NASAHA
Na. 041 Jumatano Machi 29 - Aprili 4, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA 
 
 

Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (4)
Wananchi na vyombo vya habari 



MARA zote, uhuru wa vyombo vya habari ndio umechukuliwa kuwa ni muhimili wa demokrasia katika nchi nyingi ulimwenguni. Kwa kawaida serikali yoyote inayotenda haki kwa wananchi wake, huwa haina haja ya kudhibiti vyombo vya habari katika kuendesha shughuli zake za kutafuta na kupata habari kutoka katika vyanzo mbalimbali, zikiwemo wizara na taasisi nyingine za serikali. Mwandishi RAJABU KANYAMA anaelezea zaidi katika sehemu hii ya nne.
 

WAKATI wowote utakapoona serikali 'imekaza nati' na kuweka vikwazo katika upatikanaji wa habari na usambazaji wake, elewa kwamba serikali hiyo ni ya 'wakuda', isiyotimiza wajibu wake ipasavyo, na kwa hivyo huwa na hofu ya kufichuliwa kwa vitendo vyao vya dhulma na kubainishwa kwa wananchi waliowengi kupitia vyombo vya habari, na kwa sababu hiyo kupoteza umaarufu. 

Umaarufu!! Wanasiasa wengi hapa nchini wamekuwa wakitumia sifa hii kujinyakulia madaraka ya kisiasa hapa nchini tangu tuanze kujitawala mwaka 1961, masuala ya kutimiza wajibu na majukumu ambayo viongozi hao walipewa na wananchi halikuwa ni jambo la kuzingatiwa tena. 

Vyombo vya habari vilisaidia sana katika kujenga umaarufu huo kwa kupitia mbinu za kipropaganda kama vile kuchapisha picha kubwa kubwa katika kurasa za mbele za magazeti zikionesha viongozi fulani eti wakisaidia kulima katika shamba la 'mfumaki' na mapicha mengine ya aina hiyo. 

Na wakati mwingine hupumbaza wananchi kwa kunukuu maneno ya viongozi wa chama wakati ule wa TANU na siku hizi wa CCM na serikali yake hata kama yaliyosemwa hayana maana yoyote zaidi ya ulaghai, wanayakuza na kuyapa maana isiyokuwepo na kisha kuyapamba katika kurasa za mbele za karibu magazeti yote. 

Wakati wote huu malengo huwa ni mawili, la kwanza ni kuwatisha wananchi wasijaribu kufanya mabadiliko kwa hofu ya kusababisha machafuko na lengo la pili ni kuwahadaa ili waendelee kuwa ni nyenzo ya kuwawezesha kushika hatamu ya uongozi. Wakati wa chama kimoja kushika hatamu mambo hayo yalifanywa bila matatizo makubwa kwa vile vyombo vyote vya habari vilikuwa ni miliki ya chama tawala na serikali yake, wakati huo wenyewe wakiviita vyombo vya propoganda. 

Wananchi walitegemea kwamba wakati huu wa mfumo wa vyama vingi vya siasa na vyombo vya habari vya watu binafsi kungekuwepo na mabadiliko kutoka "vyombo vya Propaganda" na kuwa vyombo vya kuelimisha jamii. 

Kwa vile uchaguzi mkuu umekaribia tumeona ni afadhali tukumbushane kwamba haiwezekani kwa mtu, kikundi au chombo chochote cha habari kuweza kudhibiti upeo wa kifikra wa wananchi kwa muda wote, ukweli huu ni kwa sababu uwezo wa mwanadamu wa kutafsiri mazingira yanayomzunguka na tija inayopatikana kutokana kwayo na uhusiano ulipo kati ya yote mawili, mazingira na tija na hali yake ya maisha ya kila siku ni wa milele na kwa sababu hiyo ni lazima wananchi waheshimiwe, na kamwe wasifanywe kuwa ni wapumbavu. 

Wananchi wanataka viongozi walio tayari kushughulikia matatizo ya msingi ya jamii kwa lengo la kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa na kupiga vita dhana ya kuigawa jamii kwa nia ya kuitawala. 

Wana habari, wahariri na wamiliki wa vyombo vya habari, katika mazingira kama haya ni lazima waelewe kwamba wana dhamana na jukumu kubwa mno kwa wananchi, hasa tukizingatia kwamba upo uhusiano wa karibu sana kati ya ukosefu wa habari sahihi, zilizofanyiwa utafiti wa kina na vurugu ndani ya nchi. 

Upashaji habari wa kishabiki usiozingatia mantiki hudumaza fikra za wananchi na kwa hivyo kuwakosesha nguvu na kuwanyima nyenzo ya kuwawezesha kuchangia maoni au kufikia uamuzi sahihi, kwa faida ya taifa. 

Ili kudhibiti kundi la watawala wakuda ni lazima tuwanyime fursa ya kuchochea kutoelewana miongoni mwa jamii, kwa kupasha wananchi sababu halisi za maamuzi yao mbali mbali badala ya kunukuu kila wanachosema hata kama hakina ushahidi. 

Kama wananchi katika nchi nyingi za Kiafrika wangekuwa wanapashwa habari sahihi zinazohusu maisha yao, vita vingi vinavyoendelea katika bara hili vingeepukwa. 

Kwa hivyo basi, uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa kukosoa serikali, na uhuru wa kuweza kufanya mazungumzo na serikali pale maslahi ya wahusika fulani ndani ya jamii yanapokuwa yamepuuzwa, ni mambo mihimu yanayopaswa kupewa kipaumbele katika upashaji wa habari ili kuondoa dhana inayoweza kuzaa chuki ambayo mwisho wake ni umwagaji wa damu. 

Propaganda zinazoendeshwa na serikali mara zote hufanikiwa kama hakuna vyombo huru vinavyobainisha ulaghai huo. 

Vyombo vya habari vinapodharau kuelimisha jamii kuhusu ukweli huo, na mara nyingine kushiriki katika propaganda hizo, ni kuitusi taaluma ya uandishi. 

Bila msaada wa vyombo vya habari, serikali za kidhalimu haziwezi kudumu madarakani. 

Ni vema wananchi wakajulishwa kwamba sababu kama vile kulinda usalama wa taifa na maslahi ya jamii bila maslahi hayo kuainishwa kisheria ndio vichaka vya wakuda wanavyotumia kupiga vita mwamko wa kisiasa ndani ya jamii. 

Inashangaza mno kuona kwamba mapicha, vitabu na magazeti yanayoandika mambo ya ngono hayachukuliwi hatua, lakini panapoandikwa masuala ya kuamsha wananchi ili wajue haki zao za msingi, mara moja utasikia makelele kwamba huo ni uchochezi. 

Wananchi wanapokosa taarifa sahihi na habari za matokeo mbali mbali muhimu ya kisiasa, inakuwa ni vigumu kwao kuweza kutoa uamuzi muafaka kuiwajibisha serikali. 

Ni wajibu wa vyombo vya habari kutofautisha ukweli na kutofautisha maoni au tuseme ndoto za viongozi wa chama cha mapinduzi na kuwajulisha wananchi ipasavyo, vinginevyo bila kujua vyombo vya habari kwa kiwango kikubwa vitakuwa vinachangia katika kupanda mbegu za vurugu katika siku za usoni.Ili kusaidia ujenzi wa demokrasiaya kweli, vyombo vya habari vifanye kazi ya kuelimisha jamii kuhusu haki za binadamu, kuhusu marekebisho ya katiba yenye lengo la kuendeleza ukiritimba wa chama tawala, ubaya wa kuwa na tume ya uchaguzi iliyoundwa na mwenyekiti wa chama tawala, umuhimu wa kulinda kura baada ya kuzipiga, kuhusu njia ambazo wananchi wanaweza kudia haki zao mbali mbali wanazonyimwa na kuwajulisha umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi mkuu. 

Ni lazima sote tuzingatie kwamba mafanikio yetu ya kijamii yanategemea misingi ambayo ni lazima tuijue na tupange matendo yetu kufuatana na misingi hiyo. 

Tujifunze kutoka katika tukio la Wakristo wa Uganda kujichoma moto kwamba kila siku mwisho wa matendo yaliyochochewa na ulaghai ni msiba. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Tume ya Uchaguzi ipigwe msasa, sio wananchi

Mkapa awatahadharisha wanawake  CCM

Lipumba: Wananchi wana uwezo wa kuondoa utawala mbovu 

Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishitaki Serikali

Habari za ndani
Polisi hawana uwezo wa kuzuia mabadiliko’

Sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu kufanyika Dar

MPASHO NASAHA
Hawavumi lakini...

Ushauri Nasaha
Urafiki na makuzi ya mtoto

MAKALA
Toba ya ‘Pope' liwe somo kwa utawala wa Mkapa

WAZO  LA  WIKI
Viva Senegal

MAKALA
Tatizo la ubakaji katika jamii yetu:
Mazingira katika shule zetu

Kalamu ya Mwandishi
Tahadhari isipochukuliwa huenda damu ikamwagika Zanzibar

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (4)

Habari za Kimataifa

Barua

Riwaya
Kisasi cha mauti

Lishe
Baba kulea ujauzito

MICHEZO

  • Ndoa ya Mobitel na Yanga mashakani
  • Homa ya pambano la Ghana na Stars yapanda

  • Makoye: Fedha za Simba nimetafuna mwenyewe 



     
     



       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com



     
     
     
     
     
     
     
     
     
     
     
     

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita