|
Mashairi
Ni sheria au woga? (Swali)
Malenga ninaingia, uwanjani nina hamu,
Swali nina watupia, nipate jibu fahamu,
Siku nyingi nawazia, nashindwa jibu fahamu,
Ni sheria Isilamu, au woga wa safari?
Isilamu napotaka, kwenda Makka kuhijia,
Ndugu na jamaa hata, huanza kuzungukia,
Msamaha kuutaka, wote alowakosea,
Ni sheria Kiislamu, au woga wa safari?
Nusra Marijani,
S.L.P. 800, Bukoba
Mbona twapigana vita
Ar-hamani jalia, Mola aso na kifani,
Uliye umba dunia, na ambavyo vilo ndani,
Japo nipate pambia, NASAHANI gazetini,
Mbona twapigana vita.
Shangazi lao naomba, kwa Mola alo niumba,
Niepushe na kuomba, vita visije nikumba,
Vita vya kuyumbayumba, sio vita ila vumba,
Mbona twapigana vita.
Siwezi shika silaha, wala mdomo chongoa,
Kwani nisije kuhaha, malumbano kujutia,
Wala huu si mzaha, ndugu zangu kuwambia,
Mbona twapigana vita.
Sambamba vita siwezi, lazima nitaumia,
Kwani siyo yangu kazi, ambayo nilo zoea,
Vita vyataka ujuzi, kwa walio na vifua,
Mbona twapigana vita.
Beti tano naishia, Editori zatoshea,
Mbele sinto endelea, maneno yamenishia,
Dua yangu naombea, vita kuniondolea,
Mbona twapigana vita.
Bint Swaleh (Shangazi lao),
Kinondoni.
Natafuta kadi nembo ya mizani (ushauri)
Zainab dada yangu, wala usihuzunike,
Yapoze yako machungu, sasa usihangaike,
Sikia shauri wangu, ili KADI uishike,
Kuipata ndugu yangu, Tawi la CUF ufike.
Kwani hapo ziko chungu, yanini uhangaike,
Ukikosa uje kwangu, zipatikapo tufike,
Naapahaki ya Mungu, USAWA msingi wake,
Kadi hiyo dada yangu, rahisi kupata kwake.
Ila kwa wake RUBANI, ngoja chaguziifike,
Utamuona KURANI, ni LIPUMBA jina lake,
Au kwenye kampeni, lazima hukoafike,
Zainab dada yangu, ushauriuushike.
Kafuzu wake rubani, kadi hiyo chama chake,
Miongoni Duniani, uchumi rahisi kwake,
Kadi ya CUF jamani, MIZANI ninembo yake,
Kuipata dada yangu, TAWI LA CUF ufike.
Kaditama mwisho wangu, wakuige wanawake,
Wote wawe namachungu, kadi hiyo waisake,
Waache yao majungu, HAKI SAWA ipatike,
Kuipata dada yangu, TAWI LA CUF ufike.
Almasi H. Shemdoe,
“Tunda la Matumaini”,
Dar es Saaam.
Sera gani (Jibu)
Kwanza kwako Mola wangu, utukuke Rahmani,
Unilinde wangu Mungu, na madhalimu nchini,
Nimjibu ndugu yangu, ili sera abaini,
Sera kwa upeo wangu , kwa CCM UONGO.
Sera gani manenoni, kutimiza hatuoni,
Sera ganichaguzini, wakishinda huwaoni,
Sera gani za udini, na kwao ndiko jikoni,
Sera kwa upeo wangu, kwa CCM UONGO.
Sera gani za amani, na vita hatuvioni,
Sera gani za utuni, Zanzibar wafanya nini?
Sera gani za madeni, kuomba waacha lini?
Sera kwa upeo wangu,kwa CCM UONGO.
Sera ganiza rushwani, nao washika sukani,
Sera gani za dumuni, wenyewe wanadi nini?
Sera mimi sizioni, Mtagaluka amini,
Sera kwa upeo wangu, kwa CCM UONGO.
Tasa beti ni mwishoni, ninakuaga mtani,
Wallahi nishasaini, beti fupi kwenye fani,
Sera ni hiyo amini, mimi kwangu akilini,
Sera kwa upeo wangu, kwa CCM UONGO.
Almasi H. Shemdoe, “Tunda la Matumaini” S.L.P. 33265, Dar es
Salaam,
Tanzania.
Hafai kuwa kiongozi
Kwa jina la Maulana, Mola wa Mbingu na Nchi,
Mungu alosifikana, kwa wakongwe na wabichi,
Ujumbe twaelezana, sote raia wa nchi,
Hatufai kiongozi, mwenye chuki za kidini.
Udini ukilitana, kwa viongozi wa nchi,
Raia watakitana, na kisha iyumbe nchi,
Makoo watachinjana, wakongwe hata wabichi,
Hatufai kiongozi, mwenye chuki za kidini.
Mtanzania mwanana, uishike hii tochi,
Njia uwe waiona, usijitie ubishi,
Tutajakukamatana, na hiyo ndio nukusi,
Hatufai kiongozi, mwenye chuki za kidini.
Yeyote yeyote Watanzaia, aliyekaa kitini,
Bora tukimchunia, asirudie kitini,
Dhamana aloishikia, shukrani kanisani!
Hatufai kiongozi, ana chuki za kidini.
Yeye nawakumbushia, aliyekaa enzini,
Amrialiyeridhia, piga yule msikitini,
Hakikahii kadhia, alipanga kanisani,
Hatufai kiongozi ana chuki za kidini.
Zinduka Mtanzania, ubaya huu oneni,
Haya mkiyafumbia, lana itakukuteni,
Wapi tutakimbilia, dhoruba kikukuteni?
Hatufai kiongozi, ana chuki na raia.
Haya ndugu wananchi, mijini na vijijini,
Na wala sio Wadachi, mlozaliwa nchini,
Shikeni hii ndio tochi, tumuondoe kitini,
Dhalimu kumrudisha, ni kuiharibu nchi.
Haya wana Tanzania, ya dini tuyajadili,
Kuacha kurupukia, wewe shika maadili,
Waloacha Manabia, ya Mungu aso mithili,
Ya dini yende kidini, dola acha kutumia.
Yadini ni ya raia, siyo ya kuparamia,
Wapo wanayajulia, ndugu acha kujitia,
Viongozi slamia, wa kanisa nao pia,
Ya dini yende kidini, dola nini watakia?
Haya wa maofisini, polisi nako jeshini,
Mungu wenu abuduni, na haki pia shikeni,
Yule alo Mumiani, asiwatie dhambini,
Hawafai viongozi, wasiojali raia.
Jehannamu yake Mungu, nani atakuondoa,
Si mweusi, si mzungu, nani aje kutetea?
Jiondowe hilo fungu, la motoni kuingia,
Dunia isiwe pingu, hebu anza jitetea.
Kumi na mbili vifungu, hapa ndio naishia,
Ninayaona machungu, wafalme wa dunia,
Watu wa Mwenyezi Mungu, ndio wanawachukia,
Sijuwi kwa yeye Mungu, vipi watajitetea?
Juwa dunia mapito, kwa Mungu utarejea.
Na Hanaphy B.J. Mtinga,
Masasi Mtwara
Hilo ni tunda gani? (Washindi)
Naja nikifarajika, Wallahi nafurahika,
Namshukuru Rabuka, tunda jibu kupatika,
Fumbo lililo fumbika, wazi limebainika,
Tunda ni mimi hakika, Shemdoe natamka.
Tunda la Matumaini, mwishoni huwa naweka,
Ni langu ushairini, jina linalotumika,
Ni Mtanga asilini, Lushoto ndiko natoka,
Tunda ni mimi hakika, Almasi Shemdoe.
Ni mweusi kubalini, ameniumba Rabuka,
Ninapendeza machoni, sijui kukasirika,
Mimi si tunda mtini, hapo mmepakumbuka,
Tunda ni mimi hakika, Shemdoe natamka.
Ninauzwa Nasahani, wangu ujumbe kumbuka,
Rafiki wa karibuni, kwa JUSHAKA nimefika,
Ndio mana wa mwanzoni, tundajibu kutamka,
Tunda ni mimi hakika, Almasi Shemdoe.
Wacha niwapitisheni, washindi mliopata,
Bure nisiwachosheni, tama mkaja kukata,
Mtagaluka kawini, “Sugu” Jushaka kapata,
Tunda ni mimi hakika, Shemdoe natamka.
Pole ndugu Mtaun, Kilwa Kiwawa nakupa,
Sio CUF Mtaun, tunda ni mimi naapa,
Niamini Mtaun, vigezo nimeshakupa,
Tunda ni mimi hakika, Shemdoe natamka.
Kupitia Nasahani, jamii naelimisha,
Mimi mwalimu ummani, umma ninaadilisha,
Mimi niwapo fanini, jamii nawaidhisha,
Tunda ni mimi hakika, Almasi Shemdoe.
Shufwa beti ni mwishoni, nawapongeza kabisa,
Nliofuza fumboni, nimeridhika kabisa,
Kweli tu-moto fanini, NASAHA sasa latesa,
Tunda ni mimi hakika, Almasi Shemdoe.
Almasi H. Shemdoe “Tunda la Matumaini”
S.L.P. 33265, Dar es Salaam.
Mkorogo ni haramu (Sisitizo)
Kwa mara nyingine tena, Mhariri nipokee,
Nasema nikiungana, haya tusiyamezee,
Ndugu Zalia kanena, Mkorogo siendee,
Mkorogo ni haramu, jambo hili mfahamu.
Siendee Mkorogo, wala usisogelee,
Akina dada wadogo, vijana hata wazee,
Swala hili la mikogo, lazima tulikemee,
Mkorogo ni haramu, jambo hili mfahamu.
Weusi kakupa Mungu, ili wewe uvutie,
Hatujaona Mzungu, weusi akimbilie,
Iweje wewe Mwenzangu, maradhi jitafutie,
Mkorogo ni haramu, jambo hili mfahamu.
Mola hajawakataza, vipodozi mjitie,
Vikwatuzi vyashangaza, ngozi mkazichubue,
Jama mnajitatiza, lazima niwaambie,
Mkorogoro ni haramu, jambo hili mfahamu.
Waume kwetu muhimu, hili kamwe sililee,
Haya kwetu majukumu, elimu tulitolee,
Tumepewa na karimu, wanawake tuwalee,
Mkorogo ni haramu, jamho hili mfahamu.
Hebu Kaka Kijukuu, kwa yakini tuambie,
Shemeji akija juu, wewe umuangalie?
Awaka kama kifuu, sheria ulegezee?
Mkorogo ni haramu, jambo hili mfahamu.
Naona nisiwachoshe, beti saba niishie,
Mtakuja mchemshe, wanandani msikie,
Ya Raufu sijivishe, kwake ssote kimbilie,
Mkorogo ni haramu, jambo hili mfahamu.
Rajab Saidi Kidangi (Rasaki),
S.L.P. 90329, Dar es Salaam.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Acheni kuwacheza shere
Waislamu, ondoeni udini
Serikali
iache udini, kuwagawa wananchi - Sheikh Mbukuzi
Wakati
Kanisa Katoliki likitoa miongozo ya kisiasa:
Sheikh
mwingine ahojiwa Mwanza
Hakuna
maendeleo bila Demokrasia - Lipumba
MPASHO NASAHA
KAMCHEZO
AU?
HABARI
Sheikh
Jongo asababisha mtafaruku mbele ya Al-Haji Mwinyi
‘Suala
la kuirekebisha jamii lisiachwe mikononi mwa Serikali pekee’
Jiandikisheni
na pigeni kura -Balozi
Tanzania
kufutiwa madeni:
Wananchi
hawatarajii nafuu yoyote
Ushauri Nasaha
Vyombo
vya habari na vijana - 2
MAKALA
Sababu
‘1000’ kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani - 4
Kalamu ya Mwandishi
Muungano
watimiza miaka 36 kwa migogoro
MAKALA
Chama
cha Mapinduzi na sera za maendeleo (1)
Lishe
Jinsi
ya kutunza virutubisho wakati wa maandalizi ya vyakula
Habari
za Kimataifa
RIWAYA
Maisha
mema ya akhera
MASHAIRI
MICHEZO
Raoul Shungu apigwa ‘Dafrao’
Yanga wamfurusha Waziri Mudhihir
uwanjani
Simba wampongeza Msajili wa
Vyama
|