AN-NUUR
Na.162 Rabiul Thani 1419, Agosti 14 - 20, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Kina Ngatara na wenzake ndio urithi tulioachiwa na Wakoloni
Na J. Hussein

"Ukiondoa Ukristo, bila shaka kuna dini nyingine nyingi. Dini hizo nyingine siwezi nikazisemea kwa sababu sizifahamu vizuri. Ila kuhusu Ukristo nina uhakika kabisa kwamba dini hii haitoki kwa Mungu’ 

Maneno haya aliyasema Mwingereza Robert Tresell katika kitabu chake maarufu - "The Ragged Trousered Philanthropists ambacho kwa tafsiri ya juu juu tunaweza tukakiita - Watenda wema waliojaa viraka. 

Alichojaribu kukibainisha ndani ya kitabu chake hicho ni kuhusu mchango mkubwa uliotolewa na mafundisho ya kanisa katika kupumbaza akili za walalahoi wa Uingereza enzi hizo wasiweze kubaini dhulma kubwa iliyokuwa inaendeshwa dhidi yao na mtandao wa mabwenyenye ambao ulikuwa ni ushirika kati ya viongozi wa makanisa, watawala na matajiri. Tresell alikuwa akistaajabu kuwa mbali ya kuishia na kuwa matambara yaliyoshona viraka na kuzungukwa na wingu zito la njaa na maradhi, bado walalahoi walionyesha utii, heshima na kukongowea kukubwa mbele ya mabwenyenye. Hali hii ndio iliyomfanya awakejeli kwa kuwaita watenda wema. Baadhi ya wachunguzi wa mambo wanaamini kuwa ni kuchapishwa kwa kitabu hiki cha Tresell ndiko kulikowaamsha walalahoi wakaweza kukisaidia chama cha Labour kilichokuwa kinatetea maslahi yao kwa miaka mingi; kuweza kuibuka na ushindi kwa mara ya kwanza dhidi ya Chama cha Mamwinyi cha Conservative wakati wa uchaguzi. 

Ukimwondoa Robert Tresell, wako wengine wengi ambao pia waliuchukulia Ukristo kama ganzi iliyotumiwa na madhalimu kuviza akili ya wale waliodhulumiwa. 

Huenda maarufu zaidi katika hawa ni wale waasisi wa siasa za Kikomunisti duniani ambao kwa kichefuchefu kikubwa waliufananisha na kasumba. 

Ukiwaacha wote hawa ambao wametoa tahadhari zao kupitia makabrasha yaliyosheheni falsafa na taaluma nzito ambazo zinaweza kuwa mzigo kuzielewa kwa mtu wa kawaida, miongoni mwa watu wa kawaida kabisa wapo ambao wamezinduka na kupitia fani mbali mbali rahisi wamejaribu kutufikishia tahadhari hiyo hiyo. Mwanamuziki wa Kijamaika, marehemu Bob Marley katika wimbo wake uitwao Babylon System anatutahadharisha kuwa mfumo wa Kimagharibi ni kama popo bawa kwani kwa kupitia makanisa, vyuo, na taasisi mbali mbali huviza akili za vijana ulimwenguni kote kwa lengo la kudumisha unyonyaji na udhalimu. 

Bila shaka msomaji ambaye hana uzoefu wa awali na haya yote, atakuwa keshaanza kujiuliza ni upi uhusiano wa maelezo haya yote yaliyotangulia na Ludovick Ngatara na wenzake ambao wametupambia kichwa cha makala hii. Nakuomba msomaji uvute subra kwani kila jambo litakuwa bayana hivi punde. 

Wachambuzi wa historia ya siasa za Kimataifa wanatuambia kuwa kunasababu kubwa tatu zilizopelekea kuibuka kwa siasa za Kikoloni ulimwenguni. Sababu hizi zinaelezwa kuwa ni: moja kuwa na sehemu ya kupatia malighafi kwa urahisi, mbili kupanua masoko mapya kwa bidhaa zilizozalishwa Ulaya na tatu, kunufaika na nguvu kazi rahisi katika maeneo yaliyogeuzwa kuwa makoloni. Sababu ya kwanza na ya pili ni sahihi kwa kiwango fulani tu kwani malighafi na masoko ni masuala ya kibiashara ambayo mafanikio yake hayategemei nchi moja kutawala nchi nyingine. Sababu ya tatu ni sahihi zaidi kwani unapozungumzia suala la nguvu kazi rahisi hisia za kudhulumu zinaingia na ufanisi katika dhulma siku zote hupatikana kwa kushinikizwa na mabavu ya dola. 

Kuzinduka kwa tabaka la walalahoi Ulaya kupinga udhalimu wa muda mrefu kulitishia kuusambaratisha mtandao wa mabwenyenye. Ili kujiokoa mabwenyenye walibuni utaratibu wa kupunguza dhulma ndani ya nchi zao lakini ili kutoathiri viwango vyao vya ulafi ikawa ni muhimu kutafuta kundi au makundi ya wadhulumiwa wengine. Hawa wangeweza wakapatikana katika mataifa mengine nje yaUlaya lakini hakuna namna yoyote ambayo ingekuwa rahisi kuwadhulumu bila kwanza kuwatawala. Hivi ndivyo ukoloni ulivyozaliwa. 

Mabwenyenye wa Ulaya wakikumbuka jinsi mafunzo ya kanisa yalivyotumika kama ganzi iliyoviza akili za walalahoi wa huko kwa karne nyingi na kuleta ufanisi mkubwa katika dhulma waliokuwa wakiwafanyia, hawakuwa tayari kuanza maisha mapya ya Kikoloni bila sambamba na hilo kuwakoleza wenyeji wakoloni wa dozi ya hiyo ganzi. 

Wamishenari waliomiminika Afrika sambamba na maafisa wa Kikoloni walifanya kazi kubwa na kwa ufanisi wa ajabu. Kupitia imani zao za mafumbo na mikorogo ya falsafa za ajabu ajabu walifanikiwa kutengeneza kizazi kisichojua kabisa namna ya kufikiri na ambacho thamani ya hoja na tunu ya utafiti havina maana yoyote. Nadhani sababu kubwa iliyowafanya Wakoloni wa Kifaransa na Kiingereza kugawa uhuru (wa bendera) kama pipi kwa mataifa ya Kiafrika mwishoni mwa miaka ya hamsini na mwanzoni mwa miaka ya sitini, ni mafanikio haya. Walikuwa na wasiwasi gani iwapo hao waliokuwa wanawarithisha unokoa wa makoloni yao waliyoyaacha walikuwa watupu kiasi ambacho wasingeweza kuwapa changamoto yoyote kwa miaka mia tano inayofuata? 

Katika toleo lake la tarehe 5 Julai 1998, Gazeti la Sunday Observer lilichapisha makala ya Bwana Ludovick Ngatara yenye kichwa cha habari: Kuanzishwa "Islamic Cllub" ni agenda ya siri inayoweza kuhatarisha amani Tanzania. 

Mbali ya kwamba makala hiyo ya Bwana Ngatara imejaa upuuzi wa kutisha, lakini haishangazi hata kidogo. Itashangaza vipi iwapo Bwana Ngatara kama ambvyo tumekwishaona ni mmoja wa wale ambao wamepewa dozi? 

Kunako majaliwa katika toleo lijalo hatua kwa hatua nitajaribu kuzijadili na kuziweka bayana porojo zilizojaa kwenye makala ya Bwana Ngatara ambazo bila shaka yeye anaamini kwamba ni hoja nzito kabisa. 
 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI 

Serikali yaipongeza Africa Muslim Agency 
Na Mwandishi Wetu, Moshi 

Wanafunzi Wakatoliki darasa la saba 1998: 
Afisa Elimu akiri kutaka orodha ya wanafunzi 
Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

Athari ya milipuko Dar, Nairobi: Waliokufa wafikia 258 
Na Mwandishi Wetu 

Wakuu wa mashule waache ubaguzi 
Na Mwandishi Wetu 

ABU AMEENA: Mwana harakati aliyesilimisha wanajeshi 3000 wa Marekani -2 

Kisiwa cha Karafuu chageuzwa cha ulevi 

Twalaban wadhibiti Afghanistan yote 

Madina yachapisha kitabu cha rejea 

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA 

Maoni: Nyerere kasema kweli Ujamaa na Ukristo vimeshindwa 
Na Abdul Gullam 

Kina Ngatara na wenzake ndio urithi tulioachiwa na Wakoloni 
Na J. Hussein 

HOJA BINAFSI: Suala la Mwembechai, serikali imeumbuka 
Na Mwinjilisti Kamara Kusupa 

Kupigwa mabomu misikitini: Waislamu tumejifunza nini? 
Na RAJAB RAJAB

MAONI: Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu na ni uzushi mtupu!
Na Muhibu Said

Utangazeni Uislamu kwa nguvu zote – Sheikh Jongo
Na Badru Kimwaga

Salafiya wataka wanawake wawe macho na vyombo vya habari
Na Mwandishi Wetu

Waumini Misufini Morogoro waazimia kujenga Msikiti
Na Rajab Rajab, Morogoro

Serikali yatakiwa kuondoa askari Mwembechai
Na Badru Kimwaga

Mafunzo ya Quran 

Barua za wasomaji 

Mashairi 

Masomo 

Chakula na Lishe  
 
 

 

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita