|
Na. 045 Jumatano Aprili 26 - Mei 2, 2000 |
|
|
|
|
|
Muungano watimiza miaka 36 kwa migogoro NA MAALIM BASSALEH LEO ni tarehe 26 Aprili, 2000. Ni siku ya kumbukumbu ya muungano wa nchi zetu mbili, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzinbar. Ilikuwa ni tarehe kama hii ya leo, miaka 36 iliyopita, wakati Marais wa nchi mbili hizi, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanganyika, na Marehemu Abeid Amani Karume wa Zanzibar, walipokubaliana kuziunganisha nchi mbili hizi na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muungano huu ungelikuwa ni chombo cha baharini, basi chombo hicho kitakuwa kimefika hapa kilipo baada ya kukumbana na mawimbi na dhoruba za kila aina. Ingawa hivi sasa inaonekana kana kwamba, mambo, ndani ya muungano ni shwari, lakini, kamailivyo bahari, wakati wo wote, inaweza kuchafuka na kuiyumbisha muungano kwa mara nyingine tena. Waasisi wa muungano huu wamekuwa wakieleza kuwa waliamua kuziunganisha nchi mbili hizi, kutokana na sababu za kihistoria. Wanasema wananchi wa nchi mbili hizi wana asili moja na uhusiano wa karibu. Ni kweli Watanganyika na Wazanzibar wote ni Waafrika. Hilo halina ubishi. Na wala Zanzibar kuwa ni kisiwa hakuwezi kuwa ndiyo sababu ya kuvitenganisha visiwa hivyo vya Zanzibar na Bara la Afrika. Kwa vile wahenga wamesema "umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu", basi kitendo cha kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar, ni hatua moja ya kutupeleka katika umoja wa Bara la Afrika. Hakuna ye yote anayelitakia mema bara hili akapinga nchi mbili au zaidi za Afrika kuungana. Lakini muungano wa nchi ni maridhiano baina ya wananchi wa zile nchi zinazohusika. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwa na migogoro mingi tokea ulipoundwa. Nini kilichosababisha migogoro hiyo? Au kwa vile wananchi hawakushirikishwa? Japo kuwa Watanzania wanatakiwa waamini kuwa muungano huu umezaliwa kutokana na fikra za waasisi wake, Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume, lakini wapo wanaodhani kuwa kuna mkono wa nje uliouzaa mpango huu na kufanikisha utekelezaji wake. Miongoni mwa wenye mawazo hayo ni Babu, aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Umma kilichokuwa kikifuata siasa za mrengo wa kushoto za nchi za kisoshalisti. Komredi Abdul-Rahman Babu anadai kuwa Muungano wa Tanzania ulishinikizwa na Marekani, kwa kupitia shirika lake la kijasusi la CIA, ili kuvizuia visiwa vya Zanzibar visiingie katika mikono ya Wakoministi. Katika utangulizi wake wa kitabu kiitwacho, "Uhasidi wa Marekani kwa Mapinduzi ya Zanzibar", kilichoandikwa na Amrit Wilson, Babu anasema, "Kitabu hiki kinatoa dhahiri shahiri mbele ya kadamnasi, maelezo ya kusisimua juu ya matukio ya mwaka 1964 nchini Zanzibar. Wengi wetu tuliokuwa tumehusika tulikuwa tukiamini kwamba madola makubwa (superpowers) yalikuwa yakipanga njama za kuyavuruga mapinduzi hayo, lakini hakuna mmoja kati yetu aliyeweza kutoa ushahidi wa kutosha kuthibitisha shaka hiyo." Babu anaendelea kusema, "katika kitabu hiki, kwa mara ya kwanza kabisa, tunapata ushahidi wa kutosha juu ya mbinu zilizotumiwa na Marekani ili kuyazima mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 na kuunda kwa makusudi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika muundo mahsusi wa Tanzania wenye kufuata mwelekeo wa kisiasa wa nchi za Magharibi." Babu anamalizia maelezo yake kwa kusema, "kutoka kwenye nyaraka za Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na za Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) tunaweza kuona kwa kinaganaga jinsi maafisa wa Kimarekani walivyoweza kubuni mbinu zilizowawezesha kutekeleza jukumu lao la kupinga mapinduzi na umuhimu walioutoa kwa jambo hilo." Katika kutaka kuthibitisha kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokana na mpango wa Marekani wa kutaka kulinda maslahi yake dhidi ya nchi za Kikoministi , Mwandishi wa Kitabu hicho, Bibi Amrit Wilson anaeleza, "siku ya tarehe 5 Machi (1964), Dean Rusk (Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, katika kipindi hicho) alituma simu kwenye ofisi za ubalozi wa Marekani Dar es Salaam, Nairobi na Kampala, kuwaagiza maafisa wa Marekani kuwasihi Nyerere, Kenyatta na Obote wamfahamishe Karume kuhusu hatari ya chama cha ASP kumtegemea BABU na hatari anayoleta Babu..... kwa usalama wa Zanzibar na Afrika Mashariki kwa jumla....." Uk.51. Simu hiyo ya Dean Rusk ililenga katika kuwashawishi viongozi wa nchi za Afrika Mashariki wawatanabahishe Nyerere na Karume juu ya hatari iliyokuwa inaweza kuletwa na Babu na makomredi wenziwe katika nchi zao. Kwa mujibu wa maelezo yaliyomo ndani ya simu hiyo inaonesha Marekani ilikuwa ikimwona Kenyatta kuwa alikuwa akiuelewa vyema ubaya wa Babu. Ndiyo Marekani ilipoona jitihada zake za kuwataka Nyerere aiunganishe Tanganyika na Zanzibar zimegonga mwamba ikaona imwombe Kenyatta awashawishi Nyerere na Karume juu ya kuziunganisha nchi zao, kwa usalama wao wenyewe. Simu hiyo iliendelea kusema, "Haitakuwa jambo la busara kuifufua tena kwa Nyerere, mbali ya kukataa kwake kwa awali, fikra ya shirikisho la Zanzibar -Tanganyika kama njia mojawapo ya kumpa nguvu Karume na kupunguza mamlaka ya Babu? Hatua kama hiyo kwa wakati huu itasaidia pia kuimarisha nafasi yake mwenyewe Nyerere. Siku hiyo ikamalizia kwa kusema, "vinginevyo, ukichukulia mwenendo wa Kenyatta kwa Babu, itakuwa vizuri kujaribu kwanza kumshawishi yeye atoe ushauri kwa Nyerere juu ya manufaa ya shirikisho la Zanzibar na Tanganyika, kama hatua ya kwanza kuelekea kwenye shirikisho kubwa la Afrika Mashariki Uk.51. Lakini, kama kweli muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulikusudiwa uwe ni changa moto na mfano kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki, haifahamiki kwa nini basi Uganda na Kenya zikasita mpaka hii leo kujiunga na muungano huu? Huenda migogoro iliyojitokeza ndani ya muungano huu, katika hiki kipindi cha miaka 36, ndiyo iliyopelekea nchi nyingine za Afrika Mashariki zishindwe kujiunga. Mgogoro mkubwa, ambao umekuwa ukijitokeza, mara kwa mara, ni ule wa kila upande, katika pande mbili za Muungano, yaani Tanganyika na Zanzibar, kudai kuwa unapunjwa na upande wa pili. Wakati Wazanzibari wanadai kuwa Tanzania Bara inataka kuimeza Zanzibar, na Watanganyika wanadai kwa nini Zanzibar iwe na serikali yake ndani ya Muungano wakati ile ya Tanganyika imeuawa? Hapo ndipo inapochipuka ile hoja ya kuwa na shirikisho la serikali tatu - serikali ya Tanganyika na serikali ya Muungano; jambo ambalo Mwalimu Nyerere, katika uhai wake, alilivalia njuga kwa kulipinga kwa nguvu zake zote. Na aliyejitokeza kutetea serikali tatu alimnyamazisha kwa gharama yo yote ile. Kitendo cha Rais Mstaafu wa Zanzibar, wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Aboud Jumbe, kumwandikia barua Nyerere kumweleza kuwa kwa mujibu wa waraka wa makubaliano ya Muungano ya 1974, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ulikusudiwa uwe ni wa shirikisho lenye serikali tatu, na siyo mbili, au moja, kama inavyodaiwa na CCM -Bara, kilimsababishia Jumbe ajiuzulu nyadhifa zake zote, katika chama na serikali. Na lile kundi la Wabunge 55 wa Bara, G55, walipotaka iwepo serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, Nyerere wakati huo akiwa amekwisha ng'atuka Urais wa Tanzania na uenyekiti wa CCM, alisimama kidete kuwapinga wabunge hao na kulisambaratisha kundi lao. Aliandika na kitabu kuwasema na kuwakosoa aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamo Mwenyekiti wa CCM, Mzee Malecela na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Hayati Kolimba, kwa kile alichodai, kumshauri vibaya Rais Mstaafu, wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Al-Hajj Ali Hassan Mwinyi. Lakini hilo halijaweza kuinyamazisha ile hoja ya kuwa na muungano wenye mfumo wa serikali tatu. Kama Mwalimu Nyerere alistahiki kupewa pongezi kwa kufanikisha kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar, basi pia, anastahili kulaumiwa kwa kuweka mfumo wa muungano wenye kero nyingi? Na usiokubalika! Katu migogoro ndani ya muungano, katika huu mfumo wa serikali mbili haitakoma. Kila itakapochomoza itatumiwa mizengwe kuinyamazisha. Lakini hiyo si dawa! Njia pekee ya kumaliza migogoro hiyo ni kwa pande mbili kwa kutafuta mfumo, utakaokubalika na pande zote mbili. Kudai kuwa muungano huu ni wa serikali mbili kuendea serikali moja, ndiyo sera ya CCM nindoto ya mchana! Ikawa CCM-Bara inaota hivyo, ijue kuwa CCM-Visiwani, haitakubali, hata siku moja, kuiua na kuizika serikali ya Zanzibar kwa mikono yake yenyewe. Labda ilazimishwe kwa mkong'oto! CCM-Visiwani, inakubali mfumo wa serikali mbili, kwa sababu mfumo huo unadhamini kuwapo ile serikali ya Zanzibar; lakini kama mfumo huu utataka kubadilishwa na kuwekwa mfumo wa serikali moja tu; basi CCM-Zanzibar itakuwa tayari kuukubali mfumo wa serikali tatu, unaotakiwa na CUF, kuliko kukubali mfumo wa serikali moja. Kwa sababu mfumo wa Serikali tatu utaiwezesha serikali ya Zanzibar kuendelea kuwapo. Katika huu mfumo wa vyama vingi, mfumo ya serikali mbili utaendelea kuwapo, katika ule muda ambapo chama cha CCM kitaendelea kuwapo katika madaraka; lakini jee kama CUF Zanzibar itashinda katika uchaguzi mkuu ujao itakubali kuendelea na mfumo wa serikali mbili? Itakuwa kila serikali inayoingia madarakani ibadilishe muundo wa muungano? Kwa nini hatuweki mfumo unaokubalika na wote, ili upate kuheshimiwa na wote? Hivi sasa wakati tunasherehekea miaka 36 ya Muungano, kuna habari kwamba wafanyabiashara wa Zanzibar wamegoma kuleta bidhaa Bara, kwa sababu ya kutozwa ushuru mara mbili. Wakiingiza bidhaa Zanzibar kutoka nje wanatozwa ushuru na wanapozileta Bara, kwa ajili ya kutafuta soko, hutozwa ushuru mara ya pili? Swali hili si la leo. Ni la siku nyingi sana.
Basi kwa nini halitafutiwi njia mwafaka ya kulitatua? Au sera ya muungano
huu ni kuendeleza migogoro?
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Serikali iache udini, kuwagawa wananchi - Sheikh Mbukuzi Wakati
Kanisa Katoliki likitoa miongozo ya kisiasa:
Hakuna maendeleo bila Demokrasia - Lipumba MPASHO NASAHA
HABARI
‘Suala la kuirekebisha jamii lisiachwe mikononi mwa Serikali pekee’ Jiandikisheni na pigeni kura -Balozi Tanzania
kufutiwa madeni:
Ushauri Nasaha
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Lishe
RIWAYA
|
|
|
|
|