|
Na. 041 Jumatano Machi 29 - Aprili 4, 2000 |
|
|
|
|
|
Viva Senegal NA Y. KIJUKUU Ni furaha kubwa iliyoje kuwakaribisha tena wapendwa wasomaji wa safu hii ili tuiangalie nchi yetu Tanzania na dunia kwa ujumla, jinsi zinavyokwenda. Tukosoe na tusifie kwani hivyo ndivyo miongoni mwa vipimo vya uungwana. Leo tuangalie kwa uchache funzo linalopatikana kutoka kwa mashujaa wanamapinduzi wa Senegal. Ikiwa ni juma moja tu tokea dunia ishikwe na mshangao pasipo na kwanini kile kilichotokea kule Senegal, ni vema wananchi wa Tanzania na Afrika kwa jumla tukashikanana kuutoa ule unaoonekana kuwa ni udhalimu nambari moja kwa kushirikiana bila kujali tofauti zetu. Watanzania lazima tuelewe kuwa wananchi wa Senegal ambao wameamua kuacha yaliyozoeleka na kufanya yanayotakikana kwa kuutoa madarakani utawala mkongwe, kwenye mizizi kuliko huu wa CCM, ni watu wa kawaida kabisa na wala hawakuhitaji wingi wa digrii kuchambua na kuziondoa mbovu za Rais Abdou Diouf na kuziweka mbivu za Bwana Wade. Hili la Wasenegali ni vema likafuta dhana potofu kuwa mizizi ya CCM iliyopo nchini haiwezi kukatika kwani wenzetu wameung'oa mti kama huo ambao umeshamiri kwa miaka 40, sasa vipi ushindikane huu CCM ambao una umri wa miaka 39 tu. Kuing'oa CCM madarakani kunawezakana kama nia tunayo. Nasema hivi kwa kuwa uwezo wa kutoipigia kura za ndiyo tunao na sababu madhbuti za kufanya hivyo tunazo. Kwani ni wangapi wasiotambua uovu wa CCM nchini, tukiachilia mbali makada ambao wanaamua kuufumbia macho uovu huo? Sote ni mashahidi waonjao 'joto ya jiwe' kwa utawala huu mbovu ambao mwana CCM mashuhuri hayati Kolimba ameuita kuwa ni utawala usio na dira, hivyo ni vipi Watanzania sisi tunakubali tena kwa hiari yetu kuendelea kusafiri ndani ya chombo hiki kisicho na mwelekeo, tusichofahamu wapi kitatufikisha? Hakuna chochote bali huu ni uzembe. Nasema huu ni uzembe siyo kwamba ninalenga kuwatukana Watanzania, bali ni kutokana na uchungu dhidi ya mdidimio wa taifa letu katika nyanja zote yaani kichumi, kijamii na kisiasa huku wenye Taifa lao wakitambua hilo bila kujali, wakati wenzetu Wasenegal wanapiga hatua. Hata hivyo, kwa sasa sioni kama kuna haja kubwa ya kulaumiana kwa linalotupata, bali ni vema tukaziba mianya yote ambayo kwa namna moja au nyingine ndiyo iliyotufikisha huku tuliko, ili tuwafuate Wasenegali kule waliko tena si kwa kutembea bali kukimbia bila 'luku'. Moja ya mianya ni ule wa watu wachache kuamua kuzua tafrani ndani ya jamii ili kukidhi njaa zao kwa wao kuonekana wabora kwa watawala na hatimaye kuwekwa katika meza kuu ya wakuu (high table) kwa kipindi fulani huku wakijaza matumbo yao pasipokujali ni kwa jinsi gani wanalididimiza Taifa. Wenye tabia hiyo ya kupenda 'high table' kwa kuwasaliti wengine, nahisi ndicho kikwazo kikubwa dhidi ya kuung'oa utawala huu mbovu. Lau kama wapendwa wanamapinduzi wa Senegal wangelikuwa na tabaka hili la wapenda 'high table', basi kamwe wasingelimudu kuung'oa utawala ule. Aidha katika kipindi hiki kinachoonesha mwelekeo bora wa kimapinduzi, ni vema wanasiasa wa upinzani wa Tanzania wakawaiga wenzao wa Senegal na kuanza kufanya kazi ili kutuletea mabadiliko ya utawala ambao huenda ukabadili uvundo huu wa maisha ya kila siku ya Mtanzania. Achaneni na umimi wa kupenda 'high table' huku mkizua majungu na fitna ndani ya siasa. Ni vema mkamtafuta haraka mwakilishi bora mnaomuona anakubalika na wananchi mumsimike ili tumpe kura zetu kama walivyofanya Wasenegal kwa Bwana Wade. Nimalizie kwa ukweli ulio wazi ya kwamba ili tufikie walikofika wenzetu kila mmoja yaani wananchi wapiga kura kwa upande mmoja na wanasiasa wa upinzani kwa upande mwingine, tunao wajibu mkubwa wa kuifikisha nchi pazuri. Wanasiasa wa upinzani wayaseme ya kisiasa tena peupe bila kuhofu lolote huku wakiimarisha umoja na mshikano ndani ya upinzani. Wakati huo huo wananchi waachane na propaganda za chama tawala, wayasikie ya wapinzani huku wakichunguza ukweli kisha wajiandikishe na hatimaye kupiga kura kwa wingi. Kwa mtaji huo nasema tutaung'oa utawala huu uliotuletea na kutuendelezea umaskini mkubwa na tutamsimika 'Wade' wa Tanzania angare katika kiti cha enzi alete mabadiliko. Lakini endapo Watanzania wataweka pamba masikioni mwao wakati wapinzani 'wanapopasua' ukweli dhidi ya udhalimu, basi hatutofika popote. Tulio wengi tutaendelea kula tunachokipata kwa wakati wowote tunapokipata, wakati 'mabwenyenye' wachache wakiendelea kutesa kwa kula wanachokitaka kwa wakati wanaoutaka. Haya sasa tumeshapashwa Jangwani hivi juzi tu kuwa mauzo ya NBC ni kituko tu. Umati wa Watanzania unalalama kuwa dhiki ya maisha, miundo mbinu haitamaniki, tazama jiji muhimu la Dar es Salaam limegeuka choo kwani linanuka popote upitapo na ubadilifu haupo kwa watendaji wa serikali dhidi ya raia zake. Shime Watanzania, 'high table' zinanuka ubadhilifu ingawa hamtambui,
tushikamane, tushikane mikono, tuinue juu na tuseme, "Viva Senegal Viva".
|
YALIYOMO
Tahariri
Mkapa awatahadharisha wanawake CCM Lipumba: Wananchi wana uwezo wa kuondoa utawala mbovu Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishitaki Serikali Habari za ndani
Sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu kufanyika Dar MPASHO NASAHA
Ushauri Nasaha
MAKALA
WAZO LA WIKI
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Riwaya
Lishe
Makoye: Fedha za Simba nimetafuna mwenyewe |
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza
hapa
Au
Andika barua kwa: nasaha1420@yahoo.com
|
|
|
|