|
Na. 054 Jumatano Juni 28 - Julai 4, 2000 |
|
|
|
|
|
Kuchanganya siasa na ushirikina Na Mwinjilisti Kamara Kusupa TUMESIKIA mengi sana yakisemwa juu ya kuchanganya siasa na dini. Wengine wametahadharisha, wengine wameonya, wengine wamekaripia na wengine wametisha. Lakini kati ya wasemaji wote hakuna hata mmoja aliyesema kitu kuhusiana na suala la kuchanganya siasa na ushirikina, maana ushirikina nayo ni dini isipokuwa haimwongozi mtu kwa Mungu wa kweli. Wala hakuna aliye tuthibitishia kwa uhakika kabisa kwamba katika historia iliwahi kuwako siasa yoyote ambayo ni safi, iliyotakata, na ambayo haikuchanganyika na chochote kile isipokuwa imebaki kama ilivyo yaani siasa peke yake. Baya kuliko yote ni kwamba wapiga debe hao wa kutaka dini itenganishwe na siasa hawajatuthibitishia kwamba siasa nayo ina mipaka. Hawajatueleza kwamba wenye dini wakibaki na dini yao basi wanasiasa nao watabaki na siasa yao wala wasihusishe wengine. Lakini kinyume chake umekuweko unafiki mtupu wa kutaka viongozi wa dini wasijihusishe na siasa bali siasa ikiisha pikwa na wanasiasa basi iwahusu watu wote, imhusu kila mtu, na kila mmoja pasipo kujali imani ya dini yake. Loo! Huu ni uzandiki. Chanzo cha mageuzi duniani Mageuzi yanayoendelea sasa, ambayo yalianzia Urusi (USSR) na kusambaa hadi nchi zingine za Kikomunisti na zile zilizoenenda katika mfumo wa Kikomunisti lakini ukomunisti wao ukafichwa kwa maneno ya ujamaa, au socialism, au humanism n.k. yalisababishwa na mambo makuu manne:- (a) Kukosekana kwa uhuru watu binafsi, (b) Kukosekana kwa demokrasi ya kweli, (c) Ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, na (d) Umma kutenganishwa na siasa za nchi. Kukosekana uhuru Katika nchi zote zilizotikiswa na mageuzi, kwa muda mrefu kulikuwa na uhuru wa jumla tu wa kusema taifa hili halitawaliwi na taifa jingine lakini ndani ya nchi hizo watu wakiwa katika hali ya mmoja mmoja, waliishi bila uhuru. Watu walikuwa hawana uhuru wa kusema ukweli usiotakiwa na watawala badala yake siku zote watu walisema kile ambacho watawala walitaka kusikia. Watu walikosa uhuru wa kukosoa serikali na badala yake walilazimishwa aidha kushabikia mawazo na hata maamuzi potofu ya watawala vinginevyo yeyote aliyekwenda kinyume angeishia matatani. Kwa kifupi watu kisiasa, kiuchumi na kijamii walibakia kuwa kama watazamaji tu kwenye pambano la mpira, wakishuhudia uharibifu, upotofu na maovu mengine ya watawala pasipo kuyagusa kwa kupinga au walau kuyakataa. Kukosekana demokrasi Karibu nchi zote za kijamaa, zilikuwa ma mfumo wa chama kimoja. Kulikuwa na kile walichozoea kukiita demokrasia ya chama kimoja. Ndani ya mfumo huu chama tawala kiliinuliwa juu na kuchukua nafasi ya Mungu wa taifa. Ili kuhami nafasi hiyo, hapo ndipo zilipobuniwa semi au slogan za kudai chama na serikali havina dini. Wenye dini wako huru na dini zao, wenye taaluma wabakie na taaluma zao, wanawake wabakie jikoni, wanafunzi wabakie darasani, wafanyibiashara wabakie madukani mwao, wafanya kazi wawe huru na kazi zao na wakulima nao wabakie mashambani mwao, wasijihusishe na siasa. Siasa ikabakia kuwa eneo nyeti na haki ya kundi dogo lililojifanya kama ndio wateule katika nchi na kwa sababu ya uteule wao basi hawapaswi kuchukuliwa hatua za kisheria wanapokuwa wametenda makosa ya jinai. Kwa kitambo watawala waliufaidi uhuru huo wa kishetani kwa sababu ulikuwa ni uhuru wa kufanya maovu pasipo kupingwa, huku wakiwa wamewaengua na kuwatenga kabisa wananchi wengine wasishiriki kwenye maamuzi muhimu ya kisiasa. Kwa kifupi ukawako utawala wa wachache, lakini utawala wao ukawa hauna mipaka na kwahiyo wakawa na uhuru wa kuharibu kama wapendavyo pasipo kizuizi chochote. Ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu Utawala wa hao wachache ulienda sambamba na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu. Sheria mbaya kama za kumweka mtu kizuizini pasipo hata kumfikisha mahakamani zikatungwa kwa makusudi ya kupambana na wale watakao thubutu kuleta upinzani. Watawala walikosa imani na mahakama kwamba zinaweza kutoa haki wanayoitaka wao ndiyo maana walikimbilia vizuizi kama kwamba hiyo ndiyo dawa pekee ya kuleta umoja wa kitaifa. Katika maeneo mengine ya maisha zaidi ya eneo la siasa pia kulikuwa na ukiukaji mkubwa wa haki za watu kwa mfano katika eneo la uchumi serikali ndiyo iliyopanga bei za mazao ya wakulima, ndiyo iliyopanga viwango vya mishahara, na pia ndiyo iliyopanga viwango vya bei za vitu pasipo kujali uzalishaji wala nguvu za soko. Sheria nyingi za ukandamizaji zilipitishwa na Bunge la chama kimoja, huku viongozi wa chama na serikali wakijigeuza miungu. Nafasi ya dini ikafinyangwa, serikali ikawa na madhehebu yake ambayo iliyathamini na kuona umuhimu wake, serikali ikawa na viongozi wake wa dini ambao iliwatambua na kuwaheshimu lakini Mungu mwenyewe kama alivyo, hakuheshimiwa wala neno lake halikuhesabiwa kama kitu muhimu katika maisha ya kitaifa. Uasi dhidi ya Mungu ndio uliotawala, mbaya zaidi viongozi wa dini wakaisaidia serikali (iliyoasi) katika kuwadhibiti wafuasi wa dini na kuwaweka katika ule mstari ambao ingawaje kulikuwa na madai ya kwamba kwenye nchi za kijamaa kuna uhuru wa kuabudu, lakini kutokana na udhibiti wa dola, Mungu hakuabudiwa kama inavyotakiwa bali aliabudiwa kama dola ilivyotaka. Hapo ndipo ambapo wasemaji wa dini walipokosa nguvu na ujasiri wa kukemea dhambi za taifa. Kwa maneno mengine naweza kusema dini zilikosa nguv ya kupinga dhambi ya taifa wala hazikuthubutu hata kuisema ili tu kudumisha ule uhusiano mzuri kati yao na serikali. Umma kutenganishwa na siasa Wananchi katika ujumla wao walishirikishwa kwenye siasa kama wateja tu wa kununua hicho ambacho wanasiasa wamekitengeneza katika mipango yao kila walichokipika. Watu walishirikishwa kwenye maandamano ya kuunga mkono maamuzi ya serikali, lakini wale wachache wenye kuelewa mara walipothubutu kufanya maandamano yao kudai hiki au kile, ama maandamano ya kuelezea hisia zao, ilidaiwa ni maandamano haramu na waandamanaji walipata vipigo. Watu walishirikishwa kufanya neno lile ambalo dola ilitaka lifanyike, lakini yanayohusu uendeshaji nchi. Siasa likabakia eneo maalum kwa ajili ya watu maalum. Kwa namna inayofanana na mchezo wa kuigiza, eneo la siasa likafanywa kama eneo takatifu na wote walioko ndani yake wakahesabiwa kama ni watakatifu. Kukaweko na pengo kati ya wanasiasa na wananchi, vyama vya wananchi, yaani vyama vikatekwa na dola kufanywa vyama vya kiserikali kwa hiyo hata zilipotolewa kauli za serikali na wala siyo kauli za wananchi.Kwa ufupi wananchi walifumbwa vinywa na walilazimika kuishi kwenye kibano na kabali ya dola. Sambamba na hilo wasomi na wanataaluma nao walikandamizwa kwa kulazimishwa kuwa chini ya uongozi na utawala wa mambumbumbu, ili tu kuhakikisha taaluma zao hazi-operate kwa uhuru Kutokana na hali hiyo ya viongozi kujifanya miungu na kuchukua nafasi ya Mungu wa taifa, basi inafutia kwamba ili Mungu wa kweli aweze kuchukua nafasi yake, ilipasa, na kwa hakika ilibidi mifumo ya aina hii ianguke, isambaratike, na kutokomea mabadiliko ndipo lilipozuka neno mageuzi. Kwa hiyo mtu akiangalia kwa undani yaani kwa jicho la rohoni ataona ya kwamba mageuzi ya kusambaratisha mifumo dhalimu hayakutoka kwa shetani bali yametoka kwa Mungu kwani shetani hawezi kupigana na mifumo yake mwenyewe. Bwana Yesu katika kuuelezea utawala wa Mungu, aliufananisha na upepo kisha akasema upepo huvuma kwenda kule utakako wala hatuwezi kuuzuia lakini sauti yake twaisikia. Katika tafsiri halisi upepo au kimbunga kilichoiitikisa mifumo ya mataifa mbali mbali ya dunia ndani yake kuna nguvu ya Mungu, ndiyo maana watawala pamoja na ujanja wao, ubabe wao, na nguvu zao za kishetani hawakuweza kuzuia wala kuzima wimbi la mageuzi. Sehemu nyingine ya mafundisho yake, Bwana Yesu alisema yule mtu mwenye kulishika neno langu atafanana na mjenzi mwenye busara ambaye alijenga nyumba yake juu ya mwamba, hata upepo wenye nguvu ukaja ukaipiga nyumba ile lakini isitikisike, kwa sababu ilijengwa juu ya msingi imara ,bali mwenye kuyapuuza maneno haya ni sawa na mjenzi mpumbavu ambaye alijenga nyumba yake juu ya mchanga, upepo wenye nguvu ulipokuja ukaipiga nyumba ile nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa." Ingawaje watawala wanajitahidi sana kuficha, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba taifa letu halikujengwa juu ya mwamba imara ambao ni neno la Mungu badala yake nchi imejengwa juu ya maneno ya wanasiasa, maneno ya kipuuzi, maneno yasiyokuwa na ukweli wala umakini wowote na baya zaidi nchi ikajengwa katika misingi ya ushirikina na imani isiyoeleweka kama ni imani ya Mungu au imani ya shetani. Ndiyo maana nasema wote wenye kumcha Mungu tusiukubali tena upumbavu wa kusema tusichanganye dini na siasa kwani huo ni uwongo wa shetani ambaye ndiye baba wa uwongo wote wa ulimwengu huu maana tukikubali kuitenganisha siasa na dini zetu wao wanasiasa wanafiki wataichanganya siasa na ushirikina wao kisha watatuletea siasa hiyo iliyochanganywa na ushirikina na watasmea tuitii kwa kuwa imeandikwa watiini wenye mamlaka, na hapo tutakapoanza kuitii siasa yao ama kuitekeleza basi hatutakwepa kufanya mambo ya kishirikina mwisho wa yote tutaishia kufarakana na Mungu wa kweli huku tukiwapendeza watawala. Madai ya kutaka tusiichanganye dini na siasa ni madai ya kitapeli kwa sababu tayari tunalazimika kuhusika na siasa za nchi zetu na siasa za mataifa yetu na papo hapo kuna maandiko au maagizo katika vitabu vya napokuja suala la kutii basi na tutii kitu ambacho dhamira zetu zinakubaliana kwa dhati badala ya kutii kama watu waliotekwa nyara. "Enzi za ujamaa tulielezwa kwamba ujamaa ni imani haunabudi kujengwa na watu wanaoamini na kufuata kanuni zake." Imani inayozungumzwa katika ujamaa huo haielezwi nini tofauti yake na imani za dini, wala haielezwi kwamba mhusika ama huyo mwananchi auamini ujamaa kwa kutumia nini. Je kwa kutumia akili yake, au mwili wake ili asije akachanganya imani ya ujamaa, na imani ya dini yake kama ni Uislamu, Ukristo, au Uhindu! Kwa hiyo kwa vinywa vyao walihubiri dini isichanganywe na siasa yao lakini katika uhalisi wa mambo na kwa matendo yao wakaichanganya siasa yao na dini zote zilozo nchini Tanzania kisha kwa ujanja wakasema ujamaa wetu ni tofauti na Ukomunisti walishatutengenezea mkorogo wa kuchanganya imani ya kisiasa na imani ya kidini, kutokana na ukweli kwamba mtu asingeweza kuigawa imani yake iliyoko rohoni mwake kwenye matabaka mawili yaani awe na imani kwa ajili ya siasa, na imani nyingine kwa ajili yadini. Watanzania tumeishi katika udanganyifu huu kwa miaka mingi huku wanasiasa waongo wakitaka tuyaamini maneno yao kama vile tunavyoliamini neno la Mungu, mbaya zaidi wakaufanya uwongo wao (ambacho ni kitu cha binafsi) uwe ni sehemu ya siasa hadi watu wengine wakafikia kusema siasa ni uwongo. Hadi leo hii wengi wanaamini hivyo kwamba siasa ni uwongo na ndiyo maana hawataki siasa ichanganywe na dini lakini hiyo ni imani na misimamo yao potofu kwani siasa kama ulivyo uchumi, biashara, na sayansi nyingine yoyote ile inataka ukweli na uaminifu. Lililo baya kuzidi yote ni jinsi Watanzania walivyoburuzwa kushirki kwenye mbio za mwenge ambazo ni ushirikina mtupu. Kwa sasa tunaishi katika karne ya sayansi na teknolojia kumbe kisayansi Mwenge una faida gani katika maisha ya mtu hadi ukimbizwe kila mwaka na upite kila eneo? Kisha ni kwanini liwe suala la kiserikali! Ingawaje wengi wanauonea haya lakini ukweli ni kwamba Mwenge ni ushirikina na matambiko kwa Mungu asiyejulikana, ni imani ya mshirikina mmoja akiuingiza umma kwenye matambiko yake. Vinginevyo inabidi kujiuliza ni kwanini mbio za Mwenge liwe suala la kiserikali na lisiwe la Chama Cha Mapinduzi tu? SIASA ILIYOCHANGANYWA NA USHIRIKINA NDIO INAYOIPONZA NCHI. |
YALIYOMO
Tahariri
Kishindo cha CUF chaitikisa Dar Mamia warudisha kadi za CCM Kilwa Chama cha Mugabe chupuchupu Zimbabwe Wasikilizeni wananchi wasemavyo toka kwenye meli mbovu mkabala na Posta ya zamani CCM yakasirishwa kwa kuswaliwa Mtume (S.A.W.) Wanaomzomea Bilal waambiwa Oktoba watakula jeuri yao CCM wapoteza viti 18196; CUF yaongoza kuvinyakua Ushauri Nasaha
MAKALA
MIPASHO NASAHA
MAKALA
KALAMU YA MUANDISHI
MAKALA
Lishe
RIWAYA
Pupe, Mziray wamlia ‘dip’ Shungu - |
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza
hapa
Au
Andika barua kwa: nasaha1420@yahoo.com
|
|
|
|