|
Na. 045 Jumatano Aprili 26 - Mei 2, 2000 |
|
|
|
|
AMIRI wa Shura ya Maimamu Sherikh Juma Mbukuzi ameitaka Serikali kuepuka hali inayoweza kupelekea kuwagawa wananchi kwa misingi ya dini zao. Sheikh Mbukuzi ameyasema hayo mwanzoni mwa juma hili jijini wakati alipokuwa akizungumzia uteuzi wa idadi kubwa ya Wakristo katika nafasi za usimamizi wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Oktoba mwaka huu. Hivi karibuni Serikali ilitangaza orodha ya majina 109 ya maofisa walioteuliwa kusimamia uchaguzi mkuu ujao. Orodha hiyo imelalamikiwa na Waislamu kwamba uteuzi huo umefanywa kwa misingi isiyoeleweka ambapo asilimia 90 ya walioteuliwa ni Wakristo. Katika toleo lililopita, gazeti hili lilichapisha barua ya Wazi kwa Mhe. Rais toka kwa Muislamu mmoja akilalamikia orodha hiyo kuwa ni kielelezo cha udini dhidi ya Waislam. Akitoa maoni yake juu ya suala hilo Sheikh Mbukuzi aliilaumu Serikali kwa kujenga mazingira ya udini kutokana na kuachia idadi kubwa ya Wakristo kuhodhi madaraka katika idara zake na kwenye taasisi za umma ambapo alidai Waislamu wamekuwa wakilalamika kwa ushahidi wa kutosha kwamba baadhi ya watendaji hao wamekuwa wakitumia madaraka hayo kwa misingi ya udini dhidi ya Waislamu. Pamoja na kulalamikia hali hiyo, Sheikh Mbukuzi alionesha kusikitishwa na mwenendo wa Serikali wa kutoonekana kujali hisia na malalamiko ya Waislamu hata pale wanapotoa ushahidi wa kutosha juu ya yale wanayoyalalamikia, yakiwemo yanayohusu hakizao za kidemokrasia kama wananchi na haki zao za kibinadamu. Alilalamika kwamba wakati Serikali inaonekana kupuuza malalamiko kadhaa ya Waislamu, imekuwa nyepesi kusikiliza na kutekeleza yale yanayotakiwa na Wakristo. "Yapo masuala kadhaa ambapo Serikai imetamka wazi kuwa haiwezi kupuuza maoni ya Wakristo", alisema Sheikh Mbukuzi na kuongeza, "hii inathibitisha kuwa Serikali inasikiliza maoni ya wananchi na kujali hisia zao, isipokuwa yale yanayotolewa na Waislamu tu. Sheikh Mbukuzi alitoa mfano wa suala la OIC ambapo Serikali ilonekana kujali maoni ya Wakristo dhidi ya Waislamu. "Ni wajibu wa Serikali kuandaa uchaguzi ulio huru na wa haki", alisema Sheikh Mbukuzi na kuhoji, "ati katika hali kama hiyo ya udini dhidi ya Waislamu nchini, Muislamu gani atakaeridhia na kuamini kuwa uchaguzi huu utakuwa huru na wa haki ambapo asilimia 90 ya wasimamizi wake ni Wakristo?" Akizungumzia juu ya nini cha kufanya kuhusu uteuzi huo, Sheikh Mbukuzi alisema kuwa tegemeo lake lipo kwa rais Mkapa kuuona udini huo unaofanywa na baadhi ya watendaji waliopo Serikalini na hivyo kuingilia kati ili kuepusha nchi na maafa yanayoweza kusababishwa na wadini hao. Aidha, Amiri huyo wa Shura aliwataka Waislamu na wananchi wengi kwa ujumla kuendelea kufichua na kulaani vitendo vya udini vinavyofanywa na baadhi ya watendaji waliopo Serikalini. Aliwataka vile vile kuwahoji wanasiasa wanaojitokeza kugombea uongozi katika uchaguzi ujao waeleze msimamo wao kuhusu dhulma na ukandamizaji wanaofanyiwa Waislamu katika masuala mbali mbali likiwemo suala kubwa la mauaji ya Mwembechai. Sheikh Mbukuzi alionesha pia kushangazwa na ukimya wa vyama vya siasa kuhusu uteuzi wa idadi kubwa ya Wakristo kusimamia uchaguzi mkuu ujao. "Inashangaza kuona vyama vya siasa, hasa wapinzani kukaa kimya juu ya uteuzi huu katika kipindi hiki ambao Waislamu wameonesha ushahidi wa kutosha juu ya kuwepo kwa udini nchini dhidi yao", alisema Sheikh huyo na kuwataka Waislamu kuviangalia vyema vyama endapo vinaweza kuondoa dhulma dhidi yao endapo vitaingia madarakani. Akitoa maoni yake kuhusu hatua ya Kanisa Katoliki kuandaa utaratibu wake wa kuratibu uchaguzi mkuu ujao, Sheikh Mbukuzi ameeleza kuwa haoni tatizo lolote. Alisema kuwa kanisa hilo na viongozi wake pamoja na taasisi zote za kidini pamoja na viongozi wake, wana haki ya kufuatilia suala lolote liwe la kisiasa au la, ili mradi linagusa maisha na maslahi ya jamii. Alisema kuwa viongozi wa dini ni viongozi wa jamii wana haki ya kusimamia na hata kuitetea jamii katika mambo yanayohusu mustakabali wa maisha na maendeleo yao. "Siwezi kusimama msikitini kwa mfano, kutoa hutuba za kukataza rushwa wakati kiini cha rushwa inaonesha kinatokana na kuwepo kwa viongozi wasio waadilifu na utawala usiofuata sheria", alisema Sheikh Mbukuzi na kuongeza; "badala yake nitawahimiza waumini kuchagua viongozi waadilifu." Hata hivyo Sheikh Mbukuzi alisema kuwa tatizo siyo kanisa Katoliki kutoa kitabu na kuweka mikakati ya kufuatilia uchaguzi mkuu bali Serikali kuzuia dini na madhehebu nyinginezo kutoa maoni yao ya kisiasa kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo uchaguzi mkuu ujao. "Serikali inafahamu kuwa ni haki yetu viongozi wa dini kuzungumzia na kufuatilia masuala ya siasa. Lakini imeamua kuwazuia Waislamu kwa kuwakamata na kuwafungulia mashitaka viongozi wake. Kukemea baadhi ya makanisa, mengine kuyataka radhi na mengineo hususan Kanisa Katoliki, kuliachia lifanye litakavyo na pengine kupokea ushauri wa kanisa hilo," alieleza Sheikh Mbukuzi. Sheikh Mbukuzi alimaliza kwa kusema kuwa ni tegemea lake kuwa Serikali itaacha muelekeo huu wa udini. |
YALIYOMO
TAHARIRI
Serikali iache udini, kuwagawa wananchi - Sheikh Mbukuzi Wakati
Kanisa Katoliki likitoa miongozo ya kisiasa:
Hakuna maendeleo bila Demokrasia - Lipumba MPASHO NASAHA
HABARI
‘Suala la kuirekebisha jamii lisiachwe mikononi mwa Serikali pekee’ Jiandikisheni na pigeni kura -Balozi Tanzania
kufutiwa madeni:
Ushauri Nasaha
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Lishe
RIWAYA
|
|
|
|
|