|
Na. 045 Jumatano Aprili 26 - Mei 2, 2000 |
|
|
|
|
|
Maisha mema ya akhera Mtunzi: Marcussy G. Mzee MWILI wa Josephine ukateremshwa kaburini taratibu
na huo ndio ukawa mwisho wa maisha yake hapa duniani na mwanzo wa maisha
mapya ya akhera. Waombolezaji waliendelea kufukia kaburi huku nyimbo za
maombolezo zikiendelea kuimbwa. Je, kulikoni mkasa huu? Ungana na mwandishi
katika hadithi hii ya kusisimua.
ILIKUWA ni vigumu kujizuia kwa umati wote wa watu wazee,vijana, wakubwa, watoto, wake kwa waume waliohudhuria mazishi yake, karibu kila sura ya mmoja wapo pale iligubikwa na simanzi na majonzi tele. Esther dada mkubwa wa marehemu Josephine sauti nzito ya kilio ilimtoka pale aliposikia maneno yaliyotamkwa na aliyekuwa akiongoza mazishi aliposema "Binadamu ni mavumbi, na mavumbini atarudi, eeh Bwana uliyetoa na leo umetwaa mpokee Bi. Josephine katika makazi yake ya milele na umpumzishe mahali pema PEPONI". Ulikuwa ni msururu mrefu wa watu wakitia udongo ndani ya kaburi huku kila mmoja akimuombea marehemu maisha mema ya Akhera. Baada ya kaburi kumalizika kufukiwa, ilifuata zamu ya kuweka mashahada ya maua, kisha hotuba ndefu na yenye kutia hudhuni kwa waliobakia hai hapa duniani, wakiendelea na maisha. Mzee Nyabange na Mkewe Bi. Luciana walijitahidi kwa hali na mali kumsomesha Bint yao pekee kwani katika uhai wao walifanikiwa kupata watoto wawili tu wote wa kike, Esther na Josephine. Lakini Esther aliamua kuacha shule akiwa darasa la tatu na kukimbilia mjini Dodoma kutafuta maisha mazuri. Josephine kichwa chake hakikuweza kabisa kumudu masomo,hata alipomaliza elimu ya msingi hakuweza kupata nafasi ya kuendelea na masomo zaidi, lakini baba yake mzee Nyabange akamtafutia shule ya sekondari ya binafsi, juhudi za Mzee Nyabange zilifanikiwa na kumwezesha Josephine kuanza elimu ya sekondari ya kulipia ya Jamhuri iliyopo mjini Dodoma. Kwa kuwa katika kijiji chao cha Mvumi hakukuwa na shule yoyote ya sekondari hivyo akawa anasoma shule ya Bweni,siku za mwisho wa wiki alipata fursa ya kwenda kumtembelea dada yake Esther aliyekuwa akiishi katika mtaa wa Mwangaza Mjini Dodoma. Kimaisha Esther hakuwa katika hali mbaya, kwani alikuwa anafanya kazi katika Hoteli moja maarufu sana mjini humo "Saturday Hotel". Mshahara na marupurupu aliyoyapata kidogo vilimsaidia kuona mwanga mzuri wa maisha ya mjini. Kisichoriziki hakiliki,juu ya huduma nzuri aliyokuwa akipatiwa Josephine toka kwa Baba na Mama lakini bado aliambulia alama za chini darasani, lakini wazazi walishikamana kwa pamoja ili kumsaidia mtoto wao apate elimu. Miaka minne ikakatika Josephine akawa amehitimu masomo ya kidato cha nne, hakurudi kijiweni'nyumbani', akabaki kwa dada yake kusubiri majibu ya mtihani wake, na yalipotoka Josephine akawa amefeli. Kurudi kijijini kujishughulisha na kilimo pamoja na wazazi wake akaona haina maana, Esther akamkaribisha Josephine ili kuanza maisha mapya ya utafutaji. Katika pita pita ya huko na huko hatimaye Josephine akapata kazi katika mgahawa wa 'Whimpy'. Mjini ni mjini kuna watu wengi wenye mawazo tofuati, mjini kumejaa raha, karaha na majigambo mengi. Wanaume wengi waliofika pale "WHIMPY" kupata vinywaji vidogo vidogo wakavutiwa na Josephine, maumbile ya kuvutia aliyokuwa nayo yaliwachanganya akili wanaume na waume za watu. Urefu wa wastani, rangi maji ya kunde, sura nyembamba, macho meupe ya duara yaliyo zingirwa na kope nyingi, kifua cha wastani kilichobeba matiti madogo mithiri ya ngumi ya mtoto mdogo na katikati aligawanyika vizuri hivyo kumfanya awe na umbo namba nane. Meno meupe yaliyojipanga vizuri mdomoni ya kitenganishwa na mwanya mdogo vilizidisha uzuri wa Josephine ambao ulikamilishwa na miguu iliyojengeka vizuri na afya njema. Tabia ya upole, ucheshi na tabasamu vilifanya kila mwanaume ajaribu bahati yake. Mwanzoni alikuwa na msimamo mzuri wa kutotaka kuchezewa chezewa na wanaume malaghai, lakini ahadi alizopata na kutimiziwa zilimfanya Josephine aivunje amri ya sita! Baada ya kuonja asali akachonga mzinga. Vijana watatu walimchanganya akili Josephine nao ni Mohamed Kikolo au "Baba Mwasiti" Omari Msegeju na mwingine Hashim au "Baba Titanic". Kwa kutumia ujanja wake alikutana nao wote hao kwa nyakati tofauti. Esther alipogundua mwenendo usio wa kuridhisha wa Josephine akamuweka chini na kumuonya juu ya tabia yake hiyo, lakini Josephine aliyapitishia sikio la kulia na kutokea kushoto. Asiye sikia la mkuu huvunjika guu, heka heka za Josephine za kuwachuna wanaume ziliingia dosari baada ya kujigundua ni mja mzito wa miezi mitatu. Baada ya kuwafuata mabwana zake, wote wakamtolea nje. Hakuna aliyekubali msalaba ule. Bosi wake naye akamshindilia msumali wa moto pale alipoamua kumfukuza kazi kutokana na kugundulika ya kwamba ni mjamzito. Mawazo ya kuitoa ile mimba yakawa yamekitawala kichwa chake, lakini alipewa onyo kali toka kwa dada yake kwa kumuasa asijaribu kuitoa ile mimba kwani anaweza kupata matatizo makubwa na pengine kifo. Maneno na vitisho vya Esther havikumzuia Josephine kuitoa mimba. Kwa kujiiba akafika hospitalini, hapo akakutana na daktari mmoja aitwaye Dokta John. Kwa tamaa ya pesa, Dokta John akakubali haraka kuifanya kazi ile, huku akijua wazi anafanya kosa kubwa la mauaji. Josephine akaongozwa hadi kwenye kijichumba kidogo, mlango ukafungwa na mara shughuli ikaanza. Baada ya shughuli hiyo ya hatari kumalizika Josephine alirudi nyumbani huku akilalamika kuumwa na tumbo. Esther akambana kwa maswali ili aeleze tumbo linamuuma vipi, lakini aliishia kulalamika kwa maumivu makali yaliyokuwa yakimsokota tumboni. *********** Ni wiki moja imepita tangu Josephine atoe mimba.Baada ya kuona hali ya Josephine inazidi kuzorota, Esther akamchukua Josephine mpaka Hopsitali akapata huduma ya kwanza. Akapewa kitanda katika wodi ya wagonjwa wanaokuwa chini ya uangalizi maalum. Hali ya Jose ikazidi kuwa mbaya, ndipo akakiri kwa kusema ametoa mimba kwa Dokta John. Alipopigwa picha ya 'X-RAY' ikagundulika ile mimba haikutoka yote na hakusafishwa vizuri. Hivyo kulitunga usaha kwa ndani. Matumaini ya kuendelea kuishi yakatoweka na juhudi za Madaktari kuyaokoa maisha ya Josephine zikagonga mwamba. Masikini msichana mrembo Josephine alfajiri ya Jumanne roho yake ikatengana na mwili akaiaga dunia huku anaipenda. **************** Gari ya polisi TZH 5656 inapaki nje ya nyumba ya Dokta John, anafungwa pingu kuelekea Polisi kujibu shitaka la kujaribu kuitoa mimba ya Josephine na kusababisha kifo. Kifo cha Josephine kilimshtua kila mtu pale mtaani. Watu wengi walimpenda. Tabia yake ya ukarimu na upendo ilimfanya apendwe na wengi. Mipango ya mazishi ikapangwa na watu wengi walihudhuria mazishi yake. Wazazi wa Josephine walishindwa kujizuia, wakalia mpaka wakazirai. Msafara wa kuelekea maeneo ya Kizota kwa mazishi ulianza huku waomboleazaji wakiimba: "EWE BINADAMU! BAHATI IPI KUIAGA DUNIA KWENDA MBINGUNI KWENYE TULIZO NA MAKAZI YA MILELE!" Mwili wa Josephine ukateremshwa ardhini taratibu na huo ndio ukawa mwisho wa maisha yake hapa duniani na mwanzo wa maisha mapya ya Akhera. Muongozaji wa mazishi Ndugu Anthony akaendelea na hotuba, "Ndugu mliohudhuria mazishi haya leo Josephine ameiacha dunia, lakini hiki kifo hakikimbiliki. Ingekuwa ni hivyo basi marehemu angekikimbia. Pia ikumbukwe marehemu angejua kuwa kifo chake kingetokea Hopsitali asingefika huko, tuliobaki tuwe makini na maamuzi ambayo hatima yake ni mauti. Lakini zote hizi ni njia za kupitia kuelekea mbinguni", alimalizia maelezo yake, kisha waombolezaji wakaendelea na ufukiaji wa kaburi huku nyimbo a maombolezo zikiendelea kuimbwa:- "NIAGIENI... NIAGIENI... NIAGIENI WAZAZI WANGU... MIMI NAKWENDA KWA MUNGU BABA SINTORUDI MILELE EEE!" Baada ya mazishi watu wakapanda magari kurudi majumbani mwao kuendelea na maombolezo ya mwisho. "JOSEPHINE ULALE SALAMA, KAZI DUNIANI UMEMALIZA, JOSEPHINE ULALE SALAMA, LALA, LALA, SALAMA." Tamati
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Serikali iache udini, kuwagawa wananchi - Sheikh Mbukuzi Wakati
Kanisa Katoliki likitoa miongozo ya kisiasa:
Hakuna maendeleo bila Demokrasia - Lipumba MPASHO NASAHA
HABARI
‘Suala la kuirekebisha jamii lisiachwe mikononi mwa Serikali pekee’ Jiandikisheni na pigeni kura -Balozi Tanzania
kufutiwa madeni:
Ushauri Nasaha
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Lishe
RIWAYA
|
|
|
|
|