NASAHA
Na. 054 Jumatano Juni 28 - Julai 4, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Kishindo cha CUF chaitikisa Dar 
  • Tawi la wazee lafunguliwa 
  • Wanawake watoa ahadi 
  • Vibwagizo vyawaliza wazee 


Na Rajab Nkawa 

JIJI la Dar es Salaam jana lilishuhudia kishindo kikubwa wakati Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba akiambatana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad walipofungua matawi katika maeneo mbalimbali jijini.

Umati mkubwa wa wananchi, wake kwa waume, ukiongozwa na kundi la matarumbeta lilipita katika mitaa ya Kariakoo likiwa nyuma na mbele ya viongozi hao ambao jana walithibitisha kuwa wao ni ngangari kwa kutembea masafa marefu kwa mwendo wa haraka sambamba na kundi la vijana. 

Shughuli hiyo ya ufunguzi wa matawi ilianzia katika Mtaa wa Msimbazi na Tandamti ambapo ufunguzi rasmi wa tawi la wazee ulifanyika. 

Akizungumza na wazee mara tu baada ya ufunguzi wa tawi lao Mwenyekiti huyo wa CUF alikuwakumbusha juu ya mchango mkubwa wa wazee katika kuleta uhuru wa nchi hii kupitia chama chao cha TANU. 

Hatahivyo, akawaambia, CCM ya sasa sio TANU ile walioipigania enzi za kudai uhuru na kwamba viongozi wa sasa hawana moyo wa TANU waliokuwa nao wazee hao wa kupambana na madhalimu na kuwaletea faraja wananchi. 

Katika tawi hilo la wazee, umati mkubwa wa wananchi uliongozana na msafara na Profesa Lipumba katika ufunguzi wa matawi yaliyosalia katika maeneo ya Kariakoo na Upanga kuingia mtaa wa Mindu Upanga. Miongoni mwa matawi yaliyofunguliwa Kariakoo kabla ya kuelekea Upanga ni Tawi la Mkunazini lililopo katika Mtaa wa Nyamwezi. Baada ya hapo msafara ulielekea Upanga ambako matawi kadhaa yalifunguliwa. 

Baada ya ufunguzi wa matawi ya Upanga, Prof. Lipumba na Maalim Seif walirudi maeneo ya Kariakoo na kufungua matawi yaliyosalia, kisha wakaelekea katika ukumbi wa Hoteli ya Starlight uliopo katika barabara ya Bibi Titi Mohammed. 

Katika ukumbi huo, wanawake wa mkoa wa Dar es Salaam waliandaa hafla ya kuwapongeza viongozi hao wa CUF kwa kupitishwa na chama chao kuwa wagombea wa Urais wa Muungano na Zanzibar. 

Aidha, ukumbini hapo palikuwepo na shamrashamra zilizoongozwa na bendi ya Tabora Jazz, kikundi cha matarumbeta na nyimbo za akinamama. 

Akiongea kabla ya Prof. Lipumba, Maalim Seif aliwambia wanawake hao kuwa jambo lolote haliwezi bila kuwepo wanawake hivyo akawataka kujitokeza kwa wingi katika siasa ili kuweza kupiga kura na kupigiwa kura na akawatahadharisha katu wasikae nyuma kungojea viti vya upendeleo. 

"Ingieni bungeni ili mpate kuteuliwa na serikali ya Profesa (Lipumba) kuwa Mawaziri... msisubiri nafasi za sadaka", alisema. 

Naye Bi. Asha Ndege, mjumbe wa Baraza Kuu la CUF aliwaambia wanawake kuwa wao ni watu wenye huruma na azma, na kwamba wanapoazimia jambo huwa hawarudi nyuma. Hivyo akawataka wanawake hao kuazimia kumuingiza Prof. Lipumba Ikulu ili akasaidiane na wananchi katika kuondoa dhuluma na kuleta maendeleo na haki sawa kwa wote nchini. 

Akizungumza na wanawake hao, Prof. Lipumba aliwashukuru kwa kuandaa hafla hiyo na akawataka kwenda kuwaelimisha wanawake wenzao kukataa kurubuniwa kura zao kwa khanga na vitenge. 

Aliwaambia kuwa wao ndio wenye kuyajua matatizo yanayozikabili familia zao kiuchumi kuliko wanaume, hivyo akawataka wawaelimishe wenzao umuhimu wa kuondokana na utawala wa CCM ambao umeitumbukiza nchi katika umaskini mkubwa katika kipindi chake cha utawala wa miaka 40. 

Awali, wakati msafara wa Prof. Lipumba unapita katika maeneo mbalimbali ya mitaa ya Kariakoo na Upanga, nyimbo zilizokuwa zikimbwa na vijana zilielekea kuwavutia na kuwagusa sana wananchi kutokana na mashairi yake. Baadhi ya wazee walionekana wakilengwa lengwa na machozi kutokana na maudhui ya nyimbo hizo. 

Mmoja wa wazee hao aliliambia NASAHA kuwa nyimbo hizo zilimkumbusha enzi za kudai uhuru. 

Baadhi ya vibwagizo vya nyimbo hizo ni hivi vifuatavyo: 

Vijana (ni) Taifa la leo, sio la kesho.
CCM wanasema vijana (ni) taifa la kesho.
Wananchi leo watalindwa na nani.
Vijana wa CUF ni Taifa la leo.
Profesa Lipumba tunakuamini kaka.
Mwezi wa kumi tunawapiga kapa.
CUF yasonga mbele. Wapambe na vibaraka wanaona gere.
CUF tumefikiwa viongozi bora na wa mafanikio.
Kama unaona donge panda juu ukazibe.
Bajeti hiyo (ya serikali ya CCM) bajeti gani.
Hata maji ya kunywa mitaani hayaonekani.


Mamia warudisha kadi za CCM Kilwa

Na Mwandishi Wetu, Kilwa Masoko 

MAMIA ya wa wazee wa hapa wamerudisha kadi zao za CCM kufuatia kipigo walichopata baadhi ya vijana kutoka kwa Polisi wenye silaha wiki iliyopita.

Uamuzi wa wazee hao umechukuliwa kwa madai kuwa hawawezi kubakia katika chama ambacho kinashabikia uonevu dhidi ya vijana wao. 

Wamedai kuwa video hizo zenye kumwonesha Prof. Lipumba na viongozi wengine wa CUF zilichukuliwa katika mikutano halali ya kisiasa ambayo iliruhusiwa kwa vibali vya polisi katika maeneo hayo yalikofanyika, hivyo hawaoni mantiki ya kuzuia isioneshwe hata kama ingekuwa ni kwenye maeneo ya wazi. 

Wakaongeza kudai kuwa kuwapiga vijana wao eti kwa sababu walikuwa kiangalia mikanda hiyo ni kuwakosea wao na wanaona bora waungane na vijana wao kuiaga CCM. 

Kumekuwepo na pilikapilika kubwa za wazee mjini hapa za kampeni za nyumba kwa nyumba wakihamasishana kuipinga CCM na serikali kufuatia hatua hiyo ya Polisi. 

Wakati huo huo Chama cha upinzani cha The Civic United Front (CUF) kimedai kuwa kuvamiwa kwa maskani yake yaliyoko eneo la sokoni mjini hapa ambako vijana hao walipigwa kunatoka na shinikizo la CCM. 

Katika barua iliyopelekwa kwa Mkuu wa wilaya ya Kilwa yenye kumbukumbu nambari CUF/F.2/25 na nakala yake kwenda kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi na vyombo vya habari chama hicho kimemweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa Mkuu wa Polisi wilaya (OCD) alitoa idhini ya kushambuliwa wanachama wake kwa shinikizo la CCM. 

"... Jeshi la polisi Kilwa kwa idhini ya Mkuu wa Polisi Kilwa akitumwa na CCM Kilwa, wamempiga vibaya sana kijana niliyemtaja hapo juu (Othmani Kimbendu) ambaye walimkuta katika eneo la Maskani ya CUF ambapo palioneshwa mkanda wa video unaoonesha ufunguzi wa matawi ya CUF..." Inasomeka sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu wake wilayani hapa Bw. Ngayonga S. Nagoyanga. 

Juni 20, mwaka huu majira ya saa 3 usiku kundi la askari polisi walivamia maskani hiyo ya CUF iliyopo mtaa wa Songo baada ya wana-CUF hao kukataa kutekeleza amri ya polisi hao waliotaka kusimamishwa kwa onesho hilo kwa madai ya kuonesha video bila kibali. 

Katika shambulio hilo Bw. Othamani Kimbendu alipigwa na kujeruhiwa vibaya na hatimaye kuchukuliwa na polisi hao akiwa amebakiwa na nguo za ndani tu. Katika shambulio hilo risasi zilitumika kuwasambaratisha wananchi waliokuwa na hasira ambao walianza kurusha mawe, kufuatia kilio kilichokuwa kikitolewa na Bw. Kimbandu. 

Hatua hiyo ya Poisi inafuatia Tangazo lililotolewa na Mkurungenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kilwa Bw. M.H. Senyagwa lililowapiga marufuku wananchi kuonesha kanda za video kwenye mkusanyiko watu (Public places)ikiwa ni pamoja na kwenye mikutano ya hadhara bila ya kupata kibali kutoka mamlaka inayohusika. 

"Hatua hii inachukuliwa ili kudhibiti ongezeko la uoneshaji wa mikanda ya video ambayo inapotosha maadili ya jamii." Inasomeka sehemu ya tangazo hilo lenye kumbukumbu nambari KDC/A.CO/1010/9 lililotolewa Juni 19, mwaka huu na nakala yake kwenda kwa Kamanda wa Polisi Wilaya kwa ufuatiliaji wa agizo hilo. 

Chama cha upinzani cha CUF wilayani hapa kimekuwa kikifanya maonesho ya video ya viongozi wake wa kitaifa katika mikutano yake ya hadhara pamoja na kwenye matawi na maskani za chama hicho. Siku ya tukio wanachama hao walikuwa wakiangalia mkanda wa video uliokuwa ukionesha ufunguzi wa matawi na mkutano wa hadhara uliofanyika huko Kichemchem Mbagala jijini Dar es Salaam. 

Hapa Dar es Salaam Afisa katika kitengo cha Haki za Binadamu wa chama cha CUF,Bw. Amini Rubea akiongea na gaeti hili amesema kuwa shambulio hilo ni la kisiasa kwani mkanda wa video uliokuwa ukioneshwa haukuwa ukivunja maadali yoyote ya jamii, kwani ulikuwa ukiwaonesha viongozi wa chama hicho wakiwa kwenye shughuli za kisiasa. 

Akasema kuwa chama chake kinawasiliana na wanasharia wake ili kuchuku hatua zinazofaa za kisheria. Kwa sasa, akasema Afisa huyo, kitengo chake kinamwandikia Mkuu wa Polisi nchini (IGP) Omar Mahita,taasisi za haki binaadamu pamoja Balozi za nje zilizopo hapa nchini kuelezea kadhai hiyo. 

"Vijana wetu nane wanashikiliwa na polisi na wengine (ambao ni wanachama wa CUF) kuukimbia mji wakihofia kukamatwa na polisi", amesema Bw. Ngayonga. 

Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani Juni 22 mbapo walisomewa mashtaka ya kuonesha kanda ya video bila ya kibali na kuwazuia Polisi kufanya kazi yao. 


Chama cha Mugabe chupuchupu Zimbabwe
  • Asilimia kubwa ya ushindi wa upinzani ni kura za vijana 
  • 'Ngangari' wasema wamepata muelekeo wa kuing'oa CCM 


Na mwandishi wetu 

CHAMA cha Rais Mugabe wa Zimbabwe cha ZANU-PF kimepata viti 62 katika uchaguzi wa wabunge uliofanyika Juni 24 na 25 mwaka huu ambapo chama cha upinzani cha MDC kimepata viti 57 na kile cha ZANU-Ndonga kiti 1

Uchaguzi huo ulifanyika kuchagua wabunge wa viti 120 kati ya jumla ya viti 150 vya Bunge hilo. Viti 30 hujazwa na baadhi ya watendaji wakuu wa serikali na wanasiasa ambao huchaguliwa na rais. 

Hivyo ingawa Rais Mugabe atakuwa na jumla viti 92 kati ya viti 150, itamuwia vigumu kupata uwezo wa kufanya mabadiliko yo yote ya katiba pasipo kukubaliana na wapinzani. 

Hata hivyo, lengo kubwa la rais Mugabe ni kuchukua mashamba makubwa yanayomilikiwa na walowezi wa kizungu, suala ambalo aliisha lichukulia hatua za kikatiba kabla ya uchaguzi huo. 

Katika uchaguzi huo, chama kikuu cha upinzani cha MDC ambacho kilianzishwa miezi tisa iliyopita kimepata ushindi mkubwa kuliko ilivyo tarajiwa na wengi kuotokana na umri mdogo wa chama hicho. 

Hata hivyo imeelezwa kwamba chama hicho cha MDC kimepata ushindi huo kutokana na kuungwa mkono na idadi kubwa ya vijana . 

Aidha imeelezwa kuwa sababu za vijana kuunga mkono chama hicho ni kutokana na ufafanuzi fasaha unaofanywa na viongozi wasomi wa chama hicho katika kuyachambua matatizzo yanayo wakabili wananchi ambayo yametokana na kushindwa kwa chama cha ZANU-PF kuyashughulikia. 

Matatizo hayo ni pamoja na vijana wengi kukosa ajira, wakubwa kujipendelea katika elimu na afya ambapo watoto wao husoma Ulaya na Marekani na familia zao hutibiwa nje ya nchi wakati idadi kubwa ya wananchi wanataabika kupata huduma hizo nchini mwao. 

Ushindi wa MDC katika uchaguzi huo kwa kupata viti 57 kati ya 120 vilivyogombewa na viti vitano tu nyuma ya chama tawala umepokewa kwa shangwe na kambi ya upinzani nchini. 

Miongoni mwa vyama vya upinzani vilivyo farijiwa na ushindi huo ni chama cha wananchi-CUF. 

Vijana wa chama hicho wameeleza kuwa wamefurahishwa sana kwa taarifa walizozipata toka kwa watanzania walioko Zimbabwe ambao ni wapenzi wa CUF kuwa idadi kubwa ya vijana wa Zimbabwe ni wafuasi wa MDC na ni wao ambao ndio waliosababisha ushindi mkubwa wa chama hicho kwa kuhakikisha kuwa kila mmoja wao alijiandikisha na kupiga kura. Vijana hao pia wamesifiwa kwa kufanya kazi kubwa ya kutembea maeneo mbalimbali kuwahamasisha wananchi. 

Vijana wa CUF wamesema kuwa kwanza wanatoa pongezi kwa vijana wenzao wa MDC pili wamepokea taarifa hizo za ushindi wa MDC kama changamoto kwao katika uchaguzi mkuu utakao fanyika nchini oktoba, mwaka huu. 

Mkurugenzi wa vijana CUF Bw. Shaibu Akwilombe ameliambia NASAHA kwamba pamoja na kufurahia matokeo hayo ya MDC katika uchaguzi huo wa Zimbabwe, wameyapokea pia matokeo hayo kama changamoto na hivyo "tunaandaa mikakati maalum ya 'kingangali' itakayo 'waliza akina kidumu' mwezi Oktoba mwaka huu". 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Serikali isikilize kilio cha wapinzani na Waislamu

Kishindo cha CUF chaitikisa Dar

Mamia  warudisha kadi za CCM Kilwa

Chama cha Mugabe chupuchupu Zimbabwe

Wasikilizeni wananchi wasemavyo toka kwenye meli mbovu mkabala na Posta ya zamani

CCM yakasirishwa kwa kuswaliwa Mtume (S.A.W.)

Wanaomzomea Bilal waambiwa Oktoba watakula jeuri yao

CCM wapoteza viti 18196; CUF yaongoza kuvinyakua

Tambwe huyoo anakuja!

Ushauri Nasaha
Unapomdharau mama yako mbele ya rafiki yako...

MAKALA
Uchaguzi wa Zimbabwe: Vita kati ya mabeberu na wapinga Ukoloni mamboleo

MIPASHO NASAHA
Matonya wahi, pesa zinatoka sasa!

MAKALA
Vijembe kwa viongozi wa vyama vya upinzani, huduma kwa wananchi ziro

KALAMU YA MUANDISHI
Ukongwe hausaidii kubaki madarakani

MAKALA
Kuchanganya siasa na ushirikina

Habari za Kimataifa

Lishe
Faida za vyakula vya nyuzi nyuzi

RIWAYA
Dunia ndivyo ilivyo - 4

Barua

MASHAIRI

TANGAZO

MICHEZO

  • Mpambano wa watani wa jadi: U-CCM umeiponza Yanga wasema Simba
  • Wanamichezo wamshtukia Mkapa
  • Mabosi DRFA kujulikana leo

  • Pupe, Mziray wamlia ‘dip’ Shungu
    -


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita