|
Na. 041 Jumatano Machi 29 - Aprili 4, 2000 |
|
|
|
|
|
Baada ya Mzungu kutimuliwa:
Na Hamisi Kasabe KUNA habari kuwa mkataba ulioitiwa saini hivi karibuni kati ya klabu ya Yanga ya Dar es Salaam na kampuni ya Simu za Mfukoni Mobitel umeanza kulegalega kufuatia klabu ya Yanga kumtimua kocha wao msaidizi Ronny Mintjens. Ronny ambaye ni raia wa Ubelgiji alitimuliwa Jumatatu iliyopita kwa kile kilichoelezwa kutoboa siri ya Yanga kwa viongozi wa timu ya Zamalek ya Misri. Ilidaiwa kuwa Ronny alikutwa na viongozi wa Yanga akiwa amebarizi katika hoteli ya New Africa Jijini kwa zaidi ya masaa mawili na kocha wa Zamalek Mjerumani Otto Ptister siku moja baada ya pambano kati ya timu zao lililomalizika kwa sare ya 1-1 huku akimchambulia udhaifu wa Yanga. Habari zaidi zinasema kuwa Ronny ndiye aliyefanikisha kwa kiasi kikubwa Yanga kupata mkataba wa ufadhili wa Mobitel kutokana na uhusiano wake mzuri na meneja wa kampuni hiyo Muingereza Jim Bell. Imedaiwa kuwa Bell hakupendezwa hata kidogo na taarifa kuwa Ronny ametimuliwa katika jopo la makocha lenye dhima ya kuisuka Yanga. "Kuonesha kutoridhika kwake, Bell alifuta mpango wa kuwasafirisha wachezaji wa Yanga hadi nchini Misri na hivyo kuwafanya kina Tarimba kutafuta fedha sehemu zingine", amesema mpashaji wa habari hizi. Hata hivyo, Yanga ilitarajiwa kuondoka jana alasiri kuelekea Misri kupambana na Zamalek katika mechi ya marudiano ya kombe la Washindi Barani Afrika baada ya viongozi 'kubabatiza' nauli toka kwa wafadhili wengine.
Homa ya pambano la Ghana na Stars yapanda:
ZIKIWA zimesalia siku kumi kabla ya mpambano kati ya timu ya Taifa ya Ghana na Tanzania 'Taifa Stars', wachezaji wa Stars wamekitaka chama cha soka nchini FAT kuwaita haraka wachezaji George Magere Masatu na Said Nassoro Mwamba 'Kizota' kujiunga katika timu hiyo. Wito huo umetolewa na wachezaji hao mwishoni mwa wiki katika mazungumzo ya faragha na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti 'zizini' kwao jeshi la Uokovu Jijini. Wachezaji hao ambao ni washambuliaji, wamenena kuwa wamelazimika kuomba Masatu 'GM' na Kizota 'Baba wa Taifa' waongezwe timu ya Taifa kutokana na walinzi wa timu yao kuonekana kulega lega. Masatu ni mlinzi mahiri wa timu ya Kajumulo World Soccer ya Jijini wakati Kizota ni beki hodari wa timu ya Yanga ya Dar es Salaam. "Kizota na Masatu ni muhimu sana katika timu ya Taifa kwa kuwa ni wazoefu wa mikikimikiki ya mechi za kimataifa ukilinganisha na tulionao sasa", wameongeza. Wachezaji hao ambao walikubali kuongelea suala hilo kwa sharti la kutoandikwa gazetini eti kwa usalama wao wamemtaka kocha mkuu wa timu ya Taifa Mjerumani Bukhard Pape aachwe huru kuwapima Kizota na Masatu kama wanafaa. Hata hivyo, walinzi waliopo sasa Taifa Stars sio wabaya wamesema, ila wanachotakiwa kufanyiwa ni kuongezewa nguvu. Baadhi ya walinzi wa Stars ni Kassim Issa, Omar Kapilima, Kassim Mwabuda, Gerald Hillu, Ally Mayay, Patrik Betwel, John Mwansasu na Alphonce Modest. Wito wa wachezaji wa Stars kwa FAT umekuja kufuatia mechi ya kirafiki ya Kimataifa kati yao na Malawi mwishoni mwa wiki ambapo ilionekana dhahiri beki kukatika kila iliposhambuliwa na Wanyasa. Taifa Stars inatarajiwa kupambana na timu ya Taifa ya Ghana Aprili 8, mwaka huu, katika kutafuta nafasi ya kushiriki katika Kombe la Dunia mwaka 2002.
Makoye: Fedha za Simba nimetafuna mwenyewe
Na Mwandishi Wetu
EPHRAIM Makoye winga wa Kimataifa na klabu ya Yanga ya Dar es Salaam amekanusha habari kuwa fedha alizopewa na klabu ya Simba ya Jijini zimeliwa na viongozi wa klabu yake. Hayo yamesemwa na Makoye ambaye pia ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika sekondari ya Makongo Jijini mapema wiki hii katika mahojiano na gazeti hili. "Ni kweli fedha walizonipa Simba niliwakabidhi viongozi wa Yanga ili wawarudishie viongozi wa Simba na walipozikataa (Simba) nilizichukua na kuzifanyia mambo yangu", amesema. Amesema kuwa kamwe asingekubali fedha zake kuliwa na viongozi wa Yanga hata kama wangenuia kufanya hivyo. Septemba mwaka jana, ilidaiwa Makoye kukabidhiwa shilingi milioni moja
na ushei na klabu ya Simba ili ajisajili kuichezea klabu hiyo katika msimu
huu wa ligi.
|
YALIYOMO
Tahariri
Mkapa awatahadharisha wanawake CCM Lipumba: Wananchi wana uwezo wa kuondoa utawala mbovu Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishitaki Serikali Habari za ndani
Sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu kufanyika Dar MPASHO NASAHA
Ushauri Nasaha
MAKALA
WAZO LA WIKI
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Riwaya
Lishe
Makoye: Fedha za Simba nimetafuna mwenyewe |
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza
hapa
Au
Andika barua kwa: nasaha1420@yahoo.com
|
|
|
|