NASAHA
Na. 041 Jumatano Machi 29 - Aprili 4, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Lishe 

Baba kulea ujauzito 

CHAMOS, H.J 

TUNAPOZUNGUMZIA lishe, hatuna budi kuigawanya katika makundi mbalimbali kulingana na mahitajio. Mahitajio ya vyakula kamwe hayalingani kwa watu wote, bali hutofautiana kutegemeana na umri, kazi, ukubwa wa mwili, haliya mwili, hali ya hewa n.k. Kwa kulifahamu hilo, mama mjamzito anapewa nafasi yake ya "mtu maalum" katika familia, anayehitaji lishe maalumu. Kabla ya kufahamu lishe yake tuiangalie nafasi ya baba wakati wa ujauzito wa mama.

Hakuna mjadala, ya kwamba hakuna mimba pasi na kuwepo baba. Hata kama mimba itapandikizwa maabara, lakini lazima baba yake yuko mahala fulani duniani. 

Jambo la mwanzo kabisa ambalo baba anapaswa kufanya ni kukubali ujauzito. Bila ya kuikubali mimba kamwe hawezi kuwa mshirika mzuri katika kuilea. Wajawazito wengi huudhoofika kwa kukosa lishe bora kwa sababu ya kukataliwa na waume zao. Hili hasa huwapata wasichana wadogo walioowana na wavulana. Na kwa wale ambao hawajui mimba ni ya nani, hapo kwa kweli ni msiba mkubwa! Usibebe kitu cha mtu usiyemfahamu. Kwa kinababa, punguzeni hila zisizo na msingi, wapendeni na kuwaamini wake zenu. Kama humwamini ni bora umwache kuliko kumpa mimba na kisha kuikataa. Kwani hapo utakuwa unaongeza idadi ya watoto wa mitaani. Na tunapenda kusisitiza kuwa wanawake, kwa mujibu wa Uislamu, hawatakiwi kuzaa au kushiriki ngono mpaka waolewe. 

Ama baada ya kuikubali mimba,baba ashirikiane na mkewe kujiandikisha katika hospitali au kituo cha afya kwa muda muafaka. Vilevile kufuatilia rekodi za vipimo kila anapokwenda hospitali. Hata kama hutaenda nae, lakini unaporudi nyumbani huna budi kuisoma kadi na kuelekezana na mkeo maagizo ya daktari. 

Mama mjamzito ni mtu maalum anayehitaji matunzo maalum. Hili hufanyika kwa wale wanaofahamu umuhimu huo! 

Matunzo maalumu hapa tuna maana ya lishe bora. Yaani mama mjamzito anapaswa kula zaidi ya vile alivyokuwa akila awali. Na pia kuongeza aina fulani ya vyakula zaidi kuliko watu wengine, kama vile vyakula vyenye madini ya chuma, madini ya chokaa, madini ya joto, vitamini A, n.k. Baba anapaswa kusisitiza na kufuatilia ulaji wa mkewe. Pale inapotokea mama kushindwa kula, baba ana nafasi ya pekee ya kumbembeleza mkewe ili ale. 

Mama mjamzito anatakiwa apunguziwe mzigo wa kulea familia. Baba anapaswa kuhakikisha familia inajitosheleza kwa chakula na mahitaji mengine. Iwapo mama ndiye mtafutaji, basi nafasi yake haina budi kuzibwa na mtu mwingine katika familia. Mahitaji tuliyoyataja hapo juu ni yale ya kawaida kama vile ya utafutaji wa chakula, mavazi n.k. 

Baba hana budi kumpunguzia mkewe kazi ngumu alizokuwa akizifanya kabla ya ujauzito. Mathalani kubeba mizigo mizito, kuponda mawe, kulima (sana), kutwanga, kuchota maji umbali mrefu, kupika nyakula vya watu wengi n.k. Baba anawajibu wa kuwaelimisha wanafamilia umuhimu na ulazima wa kumsaidia mama. Kama hapana budi basi awepo msaidizi maalumu atakayechukua nafasi yake katika kazi muhimu. 

Baba ajitahidi kushiriki chakula pamoja na mama angalau mara moja kwa wiki, kama ni mwenye shughuli nyingi katika kila siku za maisha yao!! Baba hatakiwi wala hastahil kuamua tu kutoonekana nyumbani hasa katika kipindi cha mama kuwa mjamzito bila ya sababu zozote za msingi, kwani jambo hili humuathiri sana mama kisaikojiia. Baba anatakiwa atafute angalau hata siku moja katika wiki ya kushinda nyumbani na kula pamoja na wanafamilia. Kamwe huwezi kufuatilia ulaji wa mkeo iwapo hata hufahamu anakula vipi, na unatakiwa umbembeleze mkeo kula vyakula muhimu ambavyo hajisikii kuvila, au akivila anatapika. Kwani maneno matamu huweza kumaliza kichefuchefu. Maneno mazuri siku moja kwa wiki ni bora zaidi kuliko kero ndogondogo za kila siku. Mathalani badala ya kusema kula bwana, sisi tumepika halafu we unaringa kula, waweza kusema, "Mtoto tumboni anahitaji chakula hiki zaidi kuliko unavyofikiria." 

Baba anapaswa kuwa mpole na mtaratibu zaidi kuliko siku zingine za kawaida. Awe mvumilivu sana kwani wajawazito wakati mwingine huwa wanaudhi. Kwa mfano, wajawazito huweza kukasirika, kulia au hata kununa bila sababu yoyote ya msingi. Baba asipokuwa na subira, siku zote, zitakuwa ni za ugomvitu na hapatakuwa na masikilizano. 

Kuna mifano ya familia ambazo zilisambaratika wakati wa ujauzito na kuwa ni majuto baada ya kujifungua. Wakati mwingine mama mjamzito humchukia kabisa baba. Lakini hii ni kwa muda tu na hutoweka baada ya kujifungua. Hivyo basi baba huhitajika kuwa mvumiluvu kupita kasi na kamwe asimkimbie mkewe, bali awe naye karibu akimuuliza maswali madogo madogo yenye kitia moyo. Mara kwa mara wajawazito huwa na homa za hapana pale, hivyo baba awe msitari wa mbele kumfariji. Ni ajabu kuwa baadhi ya mababa huamua kuwapeleke wake zao kwao, kwa sababu ya maradhi madogo madogo; hata kutapikatapika. Hilo ni jukumu lenu na si la wengine. Mleane na kufarijiana. 

Msingi mzuri ndio mwanzo mzuri wa nyumba imara. Mtoto mwenye afaya bora na maendeleo mazuri hutokana na mama mwenye matunzo na lishe bora. Shime kina baba fahamuni nafasi yenu. 
 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Tume ya Uchaguzi ipigwe msasa, sio wananchi

Mkapa awatahadharisha wanawake  CCM

Lipumba: Wananchi wana uwezo wa kuondoa utawala mbovu 

Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishitaki Serikali

Habari za ndani
Polisi hawana uwezo wa kuzuia mabadiliko’

Sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu kufanyika Dar

MPASHO NASAHA
Hawavumi lakini...

Ushauri Nasaha
Urafiki na makuzi ya mtoto

MAKALA
Toba ya ‘Pope' liwe somo kwa utawala wa Mkapa

WAZO  LA  WIKI
Viva Senegal

MAKALA
Tatizo la ubakaji katika jamii yetu:
Mazingira katika shule zetu

Kalamu ya Mwandishi
Tahadhari isipochukuliwa huenda damu ikamwagika Zanzibar

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (4)

Habari za Kimataifa

Barua

Riwaya
Kisasi cha mauti

Lishe
Baba kulea ujauzito

MICHEZO

  • Ndoa ya Mobitel na Yanga mashakani
  • Homa ya pambano la Ghana na Stars yapanda

  • Makoye: Fedha za Simba nimetafuna mwenyewe
     



     
     



       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com



     
     
     
     
     
     
     
     
     
     
     
     

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita