NASAHA
Na. 041 Jumatano Machi 29 - Aprili 4, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Kalamu ya Mwandishi 
 
 

Tahadhari isipochukuliwa huenda damu ikamwagika Zanzibar



NA MAALIM BASSALEH 
 

GAZETI moja kongwe, humu nchini, linalotoka kila siku, limeeleza kuwa Rais Mkapa alipokuwa akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake, juzi Jumapili, tarehe 26 Machi, 2000, huko Dodoma, aliwaonya wanawake nchini, wasiwape kura zao wagombea au vyama vinavyotangaza waziwazi kuwa vitamwaga damu, katika uchaguzi mkuu ujao, wa Oktoba, 2000.

Inaonekana Rais Mkapa alilenga kujibu kauli zilizodaiwa kutolewa na viongozi wa chama cha upinzani cha CUF hivi karibuni, huko Zanzibar. 

Kuna gazeti moja lime mkariri Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, akisema kuwa safari hii chama chake kitaingia katika uchaguzi mkuu ujao kwa mkakati wa "jino kwa jino, na pua kwa pua!!!" 

Pia, kuna na gazeti jingine lililoeleza kuwa Makamo Mwenyekiti wa chama hicho cha CUF,Bwana Shaaban Mloo, amegawa mapanga na mashoka kwa wafuasi wa chama chake ili wajiandae kwa lolote litakalotokea katika uchaguzi mkuu ujao. 

Aidha, gazeti hilo liliendelea kusema kuwa Bwana Mloo aliwaambia wale wanachama waliokosa zana hizo wakazinunue madukani ili wawenazo tayari wakati wa uchaguzi. 

Ama jambo la kugawa mapanga na mashoka si jambo jipya huko visiwani Zanzibar. Ni jambo lililokwisha zoeleka. Chama tawala cha CCM kilianza zamani sana kugawa zana hizo katika maskani zake mbalimbali za Unguja na Pemba. Kwa hivyo CUF ikigawa zana hizo itakuwa inaiiga CCM tu 

Mapanga na mashoka ni zana zinazotumiwa katika shughuli za kila siku. Kwa hivyo kugawa zana hizo kwa wananchi hakuna neno. Lakini linalotia wasiwasi ni kusikia kiongozi wa ngazi ya juu wa CUF akigawa mapanga na mashoka na kuwaambia wafuasi wa chama hicho waziweke tayari zana hizo kwa ajili ya uchaguzi ujao. Na hasa kwa vile chama hicho kimekwisha sema safari hii jino kwa jino!" 

Mwenye kutaka kuziita kauli hizo za Maalim Seif na Bwana Shaaban Mloo kuwa ni kauli za kuashiria shari na za vitisho, hatakosea. Ni kweli kauli hizo ni zenye kutisha sana. Na kwa vile ni kauli zilizotolewa na viongozi wa kambi ya upinzani upande wa utawala unaweza kudai kuwa upinzani umekusudia kufanya machafuko na kumwaga damu katika uchaguzi mkuu ujao. Na watu wanaweza kusadiki! 

Kwa kweli ingawa kauli hizo za viongozi wa ngazi ya juu wa chama cha CUF zinaonekana ni za vitisho; lakini wale waliodaiwa kuzitamka si watu wapuuzi, au watu wajinga wasioelewa uzito wa yale wanayoyasema. 

Kwa kuwa wenye kutamka kauli hizo ni watu makini wanaolijua kila wanalolitamka na kulitenda halitakuwa ni jambo la busara kuzipuuzia kauli zao hizo. 

Kauli hizo hazina maana nyingine yoyote isipokuwa kuonesha kuwa hali ya mambo Zanzibar si shwari. Kama hatua za makusudi na za haraka hazitachukuliwa, kuna kila uwezekano visiwa hivyo vikajikuta vimejitumbukiza katika machafuko makubwa sana. Na moto ukisha waka pana taabu ya kuuzima! 

Basi ni vyema kukinga kuliko kuponya! Njia pekee ya kuepusha shari hiyo isitokee ni kwa pande zote mbili CUF na CCM, kurejea katika mapatano ya mwafaka na kuyatekeleza kwa vitendo. 

Pande zote mbili CCM na CUF, zimekuwa zikilaumiana; kila upande ukiulaumu upande mwingine kwa kuvunja mwafaka huo. Lakini kwa jinsi mambo yanavyokwenda inaonekana kuwa upande unaostahili kubeba lawana ni ule wa chama tawala cha CCM. Kwa nini? 

Ni kwa sababu mwafaka huo ulisimamiwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Chifu Emeka Anyouko. Na hivi sasa mpatanishi huyo ndiye anayeulaumu upande wa CCM kwa kuchelewesha kutekeleza mapatano yaliyomo katika mwafaka huo. Kama katika mpira wa miguu mwamuzi akidai kuwa mchezaji fulani amecheza rafu uamuzi wake ndio unaokubalika; basi na katika mapatano, mpatanishi anaposema upande fulani, kati ya pande mbili zinazovutana, ndio unaokwamisha utekelezaji wa mapatano, kauli yake hiyo ndiyo itakayoshikwa. 

Jee! CCM inalijua hilo? Au imekwisha jiweka tayari kukabili matokeo ya kukataa kutekeleza mwafaka huo? Habari za kuaminika ni kwamba mwakilishi wa Chifu Anyauko, Dkt. Moses Annaf, amekwisha fika nchini, kutaka kujua kama CCM ikotayari kuutekeleza mwafaka huo au la. 

Jee! Kama CCM itajifanya kichwa ngumu na kukataa kuutekeleza mwafaka huo uliosimamiwa na jumuiya ya kimataifa kwa kutoa kisingizio hiki na kile, kama hivi CCM inavyoendelea kufanya, haielewi kuwa itaitumbukiza nchi katika janga kubwa? 

Kwanza, kuna kila uwezekano wa nchi wafadhili kuendelea kusimamisha misaada yao na kusababisha uchumi wa nchi uzidi kuzorota. Tumeshuhudia jinsi miaka hii mitano ya mgogoro iliyopelekea wahisani wazuie misaadayao, na kuviweka visiwa vya Unguja na Pemba katika hali mbaya ya kiuchumi. Jee! CCM imekusudia kuendeleza migogoro? Pili, kama CCM itakataa kutekeleza mwafaka, uchaguzi mkuu ujao hautaweza kufanyika katika hali ya utulivu naamani. Na hata kama CCM itaibuka mshindi katika uchaguzi huo, kamavile ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita wa m,waka 1995, haitaweza kutawala nchi kwa ufanisi. Na hilo liko wazi kabisa. 

Ili kurejesha hali ya utulivu na amani Zanzibar, inabidi uchaguzi ujao ukubalike kuwa ni wa haki na huru. Haitoshi kwa mshindi kufurahia ushindi tu, bali inataka na mwenye kushindwa akubali kushindwa. Na hilo halipatikani isipokuwa pande zote zinazohusika ziridhike na mazingira ya uchaguzi wenyewe. 

Kauli za kishabiki na jazba kama zile zinazotolewa na msemaji wa SMZ zinachangia zaidi kuukuza mgogoro uliopo na siyo kuutatua. Kwa hivyo,zisipewe umuhimuwa aina yo yote, kama kweli ipo nia ya kutaka kuendesha uchaguzu huru na wa haki. 

Msemaji huyo amedaiwa kusema kuwa mapendekezo ya muundo wa Tume ya Uchaguzi yaliyopendekezwa na wataalamu wa ndani na nje ya nchi hayawezi kukubalika kwa vile ati yameonekana yangelileta ushindani na utashi wa vyama vya CCM na CUF ndani ya Tume hiyo ya uchaguzi. 

Na akaendelea kusema kuwa kuukubali muundo uliopendekezwa na wataalamu hao ungelidhoofisha uhuru wa Tume hiyo ambalo ndilo jambo la msingi. 

Jee! Msemaji huyo anataka kutwambia kuwa Tume itakayochaguliwa na pande zote mbili, CCM na CUF, italeta utashi wa vyama hivyo, lakini Tume itakavyoteuliwa, moja kwa moja, na Rais anayotokana na chama cha CCM ndiyo itakuwa haina utashi wa chama chake cha CCM? 

Walilolipendekeza wataalamu ni kuwa Tume mpya ya uchaguzi iwe na wajumbe saba. Wajumbe wawili katika hao wateuliwe na kiongozi wa serikali katika Baraza la Wawakilishi na wajumbe wawili wateuliwe na kiongozi wa upinzani katika Baraza hilo. Na Mwenyekiti wa Tume hiyo lazima awe ni mtu mwenye hadhi ya ujaji unaokubalika na Jumuiya ya Madola. Sasa kuna ubaya gani au kasoro ipi katika Tume kama hiyo? 

Yaani Tume itakayoteuliwa na CCM ndiyo itakayo kuwa ya haki na huru lakini tume itakayoteuliwa kwa mashirikiano baina ya CCM na CUF ndiyo itakayoleta ushabiki? Jee! Hiki si kichekesho cha mwaka? 

Haifai kuongoza mambo, hasa yanayohusu maslahi ya nchi na wananchi kwa kutumia jazba na ushabiki. Uongozi wataka hekima na busara au uadilifu utatoweka! Kiongozi kabla hajanena au kutenda aangalie vyema mustakabali wa maneno na vitendo vyake. Waswahili wamesema, "Majuto ni mjukuu!" 

Kama kweli CCM inania ya kutekeleza mwafaka kwa nini imeshindwa kurekebisha muundo wa mahakama kama ilivyokubaliwa na pande zote katika mapatano ya mwafaka? Jee! Kuboresha muundo wa mahakama ni kwa maslahi ya nani? Ni maslahi ya CUF peke yake au ni maslahi ya wananchi wote? 

Au kwa nini SMZ isiuunde hiyo tume itakayosikiliza madai ya wale wananchi wanaodai kuwa walibomolewa nyumba zao kwa ajili ya kukomolewa tu. Au kwa nini wale wanaodai kuwa wamefukuzwa makazini kwa chuki madai yao yasichunguzwe na ukweli ukajulikana? Kinachofichwa ni nini? 

Kuwalaumu wale wanaotangaza JINO KWA JINO, au wanaogawa mapanga na mashoka kutakuwa hakuna maana yoyote kama mazingira yanayopelekea kuwapo na uhasama hayataboreshwa. 

Sera ya JINO KWA JINO ingawa inatisha lakini hiyo siyo sheria ya Muungu katika Qur'ani na Biblia? Kwa nini basi tuiogope? Mungu ameweka sheria hiyo kuzuia watu kudhulumiana. 

Kama atakayetoa jino la mwenziwe, na lake litatolewa; au atakayelikata sikio la nduguye na lake litakatwa, kila mtu atachunga asimdhuru mwenziwe. 

Hao wanaotangaza JINO KWA JINO wana wasiwasi kuwa watadhulumiwa kwa hivyo ndio wanasema kuwa safari hii hawatakubali kudhulumiwa. Basi njia ya kuondokana na sera za JINO KWA JINO ni kuweka mazingira mazuri ambayo kila mtu ataridhika kuwa hakuna uonevu wala dhuluma. Kama kutakuwapo na hali ya kuaminiana na woga wa kutafunana nao utaondoka. 

Tunawaomba wanaohusika waiepushe nchi yetu na fujo. Ghasia zikitokea hazitawaathiri wanachama fulani tu. Zitawaathiri wafuasi wa CUF na pia wana CCM. Zitawaathiri Wazanzibari wote. Fujo zikitokea hazijui huyu raia au askari. Zitamwelemea kila mmoja. 

Tumeshuhudia ghasia zilizofanyika hivi karibuni, watu 29 walijeruhiwa. Ingawa miongoni mwa wajeruhi hao 15 walikuwa ni raia; lakini 14 walikuwa ni askari. Isitoshe, kwa mujibu wa vyombo vya habari,mmoja wao alifikia hata ya kuvua magwanda yake ya kazi na kuomba aazimwe nguo za mchuuza samaki ili ajisalimishe maisha yake. Basi Tutahadhari kabla ya athari. 
 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Tume ya Uchaguzi ipigwe msasa, sio wananchi

Mkapa awatahadharisha wanawake  CCM

Lipumba: Wananchi wana uwezo wa kuondoa utawala mbovu 

Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishitaki Serikali

Habari za ndani
Polisi hawana uwezo wa kuzuia mabadiliko’

Sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu kufanyika Dar

MPASHO NASAHA
Hawavumi lakini...

Ushauri Nasaha
Urafiki na makuzi ya mtoto

MAKALA
Toba ya ‘Pope' liwe somo kwa utawala wa Mkapa

WAZO  LA  WIKI
Viva Senegal

MAKALA
Tatizo la ubakaji katika jamii yetu:
Mazingira katika shule zetu

Kalamu ya Mwandishi
Tahadhari isipochukuliwa huenda damu ikamwagika Zanzibar

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (4)

Habari za Kimataifa

Barua

Riwaya
Kisasi cha mauti

Lishe
Baba kulea ujauzito

MICHEZO

  • Ndoa ya Mobitel na Yanga mashakani
  • Homa ya pambano la Ghana na Stars yapanda

  • Makoye: Fedha za Simba nimetafuna mwenyewe
     



     
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com



     
     
     
     
     
     
     
     

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita