|
Na. 041 Jumatano Machi 29 - Aprili 4, 2000 |
|
|
|
|
|
Hawavumi lakini... Na Abu Halima Sa Changwa SIKU chache zilizopita,kama kawaida yangu nilipitia meza za wauza magazeti ili angalau kuangalia kama kuna chochote cha kununulika. Nilikuta magazeti ya jioni mawili tofuati yakiwa yana picha ya niliyedhani kwamba, kama si mtoto mdogo, basi ni mwehu mwanamke, kwa sababu katika picha mojawapo mwanamke huyo huyo alikuwa ametokea kavaa ama ni kichupi au nepi, na katika gazeti jingine alikuwa kama kachutama hivi lakini ima ni nepi au chupi ilikuwa ikionekana. Nilipopitisha jicho kudokoa habari zake nikaambiwa yeye ni mwanamuziki toka Kusini ya Afrika. Gazeti mojawapo lilimwita "mchizi", ambalo nijuavyo mimi ni lugha ya mtaani yenye maana ileile ya mwehu. Siku moja baadaye nilisoma gazeti jingine lililokuwa na habari za huyu dada, zikieleza miongoni mwa mambo mengine kwamba uchangamfu wa mtu hunogeza mambo yakawa mazuri hata kama nyimbo zake sio nzuri. Kwa hiyo dada huyu alikuwa akikonga nyoyo za watu, sio kwa nyimbo nzuri, wala sura nzuri(maana mimi sikuona kama anayo), bali uchangamfu. Uchangamfu wenyewe, nadhani, ni ule wa kuacha nepi zake wazi watu wakamuona. "Mchizi" huyo, yaani mwehu, habari zake zilivuma kwenye redio na magazeti yote kasoro machache tu. Na kila kona alikuwa akizungumziwa, kama vile ni malkia fulani, aliyekuwa akiiletea Tanzania kitu kikuuubwa, zaidi ya "kuzikonga nyoyo" za Wabongo kwa kuwaonesha nepi. Kanuni ni ile ile. Leo hii duniani kwa ujumla, na Bongo hususan, ukitaka kuwa maarufu, usiwe mwanafalsafa (philosopher), bali kuwa "mchizi" kama mwana dada huyo. Vaa nepi tu, na kiguo kifupi, halafu onyesha "uchizi" wako kwa "uchangamfu" wa kurusha miguu juu, hata kama nyimbo zako hazitakuwa nzuri, utavuma siku chache tu, na utakuwemo. Moja ya vitu vilivyokuwa vikielezewa wikiyote ile ni umatiuliokuwa ukifurika kwenye maonyuesho ya bibi huyo. Kwa mfano tunaambiwa ukumbi wa Diamond Jubilee ulifurika kumshuhudia "mchizi". Nikirudi upande mwingine, nilipita Jangwani siku chache zilizopita. Nikiwa kwenye daladala nilishuhudia umati mkubwa wawananchi. Niliuliza hapo palikuwa nanini, nikitegemea labda "mchizi" anaonesho la bure kwenye viwanja vya Jangwani, lakini nikaambiwa, yupo mtu mmoja anaunguruma hapo. Damu ilinisisimka, nikasema mbona sikusikia kama leo kuna mkusanyiko kama huu. Mambo yote yenye mikusanyiko hutangazwa maredioni na magazetini, lakini mkusanyiko huu sikuusikia. Lakini pia nikajiuliza, umatiule, mkubwa maanaile, umepataje habari. Kama ni kupashana tu hivi hivi ndio vile, je wangepashwa kama walivyopashwa ya "mchizi" ingekuwaje? Halafu imani yangu kwamba kuwa maarufu Bongo kunaendana na kuwa "chizi" ikatingishwa kidogo. Nikajiuliza, au Lipumba kawa "mchizi"? Nikagundua, hapana, kila ngoma ina wapenzi wake. Ile nayo ni ngoma. Ule ni mkusanyiko wa Kisiasa, nasiasa hugusa maisha ya watu. Kwa hiyo kukonga nyoyo za watu ni pamoja na kuzigusa nyoyo za watu hao kwenye mshipa wa maslahi yao. Ukiugusa ule mshipa wa maslahi sawa sawa, nasio kuutekenya tu, lazima uwakonge. Sibure, Lipumba ana mambo! Nilijisemea mwenyewe. Wenye vyama vyao wakae chonjo. Nafuu mie nisiye nacho hadi sasa. Nilitegemea kupata habari zaidi kwenye magazeti. Asubuhi niliamka mapema na kwenda kwenye meza za wauza magazeti, nikitaraji kwamba wana habari wataukonga moyo wangu kwa habari nzito za mkusanyiko ule. Kwanza nilidhani labda ingekuwa tabu kuchagua gazeti, maana yote yangekuwa yamesheheni habari za mkusanyiko ule. Lakini nilipofika kwenye meza zile nikajiuliza, hivi mimi niliona mkusanyiko kweli au niliota ndoto? Sikuona habari yoyte. Gazeti moja tu ndio lilijitahidi kuandika kwamba Lipumba kasema kura zikiibiwa damu itamwagika. Lakini sikuona habari nyingine kama zilivyokuwa za 'mchizi'. Wala Lipumba akionesha suti kama mchizi alivyo onesha nepi. Akili yangu ilinihakikishia kwamba ile haikuwa ni ndoto bali kweli, umati ulikuwepo. Nilisema bila kujitambua kwa sauti: "He, hazimo?" Muuza magazeti akasema:
"Nzuri tu, bwana, sijui weye". Akasema: "Nakuuliza habari zipi hazimo?"
Nikamwambia: "Ah, za mkutano wa jana wa Jangwani". Akacheka kidogo, halafu
akasema, "Wewe huelewi siasa? Hawawezi kuandika habari za mwanaume yule,
lakini hata wafanyeje, hatuvumi kwenye magazeti yao wala redio zao, lakini
tumo". Nikapata jibu. Kweli hawavumi, lakini wamo.
|
YALIYOMO
Tahariri
Mkapa awatahadharisha wanawake CCM Lipumba: Wananchi wana uwezo wa kuondoa utawala mbovu Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishitaki Serikali Habari za ndani
Sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu kufanyika Dar MPASHO NASAHA
Ushauri Nasaha
MAKALA
WAZO LA WIKI
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Riwaya
Lishe
Makoye: Fedha za Simba nimetafuna mwenyewe |
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza
hapa
Au
Andika barua kwa: nasaha1420@yahoo.com
|
|
|
|