|
MASHAIRI
Kwaheri Mkapa
Natanguliza kulitaja jina,
La muumbaji wa viumbe tena,
Na yastahiki kusifiwa sana,
Mwaabudiwa hasiye fanana,
Asiyemzazi asiye na mwana.
Kaka Lipumba watufaa sana,
Unapendeza ungali kijana,
Upresidenti unakufanana,
Ukivaasuti hata fulana,
Walio CCM wakimbiana.
Ndugu Mkapa hana chake tena,
Afanye haraka bado mchana,
KurudiMasasi bila kuchana,
Apatiwe shamba lililopana,
Na aweze kulima nakuvuna.
Urais una mwenyewe bwana
Huyo ni Profesa wa uchumi tena,
Wewe nenda Masasi kwa vijana,
Kaandike habari kwa mapana,
Uandishi bado hujaachana.
Watanzania CCM hakuna,
Wakosa sera huruma hawana,
Wao ni mabwana sisi watwana,
Watoa vyeo kwa kupokezana,
Pia mishahara iliyonona.
Octoba yaja najua tutapona,
Lipumba haja na mambo ya mana,
Yasio na sifa ya kujuana,
Na asiyefaidika hakuna,
Kweli ni CCM haina mana.
Katu Lipumba hatajibizana,
Yeye hutangaza sera bayana,
Najua CCM sera hawana,
Matusi kwao kitu cha maana,
Ushindi kwa Lipumba ubayana.
Najua wengi Wataongozana,
Misululu wakisukumana,
Profesa Ikulu yako amana,
Maendeleo hasa kwa vijana,
Kwani mitaani tunazongana.
Na nina ushahidi wa majina,
Wabunge wengi CCM kuachana,
Lipumba jiandae kwa mapana,
Kupokea wabunge wengi sana,
Tena CCM kwao ni hapana.
Vijana ngangali twatambuana,
Jino kwa jino hata na mchana,
Wakiiba kura tutapambana,
Kwa kherini twaenda kuandaana
Lipumba Ikulu ni yako bwana.
Na Dk. Archiduke H.H.
S.L.P. 90329,
Safarini Masasi.
I.Q.Imepanda
Wewe unaejigamba, kuwa ndiye stahili,
Unapita ukitamba, nchi unaihimili,
Waenda nayo sambamba, kukuchagua sahili,
Umesahau ya kwamba, sasa tunazo akili.
Zamani mlituona, mno tungali wachanga,
Mlizifanya khiyana, na mali kuzibananga,
Msituone wa mana, mkatudhani wajinga,
Sasa roho tarushana, tumezitoa mhanga.
Hivi sasa tumekua, twatambu akusagura,
Twajua safi nachua, hapana kutuburura,
Mambo yanabatuelea, twayapata barabara,
Huwezi kutuzingua, tumesimama imara.
Eti wewe unafaa, kipindi kuendeleza,
Mengi umetufanyia, unataka kuyakuza,
Nafasi kukiachia, mengine utaongeza,
Hujui kukuchagua, ni kama kujiapiza.
Akili zetu timamu, I.Q. imepanda,
Tunazo kubwa elimu, huwezi kutuvurunda,
Meonja chungu na tamu, twaelewa vya kudanda,
Wala haitulazimu, tafanya tunavyopenda.
Usijifanye muhimu, bila wewe tutavunda,
Ni lazima ufahamu, wapo chati wamepanda,
Wazuri wataalamu, nchi wanaoipenda,
Raia walohitimu, wanaweza kuilinda.
Sijifanye namba wani, ili uweze tuteka,
Ukajidai amani, wewe umeisimika,
Kukasahau yakini, wananchi tumeweka,
Hivyo ukituhaini, tukitaka tageuka.
Sikifanye kichochoro, kutaka kujichimbia,
Hebu ziondoe ndaro, situfanyie udhia,
Tumechoka zako kero, situletee kujua,
Sasa usawa na ziro, hesabu hujatimia.
Hebu tupe mantiki, kwa hayo unayonena,
Amani bila ya haki, wapi ulipoyaona?
Kutugawa mediriki, dhaifu na bora sana,
Leo hii wajinaki, kwamba nawe wa maana.
Wengine wametokea, wanaojua kupanga,
Uchumi wamesomea, na hauwapigi chenga,
Iwapo tawachagua, hawatofanya ujinga,
Kama ulivyozea, kuvunja na si kujenga.
Mara hii huna ngoma, wachezaji metimka,
Hata ukiirindima, kucheza wamekuchoka,
Mikono itakuuma, na ngoma itapasuka,
Bora achie mchuma, usije ukaumbuka.
Sasa ungetulizana, hayo uyaweke kando,
Uwaachie vijana, wauondoe uvundo,
Nchini ulojazana, wauweke kwenye gando,
Maisha yawe mwanana, tuufaidi uhondo.
Tuliza boli kitambi, umeshakula yatosha,
Sifuate sakubimbi, njia watakupotosha,
Mara hii hautambi, mapema twakujulisha,
Sisi si mahavinimbi, visa vyako metuchosha.
Wazi twakupasulia, mwaka huu kuna fensi,
Hivyo kaa zingatia, tutakupeleka resi,
Dhuluma kitufanyia, hatuachi kirahisi,
Haki taipigania, hadi nchini ipasi.
Tama twasisitizia, acha kujikoshakosha,
Mambo yako twayajua, hadaa hutatuvisha,
Makini tumetulia, huwezi tubabaisha,
Unahodha hujajua, hufai kutuendesha.
SIHABA
DAR ES SALAAM.
Ukweli unauma
CCM wanalia, Lipumba kamwaga sela,
Dodoma kaunguruma, hakuna alie lala,
Kafunua blanketi, ya Wagogo walo lala,
Ukweli unauma, Mangula wacha kulia.
Machozi yanakutoka, Lipuumba ukimuwaza,
Sasa utafanya nini, na hivi kaenda Mwanza,
Huyo si saizi yako, cheo chake ni cha kwanza,
Ukweli unauma, Mangula wacha kulia.
Huyo ndie Profesa, mkubwa wa maofisa,
Jina lake linatajtwa, hata kule Ufaransa,
Yeye akitaka kwenda, ng’ambo hangoji ruhusa,
Ukweli unauma, Mangula wacha kulia.
Chama hicho CCM, kinaongoza kwa wizi,
Mashirika kimekomba, mambo yote yako wazi,
Wananchi tu tabani, mfano wa wakimbizi,
Ukweli unauma, Mangula wacha kulia.
Beti tano zinatosha, Mhariri usaini,
Watu sasa ni ngangari, hakuna tena utani,
Visenti vyenu vya rushwa, sisi hatuvitamani,
Ukweli unauma Mangula wacha kulia.
Mwela Bondo (Kipupwe),
Makumbusho,
Dar es Salaam.
Nyumba kwa nyumba
Mwanzoni Bismillahi, natamka ya Karima,
Mtukufu ya Hillahi, Rabi mwingi wa rehema,
Nakuomba ya Hillahi, lishikwe ninalosema,
Katika kujenga CUF, nyumba kwa nyumba muhimu.
Nyumba kwa nyumba muhimu, nawaomba wanadamu,
Hasa kwenu CUF damu, ili sera tufahamu,
Lipumba tumfahamu, kwa kwote kila sehemu,
Katika kujenga CUF, nyumba kwa nyumba muhimu.
Tuhamasishe wenzangu, kazi bado mtambuwe,
CCM bado chungu, hili hasa muelewe,
Tena wanayo machungu, kwa haya yetu mayowe,
Katika kujenga CUF, nyumba kwa nyumba muhimu.
Kwa Bara na Visiwani, nyumba kwa nyumba jamani,
Mijini na vijijini, nyumba kwa nyumba jamani,
Matawi nawaombeni, nyumba kwa nyumba jamani,
Katika kujenga CUF, nyumba kwa nyumba muhimu.
CCM bado wengi, Lipumba nakueleza,
Ten awameapa wengi, CUF kukiangamiza,
Ila wana kimya kingi, wana mengi naeleza,
Nyumba kwa nyumba jamani, haki isijepotea.
Mtauni na Sabaya, jamani nyumba kwa nyumba,
Nawe Mshirazi haya, ingia nyumba kwa nyumba,
Kiko nawe haya haya , nenda mnadi Lipumba,
Katika kujenga CUF, Dikupanyumba kwa nyumba.
Nawe K.S. Luanda, na Kassimu mwana Mbava,
Tuepukeni kuvurunda, na mambo sasa yameiva,
Tuvue yao magwanda, huko Tanga mwaniiva,
Katika kujenga CUF, nyumba kwa nyumba jamani.
Mtaguluka Rashidi, nawe usaini wito,
Lipu tuzidi mnadi, kwa watu awe mvuto,
Na wewe bwana Jihadi, upokee wangu wito,
Katika kujenga CUF, nyumba kwa nyumba jamani.
Na wewe dada Sihaba, sihaba kweli sihaba,
Uzidishe kuwakaba, ukishindwa piga roba,
Nakuhusia Sihaba, tumnadi LIPU baba,
Katika kujenga CUF, nyumba kwa nyumba jamani.
Kaditama natamati, na hapa ni hitimisho,
Hapa nazifunga nati, nimefika kwangu mwisho,
Tuhamasishe kwa dhati, pasi woga na vitisho,
Katika kujenga CUF, nyumba kwa nyumba jamani.
Almasi H. Shemdoe,
“Tunda la Matumaini”,
Dar es Salaam.
|
YALIYOMO
Tahariri
Serikali isikilize kilio cha
wapinzani na Waislamu
Kishindo
cha CUF chaitikisa Dar
Mamia
warudisha kadi za CCM Kilwa
Chama
cha Mugabe chupuchupu Zimbabwe
Wasikilizeni
wananchi wasemavyo toka kwenye meli mbovu mkabala na Posta ya zamani
CCM
yakasirishwa kwa kuswaliwa Mtume (S.A.W.)
Wanaomzomea
Bilal waambiwa Oktoba watakula jeuri yao
CCM
wapoteza viti 18196; CUF yaongoza kuvinyakua
Tambwe
huyoo anakuja!
Ushauri Nasaha
Unapomdharau
mama yako mbele ya rafiki yako...
MAKALA
Uchaguzi
wa Zimbabwe: Vita kati ya mabeberu na wapinga Ukoloni mamboleo
MIPASHO NASAHA
Matonya
wahi, pesa zinatoka sasa!
MAKALA
Vijembe
kwa viongozi wa vyama vya upinzani, huduma kwa wananchi ziro
KALAMU YA MUANDISHI
Ukongwe
hausaidii kubaki madarakani
MAKALA
Kuchanganya
siasa na ushirikina
Habari
za Kimataifa
Lishe
Faida
za vyakula vya nyuzi nyuzi
RIWAYA
Dunia
ndivyo ilivyo - 4
Barua
MASHAIRI
TANGAZO
MICHEZO
Mpambano wa watani wa jadi: U-CCM
umeiponza Yanga wasema Simba
Wanamichezo wamshtukia Mkapa
Mabosi DRFA kujulikana leo
Pupe, Mziray wamlia ‘dip’ Shungu
- |