AN-NUUR
Na.162 Rabiul Thani 1419, Agosti 14 - 20, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Hoja binafsi
Suala la Mwembechai, serikali imeumbuka

Na Mwinjilisti Kamara Kusupa 

Awali ya mambo yote napenda nijitambulishe kama ifuatavyo:- 

(a) Kwa makufuru yenu mnayoyasema dhidi ya Bwana Yesu kama mwana wa Mungu na Mwokozi wa Ulimwengu, mimi siko pamoja nanyi. 

(b) Katika harakati zenu za kuichambua Biblia na kutoa tafsiri potofu za neno la Mungu mimi siko nanyi maana najua fika kwamba mnahitaji "ufunuo" wa Mungu mwenyewe ili kuyaelewa maneno ya Mungu na mafumbo ya Mungu ambayo yalitolewa na watu wa rohoni yaani mitume na manabii wake, hivyo ninyi kwa kutumia akili na fahamu za kibinaadamu kabisa hamwezi kuyaelewa, kwa nukta hii siwezi kubishana nanyi. 

(c)Wala katika lugha yenu mnayoitumia kwenye mihadhara yenu kuielezea (to define) BAKWATA, na jinsi mnavyowaelezea Sheikh Mkuu Mufti Hemed bin Jumaa, Mkuu wa mkoa Mheshimiwa Yusuf Makamba, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Ali Ameir, Makamu wa Rais Alhaji Omari Juma, na wengineo, mimi siko nanyi. 

Lakini katika harakati zenu za kupinga dhuluma na uonevu unaofanywa na dola dhalimu na utawala wa kikandamizaji, mimi ni "mjahidina" mia kwa mia, niko pamoja nanyi, na ninaunga mkono yote mnayoyasema na yote mnayoyadai, na pia ninawapenda kuwasababu ya ujasiri. 

Suala la mauaji ya kutumia risasi dhidi ya watu wasiokuwa na silaha pale Mwembechai, ilipasa lilaaniwe na Watanzania wote pasipo kujali tofauti za kidini au kisiasa miongoni mwetu kwasababu serikali ilitumia nguvu kubwa na zisizohitajika, maana ni mfano wa mtu anayetumia nyundo kuua nzi aliyetua juu ya meza ya kioo, matokeo yake anavunja meza yote. 

Dini zingine kuyanyamazia mauaji ya Mwembechai ni kujidanganya kwani kisingizio hicho hicho kilichobatizwa jina jipya la "vurugu za kidini za Mwembechai" kinaweza kutumiwa kuzuia injili isihubiriwe na pengine kuendeleza wimbi la mauaji kwa wananchi wengine watakaotumia lugha yenye kuiudhi serikali. 

Wabunge wote walipaswa kukemea tabia hii ya kishetani ya serikali ya kuua watu kirahisi kama vile kuua swala au digidigi na pia walipaswa kumlazimisha Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Ali Ameir kuomba radhi, na kuahidi serikali kuwalipa fidia ndugu wa marehemu badala ya kutetea. 

Sijui Ali Ameir alikuwa anatetea nini na kwa niaba ya nani maana hata kama anataka tuamini kwamba Wahubiri hao wa Kiislamu (waliokuwepo siku hiyo) ni wakorofi wa kupindukia, na vijana kama akina Chuki Athmani walikuwa na makaratasi ya uchochezi tena yanayotoka nchi za nje, bado kuna swali. Je dawa yake ndiyo iwe hiyo ya kupiga mtu risasi? Tangu lini serikali ikafanya vita na wananchi wake wanaodanganywa na mataifa mengine badala ya kupambana na mataifa hayo! 

Nasema wazi kwamba kwa jinsi Waziri Ameir alivyojigonga katika kujibu hoja ya Mbunge Kitwana Kondo, serikali imeumbuka. 

Kwanza Waziri Ameir alisema mengi yasiyokuwa na uhakika kiasi cha kusababisha mtu yeyote aliye mkweli mbele ya nafsi yake, hata kama si mshiriki wa mambo ya Mwembechai ajiulize ni kwanini serikali iseme uwongo? 

Kama kuna ukweli wowote, basi ilikuwa ni jukumu la serikali kuuthibitisha, lakini cha ajabu ni kwamba baada ya watu kufunguliwa mashitaka na kusota rumande kwa siku kadhaa waishie kuachiwa kwa kufutiwa mashitaka kwa madai kwamba hawana mashitaka ya kujibu, kumbe walikamatiwa nini, na awali walishitakiwa kwa kosa gani? Au walishitakiwa kwa makosa ya kubuni? Hapa yanahitajika maelezo (definition) ya kisheria kutoka kwa Andrew Chenge kama mwanasheria mkuu na siyo blah! blah! za Ameir kama wanahabari. Vinginevyo kama Mheshimiwa Ameir bado anang’ang’ania msimamo wa kutaka tusadiki maneno yake, basi mwisho wa yote itabidi ajiuzulu kwasababu majibu na maelezo yake yamepwaya sana maana mauaji ya Mwembechai hayawezi kuhalalishwa kwa namna yoyote ile, yanafanana na mauaji ya 1976 huko Mwanza na Shinyanga dhidi ya waliotuhumiwa uchawi ambayo mwisho wa mambo yote Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi kama Waziri wa Mambo ya Ndani alilazimika kujiuzulu, kumbe Ameir anangoja nini? 

Imekuwa ni kawaida kwa serikali hii kuwafutia washitakiwa mashitaka dhidi yao kwa kutumia kifungu hicho cha NOLI PROSECUI lakini hii inaweza kufanya wananchi wengine tusiojua kinachoendelea kwenye mfumo wa sheria tuhisi kwamba ni aidha watu wamepewa hongo ama serikali imeshindwa kupata ushahidi wa kuthibitisha mashitaka, hata baada ya upelelezi wa muda mrefu. Sasa kama serikali ndiyo imeshindwa, ina maana imetumia mwanya huo kuonea tu raia asiye na hatia na pengine kukomoa mtu aliyeiudhi, ni kwanini watu wasiwajibike? Ni kwanini serikali haikupeleleza kwamba kabla ya kuwakamata watu na kuwashitaki? 

Serikali haiwezi kuwa mlinzi wala mtetezi wa imani 

Dhana ya baadhi ya Waislamu kwamba serikali ya CCM inawapendelea Wakristo ni dhana potofu kwani serikali haiwezi kuwa mlinzi wala mtetezi wa imani ya Kikristo, hivyo kama ilichukua hatua za aina ile pale Mwembecahi, ni kwakuwa ilikuwa na lake jambo. 

Inavyoelekea viongozi wakuu wa serikali walikuwa wamekasirishwa na mashutumu ya wahadhiri na kwahiyo kila neno lilifanywa kwa niaba ya hasira zao na siyo uchungu wa kuitetea imani ya Kikristo, kwani tangu lini YESU akatetewa na nguvu za dola? Tangu siku za kuwepo kwake duniani, Bwana Yesu hakuruhusu nguvu yoyote toka nje itumike kumlinda au kumtetea. Kwa mfano alipokuwa kwenye Bustani ya Getsemane wakati wa kukamatwa kwake ili aende kusulubiwa, mwanafunzi wake mmoja aitwaye Petrol (Kifa) alichomoa upanga na kutaka kumuua mmoja wa wale waliokuja kumkamata Yesu, lakini kwa bahati mbaya pigo lake Petro likakosa shabaha, mtu yule aliepa na upanga ukampitia sikioni, ukamkata sikio lake likaanguka chini. Lakini Bwana Yesu akaliokota sikio lile na kumfanyia mtu yule uponyaji ambao ulikuwa ni muujiza wake wa mwisho, kisha akamwamuru Mtume wake Petro kwa kusema, rudisha upanga wako alani mwake kwani kila atumiaye upanga, naye ataanguka kwa upanga au wadhani siwezi kumwomba baba naye akaniletea majeshi kumi na mawili ya malaika? Ndiyo maana nasema Yesu hawezi kutetewa na nguvu za dola, hivyo kama serikali imeua pale Mwembechai isihusishe mauaji yake na imani ya Kikristo ni bora iseme wazi kwamba ilikusudia kuwakomoa wale waliotaka kushindana nayo, kwasababu ilikuwa na uchungu wa kutukanwa. 

Kitendo cha Wakristo kukaa kimya na kutokukemea mauaji ya Mwembechai kinatokana na ukweli huu kwamba kwa ndugu zangu Walokole, ni woga na kukosa ujasiri wa kuiambia ukweli serikali kwa hofu kwamba wasije kuharibu uhusiano mwema na kujitia katika misukosuko. Ambapo kwa watu kama Wakatoliki ni sera ya kanisa lao ndiyo ambayo hairuhusu muumini wa kawaida kusema lolote linalohusiana na kanisa badala yake viongozi wakuu hasa maaskofu ndiyo wasemaji. 

Kwahiyo kwa watu kamaWaislamu wasioelewa kinachoendelea katika madhehebu mbali mbali ya Kikristo wanaweza kudhani Wakristo wanaafiki au wanafurahia vitendo vya serikali kama lile tukio la Mwembecahia kumbe sivyo. Zaidi ya yote ni vema ikaeleweka wazi kwamba kanisa katoliki la Roma halina historia ya kupigania haki popote pale duniani ambapo haki inakiukwa badala yake lina historia ya kujitambulisha na watawala wakandamizaji na wadhulumaji na hasa itokeapo kwamba watawala hao wapo kudumisha maslahi ya ubeberu wa aina fulani. 

Kwa kutoa mifano iliyo hai wakati inatokea vita kuu ya pili ya dunia, kanisa lilikuwa na nguvu sana nchini Ujerumani na sehemu zingine za Ulaya hata hivyo, lilishindwa kukemea na kudhibiti Ubeberu wa Adolf Hittler na kusababisha dunia nzima kuingia katika maafa na hasara isiyoweza kufidiwa. Hata wakati wa harakati za kuikomboa Afrika, kanisa halikutaka kabisa kujitambulisha na wapigani uhuru ingawaje lilibaini na kuona dhahiri madhambi ya Ukoloni wa Wazungu katika Afrika. 

Pamoja na kuujua fika ukweli kwamba YESU kama mwana wa Mungu alikuja duniani ili kuwaweka wanadamu huru, maana anena wazi katika injili yake kwamba, "Basi mwana akiwaweka huru, nanyi mtakuwa huru kweli kweli." 

Uhuru unaozungumzwa hapa ni uhuru kamili yaani uhuru wa kiroho na kimwili pia. Uhuru wa kimwili ni pamoja na uhuru wa kimawazo, uhuru wa kiuchumi, uhuru wa kisiasa, na uhuru wa kijamii, hata hivyo bado kanisa halikusimama na kweli. Matokeo yake ni kwamba baadhi ya nchi ziliunda misimamo mibaya na mikali dhidi ya dini ya Kikristo. 

Kwa mfano nchi kama Msumbiji chini ya utawala wa Samora Machel ilisigana sana na kanisa Katoliki, dhana ya kwamba Wakoloni wa Kireno ni Wakatoliki iliichachua sana FRELIMO hali ambayo ilipelekea hata Injili kuhubiriwa kwa taabu sana nchini Msumbiji. Lakini mambo hayakuishia hapo, kwani hata baada ya uhuru Kanisa liliendelea kushikamana na watawala dhalimu na madikteta kwa Afrika walioridhia nafasi za wakoloni. Kanisa liliona haya kukemea udikteta na ukandamizaji wa marais kuzidi mkoloni. 

Ni katika ukimya huo ndipo hata kanisa likakwepa kuchukua majukumu dhidi ya mauaji ya halaiki nchini Rwanda, ingawaje asilimia kubwa ya Wanyarwanda ni Wakatoliki. 

Ni utawala wa Vatikani peke yake ndio uliodumisha uhusiano mwema na serikali zote za Makaburu wa Afrika Kusini enzi za mfumo wa kibaguzi pasipo kulaumiwa licha ya kwamba Afrika Kusini zamani hizo ilikuwa imetengwa na Jumuia ya Kimataifa. 

Hata Rais Nyerere ambaye zamani hizo alisifika kwa kuwaambia ukweli mataifa makubwa lakini alipofikia kwenye suala la uhusiano kati ya serikali ya Vatikani na serikali za akina Johannes Vorster na akina Pik Botha, Nyerere alisema kwa adabu na unyenyekevu wa hali ya juu kwamba "kwa bahati mbaya kumbe hata serikali ya Baba Mtakatifu nayo imo." 

Ieleweke wazi kwamba hapa nalitaja kanisa kama taasisi ya kidunia na siyo lile kanisa la Yesu linalonenwa katika Biblia, kwani neno kanisa kibiblia lina maana tofauti kabisa na maana ya kanisa kama inavyoelezwa kwenye kamusi, au kama ilivyozoeleka kwenye msamiati wa dunia hii. Hata baada ya kuja wimbi la mageuzi ya kisiasa ya kuondoa ukiritimba wa chama kimoja bado kanisa halikutaka kutubu balilikajiepusha kabisa na wote wenye harakati za kuleta mabadiliko. 

Nakumbuka mnamo 1991 wakati huo nikiwa kwenye kamati ya kuiandaa Tanzania kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi, kamati ambayo tuliita "The Steering Committee for Transition to Multi-Party Democracy", chini ya Uenyekiti wa Chifu Abdallah Fundikira, na umakamu wa Mzee James Mapalala, na ukatibu wa Wakili Mabere Marando, na uweka Hazina wa Mwandishi Ndimara Tegambwage, niliwahi kuitgwa na muadhama Polycarp Pengo ofisini kwake wakati huo akiwa bado Askofu Mkuu wa jimbo la Dar es Salaam. 

Katika mazungumzo yake alionyesha wazi kwamba mimi nahitaji kusaidiwa kwasababu nimepotea katika kujumuika na watu kama hao niliowataja hapo juu. 

Askofu Pengo hakuona "logic" ya mtumishi wa Mungu kuipinga serikali, nilipomuuliza ni kwanini Pope John Paul wa II amejumuika tena mstari wa mbele katika kupinga na kuipiga vita siasa ya kikomunisti alijibu ni kwasababu ukomunisti unamnyima mtu haki ya kumwabudu Mungu. Nilipomuuliza tena kwamba lakini binaadamu ana haki zingine zaidi ya ishirini zilizo sawa na hiyo haki ya kuabudu, na kwamba waliozitangaza walizitoa (extract) kutoka kwenye Biblia, hapo Askofu alipoteza uvumilivu baada ya maneno mengi akajibu kwa jazba kwamba "nadhani I am not prepared", akaondoka kwenda kupata chakula cha mchana. 

Jioni ya siku hiyo, nilipokwenda nyumbani kwa Mwenyekiti wangu Chifu Fundikira kumweleza juu ya mazungumzo yangu na Askofu, naye Chifu Fundikira akanieleza mambo yanayofanana na hayo niliyokutana nayo mimi, akanieleza kwamba aliitwa nyumbani kwa Sheikh Mkuu Mufti Hemed bin Jumaa, naye Mufti alitaka kujua sababu hasa inayomfanya yeye Fundikira kuanzisha "movement" ya kuipinga serikali wakati nchi imeshikwa na Mwislamu mwenzake! Hapo nikaanza kubaini udhaifu wa viongozi wa dini katika kuleta mabadiliko ya msingi katika jamii. 

Serikali na tabia ya usingiziaji 

Nasema serikali imeumbuka kwa sababu imeshindwa mambo mengi kwanza imeshindwa kulichukulia suala la mihadhara kama inavyotarajiwa kufanywa na serikali iliyopevuka na yenye uzoefu katika mambo ya utawala, kufanya uchunguzi, kupata hakika ya mambo yote, na kujua hatua gani ianze na ifuatie nini. Kwa kutoa mfano hai mnamo miaka ya 1987 na 1988 wakati kitabu cha Bw. Salmin Rushidie kinachohusu Aya za shetani (stanic Verses) kilipoingia nchini, Sheikh Mkuu alikisoma na kuishauri serikali kwamba baada ya kukipitia ana uhakika kwamba maandiko yake yanaukashifu Uislamu na yanaweza kuumiza hisia za waumini kama kitaendelea kuuzwa nchini hivyo serikali ikaitikia wito wake ikakipiga marufuku na kuamuru yeyote mwenye nacho akipeleke serikalini au kwa Sheikh Mkuu. Vivyo hivyo ingetazamiwa kwamba katika suala la mihadhara ya Waislamu, Serikali ingefanya uchunguzi na kupata hakika ya mambo yote kiasi kwamba hata inapomkamata mtu haifanyi kwa kubahatisha bali kwa uhakika kabisa kwamba fulani bin fulani, ukiwa mahala fulani, saa fulani, umetoa mahubiri yanayofanana na aya za shetani, umeumiza hisia za akina fulani, hivyo umetenda kosa kinyume na kifungu fulani cha sheria, sasa tunakushitaki. Kwa njia hiyo hatia ya mtu ingekuwa dhahiri na kwa mantiki hiyo pia tofauti kati ya mahubiri ya kweli yenye nia ya kueneza Uislamu ingekuwa dhahiri, na mahubiri yenye nia ya kuumiza hisia za wengine nayo yangekuwa dhahiri lakini kinyume chake serikali imefanya usingiziaji mwingi ambao haijulikani ni kwa manufaa ya nani na unamnufaishaje huyo! 

Tabia ya usingiziaji ni ya hatari sana na hasa inapofanywa na serikali, leo anasingiziwa Chuki Athumani lakini kesho atasingiziwa mwananchi mwingine awaye yote hata hao wanaojidhania wana uhusiano mzuri na serikali iliyoko madarakani. Tayari mfano umejionyesha kuwa Kanisa la Full Gospel linaloongozwa na Askofu Kakobe mara atishiwe kufutiwa usajili kwa kisingizio kwamba anapora mikufu ya dhahablbu ya wanawake, mara asingiziwe kwamba ana mali nyingi, mara asingiziwe kuhubiri siasa madhabahuni, lakini mimi najua wazi kwamba sababu iliyoiudhi sana serikali ni moja nayo ni ile ya Kakobe kupigania katiba mpya basi. Haifai serikali kubeba ajenda za siri na kulipiza visasi. 

 
 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI 

Serikali yaipongeza Africa Muslim Agency 
Na Mwandishi Wetu, Moshi 

Wanafunzi Wakatoliki darasa la saba 1998: 
Afisa Elimu akiri kutaka orodha ya wanafunzi 
Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

Athari ya milipuko Dar, Nairobi: Waliokufa wafikia 258 
Na Mwandishi Wetu 

Wakuu wa mashule waache ubaguzi 
Na Mwandishi Wetu 

ABU AMEENA: Mwana harakati aliyesilimisha wanajeshi 3000 wa Marekani -2 

Kisiwa cha Karafuu chageuzwa cha ulevi 

Twalaban wadhibiti Afghanistan yote 

Madina yachapisha kitabu cha rejea 

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA 

Maoni: Nyerere kasema kweli Ujamaa na Ukristo vimeshindwa 
Na Abdul Gullam 

Kina Ngatara na wenzake ndio urithi tulioachiwa na Wakoloni 
Na J. Hussein 

HOJA BINAFSI: Suala la Mwembechai, serikali imeumbuka 
Na Mwinjilisti Kamara Kusupa 

Kupigwa mabomu misikitini: Waislamu tumejifunza nini? 
Na RAJAB RAJAB

MAONI: Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu na ni uzushi mtupu!
Na Muhibu Said

Utangazeni Uislamu kwa nguvu zote – Sheikh Jongo
Na Badru Kimwaga

Salafiya wataka wanawake wawe macho na vyombo vya habari
Na Mwandishi Wetu

Waumini Misufini Morogoro waazimia kujenga Msikiti
Na Rajab Rajab, Morogoro

Serikali yatakiwa kuondoa askari Mwembechai
Na Badru Kimwaga

Mafunzo ya Quran 

Barua za wasomaji 

Mashairi 

Masomo 

Chakula na Lishe  
 
 

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita