali ya kisaisa Afrika inabadilika na tayari CCM imeingiwa na hofu. 

"...hali ya kisiasa barani Afrika inabadilika, wenzetu wa Senegal wametuonesha mfano... hapa nyumbani CCM wamepata 'presha'" alisema Prof. Lipumba. 

Katika uchaguzi wa Rais uliofanyika hivi karibuni nchini Senegal, chama kilichokuwa kikiitawala nchi hiyo kupata uhuru wake, mwaka 1960, kilishindwa. Mgombea wa chama hicho alikuwa Bw. Abdou Diofu. 

Akitoa kielelezo cha kuwepo hofu ndani ya chama tawala cha CCM, Prof. Lipumba alisema mabadiliko ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 'yamelazimishwa' kujaribu kumsaidia mgombea urais wa chama hicho apite kwa urahisi. 

"Mabadiliko ya 13 ya katiba ni kielelezo kuwa mgombea wao (CCM) hakubaliki.... hawezi kupata asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa", alisema Mwenyekiti huyo wa CUF, na kuongeza kuwa wabunge wa CCM walitishwa na kulazimishwa kuyaunga mkono marekebisho hayo ya Katiba. 

Katika marekebisho hayo ya 13 ya Katiba ilipendekezwa na kupitishwa Bungeni kuwa, kuanzia uchaguzi mkuu wa mwaka huu, mgombea urais atakayepata kura zaidi ya wagombea wenzake ndiye atakayetangazwe kuwa rais hata kama mgombea huyo hakuvuka nusu ya kura zote zilizopigwa. 

Akizungumzia hali ya kiuchumi ya wananchi Prof. Lipumba alielezea hali ya kidhalili aliyoiona katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wakati wa ziara yake ambako ameshuhudia shule ina mwalimu mmoja, wanafunzi wote hawana viatu na huyo mwalimu amevaa kandambili. 

Akizidi kusimulia aliyoyaona Handeni Mwenyekiti huyo wa Chama cha Wananchi alisema amewaona akina mama wakifanya biashara ndogo ndogo na kutozwa ushuru mkubwa zaidi ya mapato yao. 

"....akina mama wale wanauza fungu moja la mboga za majani kwa shilingi 10 na hawapati mnunuzi, lakini wanatozwa ushuru wa soko kati ya shilingi 50 na 100 kwa siku... na soko lenyewe ni chini ya mti", alisimulia Prof. Lipumba simulizi ambalo liliwafanya wanawake wengi waliohudhuria mkutano huo kufuta machozi kwa kile kilicholezwa na baadhi yao kuwa ni "serikali kukosa huruma kwa wanawake". 

Prof. Lipumba ambaye ni mtaalamu wa uchumi aliyebobea alieleza pia athari za uuzaji holela wa mashirika ya umma ambapo amesema utajiri mkubwa wa Tanzania umekuwa "ukiporwa." 

Aliwaeleza wananchi waliokuwa wakimsikiliza kwa makini kwamba Serikali ya CCM imeiuza Benki ya NBC (1997) katika mazingira ya kutatanisha. 

Alisema zabuni ya kuiuza benki hiyo kubwa kuliko zote nchini ilipotangazwa Benki ya Barclays ya Uingereza ilitaka kuinunua NBC (1997) kwa bei nzuri sana lakini siku chache kabla Barclays hawajaidhinishwa kuinunua benki hiyo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Ubinafsishaji Mashirika ya Umma (PSRC), Bw. George Mbowe aliondolewa katika wadhifa huo. 

"Kilichofuatia', alieleza Prof. Lipumba, "ni benki hii kubwa nchini kuuzwa kwa Kampuni ya Muungano wa Mabenki ya Afrika ya Kusini kwa bei poa." 

Sambamba na hilo, Mwenyekiti huyo wa CUF aliilaumu CCM kwa kushindwa "kuiheshimu" na kuitekeleza Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 1995 ambayo imeagiza kuwa mabenki makubwa ya serikali yasiuzwe. 

"Ilani ya uchaguzi ya CCM, katika ukurasa wa 20, wamesema hawatauza mabenki makubwa ya serikali, lakini NBC tayari wameiuza", alieleza Prof. Lipumba. 

Aidha Mtaalamu huyo wa uchumi alieleza jinsi machimbo ya dhahabu ya Bulyankulu Gieta, yanavyoitajirisha Ulaya na kuiacha Tanzania ikiwa masikini. 

Alieleza katika hadhara hiyo kwamba Kampuni ya Ashanti Gold Mines iliyouziwa machimbo hayo inailipa serikali ya Tanzania dola tatu tu za Kimarekani kwa kila mauzo ya dhahabu ya thamani ya dola 100 za Kimarekani. Akifafanua alisema fedha hizo ni sawa na Tanzania kupewa Shs.2400/- katika kila mauzo ya shilingi 80,000/-. 

Ameeleza kuwa mbali na kampuni ya Ashanti kulipa kodi ya machimbo (royalities) ndogo kiasi hicho ikilinganishwa na mapato yake, kampuni hiyo pia imepewa misamaha ya kodi. 

"... hata mashirika ya kimataifa yanatushangaa jinsi tunavyotoa misamaha ya kodi kwa makampuni makubwa," alieleza mchumi huyo. 

"Ajabu zaidi ni kwamba TRA (mamlaka ya kodi nchini) inawabana wafanyabiashara wa hapa nchini na hali hii inasababisha biashara zao zishindwe kukua, na hivyo inapunguza ajira kwa Watanzania mwaka hata mwaka", alieleza. 

Akitaja takwimu zaidi kuonesha jinsi utajiri wa Tanzania unavyoporwa, Prof. Lipumba alisema wakati Ashanti ilinunua hisa moja kwa dola za kimarekani 50, kampuni hiyo ya madini imekwishauza asilimia 50 ya hisa hizo katika soko la hisa la Ulaya kwa thamaniya dola za kimarekani 400 kila hisa. 

Katika kile alichokieleza kuwa ni CCM kutowajali Watanzania, Mwenyekiti huyo wa CUF Taifa alisema kuwa serikali ya CCM imepunguza sana bajeti ya afya ya wananchi. 

Akitolea mfano, alisema mwaka wa mwisho wa serikali ya Awamu ya Pili chini ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, 1994/1995, fedha iliyotengwa kwa ajili ya kununulia dawa katika Wizara ya Afya ilikuwa ni shilingi bilioni 27.8 lakini mwaka wa kwanza wa Rais Mkapa bajeti hiyo ilipungua na kubaki shilingi bilioni 7.1. 

Akiendelea alisema, "fedha za kununulia dawa ziliendelea kupungua na mwaka 1996/97 zilitengwa shilingi bilioni 4.2 tu lakini wapo (Serikali ya Awamu ya Tatu) tayari kutenga bilioni 3.2 kwa ajili ya kupaka rangi Ikulu." 

Katika mkutano huo wa Jangwani Prof. Lipumba aliwatahadharisha Watanzania kuwa CCM imekusudia kufanya "hila" katika uchaguzi ujao. 

"CCM inafanya kusudi kutofanya sensa (ya watu), na pia CCM haitaki kutoa vitambulisho vya kitaifa ili kurahisisha wizi wa kura", Profesa huyo na kutoa changamoto kwa wananchi wajiandae kudhibiti wapiga kura 'hewa'. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Tume ya Uchaguzi ipigwe msasa, sio wananchi

Mkapa awatahadharisha wanawake  CCM

Lipumba: Wananchi wana uwezo wa kuondoa utawala mbovu 

Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishitaki Serikali

Habari za ndani
Polisi hawana uwezo wa kuzuia mabadiliko’

Sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu kufanyika Dar

MPASHO NASAHA
Hawavumi lakini...

Ushauri Nasaha
Urafiki na makuzi ya mtoto

MAKALA
Toba ya ‘Pope' liwe somo kwa utawala wa Mkapa

WAZO  LA  WIKI
Viva Senegal

MAKALA
Tatizo la ubakaji katika jamii yetu:
Mazingira katika shule zetu

Kalamu ya Mwandishi
Tahadhari isipochukuliwa huenda damu ikamwagika Zanzibar

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (4)

Habari za Kimataifa

Barua

Riwaya
Kisasi cha mauti

Lishe
Baba kulea ujauzito

MICHEZO

  • Ndoa ya Mobitel na Yanga mashakani
  • Homa ya pambano la Ghana na Stars yapanda

  • Makoye: Fedha za Simba nimetafuna mwenyewe


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com
    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita