AN-NUUR
Na.162 Rabiul Thani 1419, Agosti 14 - 20, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
MAONI
Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu na ni uzushi mtupu!

Nabii Issa ndio Yesu 
Lakini siyo ‘Yesu mfufuka’ aliyesulubiwa na Paulo 

NI upotofu wa dhahiri kudai kuwa Nabii Issa au Yesu hawahusiani, kwa kupachika shuhuda zisizohusiana na mada husika. Na baya zaidi ni kule kutumia hoja dhaifu na za uzushi kama alivyofanya Bw. Augustine F. Mwinuka na mwenzie Bw. Elia Batendi katika gazeti la Msemakweli toleo la Juni 28 hadi Julai 4 na Julai 5 hadi 11, 1998. 

Na Muhibu Said 

Kabla sijauweka bayana na kuujibu upotofu wao huo, yafaa kwanza nikaweka wazi hisia zangu kuhusu tabia na mwenendo mnaokwenda nao, Mhariri dhidi ya wasomaji wake hasa wa Kiislamu katika mjadala huu. 

Kwa kuathiriwa na imani yake ya Kikristo, Mhariri huyo amekuwa na msimamo lemavu wa kuwapendelea Wakristo wenzake na kutowatendea haki Waislamu katika kusimamia na kuzifanyia kazi barua zao katika mjadala huu. 

Inafahamika wazi kwamba kupitia gazeti lake hilo, mwanzilishis wa majadala huu ni Mkristo Bw. Elia Batendi wa S.L.P. 538 Dar es Salaam, ambaye chini ya kichwa cha habari "Issa wa Qur’an sio Yesu wa Biblia" alidai kuwa Waislamu wanaposema Yesu sio Mwana wa Mungu hiyo ni kashfa kubwa na wanastahili kuchukuliwa hatua kwa kuwa Yesu wa Biblia sio Issa wa Qur’an. Ni watu wawili wenye historia tofauti. 

Kufuatia madai na chonjo (fitna) hiyo ya Bw. Batendi dhidi ya Waislamu nilimpelekea Mhariri huyo barua fupi isiyozidi paragrafu tano yenye majibu kwa msomaji wake huyo (Bw. Batendi) ili afanye uadilifu kwa kuichapisha katika gazeti lake kama ilivyo. 

Katika barua yangu hiyo, chini ya kichwa cha habari "Yesu na Issa ni mtu mmoja" nilijaribu kumwonyesha Bw. Batendi kwamba majina kama vile Mussa, Moses, Yesu, Issa au Jesus ni maneno yanayomhusu mtu yule yule mmoja, yaliyo katika lugha tofauti lakini hudhihirishwa na historia za kauli na matendo yake hapa duniani. 

Nikamwonyesha pia kwamba "Uana" wa Yesu kwa Mungu umepelekea Wakristo wengi kumfanya naye (Yesu) kuwa Mungu na hivyo kuwafanya Miungu kuwa wawili, Yaani "Mungu Baba" aliyemtuma Yesu na "Mungu Mwana" ambaye ndiye Yesu mwenyewe! Ambapo ni kinyume kabisa na mafundisho yake (Yesu) mwenyewe ya kwamba Mungu ni mmoja (Marko 12:29) ambaye ni Baba yake na Baba yetu sote pia (Yohana 20:17). 

Nikamwambia ndio maana Qur’an Tukufu imeukana vikali Uana huo (9:30-32, 19:90-91, 112:1-4 na 6:101 -102). 

Mwisho, nikamsihi Bw. Batendi kwamba msimamo huo wa Qur’an Tukufu siyo kashfa na kama ameshindwa hoja aache kutia chonjo kwa kutaka kitabu hicho na waumini wake wachukuliwe hatua! 

Lakusikitisha, baada ya kupokea barua hiyo, Mhariri huyo kwa shingo upande akaichapisha katika gazeti lake, toleo la Juni 14-20, 1998 lakini akapotosha maudhui na mtiririko mzima wa barua yangu hiyo. 

Kwanza aliweka alama ya kuuliza (?) kwenye kichwa cha habari cha barua yangu hiyo kilichosema "Yesu na Issa ni mtu mmoja". Kichwa hicho kilibadilika na kusomeka "Yesu na Issa ni mtu mmoja?" Kana kwamba nilikuwa nauliza, wakati maudhui ya makala yangu yalilenga moja kwa moja kuonyesha kuwa Yesu na Isa ni mtu mmoja. 

Pili, ili kulidna madai potofu ya Bw. Batendi (Mkristo mwenzake) akapachika maneno mengi katika barua yangu hiyo kama vile kusema "maoni ya Batendi yamebainisha... n.k." kuonyesha kwamba ni mimi ndiye niliyesema maneno hayo wakati katika barua yangu hiyo sikutamka kitu kama hicho. Nilichotamka ni "Batendi amedai" na siyo "amebainisha". Ni kinyume cha maadili kubadili maana, tafsiri au muelekeo wa makala kama. Kama huridhishwi nayo ni uache kabisa kuichapisha. 

Lakutisha zaidi, Mhariri akakata maneno mengi niliyoandika badala yake akaweka maneno mengine ambayo hayahusiani kabisa na shuhuda (aya za Qur’an na Biblia) nilizozitaja katika barua yangu hiyo! 

Kwa hali hiyo, ikadhihirika wazi kwamba Mhariri ameathiriwa na imani yake ya Ukristo kiasi cha kupuuza maadili mazima ya Uhariri. Ikabaini pia kwamba Mhariri huyo alidhamiria makusudi kuniweka katika kona ili wasomaji wake Wakristo wapate kunishambulia mimi binafsi kwa maneno badala ya hoja zangu nilizotoa. 

Na kweli alikuwa ni Bw. M.N. Mshamu wa S.L.P. 22637 Dar es Salaam aliyeitumia fursa hiyo aliyopewa na Mhariri wake kwa kutupia kombora la maneno ya dharau na jeuri kwamba mimi ni dhaifu mwenye kufuata simulizi! (Rejea barua yake Uk. 4 katika gazeti la Msemakweli la Julai 12-18, 1998, chini ya kichwa cha habari kilichopewa wino mzito "Muhibu huna hoja". 

Pamoja na mashambulizi hayo, barua yake hiyo haikuwa na jipya zaidi ya kurudia madai yale yale yaliyo kwenye barua ya akina Batendi na Bw. Augustine aliyenishutumu mimi na Waislamu wengine wote kwamba hatujui kitu na tukajifunze kwake! 

Pamoja na kukilaani kitendo hicho cha kupotosha barua yangu, chini ya barua yangu hiyo, Mhariri huyo hakusita kujibu mapigo akitumia mbinu za ndumilakuwili kwa maneno yafuatayo: 

"Nakushukuru sana kwa busara uliyoitumia ya kuweka wazi yanayokukera. Tunapenda kuwa na wasomaji wa namna yako. Hata hivyo, naomba univumilie niseme kwamba kanuni za kazi yangu ya Uhariri ndizo zilizonilazimisha kupunguza baadhi ya maneno katika barua yako ndefu. Pili ningekuomba mara nyingine uzingatie tangazo letu katika ukurasa huu la kuleta barua fupi fupi na zisizo na lugha ya mzunguko. Ningependa kukuondoa wasiwasi kwamba nimeathirika na imani yangu kiasi cha kushindwa kukutendea haki, hilo si kweli na ninakaribisha barua nyingi kutoka kwako bila kujali ziko kinyume na imani yangu kiasi gani". Mwisho wa kunukuu. 

Kwa kweli ukiyatazama madai haya ya Mhariri wa Msemakweli utaona hayana kweli yote, kwani kazi ya Uhariri hairuhusu kupotosha barua, makala wala habari ya mtu kama alivyofanya katika barua yangu ile. 

Kanuni hizo alizodai kuzifuata mbona hakuzitumia kuwekea alama za kuuliza katika vichwa vya habari vya barua za wasomaji wake Wakristo walipoandika "Yesu wa Biblia sio Issa wa Qur’an" Kama alivyofanya kwenye barua yangu? Au kanuni hizo zinatumika tu katika barua za Waislamu? Pamoja na kumpelekea maswali haya mpaka leo bado hajajibu wala kuyachapisha. 

Pia nimempelekea barua ya tatu kujibu barua za wote walionishambulia na mwenyewe kukiri kuzipokea lakini hakuchapisha. 

Isitoshe, pamoja na kumwendea ofisini kwake huko Kurasini na kumtolea malalamiko yangu hayo kuhusu tabia yake hiyo ya upendeleo, alinishauri nisikate tamaa ya kumwandikia na kuniomba niwe nikimpelekea makala badala ya barua. 

Pamoja na kumpelekea makala hiyo, mpaka leo yapata zaidi ya mwezi mmoja bado hajaichapisha! Makala hiyo ni mfano wa hii ninayoiandaa sasa yenye majibu kwa ndugu Wakristo kuhusiana na mjadala huu wa "Yesu na Issa". 

Matokeo yake, amekuwa akiwapa akina Batendi na Bw. Augustine (Wakristo wenzake) uwanja mpana katika gazeti lake kutoa madai yao potofu kwa mapana na marefu. (Rejea Msemakweli la Juni 28 hadi Julai 4 na la Julai 5 hadi 11, 1998). 

Lakusikitisha, wakati Mhariri huyo anafanya upendeleo huo, ikumbukwe hapo kabla (kabla mwenyewe alivyokiri) alilazimika kukata na kupotosha barua yangu fupi iliyokuwa na paragrafu zisizopungua tano, lakini akarahisika kuchapisha barua ndefu ya Bw. Augustine iliyokuwa na paragrafu zaidi ya ishirini, maadam inatetea imani ya baadhi ya Wakristo! Kama huku si kuathiriwa na Ukristo badala ya kuzingatia maadili ya Uhariri ni nini?! 

Na ndio maana katika barua yangu moja ya majibu niliyompelekea ambayo hakuichapisha nilimshauri Mhariri huyo kama amenogewa na mjadala huu ni vizuri iwapo angejitokeza hadharani ijulikane wazi kwamba yeye pia ni mshiriki mmojawapo au aheshimu taaluma nzima ya habari kwa kubaki kuwa "refa wetu" vinginevyo, ningechukua fursa hii kuwaomba Waislamu wasijaribu kupeleka maoni yao katika gazeti hilo (la Msemakweli) kwa kuwa hawatotendewa haki hata kidogo. 

Kwa ufupi, hizi ndizo zilikuwa hisia zangu dhidi ya udhaifu huo wa Mhariri wa Msemakweli ambao naona nimwachie mwenyewe ataamua la kufanya. Baada ya hayo, sasa naona niingie katika kuzijibu hoja zote zilizotolewa katika katika nyakati tofauti na Bw. Batendi na mwenzake Bw. Augustine. 

Katika barua yake hiyo (Rejea Msemakweli toleo la Julai 5-11, 1998) Bw. Augustine alijaribu kutoa sababu sita, ikiwemo jina, ukoo, kuumbwa, kuzaliwa, Utume na matendo ya Nabii Issa au Yesu (a.s) kama hoja za kutofautisha majina hayo. 

Kwanza ningependa ieleweke kwamba hakuna tofauti kati ya Yesu na Issa kama anavyotaka kupotosha Bw. Augustine. Ila ninachoweza kukiri hapa ni kwamba "Yesu mfufuka" anayehubiriwa na Bwana Paulo huyo ni tofauti kabisa na Nabii Issa bin Mariamu. Na kwa mtu asiyeelewa vema maandiko kwa hali yoyote ile ndiye anayeweza kuchanganyikiwa juu ya "Yesu sahihi" ambaye ndiye Nabii Issa bin Mariam (a.s.). Na dawa yake ni kukubali kuelimishwa na si kujifanya kujua, matokeo yake ukapotosha ukweli. Hii ni hatari sana! Sasa hebu tuone upotofu wa sababu hizo alizozitaja Bw. Augustine za kutofautisha "Yesu na Issa". 

JINA 

Bw. Augustine anasema kimatamshi jina "Yesu" kwa Kiarabu ni "Yasu". Hivyo ndivyo aitwavyo na Waarabu Wakristo tangu zama za kabla ya Muhammad na ndivyo aitwavyo ndani ya Injili ya Kiarabu iliyotafsiriwa na Waraqa bin Naufal bin Asad kabla ya Utume wa Muhammad (Sahihi Muslim 1, Hadithi 301). Jina Issa linatokana na jina Ayas lenye maana ya "Wekundu uliozidiana na weupe" (Baidawi, Vol 1 Uk. 160) mwisho wa kukunuu. 

Jibu ni kwamba siyo kweli jina "Yesu" kwa Kiarabu ni "Yasu" kama anavyodai Bw. Augustine. Ukweli ni kwamba Waarabu Wakristo jina "Yasu" ndilo jina walilolipokea kutoka kwa wale waliowapelekea Ukristo ulianzishwa nje ya Uarabuni miaka mitatu baada ya Yesu au Nabii Issa (a.s) kuondoka. Na ndilo jina waliloliingiza ndani ya Injili ya Kiarabu. Na hii inafanana na jinsi baadhi hata ya Watanzania walivyopokea jina la yule Nabii Mbatizaji kwa matamshi tofauti. Baadhi yao walipokea kwa tamshi la "Yohana" (Kiyunani), wengine "John" (Kiingereza) na wengine "Yahya" (Kiarabu). 

Ataonekana wa ajabu atakayedai leo kwamba tamshi mojawapo katika jina hilo hapo juu kwamba ni la Kitanzania (Kiswahili) eti kwa vile wanaolitumia jina hilo ni Watanzania na limeandikwa ndani ya Injili ya Kiswahili! 

Pia Yesu kuitwa "mwokozi" hiyo siyo maana ya jina lake. Lakini "uwokozi" ni jina la kazi yake aliyopewa kuifanya (Mathayo 18:11). Hivyo, majina ya Yesu na Issa hayana maana yoyote zaidi ya kubaki kuwa ni majina tu. Na siyo lazima jina liwe na maana. Ila neno lenye maana ya "Wekundu uliozidiana na weupe" kwa Kiarabu (Baidawi Vol 1 Uk. 160) na siyo neno Issa. 

Kwa mantiki hiyo, sababu hiyo (ya jina) bado haijamtofautisha Yesu na Issa. Lakini kama ilivyo kwa Yohana, Yahya au John, basi Issa na Yesu ni yule yule mmoja aliyezaliwa na Bikira Mariam (Qur’an 3:45 na Luka 1:26-31). 

Isitoshe, Qur’an Tukufu ilipoeleza kwamba Nabii Issa siyo Mungu (5:72), hakusulubiwa (4:157-158), na ametumwa kwa wana wa Israeli peke yao (3:49), Waarabu waliokuwa Wakristo hapo kabla walimfahamu kwamba huyo ndiye "Yesu sahihi" aliyekana "Uungu" katika Biblia pia (Marko 12:29-34) na ndiye aliyenusuriwa kuuawa kama ilivyoelezwa na Qur’an Tukufu na Biblia pia (Waebrania 5:7) na kweli katumwa kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli peke yao (Mathayo 2:6 na 15:24). 

Kilichofuatia baada ya kuelewa hivyo walisilimu na kumfuata Mtume Muhammad (s.a.w) ambaye ndiye Mtume pekee aliyetumwa ulimwengu mzima (Qur’an 21:107 na Yohana 16:7-14). 

Pamoja na Waarabu hao, alisilimu pia aliyekuwa mfalme wa Ethiopia ya sasa (zamani Uhabeshi) Bw. Najash (Rejea historia ya maisha ya Nabii Muhammad (s.a.w.). 
 

Itaendelea toleo lijalo

  

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI 

Serikali yaipongeza Africa Muslim Agency 
Na Mwandishi Wetu, Moshi 

Wanafunzi Wakatoliki darasa la saba 1998: 
Afisa Elimu akiri kutaka orodha ya wanafunzi 
Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

Athari ya milipuko Dar, Nairobi: Waliokufa wafikia 258 
Na Mwandishi Wetu 

Wakuu wa mashule waache ubaguzi 
Na Mwandishi Wetu 

ABU AMEENA: Mwana harakati aliyesilimisha wanajeshi 3000 wa Marekani -2 

Kisiwa cha Karafuu chageuzwa cha ulevi 

Twalaban wadhibiti Afghanistan yote 

Madina yachapisha kitabu cha rejea 

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA 

Maoni: Nyerere kasema kweli Ujamaa na Ukristo vimeshindwa 
Na Abdul Gullam 

Kina Ngatara na wenzake ndio urithi tulioachiwa na Wakoloni 
Na J. Hussein 

HOJA BINAFSI: Suala la Mwembechai, serikali imeumbuka 
Na Mwinjilisti Kamara Kusupa 

Kupigwa mabomu misikitini: Waislamu tumejifunza nini? 
Na RAJAB RAJAB

MAONI: Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu na ni uzushi mtupu!
Na Muhibu Said

Utangazeni Uislamu kwa nguvu zote – Sheikh Jongo
Na Badru Kimwaga

Salafiya wataka wanawake wawe macho na vyombo vya habari
Na Mwandishi Wetu

Waumini Misufini Morogoro waazimia kujenga Msikiti
Na Rajab Rajab, Morogoro

Serikali yatakiwa kuondoa askari Mwembechai
Na Badru Kimwaga

Mafunzo ya Quran 

Barua za wasomaji 

Mashairi 

Masomo 

Chakula na Lishe  
 
 

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita