NASAHA
Na. 041 Jumatano Machi 29 - Aprili 4, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA

Toba ya 'Pope' liwe somo kwa utawala wa Mkapa

Na Mwijilisti Kamara Kusupa 

PAPA Yohane Paulo wa Pili ameomba msamaha kwa mabaya yote yote ambayo yametendwa na Kanisa Katoliki kama taasisi hasa katika milenia ya pili. Kwa maneno mengine ni sawa na kusema Papa ametubu, ameungama na kukukiri hadharani kwa yote yale yasiyo haki ambayo Kanisa lilifanya kwa nyakati mbalimbali yaani hata mabaya yale yalitotendwa karne nyingi kabla yeye 'Pope' hajazaliwa. Nia na madhumuni ya kufanya hivyo anaijua vyema yeye Papa, na lengo la toba yake analielewa mwenyewe. Lakini hata hivyo toba ya Pope, mbali na kuacha maswali machache nyuma imemfanya Pontif Yohana Paulo wa pili kuwa muungwana nambari wani tangu kuanza kwa milenia hii ya tatu.
 
 

KUKIRI kosa kunahitaji ujasiri, ndio maana wanaadamu wachache sana wanaoweza kusema "ni kweli tulikosea". Mwaka jana Rais Clinton alifanya ziara katika nchi kadhaa za kiafrika na alipokuwa Ghana alifanya kitu kinachofanana na toba ya Papa kwa kusema: "Kuendesha biashara ya utumwa sisi tulikosea". Kukiri kwa Clinton ni kwa kinafiki kwa sababu ziara yake katika Afrika ilikuwa ni kusimika kizazi kipya cha madikteta ambao kupitia kwao, wazungu watafanikisha mfumo mpya wa utumwa duniani na Mwafrika atafanywa mtumwa ndani ya nchi yake, kwa hiyo ukiri wa namna hiyo hatuwezi kuuita toba wala kuufananisha na ukiri wa Papa. Kanisa Katoliki limefanya maovu mengi dhidi ya ubinaadamu ikiwa ni pamoja na kuibariki biashara ya utumwa, kuukubali mfumo wa utumwa hata baada ya biashara ya utumwa kukomeshwa katika Afrika, na dhambi ya hivi karibuni ya kushirikiana na utawala wa kibaguzi wa makaburu ambao walifikia kiwanmgo cha juu kuhalalisha 'apartheid' kwa kutumia vifungu vya Biblia (Neno la Mungu). 

Wakati utawala wa Papa unashirikiana mia kwa mia na utawala wa kibaguzi wa makaburu, dunia haikumlaumu Papa, badala yake ilimstahi na kumnyamazia wakati serikali za nchi nyingine kama Malawi zilibanwa na kusutwa hadharani kutokana na uhusiano wake na makaburu. 

Lakini pia utawala wa Papa umekuwa na uhusiano mzuri na utawala wa Tanzania tangu siku za uhuru, hasa enzi za Papa Paul wa Sita. Mnamo miaka ya sabini hadi themanini wakati rais wa wakti huo, Hayati Nyerere, alipotangaza siasa ya ujamaa na utaifishaji, nchi za magharibi zilimsusia, hazikutoa msaada kwa wingi, chuki yao iliongezwa na harakati za ukombozi kusini mwa Afrika, zilizoendeshwa hapa nchini Tanzania. Kwa hiyo ni wakati huo ambapo Vatican ilibakia mfadhili pekee mkubwa wa nchi hii baada ya nchi za Nordic na Skandinavia. Kutokana na kuifadhili serikali, Kanisa nalo lilipata upendeleo wa kipekee tofauti na makanisa na madhehebu mengine ya kikristo. 

Hata kama haikutangazwa wazi wazi ukweli ni kwamba kulikuweko na sera ya kufadhiliana kati ya Kanisa Katoliki na Serikali. Huko serikalini mtu huwezi kufananisha au kulinganisha uzito wa Kanisa katoliki na makanisa mengine kama Pentekoste. Sasa ngoma iko uwanjani, ikiwa Kanisa, chombo kinachohesabiwa kuwa kitakatifu, linakiri makosa, kumbe si zaidi ya serikali au chama tawala? 

Katika muda wake wa miaka 40 ya kutawala, TANU/CCM imefanya madhambi lukuki, dawa ya dhambi ni kutubu, kuungama hadharani na kuziacha. Kwa mtu mjinga kukiri makosa ni sawa na kujiaibisha, kujifedhehesha, na kudhihirisha udhaifu, lakini kwa muungwana kukiri kosa ni sehemu ya ushujaa na utu wema. 

Kukiri makosa yaliyotendwa hadharani au yaliyotendwa dhidi ya halaiki ya watu, ni njia mojawapo ya kuleta upatanisho na pia kutibu tatizo la majeraha ya rohoni, maana kama kuna watu walioumizwa na makosa hayo basi kukiri ni njia mojawapo ya kuganga majeraha yao. Kwa mfano, nchini Afrika ya Kusini kwa miaka zaidi ya mia tatu Waafrika (weusi) walinyanyasika na sheria za kibaguzi, watu waliuawa, watu waliumizwa roho kutokana na kukiukwa kwa haki zao za msingi, kwa hiyo kulikuwa na donge au shina la machungu mioyoni mwa watu, yaani 'bitterness' kwa kiwango cha kutisha. 

Mara baada ya Waafrika kupata uhuru wao njia pekee iliyokuwa imebakia ya kudumisha amani ni kufanya upatanisho. 

Askofu Mkuu, Desmond Tutu, alichaguliwa kuiongoza tume ya ukweli na upatanishi, ambayo kazi yake ilikuwa ni kuhakikisha kwamba makosa makubwa au matendo yoyote mabaya yaliyofanywa na mtu au taasisi enzi ya utawala wa kibaguzi na mapambano ya wapigania uhuru ambayo kwa kiasi fulani yalimuumiza mtu au watu yanawekwa hadharani. Askofu Tutu alipoulizwa faida ya tume yake ilikuwa nini ikiwa ilikuwa inahoji watu bila ya kuwapeleka mbele ya sheria, yeye alijibu kwamba wanafanya hivyo ili kuhakikisha kwamba yaliyotendwa hayarudiwi tena milele. 

Hadi sasa utawala wa Mkapa bado una mvutano na Waislamu kuhusiana na mauaji ya Mwembechai. Suala hili lilianza na wachache, lakini sasa linapata mshiko nchi nzima, nadhani uchungu walionao baadhi ya Waislamu unachochewa na majibu ya Serikali na hasa majibu binafsi ya Mkapa mwenyewe kuhusiana na hicho wanachokidai. 

Kwake Mkapa, kama mtawala mkuu wa nchi, majibu yenye jeuri kutoka kwake au watendaji wake hayamsaidii kabisa wala kauli zisizo na staha kama za Makamba kusema Waslamu watapataje madaraka ilhali hawakusoma, sio jibu la tatizo lililopo, badala yake kauli za namna hiyo zinadhihirisha 'arrogance' au ulevi wa madaraka ulioko serikalini. Kinachotakiwa sasa sio uimara wa serikali kudhibiti watu bali upatanisho au 'reconcilliation' ili kuzuia chuki na uhasama kuenea katika jamii. Hatutaki yatokee mambo yaliyoikumba Nigeria hivi karibuni, tukumbuke ya kuwa Wanigeria sio wajinga hadi kukumbwa na tatizo la chuki na uhasama katika jamii yao. Wao ni wasomi kuliko sisi, wao ni tajiri kulko sisi, lakini wamekumbwa na janga hilo kwa sababu janga hupata nafasi kabla ya kutokea. Siku zote uhasama hauneshi kama mvua itokayo juu, bali unachochewa na kukua kama mmea. Ni juu ya Rais Mkapa kuing'oa mbegu mbaya kabla haijachipua na kama ilikwisha ota mizizi basi mizizi hiyo ing'olewe na mti huo ukatwe na shoka kama lile lililotajwa katika injili ya Yohana Mbatizaji. Mkapa inabidi awasikilize Waislamu kwa umakini wa hali ya juu na kwa mtazamo uliopevuka ambao hauna jazba wala usiotoa maamuzi ya haraka. Sababu kuu ya kusema hivyo ni hii; katika elimu ya sayansi ya jamii kuna usemi kwamba "hakuna kundi dogo". Ingawaje utawala wa Mkapa unaweza kujidanganya kwamba sio Waislamu wote wenye lugha kama Issa Ponda au Sheikh Mbukuzi, lakini ukweli ni kwamba maadamu kauli zao ni kwa niaba ya watu basi hapo hakuna kundi dogo. Zaidi ya yote, ndani ya madai yao kuna mantiki, haitoshi kukanusha tu kwa kusema madai yao hayana ukweli. Kwa hiyo ili kuondoa mzizi wa fitina, utawala wa Mkapa ungejifunza kutoka kwa Papa na kuvaa roho ya unyenyekevu badala ya ubabe, ikubaliane na dai lao la kuundwa kwa tume ya ukweli ya upatanisho, (kama ile ya Afrika ya Kusini), tume hiyo isiswe ni ya kuchunguza mauaji ya Mwembechai tu, bali iwe ni tume ya kuchunguza nchi nzima kupata ukweli kama Uislamu ulikandamizwa au unakandamizwa hadi sasa, ama hisia tu zisizokuwa na uhalisi wowote. Jawabu la tume ndilo awapelekee Waislamu na hilo linatosha kukata mzizi wa fitina. Kwa mfano kama tume itaona kwamba madai ya Waislamu kunyimwa haki za msingi kikatiba, kisiasa au kijamii si kweli, basi jibu halitakuwa ni jibu la Mkapa bali ni jibu la Kisayansi lililotokana na utafiti (uchunguzi) wa uhakika. Lakini kama tume itagundua kwa njia moja au nyingine kwamba Waislamu wa nchi hii walionewa aidha katika kipindi cha serikali ya Nyerere, au serikali ya Mwinyi, au serikali ya Mkapa mwenyewe, basi Rais Mkapa atakuwa hana budi kufuata nyayo za kiongozi wake wa kidini, yaani Papa , na kukiri kwamba kweli serikali ilifanya vibaya na kuhakikisha kwamba mianya yote iliyoruhusu uonezi inazibwa ama inaondolewa sawa na alivyoishughulikia sasa mianya ya rushwa baada ya kupokea jibu kutoka kwenye tume ya Warioba. 

Dai la kutaka iundwe tume sio baya wala halina hatari yoyote kwa kuwa tume hiyo haiundwi ili kuwahukumu watu ama kuwaadhibu bali ni tume ya kuthibitisha uongo na ukweli wa mambo, ili hatimaye haki iweze kutendeka, sasa sioni sababu za kumfanya Mkapa aogope kuunda tume hiyo alimradi tu tume hiyo ipewe "terms of reference" au hadidu za rejea zenye mambo ya msingi na pia tume yenyewe iwe ya watu makini wasiokuwa na "biasness" (uegemeo) wowote kwa watawala wala kwa Waislamu. Mpaka sasa Mkapa aliisha unda tume kadhaa ambazo zilikuja na jawabu lililo tofauti na matakwa ya serikali, hata hivyo serikali haikuathirika. 

Nakumbuka tume ya Nyalali ilieleza mambo ya kutisha kuhusu operesheni za usalama wa taifa na kutoa mapendekezo yake, hali hiyo ingawa haikutibu mia kwa mia tatizo, lakini walau iliweza kuwafariji wale walioathirika na operesheni za idara hii, na kuwapa matumaini ya kufidiwa. Tume ya Warioba iliwapa watu matumaini ya haki na hata baadhi ya nchi wafadhili zilirudisha imani yao pale ilipoweka bayana mianya ya rushwa. Tume ya Jaji Kisanga imeweka wazi dosari zilizo kwenye muungano na mfumo wa uchaguzi na kutoa mapendekezo yake. Ingawa Mkapa mwenyewe hakuyaafiki lakini ni mapendekezo hayo ndiyo yanayowapa watu tumaini la kuvumilia kwa matarajio kwamba huenda siku za usoni mambo yanaweza kuboreshwa, vinginevyo kama masuala yote niliyoyataja hapo juu yangenyamaziwa aidha kwa kupuuza au kwa kuogopa ukweli usijulikane kama serikali inavyonyamazia dai la Waislamu kuunda tume, huenda kimya cha serikali kingekuwa kimesababisha watu kuchukua hatua wao wenyewe badala ya serikali. 

Mkapa asione haya kutubu kwani kwa miaka arobaini ambayo chama chake kimeshika serikali kuna mengi amayo yamefanyika, mengine mazuri, mengine mabaya. Kwa yale mema yaliyofanyika Mkapa anayo haki ya kujisifia, na kwa yale mabaya Mkapa ana wajibu wa kuyaungama na kuhakikisha hayarudiwi tena. 

Ikumbukwe kwamba wenye manung'uniko juu ya utawala wa nchi hii sio Waislamu peke yao, bali yapo makundi mengine, isipokuwa makundi hayo bado hayajapata watu (viongozi) walioamua kusema hadharani kwamba wamedhulumiwa haki zao. Mfano hai ni wanajeshi wetu. Nidhamu ya kazi yao hairuhusu manung'uniko ya hadharani wala maandamano mara haki zao zinapokiukwa. Miaka ya nyuma ni askari wengi waliopelekwa nchi za kusini kupigana, wengine walikufa, wengine walijeruhiwa lakini hadi leo hii hakuna fidia. Aidha maisha ya askari wetu ikiwa ni pamoja na polisi, Magereza na JWTZ ni ya kutisha. Wana dhiki inayozidi kawaida, isipokuwa hawana jukwaa au "forum" ya kutolea kilio chao. 

Nao watu wa kusini wana manung'uniko yao. Wanadai kwamba serikali ya TANU na hatimaye CCM iliwakandamiza na kuwadumaza kimaendeleo ikilinganishwa na kaskazini ingawaje kusini kuna utajiri mwingi. 

Wengine wanadai kwamba serikali haikuendeleza kusini kwa sababu watu wa kusini ni wagumu sana kutawalika na kihistoria inathibitisha hivyo toka enzi za wajerumani hadi harakati za kudai uhuru, hivyo basi kama kusini ingekuwa na maendeleo kama yaliyopo Kilimanjaro na Arusha huenda ingekuwa hatari. 

Vivyo hivyo Wahaya nao wana malamiko kwamba pamoja na kusoma kwao serikali iliwatenga na kuwanyima nyadhifa kubwa kama za uwaziri, wanadai ni Rwegasira tu ambaye kwa bahati mbaya aliteuliwa kama Waziri kamili tangu atoke Barongo aliyefikia unaibu. 

Mambo kama haya yakisemwa hadharani tena kwa nguvu zote yanaweza kuonesha kama ni uchochezi lakini ndani yake kuna mantiki. Kwa kweli Kagera baada ya vita ilistahili kunufaika na malipo ya fidia (aliyoyatoa Museveni) kabla ya maeneo mengine au hata kabla ya Wizara ya Mambo ya Nje. 

Wa Kigoma nao wana yao ya kusema, tena mengi kiasi kwamba ukurasa hautoshi, labda kitabu. Mikoa ya kati nayo ina manung'uniko. Serikali iliwafanya "Wadodoma" kama maabara ya kujaribishia yote yanayohusu ujenzi wa ujamaa na matokeo ya majaribio ni huo umaskini walionao wagogo. Tofauti yake ni kwamba wagogo hawajampata Issa Ponda wao, au Mbukuzi wao wa kusema bila hofu hadharani. Kwa ajili hiyo ndiyo maana nasema madai ya kuunda tume yana msingi kwani yatasaidia kuupata ukweli na kurekebisha mambo ili kuinusuru nchi isitumbukie kwenye jamga la uhasama au chuki miongoni mwa watu wake. 
 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Tume ya Uchaguzi ipigwe msasa, sio wananchi

Mkapa awatahadharisha wanawake  CCM

Lipumba: Wananchi wana uwezo wa kuondoa utawala mbovu 

Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishitaki Serikali

Habari za ndani
Polisi hawana uwezo wa kuzuia mabadiliko’

Sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu kufanyika Dar

MPASHO NASAHA
Hawavumi lakini...

Ushauri Nasaha
Urafiki na makuzi ya mtoto

MAKALA
Toba ya ‘Pope' liwe somo kwa utawala wa Mkapa

WAZO  LA  WIKI
Viva Senegal

MAKALA
Tatizo la ubakaji katika jamii yetu:
Mazingira katika shule zetu

Kalamu ya Mwandishi
Tahadhari isipochukuliwa huenda damu ikamwagika Zanzibar

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (4)

Habari za Kimataifa

Barua

Riwaya
Kisasi cha mauti

Lishe
Baba kulea ujauzito

MICHEZO

  • Ndoa ya Mobitel na Yanga mashakani
  • Homa ya pambano la Ghana na Stars yapanda

  • Makoye: Fedha za Simba nimetafuna mwenyewe 



     
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com



     
     
     
     
     
     
     
     

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita