AN-NUUR
Na.162 Rabiul Thani 1419, Agosti 14 - 20, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Kupigwa mabomu misikitini:
Waislamu tumejifunza nini?
 

NI mwaka wa nne sasa tangu askari wa FFU walipoingia katika Msikiti wa Kiwanja cha Ndege Mjini Morogoro wakiwea na viatu vyao na kupiga watu kulikopelekea watu wawili kupoteza maisha. Waislamu tumepata fundisho gani juu ya tukio hilo na mengineyo? Fuatana na Mwandishi RAJAB RAJAB katika makala hii. 

MNAMO majira ya saa 11.30 jioni Waislamu wa Morogoro walivamiwa na askari Polisi katika viwanja vya Msikiti wa Uwanja wa Ndege ambao ulikuwa umefurika watu wa madhehebu mbalimbali. 

Ilipofika saa 3:30 usiku walifika askari wa kutuliza ghasia FFU ambao waliongozwa na OCD Nchimbi wakiwa katika gari zisizopungua nane. 

Walipofika eneo la Msikiti ambapo mhadhara ulikuwa unaendelea ukiwa chini ya Mwenyekiti wa kikundi cha AL-MALLID, Khalfani Kiumbe, bila tahadhari yoyote wakaanza kushambulia waumini kwa marungu na mateke. Walipoona waumini hawateteleki wakapiga mabomu matatu mfululizo ambayo yalianza kuwachanganya waumini. 

Walipoona waumini hao wanaanza kuchanganyikiwa wakazidisha kasi ya kutupa mabomu yaliyokuwa na sumu kali ya gesi iliyosababisha waumini kukohoa sana na kushindwa kuvuta hewa huku wakitokwa machozi. 

Waislamu baada ya kuona mabomu yamewazidia, wakaamua kujisalimisha ndani ya Msikiti, ndipo askari hao walipoamua kuwaingilia humo humo ndani na kuyamwaga mabomu hovyo na huku askari wengine wakitembeza virungu kuwakamata Waislamu na kuwatupia ndani ya magari yao na baadaye kupelekwa kituo cha polisi na kuwekwa mahabusu kulikofuatia na kufunguliwa kesi ya kufanya mdhahara bila ya kibali. 

Katika hali hiyo, wengi waliathirika hali zao za kiafya ambapo baada ya siku mbili mzee mmoja alifariki dunia kutokana na kuathirika na moshi wa mabomu yaliyokuwa na gesi kali yaliyoeneea eneo zima la Kiwanja cha Ndege. 

Si hivyo tu, bali kulipatikana taarifa za kufa mtoto mdogo na watu wengine wakiwa wameumia kiuno na miguu kutokana kutumbukia katika mashimo marefu ya vyoo vya nyumba za jirani na Msikiti huo. 

Mbali na watu hao kufa, wengine kuathirika afya zao lakini polisi iliwashikilia zaidi ya watu 30 wakiwemo wanawake na kuwapeleka mahakamani kwa kosa la kukusanyika bila kibali ambapo baadaye shitaka likabadilishwa na kuwa kosa la kutotii amri (agizo) la Waziri Mkuu la kutofanya mihadhara. 

Kesi hiyo ilifunguliwa huku baadhi ya watuhumiwa wakiwa na majeraha makubwa mwilini mwao na ilichukua zaidi ya miezi mitano bila ya kusikilizwa na huku ikiwa imegharimu maelfu ya fedha ambazo zilitumika kuendeshea kesi hiyo. Lakini kesi hiyo ilikuja kufutwa baadaye na kuonekana washitakiwa hawana shitaka la kujibu. 

Katika kipindi chote hicho cha mwezi wa saba, Waislamu kutoka sehemu mbalimbali walifika katika Msikiti huo na kutoa pole na kuwafariji Waislamu wenzao na wakati huo walishiriki katika maombi na huku wakihusiana sana suala la mshikamano. 

Kwa kweli tukio hilo lilikuwa kubwa kutokea katika nchi yetu kama si Afrika Mashariki, pia katika tukio hili waliweza kuonekana viongozi wa kweli katika serikali na waLe wanaovaa ngozi za kondoo. 

Baada ya tukio lile , Waislamu wengi mkoani humo walijizatiti katika kupigania dini ya Mwenyezi Mungu na mshikamano ukawa mkubwa sana miongoni mwa waumini wa mkoa huo. Katika kuonyesha msimamo wao, miezi minne baadaye Desemba 25, 1994 waumini wa Mkoa huo walipanga safari ya kwenda Dar es Salaam kwa miguu kulaani na kuwapa moyo Waislamu wenzao waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kutuhumiwa kuvunja mabucha ya nguruwe. 

Waislamu hao waliweza kutumia siku tatu njiani huku wakikabiliana na hali zote za jua, mvua, baridi, upepo mkali na kukutana na madudu kadhaa huku wengine wakiwa wamepatwa maradhi ya homa, kuvimba miguu na tumbo. 

Hali hiyo iliweza kubainisha imani za watu zinavyoweza kupanda kutokana na matukio na umoja na mashikamano jinsi unavyopatikana. Baada ya hapo tulitegemea kwamba umoja na mshikamano huo ungeendelea na kufanikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, lakini cha kusikitisha watu walikuwa wamesahau yote yaliyowapata miezi michache iliyopita. 

Kwa kweli uchaguzi wa mwaka 1995 ilikuwa ni aibu tupu kwa Waislamu jinsi walivyoshiriki uchaguzi huo na wengine kuondoka imani zao za awali kwa vijisenti na wake zao kupewa doti za khanga. Kwa kweli huu ni msiba mkubwa sana kwa Waislamu wa nchi hii ambao kila siku wanakubali kufanywa mshumaa. 

Miaka minne imepita sasa tangu FFU wafanye uchafu wao na kunajisi nyumba ya Mwenyezi Mungu na hatimaye mwaka huu wameibuka tena kwa kufanya tukio kama hilo Jijini Dar es Salaam katika Msikiti wa Mwembechai. 

Mnamo Februari 13 mwaka huu katika Msikiti wa Mwembechai kuliibuka vitu kama vilivyotokea Morogoro na sababu zikiwa zinafanana na wakaamua kufanya unyama zaidi ya ule walioufanya Morogoro. 

Baada ya kuwatisha, kuwagawa na kuwadhalilisha Waislamu, Serikali inajidai kuwaachia watuhumiwa kwa madai kuwa hawana kesi ya kujibu. 

Katika kuonyesha Waislamu hatujifunzi kutokana na matukio, baada ya kiongozi mmoja kumtembelea kijana aliyepigwa risasi Chuki Athumani kule Muhimbili, tumejisahau na kutoa pongezi lukuki na shukrani zisizo na kifani kwa Mheshimiwa ambapo hatujasikia hata kauli yake ya kulaani kitendo hicho ambapo damu ya Waislamu imefukiwa na mchanga. 

Imeshazoeleka tangu huko nyuma kwamba Waislamu wanafanywa mshumaa na wenyewe wakiwa wanalijua hilo, lakini wanapata kigugumizi cha kujinasua katika hali hiyo. Tukio hilo kama lilivyokuwa la Morogoro, watu wamefanya semina, makongamano mbalimbali na kupeana misimamo ya kila aina, lakini ajabu wakati ukifika na kutakiwa kutekeleza misimamo hiyo, watu wanakuwa wanasimama katika misimamo yao tofauti na ile waliyokubaliana. 

Mtume wa Mwenyezi Mungu na watu wake wakati huo alikuwa akihifadhi historia na kuifanyia kazi ambapo mpaka leo sisi tunaona na kusoma katika vitabu na kuona wenzetu wanavyojifunza kutokana na matukio. Kalenda yetu ya Kiislamu imeanza kutokana na matukio mbalimbali yakiwemo yale ya kuonewa na makafiri kama ilivyo hivi sasa hapa nchini na sehemu nyingine zenye dhulma kama hizi duniani. 

Sasa hivi kuna watu wameshaanza kuyasahau yale yaliyotokea Mwembechai na kuanza kuwakumbatia waliokuwa wanasema piga yule... ongeza nyingine...! Wakati watu walishapeana msimamo mpaka mwaka 2000 lakini yote yaliyokuwa yanafanywa sasa yataanza kuonekana ni bure. Wengine watakuambia serikali inatuhurumia bwana ndio maana imewaachia watu waliohusika na vurugu za Mwembechai. 

Umefika wakati sasa wa kuanza kujiuliza hivi sisi Waislamu kutokana na kupigwa mabomu na kudhalilishwa tangu 1994 kule Morogoro na hivi sasa Mwembechai tunajifunza nini? Hilo ni swali la msingi kwa kila Muislamu aweze kujiuliza na kujiangalia yeye binafsi amekuwa na msimamo gani kabla na baada ya matukio haya? 
 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI 

Serikali yaipongeza Africa Muslim Agency 
Na Mwandishi Wetu, Moshi 

Wanafunzi Wakatoliki darasa la saba 1998: 
Afisa Elimu akiri kutaka orodha ya wanafunzi 
Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

Athari ya milipuko Dar, Nairobi: Waliokufa wafikia 258 
Na Mwandishi Wetu 

Wakuu wa mashule waache ubaguzi 
Na Mwandishi Wetu 

ABU AMEENA: Mwana harakati aliyesilimisha wanajeshi 3000 wa Marekani -2 

Kisiwa cha Karafuu chageuzwa cha ulevi 

Twalaban wadhibiti Afghanistan yote 

Madina yachapisha kitabu cha rejea 

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA 

Maoni: Nyerere kasema kweli Ujamaa na Ukristo vimeshindwa 
Na Abdul Gullam 

Kina Ngatara na wenzake ndio urithi tulioachiwa na Wakoloni 
Na J. Hussein 

HOJA BINAFSI: Suala la Mwembechai, serikali imeumbuka 
Na Mwinjilisti Kamara Kusupa 

Kupigwa mabomu misikitini: Waislamu tumejifunza nini? 
Na RAJAB RAJAB

MAONI: Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu na ni uzushi mtupu!
Na Muhibu Said

Utangazeni Uislamu kwa nguvu zote – Sheikh Jongo
Na Badru Kimwaga

Salafiya wataka wanawake wawe macho na vyombo vya habari
Na Mwandishi Wetu

Waumini Misufini Morogoro waazimia kujenga Msikiti
Na Rajab Rajab, Morogoro

Serikali yatakiwa kuondoa askari Mwembechai
Na Badru Kimwaga

Mafunzo ya Quran 

Barua za wasomaji 

Mashairi 

Masomo 

Chakula na Lishe  
 
 

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita