NASAHA
Na. 054 Jumatano Juni 28 - Julai 4, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MICHEZO 

Mpambano wa watani wa jadi:
U-CCM umeiponza Yanga wasema Simba

  • Wao wapeta na sera ya jino kwa jino
  • Yanga wagawanyika, Dk.Omar apigwa na butwaa


Na Hamis Kasabe

KATIKA kile kinachoonekana kama siasa kuingia katika michezo,.Wanachama na washabiki kadhaa wa Klabu ya Simba ya Dar es Salaam wamedai kwamba kilichopelekea timu ya Yanga pia ya jijini kufungwa mwishoni mwa wiki ni baada ya timu hiyo kushangilia CCM, CCM.

Yanga walishangilia kwa staili hiyo mara tu baada ya Makamu wa Rais Dk. Omar Ali Juma kuwasili katika uwanja wa Taifa kama mgeni rasmi, wakati huo Yanga wakiongoza kwa bao moja kwa sifuri.

Katika mchezo huo wa ligi kuu Tanzania bara nane bora, Simba waliibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja.Mabao ya Simba yalifungwa na Steven Mapunda wakati Iddi Moshi alifunga bao la Yanga.

Wamesema kwamba kimsingi walikerwa sana na staili ya ushangiliaji huo kiasi cha kuwafanya wahisi kwamba walikuwa wakipambana na chama tawala (CCM) kilichokuwa nyuma ya mgongo wa Yanga.

Kufuatia hali hiyo wamedai ilibidi watumie nguvu za ziada (ngangari) na maarifa ya kutosha kuhakikisha wanashinda mpambano huo wa watani wa kale, kitu ambacho walifanikiwa.

Katika kile kilichotafsiriwa kuwa ni kujibu mapigo mwandishi wa habari hizi alishuhudia wapenzi wa Simba wakishangilia 'jinokwa jino' kufuatia timu yao kusawazisha bao mwanzoni mwa kipindi cha pili na kumfanya Dk. Omar kutoamini masikio yake. Dk. Omari si mfuasi wa jino kwa jino ila chama chake kiliwahi kuzungumzia sera ya mtu kwa mtu.

Msemo wa jino kwa jino unahusishwa na chama cha wananchi (CUF) kwa kuwa uliasisiwa na viongozi wa chama hicho wakimaanisha kupambana na yeyote atakayethubutu kuiba kura katika uchaguzi mkuu ujao, mwezi Oktoba 2000.

Aidha, baadhi ya wapenzi wa Yanga waliobahatika kuongea na NASAHA mara baada ya mechi hiyo walielezea kukerwa kwao na staili ya ushangiliaji wa CCM, CCM ambao wameuita wa kizamani.

Hata hivyo hakuna kiongozi si wa Simba wala wa Yanga aliyekuwa tayari kuzungumzia ushangiliaji wa 'jino kwa jino'au wa 'CCM, CCM'.

"Lakini mimi kwa maoni yangu, nadhani hii inaashiria kwamba, kutakuwa na mchuano makali katika uchaguzi ujao baina ya CUF na CCM, lakini pia nahisi kwamba CUF wanayo nafasi", alieleza mmoja wa wafuatiliaji wa siasa za Tanzania.


Wanamichezo wamshtukia Mkapa

Na Mwandishi Wetu

IMEELEZWA kuwa ukaribu anaojaribu kuuonyesha Rais Benjamin Mkapa kwa wanamichezo nchini siku za hivi karibuni ni wa kutaka kuteka kura za watu hao ni si vinginevyo.

Wakizungumza na NASAHA mapema wiki hii mjini Dar es Salaam, wanamichezo hao kutoka fani mbali mbali za michezo nchini wamedai kwamba Rais amekuwa akifanya hivyo ili kuwaremba Watanzania wenye mapenzi na michezo ili wahisi kuwa ni miongoni mwao.

"Unajua anachofanya Rais ni sawa lakini kwanini sasa, wakati uchaguzi umekaribia miaka yote iliyopita yeye alikuwa wapi", amehoji mwanamichezo Selemani Rehani.

"Mimi naona hapa, Mkapa ana agenda ya siri na sio suala la maendeleo ya michezo, na kama ni suala la kura sio siri amenowa", ameongeza Bi Aisha Saidi Bilali ambaye aliwika sana katika fani ya 'Netiboli' kunako miaka ya 1980.

Rais Makapa ambaye hata siku moja hakuwahi kujihusisha na mambo ya michezo toka alipoukwaa Urais wa Tanzania 1995 hivi karibuni alifungua michezo ya UMISETA mkoani Mwanza na jana mkoani Morogoro Rais alifungua michezo ya shule za msingi nchini (UMITASHUMUTA).


Mabosi DRFA kujulikana leo

Na Badru Kimwaga

CHAMA cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) leo kinafanya uchaguzi wake mkuu ambapo jumla ya wagombea 45 wanatarajiwa kuchuana kuwania nafasi kumi za uongozi wa chama hicho.

Uchaguzi huo unafanyika leo baada ya kuzuiliwa mapema mwezi huu na Baraza la Michezo (BMT)baada ya wagombea walioshindwa kwenye uchaguzi wa chama cha soka wilaya ya Ilala (IDFA) kukata rufaa na rufaa hiyo kutupiliwa mbali na kamati ya michezo ya mkoa (KMMD).

Akizungumza na waandishi wa habari juzi ofisini kwake mara baada ya kuwafanyia usaili wagombea, Mwenyekiti wa KMMD, Wilfred Ngilwa alisema uchaguzi huo utafanyika leo kwenye ukumbi wa Ilala Boma kuanzia saa 8 mchana.

Ngilwa alitaja idadi ya wajumbe watakaopiga kura leo kuwa ni viongozi watatu watatu toka vyama vya KIFA, IDFA na TEFA na kiongozi mmoja wa DAFCA.

Akiwataja wagombea ambao wamekidhi sifa na uzoefu wa kugombea uongozi DRFA ambao wamepitishwa katika usaili na watachuana leo kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa sasa wa DRFA Abushir Kilungo, Frank Mtani na Mohamed Missanga wanaowania Uenyekiti.

Wanaowania umakamu mwenyekiti ni Azzan Mangushi, Khamis Mattaka, Salim Dossi, Juma Simba, Erasto Mwakisisile, James Mwakamele na Mohamed Sumbizi.

Nafasi ya Ukatibu Mkuu inagombewa na Amin Bakhressa, Pater Mlinzi na Ramadhani Kafuku huku nafasi ya ukatibu msaidizi inawaniwa na Athumani Nyamlani na Khamis Ambari.

Wagombea Haroub Hassani, Salim Dossi,Ally Hasan na Mpoki Mwafenga wanachuana kwenye nafasi ya Uweka hazina Mkuu ilihali Gwakisa Mwambalaswa, Suke Mzee, Ally Hassani na Jacob Mwakisu wanagombea uweka Hazina msaidizi.

Ujumbe wa Taifa unawaniwa na Azzan Mangushi, Peter Mushi, Salum Dassi, Khamis Kissiwa, Jacob Mwakisu, Haji Mkuki, Mahsin Said wakati nafasi ya kamati ya utendaji ya chama hicho inawaniwa na wagombea 15.

Wagombea hao ni Abeid Mziba, Mlanzi Shadidu, Juma Pinto, Haji Nkiki, Khamis Kissiwa, Matata Mtono, Nurdin Hoza,Salum Chaurembo,Msafir Mohamed, AbdulRahman Wengi,Omari Kasinde, Kafuku Ramadhani, Abubakari Liongo, Ally Mbena na Azzan Mangushi.

Mwenyekiti wa KMMD alisema kuwa katika usaili huo wa juzi hakuna mgombea aliyechujwa ingawa alisema wapo walitakiwa kuwasilisha vyeti vyao vya elimu hasa wale wanaowania nafasi za uweka hazina mkuu na msaidizi wake.


Pupe, Mziray wamlia 'dip' Shungu

Edibily Lunyamila amlilia

MAKOCHA wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars)Mjerumani Bukhanol Pupe na Msaidizi wake Syllersaid Mziray Jumapili iliyopita walionekana wakibadilishana mawazo na kupanga mikakati ya kiufundi kuhakikisha timu ya Simba inaibwaga Klabu ya Yanga.

Tukio hilo lilifanyika siku hiyo wakati mahasimu wawili katika soka la bongo Simba na Yanga walipokuwa wakimenyana vikali katika uwanja wa Taifa jijini.

Mziray ambaye ni kocha msaidizi wa Simba alionekana katika kile kilichoelezwa ni kuomba msaada wa kiufundi toka kwa Pupe wakati timu hizo zikiwa mapumzikoni huku Yanga inayofundishwa na Mkongoman Raul Shungu ikiwa mbele kwa goli moja kwa yai.

Naam kipindi cha pili kilipoanza ushauri wa Pupe ulioonekana kuzaa matunda koma manga kwani Simba walifanikiwa kusawazisha na kuongeza bao la ushindi.

Naye kiungo wa pembeni wa Yanga na timu ya taifa (Taifa Stars) Edibily, Jona Lunyamila alionekana akifuta machozi siku hiyo mara mpira ulipomalizika.


Tamasha la jahazi kuanza Z'bar Ijumaa

Na Asma Mohammed, Zanzibar

TAASISI isiyokuwa ya kiserikali, Zanzibar International Film Festival (ZIFF) pamoja na kuandaa tamasha la tatu linalojulikana kama tamasha la nchi za jahazi kuanzia Juni 30 hadi Julai 9 mwaka huu, pia linakusudia kutenga eneo la muziki ili wasanii waweze kuwasilisha ujumbe kwa jamii.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni mkurugenzi wa tamasha hilo Bw. Bakari amesema, lengo kubwa la amasha hilo ni kukuza na kuendeleza sanaa, filamu pamoja na muziki kutoka nchi za Kiafrika na nchi nyingine za jahazi.

Amesema wasanii kupitia kazi zao wataonyesha jinsi vyombo vya kiasili na zana za kisasa vinavyoweza kuchanganywa na kutoa muziki bora.

Baadhi ya nchi za jahazi zitakazoshiriki tamasha hilo pamoja na Zanzibar ni Comoro na Shelisheli.

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Serikali isikilize kilio cha wapinzani na Waislamu

Kishindo cha CUF chaitikisa Dar

Mamia  warudisha kadi za CCM Kilwa

Chama cha Mugabe chupuchupu Zimbabwe

Wasikilizeni wananchi wasemavyo toka kwenye meli mbovu mkabala na Posta ya zamani

CCM yakasirishwa kwa kuswaliwa Mtume (S.A.W.)

Wanaomzomea Bilal waambiwa Oktoba watakula jeuri yao

CCM wapoteza viti 18196; CUF yaongoza kuvinyakua

Tambwe huyoo anakuja!

Ushauri Nasaha
Unapomdharau mama yako mbele ya rafiki yako...

MAKALA
Uchaguzi wa Zimbabwe: Vita kati ya mabeberu na wapinga Ukoloni mamboleo

MIPASHO NASAHA
Matonya wahi, pesa zinatoka sasa!

MAKALA
Vijembe kwa viongozi wa vyama vya upinzani, huduma kwa wananchi ziro

KALAMU YA MUANDISHI
Ukongwe hausaidii kubaki madarakani

MAKALA
Kuchanganya siasa na ushirikina

Habari za Kimataifa

Lishe
Faida za vyakula vya nyuzi nyuzi

RIWAYA
Dunia ndivyo ilivyo - 4

Barua

MASHAIRI

TANGAZO

MICHEZO

  • Mpambano wa watani wa jadi: U-CCM umeiponza Yanga wasema Simba
  • Wanamichezo wamshtukia Mkapa
  • Mabosi DRFA kujulikana leo

  • Pupe, Mziray wamlia ‘dip’ Shungu
    -



     
     

       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita