|
Na. 054 Jumatano Juni 28 - Julai 4, 2000 |
|
|
|
|
|
Vijembe kwa viongozi wa vyama vya upinzani, huduma kwa wananchi ziro Na Rajab Kanyama UCHAGUZI, ndio ushahidi wa kweli wa kuonyesha kwamba, madaraka ya kutawala kisiasa katika nchi, popote pale duniani hupatikana kutoka kwa wananchi. Kwa sababu hiyo ni muhimu kabisa kwa uchaguzi wowote, hasa ule unaohusiha kumchagua kiongozi mkuu wa nchi, Rais na baadhi ya wananchi watakao wawakilisha wenzao katika baraza la kutunga sheria (Bunge), uwe huru na wa haki, ili viongozi watakao chaguliwa iwe ni kweli wamepata ridhaa ya wananchi. Umuhimu wa jambo hili, unajulikana na wananchi wote wenye akili timamu, maana uchaguzi ulio huru na wa haki, ndio njia pekee ya kuhakikisha kwamba amani na utulivu ndani ya nchi vinaendelea kudumishwa. Kufanya vinginevyo, kwa njia yoyote ile, ni sawa na kukabidhi shetani amana ya vitu hivyo. Chanzo cha vurugu katika nchi nyingi za kiafrika, ni tabia ya viongozi wale wanaokuwepo madarakani, kutokutaka wananchi watumie haki yao ya msingi kabisa, katika utashi wa kuchagua kiongozi au viongozi wanaowataka. Mara zote, viongozi madhalimu, wasiopenda haki, huwa ndio wa kwanza kujipa haki ya kufikiri kwa niaba ya wananchi, na kutahadharisha juu ya mambo ambayo kimsingi ni wao ndio wanaoyatenda. Lengo lao kuu, ni kuwazuga wananchi waendelee kulala usingizi, huku wao wakiendelea kupeta. Katika makala ya wiki iliyopita, tulifanya doria na tukaeleza kwamba, tutapitia baadhi ya matamshi ya viongozi wa vyama vya siasa hapa nchini ili tuangalie matamshi hayo kimantiki na malengo yake ya kisaisa. Nitanza kwa kunukuu "Wamefikia pahala pa kuthubutu kuamini kuwa damu ya Watanzania ni bei inayofaa kutozwa ili waingie Ikulu.Natanabaisha kwamba hatari hiyo siyo imedhihiri tu Visiwani, bali zipo juhudii za wazi kueneza sarakani hiyo ya mfarakano na uhasama wa kijamii Bara." Haya yalikuwa ni matamshi ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, wakati akifungua mkutano wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi. Kimsingi, katika maneno hayo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi alikuwa anapandikiza hofu katika mioyo ya wasikilizaji wake kwamba, kukichagua Chama Cha Wananchi (CUF) katika uchaguzi mkuu ujao kutaleta machafuko na umwagaji wa damu nchini. Wananchi, walitegemea mwenyekiti atoe ushahidi ili kutilia nguvu hoja, lakini, kwa vile alikuwa na mambo mengi yakueleza, hakufanya hivyo. Kama angetaja baadhi ya matendo yaliyokwisha kufanywa na Chama Cha Wananchi (CUF) ambayo kwa namna moja au nyingine yangetilia nguvu hoja hiyo ,wananchi wangemuelewa, lakini sasa ametuacha gizani. Juhudi za wazi alizokusudia katika hotuba yake, ni harakati za Chama cha Wananchi (CUF) zinazofanywa na mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, katika kuelimisha jamii, na kuhamasisha wananchi ili wakiunge mkono chama chake (CUF). Kwa mtazamo wa hotuba ya mwenyekiti wa chama cha mapinduzi, ni hatari kwa wananchi kutambua ukweli wa mambo ya kwamba hali mbaya ya uchumi, pamoja na maisha ya jamii ni matokeo ya sera mbovu za Chama Cha Mapinduzi na serikali yake. Badhi ya wananchi wanasema walilazimika kutafakari kwa kina kuhusu matendo ya Chama cha Wananchi (CUF) ili waweze kukubaliana na mtazamo wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, lakini wanasema wameshindwa kupata ushahidi wa kuunga mkono hoja hiyo. Wananchi wanasema, kwa kutumia kigezo hicho hicho,wakaanza kuangalia matendo ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi, kuanzia Visiwani mpaka huku Bara. 1. Kuwekwa ndani kwa wanachama wa Chama cha Wananchi na viongozi wao, kwa tuhuma za uhaini, kulikofanywa na serikali ya muungano huko Zanzibar kwa sababu za kisiasa. 2.Kutokutekelezwa kwa muafaka uliofikiwa kati ya Chama Cha Mapinduzi na Chama cha Wananchi (CUF) uliosimamiwa na Jumuiya ya Madola, kuhusu mtafaruku wa kisiasa uliokuwepo Zanzibar, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995. 3. Kupigwa kwa wananchi, na polisi wa serikali ya muungano huko Zanzibar na Kigoma kwa sababu za kisiasa na 4. Kuuawa kwa waandamanaji wa Kiislamu, kulikofanywa na Polisiw a Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kadhia ya Mwembechai. Ni baadhi ya matendo yaliyowajia wananchi hao kwa haraka,ambayo, hata wataalamu wa mambo ya kijamii wanakubali bila mjadala kwamba, ni matendo yanayopanda mbegu ya uhasama mbaya kabisa ndani ya jamii, na uhasama kati ya Polisi na raia, mambo ambayo ndio huwa chanzo cha mapambano ya wenyewe kwa wenyewe ndani ya nchi. Nikapata mshituko, kumbe,nikabaini kwamba, maneno tunayoambiwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na serikali yake yanahusu mambo wanayotenda wao wenyewe. Kwa nini? Ndiyo hoja iliyofuata. Ni, nia ya kuendelea kushika madaraka au kwa lugha ya Chama Cha Mapinduzi kwa viongozi wa vyama vingine vya siasa nchini, uchu wa madaraka? Bila shaka, wananchi wamekwisha kubaini kwamba, wenye uchu wa madaraka ni viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na serikali yake na wala si viongozi wa vyama vya upinzani kama CCM wanavyodai. Si hivyo tu, hata matokeo ya siku za karibuni huko Mererani na msitu wa mbogo yanathibitisha kwamba, ni Chama Cha Mapinduzi na serikali yake ndio wanaopanda mbegu ya umwagaji wa damu nchini. Katika gazeti la NIPASHE la tarehe 24 Aprili 2000, tulisoma kwamba, wananchi wa kijiji cha Msitu wa Mbogo, Mbuguni, Arusha, wamenyang'anywa ardhi waliyokuwa wanalima na kupewa tajiri mmoja mwenye asili ya Kiasia. Kwa vile tajiri huyo hana uwezo wa kulima ardhi yote, siku hizi anafanya biashara ya kuikodisha ardhi hiyo kwa wananchi kutoka mjini Arusha, na baadhi ya wananchi wanaomiliki mgodi huko Mererani. Mifugo ya wananchi ikiingia katika shamba hilo, hukamatwa na hairudishwi kwa wenyewe mpaka wamlipe huyo Muasia kiasi fulani cha fedha kama faini. Viongozi wa kijiji wamekuwa marafiki wakubwa wa tajiri huyo, na wao hulima katika eneo hilo kila watakapo, lakini kijiji hakina shamba. Hii ndio hali halisi ya sera za kilimo za Chama Cha Mapinduzi na serikali yake. Wananchi, tunatakiwa kuwa macho katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huuwa 2000. Tusiposhituka mapema,tutageuzwa kuwa vibarua ndani ya nchi yetu wenyewe. Mada hii tutaendelea nayo wiki ijayo. |
YALIYOMO
Tahariri
Kishindo cha CUF chaitikisa Dar Mamia warudisha kadi za CCM Kilwa Chama cha Mugabe chupuchupu Zimbabwe Wasikilizeni wananchi wasemavyo toka kwenye meli mbovu mkabala na Posta ya zamani CCM yakasirishwa kwa kuswaliwa Mtume (S.A.W.) Wanaomzomea Bilal waambiwa Oktoba watakula jeuri yao CCM wapoteza viti 18196; CUF yaongoza kuvinyakua Ushauri Nasaha
MAKALA
MIPASHO NASAHA
MAKALA
KALAMU YA MUANDISHI
MAKALA
Lishe
RIWAYA
Pupe, Mziray wamlia ‘dip’ Shungu - |
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza
hapa
Au
Andika barua kwa: nasaha1420@yahoo.com
|
|
|
|