|
Na. 041 Jumatano Machi 29 - Aprili 4, 2000 |
|
|
|
|
|
Tume ya Uchaguzi ipigwe msasa, sio wananchi MFUMO wa siasa za vyama vingi hapa nchini haukuanza mwaka 1992 kama ambavyo imekuwa ikivumishwa na baadhi ya taasisi za kisiasa hapa nchini. Mfumo huu wa siasa ulikuwepo kabla na mara tu baada ya uhuru kabla ya kupigwa marufuku ili kufikia malengo fulani ya kisiasa ya viongozi waliokuchukua uongozi baada ya uhuru, na kilichofanyika mwaka 1992 ni kuurejesha mfumo huo ukiachwa huru kukuza demokrasia katika jamii husika. Aidha, Watanzania hawajatindikiwa elimu ya uraia kiasi cha kushindwa kupiga kura kwa mujibu wa taratibu halali zinazowekwa (zilizopo). Ingawa ni kweli kuwa wapo wananchi (wapiga kura) ambao hawajawahi kushiriki chaguzi zozote huko nyuma, hawa si mbumbumbu wa kupiga kura kwa vile huwa wanasikia simulizi za taratibu za upigaji kura toka kwa wazazi na wazee wao, wanapata habari kwa kusikiliza redio, kutazama TV, kusoma magazeti na pia katika mtandao wa Internet juu ya chaguzi kadhaa zinazofanyika ulimwenguni. Na pia si sahihi hata kidogo mtu, taasisi au chama cha sisaa kudai kuwa wananchi hawana uzoefu katika upigaji kura. Watanzania wamekuwa wakipiga kura tangu kabla ya uhuru. Tumetanguliza kuyasema hayo kwa sababu zimekwishaonekana 'kampeni ya aina hiyo' ambayo kidogo kidogo wananchi wanalazimishwa kukubali kuwa vyama vya siasa vimeanza hivi karibuni tu, kwamba Watanzania wanahitaji elimu ya uraia kuwawezesha kupiga kura na kwamba wao hawana uzoefu, na hivyo zinatakiwa semina na makongamano 'kuwapika' wananchi. Tunasema kwamba Watanzania hawayahitaji hayo. Watanzania wa leo hawana mapungufu hayo ambayo yanataka kuundiwa semina na makongamano. Watanzania wa leo ni bora katika masuala ya siasa kuliko hata mababu na mabibi zao walioshiriki siasa na chaguzi katika miaka ya 1960. Wananchi katika miaka hiyo ya 1960, mbali na hila za serikali ya mkoloni walikuwa hadhari na taratibu za uchaguzi, na hivyo hata ile hila ya wakoloni kupitisha utaratibu wa kupiga kura tatu haukuwateteresha, walikuwa wakijua ni nini cha kufanya na chama chao cha TANU kilipata ushindi mzuri. Watanzania leo hii wana hali nzuri kuliko hao wa miaka ya 1960. Wana elimu kubwa au zaidi kuliko, ikiwa ni ya darasani au ile isiyo rasmi. Bila shaka kueneza habari hizo kwamba Watanzania hawajaelewa siasa za vyama vingi, kwamba elimu yao ya uraia ni duni na hivyo wanahitaji kufundishwa, na kwamba wapo Watanzania wananchi wasio na maamuzi thabiti kiasi kwamba wanaweza kuhongwa au kuuza kura zao ni vita vya kisaikolojia. Vita hii imelenga kuwafanya wananchi wajione kuwa wao ni 'watupu' na hivyo wakae wakingojea kuelekezwa namna ya kupiga kura kupitia katika semina na makongamano. Tunaamini kwamba yapo mambo ambayo yangefaa zaidi kuzingatiwa na juhudi ya serikali kuelekezwa huko. Katika uchaguzi uliopita, mwaka 1995, ulijitokeza udhaifu katika utendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa. Kwa mfano katika baadhi ya vituo vya kupigia kura palikosekana karatasi za kupigia kura, katika vituo vingine masanduku ya kuwekea kura yalikosekana na hata baadhi ya waliokuwa wamejiandikisha kupiga kura walikosa majina yao katika vituo walivyokuwa wamepangiwa! Matatizo kama haya na mengineyo yalipelekea taratibu za uchaguzi katika mkoa wa Dar es Salaam kuvurugika sana kiasi cha kulazimika kurudiwa kwa zoezi la kupiga kura. Tunadhani haya ndiyo mambo ambayo kwayo serikali 'ingewekeza' nguvu zake kurekebisha kasoro hizo zisijitokeze katika uchaguzi wa mwaka huu na hivyo kuufanya uchaguzi huu kuwa wa haki na huru zaidi. Kuyashughulikia hayo itakuwa ni hatua mojawapo ya kukuza demokrasia nchini. Demokrasia nchini haitakuja kwa utaratibu wa kumtangaza Rais kwa wingi wa kura dhidi ya wenzake (simple majority) au hata kwa mgombea kupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa (absulute majority) tu. Tunaamini kuwa wapiga kura wa Tanzania hawatatishika na vita hivyo vya kisaikolojia, wala utajiri wa chama fulani, au ukongwe katika madaraka wa chama fulani. Tayari Watanzania wamezipata salamu toka Taiwan ambako chama cha siasa cha KTM kinachoaminika kuwa ni tajiri zaidi duniani kimepigwa mweleka. Kadhalika Watanzania wanazo salamu toka Senegal ambako chama kilichokuwa madarakani toka uhuru (miaka 40 iliyopita) kimepokonywa uongozi katika uchaguzi wa kidemokrasia. Leo hii Taiwan na Senegal wanazo serikali mpya chini ya vyama vipya. Tunachosema ni kwamba ili tupate uchaguzi wa kidemokrasia Watanzania wasijengwe hofu, vita ya kisaikolojia iepushwe dhidi ya wananchi na haki yao. |
YALIYOMO
Tahariri
Mkapa awatahadharisha wanawake CCM Lipumba: Wananchi wana uwezo wa kuondoa utawala mbovu Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishitaki Serikali Habari za ndani
Sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu kufanyika Dar MPASHO NASAHA
Ushauri Nasaha
MAKALA
WAZO LA WIKI
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Riwaya
Lishe
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza
hapa
Au
Andika barua kwa: nasaha1420@yahoo.com
|
|
|
|