|
Na. 054 Jumatano Juni 28 - Julai 4, 2000 |
|
|
|
|
|
Unapomdharau mama yako mbele ya rafiki yako... KUNA msemo wa Kiswahili usemao "ukikuta wenyeji wanacheza ngoma na wewe cheza. Kama ilivyo katika msemo huu kuwa mgeni hatakiwi kucheza tu bali analazimika kucheza kwa muondoko ule ule sawa na wa wenyeji wake, ndivyo ilivyo pia katika maana ya msemo huu. Kwamba mgeni huiga kufanya jambo lifanywalo na wenyeji na kwa namna hiyo hiyo ifanywavyo na wenyeji hao. Mwandishi KHADIJA M. IDD anaeleza zaidi. MSEMO kama huu unawiana sawa sawa na mada yetu ya leo kwamba iwapo utamdharau au kumchukia mama yako mbele ya rafiki yako au mgeni wako, unaweka mazingira ya kumfanya mgeni au rafiki yako naye amdharau. Labda nitoe tahadhari hapa kuwa mada hii hailengi kuhalalisha dharau au chuki ifanyike wakati ambapo hakuna mgeni, bali leo tunalenga kudhibiti hisia zetu ili tusiwaingizie wasiohusika. Katika familia huweza kutokea kuwa watu wote wana mtazamo mmoja juu ya mtu fulani katika familia hiyo. Wanafamilia wanaweza kumchukia mmoja wa wanafamilia hiyo kwa sababu mbalimbali. Hata hivyo si lazima iwe kweli kwamba mtu huyo awe mbaya kama anavyosemekana, lakini kutokana mazingira yalivyojengwa hakuna uzuri au wema wa mtu huyu utakaoonekana na kila mtu atauona ule ubaya wake tu. Inawezekana kuwa mtu huyu anayechukiwa akawa ni mama yako au mke/mume wako. Na inawezakana pia kuwa wewe ni mtu pekee unayemdharau au kumchukia mama au mke/mume wako. Huweza kutokea siku umekasirika na ukaanza kumgombeza na kumuonesha dharau mtu huyo unayemchukia mbele ya mgeni wako. Labda ulikuwa hujakaa ukafikiri kwamba yule dada yako uliyemgombeza mbele ya rafiki yako alijisikiaje wakati ule. Labda pia hivi sasa ni wakati muafaka wa kukaa katika nafasi yake na kufikiri kama ungekuwa wewe ungejisikiaje kudharauliwa mbele ya wageni. Pamoja na haya yote, kitendo hiki kinamfanya mgeni wako naye amdharau mama au kaka yako kwa kuwa nawe unamdharau. Kwa kweli kitendo hiki unachokifanya kinawafanya wageni wako washindwe kuangalia hali halisi bali nao kuingia katika ngoma unayoicheza bila kufikiri. Katika mazingira kama haya, Ushauri NASAHA unakuambia, "Pamoja na kwamba unaweza kuwa na tofauti au kutoelewana na ndugu au rafiki yako onesha tofauti zako kwa namna ambayo hutamdhalilisha mwenzako. Na hili litawezekana iwapo utaheshimu uamuzi wa wenzako kwa kujua kwamba walitumia akili kufikiri kabla ya kufanya jambo lolote. Vile vile katika kusawazisha mambo, jaribu kumnasihi yule anayeonekana kama mbaya katika familia. Msaidie aweze kujirekebisha katika mambo ambayo wengine wanamchukia. Kwa mfano ndugu yako mbinafsi na anayejijali yeye tu na kutojali wengine, anayefua nguo zake tu na kusafisha chumba chake tu na kuacha wengine "wajaze" wenyewe, unaweza kumsaidia kuja kujaribu kufikiria angejisikiaje anayofanyiwa yeye. Unaweza kumsaidia pia kwa kumwelemisha kuwa maisha katika familia hulenga kusaidiana na kujaliana kwa shida na raha. Hili likifanyika huku ukimwonesha unampenda wakati wengine wanamchukia unaweza kubadilisha tabia yake. Pamoja na kwamba utakuwa na tofauti na ndugu yako, bado unatakiwa kumpenda na kumheshimu; katika hali kama hii rafiki na wageni wako pia watampenda na kumheshimu na pengine zaidi ya unavyomheshimu wewe. Waelimishe wanafamilia wengine pia juu ya kuheshimiana na kumpenda ndugu yao, waelimishe kuwa kumpenda ndugu yao, waelimishe kuwa kumpenda ndugu yao ndio njia bora ya kumaliza chuki baina yao. Kuvumiliana na kurekebishana ni bora kuliko kutangaza aibu na ugomvi uliopo. Kwa kumalizia tukumbuke tu kuwa wageni na rafiki zetu watatenda kama vile ambavyo sisi wenyeji wao tunavyotenda. Wakiona tunawadharau ndugu zetu ni rahisi sana kwao kuiga tunavyofanya, kama Waswahili wasemavyo "ukikuta wenyeji wanacheza ngoma nawe..." |
YALIYOMO
Tahariri
Kishindo cha CUF chaitikisa Dar Mamia warudisha kadi za CCM Kilwa Chama cha Mugabe chupuchupu Zimbabwe Wasikilizeni wananchi wasemavyo toka kwenye meli mbovu mkabala na Posta ya zamani CCM yakasirishwa kwa kuswaliwa Mtume (S.A.W.) Wanaomzomea Bilal waambiwa Oktoba watakula jeuri yao CCM wapoteza viti 18196; CUF yaongoza kuvinyakua Ushauri Nasaha
MAKALA
MIPASHO NASAHA
MAKALA
KALAMU YA MUANDISHI
MAKALA
Lishe
RIWAYA
Pupe, Mziray wamlia ‘dip’ Shungu - |
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza
hapa
Au
Andika barua kwa: nasaha1420@yahoo.com
|
|
|
|