NASAHA
Na. 045 Jumatano Aprili 26 - Mei 2, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
HABARI

Tanzania kufutiwa madeni: 
Wananchi hawatarajii nafuu yoyote

Na Mwandishi Wetu

HOTUBA ya Rais Benjamin Mkapa juu ya azma ya nchi wahisani na mashirika ya fedha ya kimataifa kuifutia madeni Tanzania imepokewa kwa hisia tofauti huku idadi kubwa ya wananchi waliotoa maoni yao ikionesha kutotarajia nafuu yoyote katika hali ya maisha kutokana na misamaha hiyo ya madeni.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili wameonesha kushitushwa na kiwango kikubwa cha fedha kilichokuwa kimekopwa lakini hawaoni jambo lililofanyika nchini kulingana na fedha hiyo. 

Aidha, wananchi hao wameliambia NASAHA kwamba, hivi sasa maisha ni ghali sana ikilinganishwa na hali ilivyokuwa huko nyuma, maoni ambayo yameonekana kutoa picha tofauti na kauli ya serikali kwamba MFUMUKO WA BEI UMEPUNGUA HAPA NCHINI. 

Bw. Eudes Msaki ambaye alijitambulisha kuwa ni mfanya biashara na mkazi wa Tabata jijini, amesema anaamini fedha hizo zilikopwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini haoni kama malengo ya mikopo hiyo yalifikiwa "tulikopa kwa ajili ya kuleta maendeleo lakini leo hatuoni tulichofaidika kutokana na mabilioni yote hayo", alisema Bw. Msaki. 

Bw. Msaki pia alionesha wasiwasi iwapo mikopo mipya itakayoingia Tanzania baada ya kufutiwa madeni yake itawafaa wananchi kama inavyokusudiwa. 

"Sasa tumesamehewa (madeni) natunakopeshwa tena lakini sijui kama manufaa tutayaona hata baada ya hiyo miezi tuliyotangaziwa tusubiri" alisema mfanyabiashara huyo na kisha kuhoji kwa hamaki, "....lakini hawa sio ndio wale wale waliopokea mikopo ya kwanza na CCM ndio ile ile?!" 

Wakati akilihutubia taifa kwa njia ya radio hivi karibuni, Rais Mkapa alisema manufaa ya msamaha ya madeni yataanza kuonekana katika kipindicha miezi 18 baada ya mpango wa kufutiwa madeni kutekelezwa. Hata huyo Mhe. Rais hakutaja mpango huo ungeanza kutekelezwa lini. 

Mwananchi mwingine ambaye alidai kuwa ni mhasibu katika hoteli moja maarufu hapa jijini alisema, kushuka kwa mfumuko wa bei kulikotangazwa na serikali hakujaonekana katika maisha ya kila siku. Kwa vile bei za mahitaji ya wananchi zipo juu sana. "Sidhani kama inflation imeshuka kwa sababu chochote unachokigusa dukani bei yake utazimia.... Hata hotelini kwetu tunalazimika kutoza boarding fee kubwa kwa sababu hiyo" alisema mwanchi huyo alipozungumza na NASAHA katika kivuko cha Magogoni akielekea nyumbani kwake Kigamboni. 

Bi Situmai Masudi anayefanya biashara ya chakula (Mama Lishe) eneo la Feri Magogoni aliliambia NASAHA kuwa hali ya miasha na ngumu sana ambapo uwezo wa shilingi kununua mahitaji umepungua. 

"Labda mimi sielewi huu mfumuko wa bei kaka yangu (akikusudia mwandishi) mwaka jana nikienda sokoni nilikuwa ninajaza (mfuko wa) rambo kwa shilingi 5,000, lakini mwaka huu elfu tano inakatika na ninachonunua hakifiki hata nusu tu ya rambo", alieleza Bi. Situmai. 

Akiendelea kusimulia jinsi hali ya maisha ilivyopanda siku hizi, Mama Lishe huyo ambaye kwa jina la biashara anajulikana kama "Mama Ntilie" alisema, huko nyuma biashara ilikuwa inatoka sana nilikuwa ninalipa hata 'skulifiz' za wanangu, lakini sasa hata ya madaftari inanipiga chenga, wateja hawana hela, wanashinda hapa Feri bila kula. 

"Kaka yangu nikwambie nini wauza chakula wenzangu wawili mambo yamewashinda.... Meza zao zilikuwa moja hapo na mwingine pale....." alisema 'Mama Lishe' huku akionesha sehemu walizokuwa wakifanyia biashara wenzake wawili. 

Mwananchi mwingine, Bw. Kitenge, aliyejieleza kuwa ni mstaafu wa iliokuwa Jumuiya alitoa maoni yaliyoonesha msimamo ulioonesha kuwavuta watu wakimsikia akizungumza na mwandishi wa habari hizi. 

Bw. Kitenge alisema, imefutiwa madeni iliyokuwa ikidaiwa na nchi za nje tu na mashirika ya fedha lakini madeni yake kwa wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki yapo hayakufutika. 

"...madeni ya Mwingereza yamefutiwa, madeni ya Mfaransa yamefutwa madeni ya IMF... yamefutwa lakini.... Lakini sisi tuliokuwa community bado tunaidai serikali", alisema Bw. Kitenge kwa sauti ya juu kiasi cha kuwavuta watu waliokuwa karibu. 

Miezi michache iliyopita, serikali iliwalipa mafao wastaafu wa Jumuiya hiyo, mafao amnbayo wengi wa wastaafu hao waliyalalamikia kwamba ni madogo sana. Wakati wa malipo ya mafao hayo yaliyofanyika mwishoni mwa mwaka uliopita, mstaafu mmoja aliambulia hundi ya sh.130/- tu. Wastaafu hao hivi sasa wamefungua kesi mahakamani wakidai serikali haikufanya hesabu sahihi katika kutathmin mafao yao. Aidha, wastaafu hao wanadai kuwa malipo waliyopewa yanahusu nini hasa kwa mujibu wa mkataba wao wa kazi. 

Mwanafunzi mmoja wa kidato cha sita, Devota Mrindoko, amesema nchi za Ulaya na mashirika ya kimataifa kuifutia madeni Tanzania sio hisani wala huruma kwa vile nchi hizo huzikopesha nchi maskini baada ya kuzinyonya. 

"Kwa miaka kadhaa Ulaya imekuwa ikizinyonya nchi changa kama yetu (Tanzania) hivyo wanapotufutia madeni hawahifanyii hisani bali wanaturudishia kilicho chetu", alieleza mwanafunzi huyo. 

Mama Sumari aliyejitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa siku nyingi serikali hakuilaumu serikali kwa lolote bali anaona ni vema Wantanzania wakaendelea kuvuta subira. 

"aliyoyaeleza Rais ndio hali halisi, tuvute subira, hiyo miezi kumi na nane hakuanza leo na kama ni kuumia tumekwisha umia siku nyingi", alisema Mama Sumari.

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Acheni  kuwacheza shere Waislamu, ondoeni udini

Serikali iache udini, kuwagawa wananchi - Sheikh  Mbukuzi

Wakati Kanisa Katoliki  likitoa miongozo ya kisiasa:
Sheikh mwingine ahojiwa Mwanza

Hakuna maendeleo bila Demokrasia -  Lipumba

MPASHO NASAHA
KAMCHEZO  AU?

HABARI
Sheikh Jongo asababisha mtafaruku mbele ya Al-Haji Mwinyi

‘Suala la kuirekebisha jamii lisiachwe mikononi mwa Serikali pekee’

Jiandikisheni na pigeni kura -Balozi

Tanzania kufutiwa madeni:
Wananchi hawatarajii nafuu yoyote

Ushauri Nasaha
Vyombo vya habari na vijana  - 2

MAKALA
Sababu ‘1000’ kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani - 4

Kalamu ya Mwandishi
Muungano watimiza miaka 36 kwa migogoro

MAKALA
Chama cha Mapinduzi na sera za maendeleo (1)

Lishe
Jinsi ya kutunza virutubisho wakati wa maandalizi ya vyakula

Habari za Kimataifa

RIWAYA
Maisha mema ya akhera

MASHAIRI

MICHEZO

  • Raoul Shungu apigwa ‘Dafrao’ 
  • Yanga wamfurusha Waziri Mudhihir uwanjani
  • Simba wampongeza Msajili wa Vyama

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita