AN-NUUR
Na.162 Rabiul Thani 1419, Agosti 14 - 20, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 Utenzi wa tamasha la aonyesho ya mavazi Songea
(unaendelea kutoka toleo lililopita..

15. Waheshimiwa wa Mbeja, 
 Wakubwa mliokuja, 
 Mmetutia faraja, 
 Kuja Songea Kumili. 

16. Mahuji Mkajitoa, 
 Kutoka kila mikoa, 
 Hapa sote twakohoa, 
 Kwa raha za maadili. 

17. Maadili ya Kidini, 
 Yasema shikamaneni, 
 Kwa kamba moja ya Dini, 
 Ya Muhammad Rasuli. 

18. Mola Amba Mkikana, 
 Aya zangu Mtaona, 
 Mtakapokonywa mchana, 
 Roho na viwili wili. 

19 Haki zenu ziwatupe, 
 Maadui wawachape, 
 Kwa Mola mtapetape, 
 Kwa kuasi jambo hili. 

20. Ama leo ni sahihi, 
 Alhamdu Lillahi, 
 Mola katutia zihi, 
 Kuepuka ubatili. 

21. Mmesafiri mkesha, 
 Tena kujigharimisha, 
 Kulikeshea tamasha, 
 Hadi huku kwetu mbali. 

22. Kina baba kina mama, 
 Karibuni Waadhama, 
 Mji wetu ni Ruvuma, 
 Na hauna mushkeli. 

23. Tunduru, Mbinga, Songea, 
 Tupo hapa kupokea, 
 Ni miji ilobobea, 
 Wakazi wa dini mbili. 

24. Na watu wote imani, 
 Ipo kwenye zao dini, 
 Islamu na Misheni, 
 Hatuishi kwa mihali. 

25. Islamu kidiriki, 
 Utata na Katoliki, 
 Huelezwa kirafiki, 
 Ukatoka mushkeli. 

26. Katoliki kadhalika, 
 Kwa Islamu hufika, 
 Kuteguliwa mashaka, 
 Na kutokwa shitighali. 

27. Wengi waliocharuka, 
 Kumtafuta Rabuka, 
 Sasa wameshazinduka, 
 Tunao humu Mahali. 

28. Kwa hilo tunashukuru, 
 Kwa Mola wetu Ghafuru, 
 Na Mtume mwenye Nuru, 
 Ya Muhammad Rasuli. 

29. Dibaji ilipofika, 
 Kala tulilojia, 
 Muumba mbingu na dunia, 
 Tumdhukuru Awali. 

30. Ewe wanadamu wenzangu, 
 Tumsifu Bwana Mungu, 
 Bismilah wa tangu, 
 Aso mwisho na awali. 

31. Sifa za Mola Karima, 
 Hana Baba hana Mama, 
 Kaka Dada lau kama, 
 Au mwana kwa mithili. 

32. Hana sifa za uzazi, 
 Si mlala usingizi, 
 Na hana msaidizi, 
 Katika zake fiili. 

33. Mola hana mfanowe, 
 Na bahari wala jiwe, 
 Takriba viumbewe, 
 Si watu si majabali. 

34. Hapa nayakumbushia, 
 Siku niliopita njia, 
 Nikakuta wabishia, 
 Ubishi wa kwelikweli. 

35. Kwamba Mola kamuumba, 
 Adamu kinena kwamba, 
 Tutamuumba sambamba, 
 Mfano wa yetu hali. 

36. Kwa hiyo Mola mkwasi, 
 Yu sawa sawa na sisi, 
 Wakataka nijilisi, 
 Nitasue masuali. 

37. Nikajibu si msomi, 
 Ila nijuavyo mimi, 
 Bismillah Rahim, 
 Alineena mithali. 

38. Baadhi yasifa ndiyo, 
 Katupa yafananayo, 
 Si utu na kama hayo, 
 Hebu zikilizeni hili. 

39. Kwanza Mola mfahamu, 
 Ana sifa kem kem, 
 Moja wapo ni Hakimu, 
 Hiyo siku ya shughuli. 

40. Ndiyo Hakimu wa mwisho, 
 Hiyo siku ya kitisho, 
 Nasi kwa ufananisho, 
 Tuna wengi mali wali. 

41. Pili Mungu Mfalme, 
 Wa Dhamu ndiyo ngome, 
 Sasa mtu mtazame, 
 Duniani, hatawali? 

42. Tatu kaa fikiria, 
 Hizi roho zetu pia, 
 Ulipata fumania, 
 Hata katika ajali. 

43. Ukaijua umbole, 
 Huku nyuma huku mbele, 
 Wakanijibu milele, 
 Hatujaona asili. 

44. Nikawaambia mfano, 
 Wa Bwana Mungu ni huno, 
 Si wa macho na mikono, 
 Kichwa na kiwiliwili. 

45. Alinganeje vitoto, 
 Mungu ni Muumba moto, 
 Kwetu sisi ni maguto, 
 Kwake hauna makali. 

46. Siku hiyo ya kiwewe, 
 Yatalia hata mawe, 
 Kabla siku yenyewe, 
 Atajisifu Jalali. 

47. Wa wapi Masultani, 
 Waliokaa duniani, 
 Wakamba ulimwenguni, 
 Ndisi hapa Majabali. 

48. Wakila zangu riziki, 
 Na kutesa halaiki, 
 Mimi wasinisadiki, 
 Wakiabudu batili. 

49. Kama leo yupo mwambi, 
 Aje hapa kwa ugambi, 
 Wote kimya kwenye vumbi, 
 Mungu tena ajadili. 

50. Ndimi sina mwinginewe, 
 Silingani kilichowe, 
 Je mtu kama wewe, 
 Utajibuje kwa hili. 

51. Jambo kuu tena lipo, 
 Mungu kaziumba pepo, 
 Kaya za wenye malipo, 
 Wafungao na kusali. 

52. Pepo nane Ashirafu, 
 Zashindana utukufu, 
 Hayupo muweza sifu, 
 Hata hizo kwa dalili. 

53. Wacha Mungu kwa hakika, 
 Wawe kama malaika, 
 Na mahuri wametuka, 
 Hata hizo kwa dalili. 

54. Nikauliza unasi, 
 Yupo mwenye wasiwasi, 
 Wakanijibu mkwasi, 
 Hana mfano ni kweli. 

55. Na sasa twajirudisha, 
 Hapa kunako tamasha, 
 Mola katuamrisha, 
 Amri zake halali. 

unaendelea toleo lijalo
 

Kushamiri kwa Bida'a 

Mhariri msifika, naja kwako gazetini, 
Ingawa nachechemeka, nitafika ulingoni, 
Naomba kwake Rabbuka, aombwaye ya Manani 
Kushamiri kwa Bida’a kumezorotesha dini. 

Imezorota hakika, kila pembe duniani, 
Mambo yasiyopasika, yamejazwa kwenye dini, 
Mfano bora hakika, nitataja gazetini, 
Kushamiri kwa bida’a, kumezorotesha dini. 

Moja moja taandika, mpate soma makini, 
Hofu sina wala shaka, nitasema hadharani, 
Waje pia wahusika, wayaweke akilini, 
Kushamiri kwa bida’a, kumezorotesha dini. 

Arobani  hakika, zimefanywa ndizo dini, 
Pasi na hilo hakika, kufanyiwa maitini, 
Haamini atafika, mbele ya Alwah Dayani, 
Kushamiri kwa bida’a, kumezorotesha dini. 

Ziara pia yashika, kudumaza namba wani, 
Mtu pasi na kupika, hajaingia peponi, 
Hivyo ndivyo wapayuka, kwenye hadhara na ndani, 
Kushamiri kwa bida’a, kumezorotesha dini. 

Hadithi ziso hakika, wazitunga akilini, 
Kupoteza wahusika, waso elimu vichwani, 
Ole wao watafika, siku iso kifani, 
Kushamiri kwa bida’a, kumezorotesha dini. 

Mbele watawajibika, wenyewe waje baini, 
Yote yaliyotendeka, hapa hapa duniani, 
Hili nalo si dhihaka, Thumma yatasa Alun, 
Kushamiri kwa bida’a, kumezorotesha dini. 

Nafasiri kwa nyaraka, neno bid’aa shikeni, 
Sunna ziliongezeka, Mtume hakubaini, 
Azimegeuzwa hakika, ndiyo dini duniani, 
Kushamiri kwa bida’a, kumezorotesha dini, 

Ukweli wamejizuka, na hii dunia nini? 
Starehe yakomeka, ya Akhera mileleni, 
Vipi waje haribika, kusahau ya mbeleni, 
Kushamiri kwa bida’a, kumezorotesha dini. 

Badili mwendo hakika, kwa Mola murejeeni, 
Aya zinavyopasika, elezeni hadharani,. 
Pasipo kukengeuka, kuficha yalo bayani, 
Vipi mnanufaika, kwa aya zake Manani? 

Mwenye kuzuwa hakika, jambo lisilo Qur’an 
Wala Sunna za hakika, japo lawapendezeni, 
Laendea hakika, koteni ulimwenguni, 
Na kwake litarudishwa, lije mkwame kooni. 

Ashindwe kueleweka, lipo wapi kitabuni, 
Dini ilokamilika, vipi mwaita mageni? 
Ili ujenufaika, thamani ndogo ya nini? 
Kushamiri kwa bida’a, kumezorotesha dini. 

Hapa mwisho nimefika, nimesema hadharani, 
Nimesema, sikufoka, akilini yashikeni, 
Kwa Mola muje ongoka, peponi mtulieni, 
Rudini kwake Rabbuka, mambo yakiwashindeni. 

Ustadh Muhammad Ibn Hakika Machellah, 
Almasjid Answari-Makonga, 
Box 298 Newala 
Yarabi tupe elimu 
Bismillah naanza, jina la Mola Karima, 
Mjuzi alotufunza, kwa Wahay na ili hama, 
Na Mitume kwa kujaza, yalomema na harama, 
Yarabi tupe elimu, tupiganie Isilamu. 

Iqraa inasema, wajibu sote kusoma, 
Si kwa baba si kwa mama, kusoma kufanya hima, 
Uingereza Panama, kote twendeni kusoma, 
Yarabi tupe elimu, tupiganie Isilamu. 

Islamu ni elimu, shime nawahusieni, 
Muhammad wa Adamu, wote watu taalamani, 
Hima hima Isilamu, tujitoe ujingani, 
Yarabi tupe elimu, tupiganie Isilamu 

Elimu kwetu faradhi, yatangulia hata sala, 
Elimu kwetu ni hadhi, japo Isilamu twalala, 
Qur’an na Hadithi, kote elimu melala, 
Yarabi tupe elimu, tupiganie Isilamu 

Enyi mlo mashuleni, elimu piganieni, 
Hata kufia mezani, kwenu jitahidini, 
Ameahidi Manani, peponi kuwaficheni, 
Yarabi tupe elimu, tupiganie Isilamu. 

Hala hala wanafunzwa, elimu si ya kuchezwa, 
Hata Mtume ajuzwa, kwa kubanwa na kutunzwa, 
Hata wale walojuzwa, kwahilo walihimizwa, 
Yarabi tupe elimu, tupiganie Isilamu. 

Kaditama namaliza, husiya walomaliza, 
Tumieni mlojuzwa, ondosheni umma giza, 
Qiyama waja ulizwa, manufaa ya kujuzwa, 
Yarabi tupe elimu, tupiganie Isilamu. 

Mwanawetu Hamza (Mujahidat), 
Dar es Salaam 
 

Iundwe Tume haraka 

1.Bismillah Rabuka, kalamu imkononi, 
Makubwa yalotofika, fundo kubwa li moyoni, 
Kudanganywa tumechoka, tunasema hadharani, 
Iundwe tume haraka, aliyeua mahakamani. 

2. Muda mrefu hakika, tangu tuone jijini, 
Polisi walipofika, kuua msikitini, 
Sababu zinosemeka, hazingii akilini, 
Ukweli tunautaka, aliyeua ni nani? 

3. Serikali metamka, wasiopenda amani, 
Balozi nne hakika, zataka kutufitini, 
Mapesa yanatumika, kuvuruga amani, 
Ukweli tunautaka, aliyeua ni nani? 

4. Mara ikaja geuka, sio wa Uarabuni, 
Tunao ndani hakika, wachuuzi wa nchini, 
Amani wamechoka, vurugu wanadhamini, 
Ukweli tunautaka, aliyeua ni nani? 

5. Waziri akatamka, siasa msikitini, 
Eti sisi twatumika, na wasopenda amani, 
Ni wapenda madaraka, ambao huturubuni, 
Iundwe tume haraka, ukweli itabaini! 

6. Ikawa wanatusaka, kama kongoni porini, 
Kwetu walichokitaka, tunatumiwa na nani, 
Ameagiza Rabuka, tukaitangaze dini! 
Ukweli tunautaka, aliyeua ni nani? 

7. Dunia mefedheheka, udanganyifu bungeni, 
Waheshimiwa kucheka, bila ya kutathmini, 
Wajue lipi tashika, ambalo wangeamini, 
Ukweli tunautaka, aliyeua ni nani? 

8. Sababu zilotajika, na waziri mambo ndani, 
Hata chizi atacheka, na fupale jalalani, 
Chuki risasi mtwika, karatasi mfukoni, 
Ukweli tunautaka, aliyeua ni nani? 

9. Huyo aliyezishika, kuzitoa mfukoni, 
Na ndipo akatamka, haya sasa mpigeni, 
Waziri tunamtaka, aletwe mahakamani, 
Hukumu hiyo hakika, haipo ulimwenguni! 

10. Wabunge la kukumbuka, nyie tumewatumeni, 
Dodoma mnapofika, mambo myatathimini, 
Ajiuzulu haraka, waziri mambo ya ndani, 
Iundwe tume haraka, tuwahi mahakamani. 

11. Tume iundwe haraka, tupate ule undani, 
Wananchi twaitaka, wala msiturubuni, 
Siasa tumeichoka, mnachelewesha nini? 
Iundwe tume haraka, tuwahi mahakamani. 

12. Pesa gani mnataka, mwatutia hasirani, 
Makodi yasotajika, pesa ziserikalini, 
Mnachota mkitaka, mamilioni sitini, 
Iundwe tume haraka, tuwahi mahakamani. 

13. Aloua twamtaka, afike mahakamani, 
Bunduki aliposhika, kaamrishwa na nani? 
Naye aliyetamka, ameagizwa na nani? 
Mauaji alotaka, kosa lilikuwa nini? 

14. Tamati nimeshafika, waziri mambo ya ndani, 
Meshindwa kuwajibika, ang’oke madarakani, 
Naitakia baraka, tume huria nchini, 
Illah Mola Rabuka, dumisha amani nchini. 

Wabillah Tauwfiq 

K.S.Luanda (Nolo), 
Dar es Salaam. 
 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI 

Serikali yaipongeza Africa Muslim Agency 
Na Mwandishi Wetu, Moshi 

Wanafunzi Wakatoliki darasa la saba 1998: 
Afisa Elimu akiri kutaka orodha ya wanafunzi 
Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

Athari ya milipuko Dar, Nairobi: Waliokufa wafikia 258 
Na Mwandishi Wetu 

Wakuu wa mashule waache ubaguzi 
Na Mwandishi Wetu 

ABU AMEENA: Mwana harakati aliyesilimisha wanajeshi 3000 wa Marekani -2 

Kisiwa cha Karafuu chageuzwa cha ulevi 

Twalaban wadhibiti Afghanistan yote 

Madina yachapisha kitabu cha rejea 

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA 

Maoni: Nyerere kasema kweli Ujamaa na Ukristo vimeshindwa 
Na Abdul Gullam 

Kina Ngatara na wenzake ndio urithi tulioachiwa na Wakoloni 
Na J. Hussein 

HOJA BINAFSI: Suala la Mwembechai, serikali imeumbuka 
Na Mwinjilisti Kamara Kusupa 

Kupigwa mabomu misikitini: Waislamu tumejifunza nini? 
Na RAJAB RAJAB

MAONI: Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu na ni uzushi mtupu!
Na Muhibu Said

Utangazeni Uislamu kwa nguvu zote – Sheikh Jongo
Na Badru Kimwaga

Salafiya wataka wanawake wawe macho na vyombo vya habari
Na Mwandishi Wetu

Waumini Misufini Morogoro waazimia kujenga Msikiti
Na Rajab Rajab, Morogoro

Serikali yatakiwa kuondoa askari Mwembechai
Na Badru Kimwaga

Mafunzo ya Quran 

Barua za wasomaji 

Mashairi 

Masomo 

Chakula na Lishe  

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita