|
Na. 045 Jumatano Aprili 26 - Mei 2, 2000 |
|
|
|
|
|
Jinsi ya kutunza virutubisho wakati wa maandalizi ya vyakula CHAMOS, H.J PAMOJA na jamii kufahamu umuhimu wa aina mbalimbali za vyakula na pia kuvitumia katika milo yao ya kila siku, bado kuna udhaifu katika matayarisho yake yanayopelekea upotevu wa virutubisho vingi muhimu. UPOTEVU huu mara nyingi hutokea katika kuhifadhi, maandalizi na hata wakati wa kupika. Waweza kuandaa chakula ambacho tayari virutubisho vyake havipo; yaani umevipoteza bila wewe kufahamu. Tunawezaje basi kuzuia upotevu huu. Unaponunua vyakula angalia vile ambavyo ni halisi (freshi) na visivyokuwa na mipasuko au matobomatobo. Hii itasaidi kuzuia mipenyo ya virutubisho na pia kuoza. Vyakula ambavyo ni fresh visiachwe muda mrefu bila kupikwa baada ya kuvunwa au kununuliwa, kwani tendo hili laweza kuhatarisha kupotea kwa virutubisho. Hili unaweza kulifahamu kwa kuchunguza ukubwa au ujazo wa kitu halisi ambao hupungua. Mathalani mboga za majani kama mchicha husinyaa na kupungua uzito na ujazo wake, ikiashiria kuwa kuna sehemu zimepotea kwa kufyonzwa. Unapohifadhi au kuvuna vyakula angalia usivitie makovu. Sehemu za kuhifadhia zisiwe na nyuso zenye kukwaruza. Vyakula vyenye makovu ni rahisi KUINGILIWA NA WADUDU NA HIVYO KUOZA HARAKA. Iwapo unakausha matunda au mboga za majani kwa ajili ya kuhifadhi ni vyema ufanye kwa haraka ili kupunguza upotevu wa vitamin C. Kwa vyakula vyenye vitamini A, kama karoti, endapo vitakaushwa kwa matumizi ya baadaye, basi ni vyema kuviweka kwanza kwenye maji ya moto kwa muda mfupi, ili kuua vimeng'enyi (enzymes) ambavyo huozesha vyakula. Baada ya hapo vyakula vianikwe kivulini ili kuzuia uharibifu wa vitamin A kutokana na jua. Mbogamboga za majani zihifadhiwe sehemu zenye ubaridi na hewa ya kutosha, si lazima iwe ni kwenye jokufu, pia unyunyuziaji wa maji maji huweza kubakiza mbogamboga katika hali yake ya uhalisia (fresh) kwa muda mrefu. Wakati wa kuosha mbogamboga, osha kiasi cha kuzisafisha tu, na wala usizioshe kwa muda mrefu kamwe usiziloweke kwenye maji kwani vitamini C hupotea kwa kuloweka au kuosha sana mbogamboga, hasa zilizokatwa katwa. Kwa upande wa mapishi, mbogamboga zipikwe kwa muda mfupi kiasi tu cha kuiva, hali ya kuwa rangi yake ni ileile. Chungu au sufuria ya kupikia lazima ifunikwe na mfuniko safi, usiokuwa na kutu. Baadhi ya watu hutumia mifuniko yenye kutoa kutu ambayo hudondokea kwenye chakula. Kutu si nzuri kwa afya zetu. Iwapo mbogamboga zimekuwa na mchuzi mwingi, mcheuzi huo usimwagwe bali utumike kutengenezea supu mbalimbali ambazo zitatumika kabla au baada ya mlo. Kamwe usimwage mchuzi huo kwani virutubisho vingi huwa vimeyeyukia humo. Kukaanga kwa muda mrefu mbogamboga kwa mafuta, hupelekea upotevu wa vitamini A. Hivyo basi ni vyema kukaanga kidogo tu kiasi cha kulainisha. Vyakula viliwe mara tu baada y kupikwa hasa mbogamboga. Ni vizuri kupika mbogamboga kiasi tu kitakachotumika ili zisibakie kwani zinapopashwa moto hapo baadaye, huwa zinapoteza vitamini hasa vitamini C. Mchele usioshwe zaidi ya mara mbili. Ikiwezekana mara moja ni vizuri zaidi. Wala usiloweke mchele ndipo uoshe, bali osha mara tu baada ya kutia maji. Na baada ya kuosha, chuja maji yote uache mchele ukilowana wenyewe bila maji. Kuloweka au kuosha sana mchele kunapunguza virutubisho (thiamine). Tukijitahidi kuthamini vitu vidogo basi na vikubwa pia tutavithamini. Vyema kuzuia upotevu wa vitu hivi vidogo vidogo lakini vinavyotufanya tuishi. |
YALIYOMO
TAHARIRI
Serikali iache udini, kuwagawa wananchi - Sheikh Mbukuzi Wakati
Kanisa Katoliki likitoa miongozo ya kisiasa:
Hakuna maendeleo bila Demokrasia - Lipumba MPASHO NASAHA
HABARI
‘Suala la kuirekebisha jamii lisiachwe mikononi mwa Serikali pekee’ Jiandikisheni na pigeni kura -Balozi Tanzania
kufutiwa madeni:
Ushauri Nasaha
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Lishe
RIWAYA
|
|
|
|
|