AN-NUUR
Na.162 Rabiul Thani 1419, Agosti 14 - 20, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Mafundisho ya Qur'an

Hakuna kulazimishwa kuingia katika dini 

Aya ya 256 

Hakuna kulazimishwa kuingia katika dini. Uongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anayemkataa Taghuut na akamwamini Allah, bila shaka yeye ameshika kishiko chenye nguvu kisichokuwa na kuvunjika. Na Allah ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. 

Inasadikiwa kuwa kabla ya kuja Uislamu Madina na baadae kufuatiwa na Mtume (s.a.w.), palikuwepo wenyeji - Waarabu wa Madina ambao ama walikuwa waumini wa dini za kishirikiana na hivyo kuabudu masanamu au waliamini dini ya Kiyahudi. 

Wale wote ambao walikuwa washirikina waliukubali Uislamu kirahisi na bila ya taabu kubwa. Kwa upande wa wale Mayahudi wao walisita kidogo licha ya kuwa jamaa zao wote walisilimu. 

Wazee au ndugu wa Mayahudi hao wa Kiarabu walijaribu kutumia nguvu ili kuhakikisha kuwa watoto au ndugu zao hao wanaukubali Uislamu kwa nguvu au hiari. 

Kwa kuwa imani si suala la kulazimishwa bali kujengeka yenyewe baada ya hoja na kuyakinisha ndipo Allah aliteremsha aya hii ili kuzuia mpango huo ambao uliletwa zaidi na msukumo na siyo hoja. 

Msimamo huu wa Kiislamu haukuwa wa muda ule na baadae kufutwa; la hasha! Msimamo huu ni wa kudumu kuanzia wakati ule hadi mwisho wa dunia. Kwa kweli haikubaliwi na hairuhusiwi kwa Mwislamu au mtu yoyote kumlazimisha asiye Mwislamu kuingia katika Uislamu. 

Kilichopo na kilichoamriwa na Uislamu ni kulingania Uislamu kwa hoja kulingana na yule anayelinganiwa na mazingira kwa ujumla kama tusomavyo: 

"Walinganie watu katika njia ya Mola wako (Uislamu) kwa hekima na mawaidha mema na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako ndiye amjuae aliyepotea katika njia Yake, Naye ndiye anayewajua walioongoka." (16:125). 

Pamekuwepo na upotoshaji mkubwa wa aya hii kwa watu tofauti kutegemea na matashi na mtazamo wa wapotoshaji hao. Wako wanaowazuia Waislamu kuwalingania wasio-Waislamu kwa kutumia aya hii na wapo aidha wanaotaka Waislamu waovu waachiwe wafanye watakavyo kwa kutumia aya hii vile vile. 

Kulingania wasio-Waislamu ili wawe Waislamu kwa kutumia hoja kama za Qur’an yenyewe, vitabu vyengine vya dini (kama Biblia, Talmud, Veda n.k.), sayansi na nyingine huko siyo kumlazimisha mtu kuwa Muislamu. 

Wala kutoa dosari zilizomo katika vitabu hivyo haijakatazwa na Uislamu licha ya jitihada za wale wanaojipendekeza kwa Wakristo kudai kuwa Uislamu hauruhusu jambo hilo. Kilicho bayana katika mafundisho ya Uislamu ni kukatazwa kuwatukana wale wanaolinganiwa au miungu yao: 

Wala msiwatukane wale ambao wanawaabudu kinyume cha Allah wasije wakamtukana Allah kwa jeuri zao bila kujua. Namba hivyo tumewapambia kila watu vitendo vyao. Kisha marejeo yatakuwa kwa Mola wao. Naye atawaambia waliyokuwa wakiyatenda. (6:108). 

"Kuonyesha udhaifu wa miungu inayodaiwa Mungu na dini nyingine hili limeruhusiwa kaama tuonavyo jinsi Qur’an yenyewe ilipokuwa ikionesha udhaifu wa waungu (masanamu) ya washirikina wa wakati wa Mtume (s.a.w.). Katika Suratul Araf (Aya ya 191 hadi 198) panaoneshwa mfano halisi wa jambo hili. Mifano iliyopo ni pamoja na: 

-Kutokuweza kuwasaidia wale wanaoabudu wala kujisaidia wao (waungu) wenyewe. 

- Kushindwa kuwapa uongofu wale wanaowaomba 

-hawana midomo wala miguu wala mikoni inayowasaidia kwa chochote 

-hawawezi kumdhuru yoyote hata wakitakiwa kufanya hivyon.k. 

Kwa upande wa Waislamu aya hii (ya 256) tunayoendelea nayo inadaiwa kuwa inawazuia wazee au viongozi wa dola kulazimisha kufuatwa kwa sheria ya Uislamu katika jamii ya Waislamu kwani hakuna kulazimishana? 

Kwa kweli huu ni upotoshaji wa wazi wa aya za Allah na ni miongoni mwa jitihada za kuupiga v ita usichukue nafasi yake katika jamii. Ukweli wa hili uko wazi ndani ya mafundisho ya Qur’an na Hadithi ambapo tunaona adhabu mbali mbali zilizowekwa kupambana na maovu na wakati wengine kuwalazimisha Waislamu kutekeleza wajibu wao kama Waislamu. Hili halihitaji maelezo mengi kwani aya zifuatazo ni vielelezo kwa yule anayetaka kufahamu: 

Basi malipo ya wale wanaopigana na Allah na Mtume Wake na kufanya uovu katika nchi ni kuuawa au kusulubiwa au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho au kuhamishwa katika nchi. Hii ndiyo fedheha yao katika dunia; na Akhera watapata adhabu kubwa. (5:33) 

Na mwizi mwanamme na mwizi mwanamke ikateni mikono yao; malipo ya yale waliyoyachuma. Ndiyo adhabu itokayo kwa Allah.Na Allah ni Mwenye nguvu na Mwenye Hekima. 

(5:28) 

Na humo tuliwaandikia ya kwamba mtu (huuawa) kwa mtu, na jicho kwa jicho, na pua kwa pua na sikio kwa sikio na jino kwa jino, na itakuwa kulipizwa kisasi katika kutiana majaraha. Lakini atakayesamehe basi itakuwa kafara kwake. (5:45) 

Aya hizi pamoja na nyingine nyingi zinatufahamisha kuwa kutokulazimishwa katika masuala ya dini ni kule kutowashurutisha wasio-Waislamu kuingia au kuukubali Uislamu. Kwa wale walioukubali Uislamu ama kwa kuzaliwa au baada ya kusilimu kwenye kipindi chochote cha umri wao baada ya upambanuzi hapa siyo kulazimishwa lakini ni kuwajibishwa kufanya wajibu wao. Dola ya Kiislamu au wazee hapa wanawajibika kuona wale walio chini yao wanafuata maelekezo ya Uislamu kwa hiari au nguvu. Na kwa yule atakayeona udhia akaamua kuhama Uislamu sheria ya Uislamu umemuwekea adhabu ya kifo. Kwa maana hii hiari ipo katika kuingia au kutokuingia kwenye Uislamu na siyo kuufuata au kuutekeleza baada ya kuukubali. 

Sehemu ya pili ya aya inasema yule ambaye amemkanusha Twaghuut na akamuamini Allah basi huyu ameshikilia mashiko madhubuti. Abul-A’la Maududi katika uchambuzi wake wa Twaghuut anaelezea: 

Neno la Kiarabu Twaghuut katika lugha linamuhusu kila mtu anayechupa mipaka. Qur’an inalitumia neno hili kwa kila mtu anayemuasi Allah na akajidai yeye mwenyewe ubwana na mamlaka yasiyo na mipaka juu ya waja wa Allah na kisha akatumia nguvu kuwalazimisha kuwa watumwa wake. 

Uasi dhidi ya Allah una daraja tatu za uovu: (1) Yule ajulikanaye kama Fasiq iwapo anakubali kuwa ni mja wa Allah lakini matendo yake ya kila siku yanakwenda kinyume na amri zake (Allah). (2) Yule ajulikanaye kuwa ni Kafri iwapo yeye hujitenga moja kwa moja na utegemezi wa Allah au anayemtumikia kwa utii mwingine kinyume na Allah. (3) Twaghuut n i yule ambaye anafanya uasi dhidi ya Allah na kisha akajitahidi kuwafanya waja wa Allah kuwa ni waja wake yeye badala ya Allah.Twaghuut anaweza kuwa ni shetani au kiongozi wa dini au kiongozi wa kisiasa kama mfalme au serikali. Kwa sababu hiyo mtu hawezi kuwa muumini wa kweli bila ya kumkanusha au kupingana na Twaghuut. 

Kwa lugha nyingine Twaghuut ni daraja ya juu ya uasi kwani inakusanya mtu kuasi yeye na kisha kuwalazimisha wengine uasi. Kwa kuwa Waislamu wanaoishi katika zama zetu karibu sote tumo chini ya mifumo ya kitwaghuut; suala la kupambana na Matwaghuut ni lazima liwe ni mfumo wetu wa maisha. Vinginevyo Uislamu wetu utakuwa mashakani kama si kutokuwepo kabisa. Kuishi chini ya hali hiyo ndiyo salama yetu kwani tutakuwemo kwenye kivuli cha hadithi ya Mtume (s.a.w.) ya njia tatu za kukataza maovu - kutumia nguvu; kukaripia maovu au kuchukia maovu. Kushabikia maovu au serikali zilizopo ni kukubali kuwa mfuasi mtiifu wa Twaghuut. 

 

Aya ya 257 

Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa wale walioamini - huwatgoa katika giza na kuwaingiza katika nuru. Lakini wale walikufuru; walinzi wao ni Matwaghuut - hjuwatoa katika nuru na kuwaingiza gizani. Hao ndio watu wa Motoni, humo watakaa milele. 

Aya tuliyoishia nayo inaeleza kuwa yule ambaye amemkanusha Twaghuut na akamuamini Allah basi huyo ameshika kitu madhubuti kabisa. Katika aya hii Allah anaeleza huo umadhubuti wa hicho kishiko ambacho kinahusiana na Yeye Mwenyewe akiwa Mlinzi wa wale walioamini. Kazi yake ni kuwatoa waliomuamini Yeye kutoka katika viza vya upotofu, ujinga, maovu ya kiroho na mengine n.k. na kuwaingiza katika nuru ya haki na ukweli wa maisha. 

Matumizi ya neno giza ndani ya Qur’an siku zote katika maana ya hapa yamekuja kwa wingi - dhulumat’; kinyume na nuru ambayo imetumika kwa uchache. Hikma ya matumizi haya inasadikiwa ni kuonyuesha kuwa viza ni vingi kwani vinaashiriwa na dini (mifumo ya maisha) zinazobuniwa na wanaadamu kuwa ni nyingi lakini hakuna hata moja inayoweza kumuongoza binaadamu kwa ufanisi. Kwa upande wa pili mfumo wa hakika (dini) unao muhakikishia binaadamu kuwa yuko salama ni mmoja tu ambao ni Uislamu. Kwa lugha nyingine, Ukristo, Uyahudi, Ubepari, Ukoministi, Uhindu, Ufursi, Ulokole, Ujamaa, Ubahai, Utalii (Tourism) n,k, ni viza wakati Uislamu pekee ndiyo nuru ambayo Allah huwaongezea huko wale waliomuaminiYeye. 

Kinyume na wale waliomuamini Allah na akawa Mlinzi wao; wale waliokufuru mlinzi wao ni Twaghuut ambaye kazi yake kubwa ni kuwatoa katika njia ya haki - Nurfu (Uislamu) na kuwaingiza katika viza (njia potofu za maisha). 

Ingawa neno lililotumika hapa ni Twaghuut kwa uchache lakini inapewa tafsiri ya wingi kwasababu mtu yoyote ambaye anamkanusha Allah na kuamua kuishi kwa kufuata mfumo wowote wa masiah usio Uislamu basi anakuwa mtumwa si wa Twaghuut mmoja bali Matwaghuut kadhaa wenye maumbile na hali tofuati. Kinara wa Matwaghuut ni Ibilisi ambaye humuandalia mtu huyu namna kwa namna za udanganyifu wenye mvuto wa aina yake. 

Mbali na Ibilisi, Twaghuut mwingine aliyefichika kwa wegni na nafsi yake mwenyewe binadamu. Nafsi ya binadamu humfanya kuwa mtumwa na matamanio na matashi na kumuongoza kwenye kila aina ya upotofu na njia zilizokwenda upogo. Matwaghuut wengvine ni mke au mume, watoto, jamaa zake, kabila au familia, marafiki au taifa. Aidha Matwaghuu wengine ni viongozi wa kisiasa au kidini na hata serikali yake. 

Wote hawa ni Matwaghuut kwa mtu mmoja huyu na kila mmoja anamvutia kwenye yale anayoyatamani yeye wakati huyu mtu anabaki kuwa mtumwa anayejidanganya kuwa ataweza kuwaridhisha wote. Ni kwasababu kama hizo Allah alisema kuwa iwapo tutawatii wengi waliomo ardhini watatupoteza aliposema: 

"Na kama ukwatii wengi katika hawa waliomo ulimwenguni watakupoteza na njia ya Allah. Hawafuati ila dhana tu, na hawakuwa ila ni wenye kuzua (tu basi).(6:116). 

Kinyume na hivyo anaeleza tena: 

"Sema: "Hii ndiyo njia yangu, ninaita (ninalingania) kwa Allah kwa ujuzi wa kweli - mimi na wanaonifuata......(12:108). 

Kwa hiyo bado tunatilia mkazo kuwa njia ya Allah (Nuru) ni moja tu ambaye aliilingania Mtume (s.a.w.) na sasa inalinganiwa wa Waislamu wa kweli siyo wale wafuasi wa Matwaghuut waliojivika vilemba na kujipachika madaraka bila ya haki. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI 

Serikali yaipongeza Africa Muslim Agency 
Na Mwandishi Wetu, Moshi 

Wanafunzi Wakatoliki darasa la saba 1998: 
Afisa Elimu akiri kutaka orodha ya wanafunzi 
Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

Athari ya milipuko Dar, Nairobi: Waliokufa wafikia 258 
Na Mwandishi Wetu 

Wakuu wa mashule waache ubaguzi 
Na Mwandishi Wetu 

ABU AMEENA: Mwana harakati aliyesilimisha wanajeshi 3000 wa Marekani -2 

Kisiwa cha Karafuu chageuzwa cha ulevi 

Twalaban wadhibiti Afghanistan yote 

Madina yachapisha kitabu cha rejea 

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA 

Maoni: Nyerere kasema kweli Ujamaa na Ukristo vimeshindwa 
Na Abdul Gullam 

Kina Ngatara na wenzake ndio urithi tulioachiwa na Wakoloni 
Na J. Hussein 

HOJA BINAFSI: Suala la Mwembechai, serikali imeumbuka 
Na Mwinjilisti Kamara Kusupa 

Kupigwa mabomu misikitini: Waislamu tumejifunza nini? 
Na RAJAB RAJAB

MAONI: Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu na ni uzushi mtupu!
Na Muhibu Said

Utangazeni Uislamu kwa nguvu zote – Sheikh Jongo
Na Badru Kimwaga

Salafiya wataka wanawake wawe macho na vyombo vya habari
Na Mwandishi Wetu

Waumini Misufini Morogoro waazimia kujenga Msikiti
Na Rajab Rajab, Morogoro

Serikali yatakiwa kuondoa askari Mwembechai
Na Badru Kimwaga

Mafunzo ya Quran 

Barua za wasomaji 

Mashairi 

Masomo 

Chakula na Lishe  

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita