NASAHA
Na. 045 Jumatano Aprili 26 - Mei 2, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA 
 

Sababu '1000' kwanini tunataka CCM ing'oke madarakani - 4

Mnyonyaji nambari wani wa walalahoi

Na Mwijilisti Kamara Kusupa

MOJA ya Sababu za TANU kutoa Azimio la Arusha mwaka 19967 ilikuwa ni kuondoa unyonyaji kati ya mtu na mtu, au kundi moja kunyonya kundi jingine. TANU kama chama cha ukombozi kilikuwa kimedhamiria kwa dhati kabisa kuondoa mfumo wa matabaka ambao uliachwa na mkoloni. Enzi za mkoloni Watanganyika waligawanywa katika matabaka matatu, kulikuwa na raia wa daraja la kwanza yaani Wazungu, na raia daraja la pili yaani Waasia na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa, na raia waligawanywa katika makundi mawili wakulima wadogo au peasants kama walivyoitwa na wafanyakazi.
 

UWEZO wa kiuchumi, maisha bora au maisha duni, umasikini au utajiri, ulitegemea mtu anatoka tabaka gani. Kwasababu ya tofauti ya kipato kati ya Mwafrika (mweusi) na Mzungu au Mhindi (mweupe) ni dhahiri kwamba wenye uraia wa daraja la tatu ndio waliokuwa maskini kuliko matabaka mengine. 

Baada ya kupatikana Uhuru 1961, yalitokea mabadiliko kidogo tu, kwani wale waliopigania uhuru hasa viongozi, na wasomi wachache wakachukua nafasi za Wazungu wakawa raia daraja la kwanza, Waasia na wafanyabiashara wakubwa wakabakia kwenye darajala kati, na Waafrika walio wengi yaani walalahoi wakabakia daraja la tatu, daraja la kufanya kazi nyingi, kazi kubwa lakini malipo kidogo, daraja la wazalishaji kwa manufaa ya watumiaji walioko daraja la kwanza na la pili. Ndiyo maana mara lilipotangazwa Azimio la Arusha, wananchi wengi katika ujumla wao walihamasika na kuunga mkono, tumaini lao lilikuwa kwamba "utabaka" utaondolewa na badala yake utajengwa mfumo wa kulinda haki kwa ajili ya wote na kwasababu ya haki watu katika ujumla wao wataishi maisha bora. 

Tumaini la namna hiyo ndilo lililomfanya Mtanzania awe mtu wa amani na utulivu. CCM inajigamba na kujitapa kama bingwa wa amani na utulivu lakini hawajui siri ya amani na utulivu. Wao CCM wanajivunia amani kwasababu hakuna lolote la kujivunia la maana walilolifanya. Ukweli ni kwamba siku zote wanadamu tunaishi kwa matumaini, kwahiyo lile tumaini ambalo lilitolewa na Azimio la Arusha liliwafanya wawe wasikivu kwa viongozi wao na watulivu. Lakini sasa tumaini lile limepotea, matazamio ya watu kuishi maisha bora siku za usoni yanazidi kutoweka kila siku ipitayo. Tumaini la kwamba haki itatawala katika nchi hii nalo limefutika kabisa, badala yake mlalahoi ni mtu anayetazamia kudhulumiwa wakati wowote. 

Kama si kudhulumiwa na dola, basi ni kudhulumiwa na mwenye nguvu (kiuchumi au kisheria) kuliko yeye. Njaaa na mashaka vimekuwa ni sehemu ya miasha ya kila siku ya mlalahoi. Hali kama ilivyo katika nchi inahitaji masihi au Mtume, mtu atakayekuwa tayari kufanya kazi kwa manufaa ya wengine pasipo kutazamia malipo ama mafao yoyote katika maisha haya. 

Hali ni mbaya kuliko ilivyokuwa mbaya enzi za Mkoloni hadi kuwasukuma baadhi ya Wazalendo kudai uhuru. Umaskini umeongezeka, umekuwa na kukithiri hadi kufikia kiwango ambacho sasa hautibiki tena. Umaskini wa Tanzania hauna tofauti na ukimwi, hauna dawa, unaua, unauma na unatesa sana kabla ya kummaliza mtu kabisa. Lakini je ni nini chimbuko hasa la umaskini wetu kama taifa? Ni nini sababu halisi ya sisi kuendelea kuwa maskini? Rais Mkapa anadai kwamba Watanzania ni wavivu wanapenda kula pasipo kufanya kazi! Mkapa huyo huyo akiwa kama Mwenyekiti wa CCM anasema Ilani ya CCM haitekelezeki, na sera za chama chake hazitekelezeki. 

Sasa hata watu wakifanya kazi kwa bidii kama wafanyavyo Wajapani watafanikiwa chini ya mpango gani? Maana ikumbukwe kwamba sera ni mpangilio au utaratibu wa kisayansi wa kutatua tatizo au kufanikisha jambo. Sasa chini ya sera za CCM ambazo hazitekelezeki, mkulima wa bongo hata angevuna tani milioni za mazao yake, bado atakuwa masikini kwasababu hakuna soko la uhakika linalompa "guarantee" kwamba atapata fedha. Vivyo hivyo mchimba madini wa bongo, hata angevuna madini yenye thamani ya matrioni ya dola bado atakuwa maskini tu kwasababu hakuna "guarantee" ya soko, baya zaidi serikali ya CCM inawapa nafasi wawekezaji ya kuvuna madini hapa nchini na kuyauza moja kwa moja kwenye masoko ya nje na mlalahoi hawezi kumudu ushindani wa namna hii kwa ajili hiyo mlalahoi hata aliyezaliwa ndani ya utajiri bado atakuwa maskini wa kutupwa mfano hai ni hao wakazi wa Tunduru (kwenye Alexandrite inayotajirisha wageni) Mererani (kwenye Tanzanite inayotajirisha wageni). Handeni (kwenye Garnet, Tomalini, Rhodrite n.k. isiyoguswa), Mahenge (kwenye Rubi inayotajirisha wageni), Geita, Ulyankulu, (kwenye dhahabu inayotajirisha wageni). 

Wenyeji wa maeneo hayo ni maskini wa kutupwa, lakini makampuni ya kigeni yaliyopewa ruhusa na serikali ya CCM kuvuna rasilimali zilizo kwenye maeneo hayo wanatajirika kwa namna isiyoelezeka. Kulingana ndata za Profesa Lipumba, kampuni ya Shanti Gold Mines ya Ghana iliyopewa leseni ya kutafiti dhahabu maeneo ya Ulyamkulu iliamua kuuza baadhi ya hisa zake kwa dola za Kimarekani milioni mia nne, kwakuwa mauzo yamefanyika nje ya nchi serikali ya Bongo haikupata hata senti tano. Mambo hayo yamefanyika baada ya serikali kuwanyang'anya wachimbaji wadogo wadogo maeneo hayo. Serikali hiyo hiyo inayolia umaskini kila siku, imepitisha sera ya kwamba kila mwekezaji anayewekeza katika Tanzania alipe dola tatu kama kodi kwa kila dola mia anazopata kutokana na kuuza nje mali za nchi yetu. Hii tafsiri yake ni kwamba kwa kila mali inayotoka nje ya nchi yetu, Watanzania tunabaki na dola tatu na mgeni anakwenda na dola 97. 

Aliye nacho anazidi kuongezewa, na yule ambaye hana ananyang'anywa hata hicho kidogo alicho nacho. Hii ni sera ya kuifilisi nchi na kumdidimiza mlalahoi, hata Mkoloni hakufanya unyonyaji kama huu. Wakati serikali ya CCM inawachia wageni kuja kuchota utajiri wa nchi yetu kana kwamba hauna mwenyewe, serikali hiyo hiyo ndio iliyomshikia bango mzalendo kuhakikisha analipa kodi hata kwenye biashara zisizompa faida, Serikali inatoza kodi ya mapato hata kabla mtu hajapata. Serikali inamlipisha mtu kodi hata kwa vitu ambavyo havizalishi kama vile baiskeli, mbwa, paka, mbuzi na kondoo. Baada ya serikali kumkamua mlalahoi namna hiyo ingetazamiwa kwamba walau ingeboresha huduma za jamii kama tiba na elimu, lakini wapi fedha zinazotengwa wakati wa Bajeti kwa ajili ya elimu na afya zinapungua mwaka baada ya mwaka. 

Kuna siku sikuamini masikio yangu wakati mganga mkuu wa wilaya ya Mpwapwa aliponiambia fedha ilizitengewa hospitali ya wilaya ni Tshs.16,000 kwa mwezi, lakini juzi wakatki Profesa Lipumba alipokuwa akieleza jinsi bajeti ya Wizara ya Afya inavyofinywa na serikali ya Mkapa ndipo nilipoamini kwamba kumbe kweli wanaweza kutoa Ths.16,000 na kutarajia hospitali ya wilaya itumie kwa mwezi mzima. Hii ndiyo roho ya Chama Cha Mapinduzi, roho inayofanana na mumiani ambaye anafyonza damu ya mtu bila huruma alimradi yeye akapate faida. 

Roho ya CCM haina tofauti na wachuna ngozi wa Mbeya kwani mlalahoi amechunwa hadi kuwa hoi zaidi wakati yenyewe CCM inakuwa juu zaidi uthibitisho wa hili ni jinsi ilivyoshughulikia malipo ya wastaafu wa Jumuia ya Afrika Mashariki, wengine walilipwa hundi za Ths. 120/-, na serikali inajigamba kwamba imelipa. 

Hii maana yake nini? Ni wazi kwamba haya ni mazoea ya unyonyaji na ukiukaji wa makusudi wa haki za msingi za binaadamu. Huko serikalini wanajua fika kwamba Shs.120/- za mwaka 1977 ni tofuati kabisa na 120/- za mwaka 2000 lakini bado wanafanya hivyo kutokana na kujua kwamba walipwaji hawawezi kufanya lolote kwani mara watakapodiriki tufanya lolote, basi rungu la dola litawainukia. 

Serikali ya uhuru iko tayari kupiga, kuumiza na hata kuua raia wema wanaodai haki zao. Kwa mkulima asiyeweza kuandamana wala kukusanyika pamoja na wakulima wenzake ili kudai haki yake kiuchumi, amekuwa kama jalala la CCM. 

Kwa muda mrefu amekopwa mazao yake na hakulipwa, si kwasababu hapendi kulipwa la hasha bali kwa kuwa tu hana njia au hajui atumie njia gani kudai haki yake.Matokeo yake mkulima amekuwa hoi bin taabani kwa umaskini, ufukara na uduni wa maisha. CCM kwa kuwa hawapati misukosuko yoyote kutoka kwa mkulima, wamemhesabu huyo kama mteja wao wa kudumu. Wanatamba kwamba CCM ina nguvu vijijini, wana uhakika wa kuzoa kura nyingi toka vijijini na baada ya hapo CCM hujihesabu wameshinda. 

Kwa umaskini wa mwanakijiji, wao hauwahusu wala hawahesabu kwamba umaskini walio nao wakulima wa bongo ni ushahidi kwamba wameshindwa kutawala. Matokeo ya udhalimu na udanganyifu wa aina hii ni kizazi kipya kisichoafiki uwongo kukimbia toka vijijini na kuja mijini "kubangaiza". 

Viongozi wa CCM kwa kuwa wana giza la ibilisi kwenye fahamu zao husimama bila haya na kutoa miito ya eti vijana kuacha kukimbilia mijini kana kwamba miito yao ndio dawa. Hawataki kukabiliana na ukweli kwamba tatizo la vijana kukimbilia mijini ni matokeo ya sera zao mbovu na zisizotekelezeka hasa zile zinazohusu vijana. Hata viongozi wa CCM wa vijana nao akili zao zimetiwa giza kama baba zao, huinuka kusema kwa niaba ya vijana lakini katika yote wanayoyasema hakuna hata moja linalohusu vijana wala linalogusa maisha ya vijana wala linalowakilisha matatizo halisi ya vijana wa nchi hii. 

Wao viongozi wa vijana wa CCM wapo kama watumishi wa itikadi mfu ya chama hao. Mfano hai ni kauli za Emannuel Nchimbi kwa Askofu Kakobe, yote aliyosema Nchimbi hayana maana wala hayawakilishi maslahi ya vijana. Sidhani kama Nchimbi anayaelewa matatizo ya vijana wenzake kwa kuwa yeye ni mtu wa kubebwa na kuufurahia huo upendeleo anaoupata kutoka kwa watawala. Vijana wenzake kila mara wanafungwa mashati na kushitakiwa kama wazurulaji wakati hakuna ajira wala mazingira ya kujitegemea. 

Vijana wenzake kila mara wanabambikiziwa kesi za kukutwa na misokoto ya bangi au ujambazi. 

Vijana wa kike wanabughudhuiwa kila mara kwamba ni wakahaba, wazurulaji na wasio na kazi. 

Vijana wenzake walioko shuleni wana lishe duni, na vifaa duni vya kusomea hali wengine wanapinda migongo kwa kukosa madawati ya kukalia wakati wa kuandika. 

Kila siku vijana wananyanyaswa kwenye daladala kwa namna ya kutisha, je mbona hayo yasimuume Nchimbi hata akafumbua kinywa chake kusema kwa niaba ya vijana wenzake? Ama kwake hoja ya kuchanganya dini na siasa imekuwa kero kubwa kuliko kero zote wanzopata vijana wa nchi hii? Najua wazi huyu kijana anakabiliwa na maradhi ya "diversion of mind".

Hii ndiyo kazi ya Nambari wani, kuzifanya akili za watu kuacha kuuelekea ukweli na uhalisi wa mambo badala yake "kuchepuka", au kupinda mithili ya treni linaloacha reli na kwenda pembeni. CCM mbali ya kunyonya watu kiuchumi na kuwaacha hoi, pia imewanyonya kiroho na kuwafyonza kiakili hadi wamefikia kiwango kile ambacho Nabii Ezekieli anaelezea kwamba "watu wana macho lakini hawaoni, wana masikio lakini hawasikii." 

Ukombozi wa kweli wa mwananchi ni lazima huende sambamba na kuing'oa CCM madarakani. 

Wiki ijayo CCM muuaji nambari wani wa walalahoi.

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Acheni  kuwacheza shere Waislamu, ondoeni udini

Serikali iache udini, kuwagawa wananchi - Sheikh  Mbukuzi

Wakati Kanisa Katoliki  likitoa miongozo ya kisiasa:
Sheikh mwingine ahojiwa Mwanza

Hakuna maendeleo bila Demokrasia -  Lipumba

MPASHO NASAHA
KAMCHEZO  AU?

HABARI
Sheikh Jongo asababisha mtafaruku mbele ya Al-Haji Mwinyi

‘Suala la kuirekebisha jamii lisiachwe mikononi mwa Serikali pekee’

Jiandikisheni na pigeni kura -Balozi

Tanzania kufutiwa madeni:
Wananchi hawatarajii nafuu yoyote

Ushauri Nasaha
Vyombo vya habari na vijana  - 2

MAKALA
Sababu ‘1000’ kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani - 4

Kalamu ya Mwandishi
Muungano watimiza miaka 36 kwa migogoro

MAKALA
Chama cha Mapinduzi na sera za maendeleo (1)

Lishe
Jinsi ya kutunza virutubisho wakati wa maandalizi ya vyakula

Habari za Kimataifa

RIWAYA
Maisha mema ya akhera

MASHAIRI

MICHEZO

  • Raoul Shungu apigwa ‘Dafrao’ 
  • Yanga wamfurusha Waziri Mudhihir uwanjani
  • Simba wampongeza Msajili wa Vyama

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita