|
Na. 054 Jumatano Juni 28 - Julai 4, 2000 |
|
|
|
|
|
Ukongwe hausaidii kubaki madarakani Na Mwandishi Maalim Bassaleh Kama ni nia ya chama tawala kubaki madarakani, basi lengo la kila chama cha upinzani ni kuingia Ikulu. Lakini Ikulu hawakai wapangaji wawili. Basi vipi vyama vya upinzani vitaweza navyo, kuingia Ikulu pasina kukiondoa katika madaraka chama tawala? Kukiondoa madarakani chama tawala, kama CCM, si lelemama! Inahitaji mikakati madhubuti, hekima, busara, na juu ya yote, umoja baina ya wapinzani. CCM ni chama kikongwe na chenye mizizi yake kila pahali nchini. Ndicho chama kilichopigania na kuleta uhuru; na ndicho chenye nguvu za dola. Wakati hakuna chama chochote cha upinzani kilichofikisha umri, angalau, wa miaka kumi tu, CCM ina umri wa karibu nusu karne. Hiyo ina maana kwamba CCM,mbali ya nguvu za dola, ina uzoefu mkubwa kuliko vyama vya upinzani. Kwa hali hiyo chama hicho kina nafasi nzuri ya kutumia uwezo, ujuzi na uzoefu wake huo, wa miaka mingi,katika kujichimbia madarakani. Lakini mara nyingine kubaki madarakani kwa kipindi kirefu, kunaweza kukiponza chama kuliko kikisaidia. Angalia mmoja katika wakongwe wa siasa KATIKA ENEO HILI LA Afrika ya Mashariki na Kati, Dk. Kenneth Kaunda. Chama chake cha UNIP ndicho kilichopigania uhuru wa Zambia na kufaulu kuutia uhuru huo mikononi, Kaunda akiwa ndiye kiongozi wa chama hicho. Lakini ulipokuja uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, Dk. Kaunda pamoja na chama chake, walishindwa na mtu mfupi wa kimo,na pia, mgeni katika uwanja wa siasa, Rais Chiluba. Hiyo ni kwa sababu Wazambia walikuwa wamekwisha choka na utawala huohuo, siku zote. Watu walikuwa tayari wamechoka, walitaka mabadiliko. Kwa mujibu wa hali ya mazingira ilivyo Tanzania, kwa hivi sasa, kuna kila sababu ya kuamini kuwa siku za kutamba kwa chama cha CCM zinakaribia mfundoni. Watanzania wamechoka na chama hicho hicho,miaka nenda miaka rudi. Wanataka mabadiliko. Inaonekana hata na chama chenyewe kimekwisha elewa hilo. Ndiyo maana tumekuwa tukisikia mara kwa mara, kuwa makada wakongwe wa chama hicho wanataka kung'atuka kuwapa nafasi damu mpya, katika safu ya uongozi. Lakini haijulikani,kwa hakika, wangapi katika wakongwe hao walio tayari kwa hilo? Na hata kama wapo watakaong'atuka wataathiri nini katika uchaguzi ujao? Pili, katika uchaguzi mkuu uliopita, wa mwaka 1995, CCM ilitoa ilani ya uchaguzi, ambayo baadaye, yenyewe ilikiri kuwa haitekelezeki. Na kweli haijaweza kutekelezwa. Jambo hilo, la kushindwa kutekeleza ilani yake, ni dhahiri, kwa kiwango fulani, limekipunguzia chama hicho nafasi yake ya kuweza kuchaguliwa tena. Aidha, ukosefu wa ajira kwa vijan, ambao ndio walio wengi katika jamii, ukata uliowakumba walala hoi, na kupanda kwa gharama za maisha kunakifanya chama hicho, mbele ya macho ya Watanzania wengi kionekane sera zake haziwezi kamwe kumkwamua mwananchi wa kawaida, katika hali duni aliyo nayo. Zinaweza kuwapo sababu miamoja na moja za kuwafanya walio wengi kutokipigia kura chama hicho safari hii. Kwa mfano, kuna wale wanaodai mafao yao tokea kuvunjwa kwa jumuiya ya Afrika Mashariki. Hawa kwa kupitia katika vyombo vya habari, wametangaza kuwa wao na familia zao hawatakipa kura zao chama tawala. Na hivi sasa wako mbioni kuifikisha serikali mahakamani, ili kudai mafao yao. Kuna wanaopunguzwa makazini kiholela kwa ajili ya kutekeleza zoezi la ubinafsishaji mashirika ya umma. Zoezi hilo limewaongezea ukata wa maisha wale walioachishwa kazi. Wamejikuta wakishindwa kuzitunza familia zao na kuendelea kugharamia elimu ya watoto wao. Jee! Hawa watakuwa tayari kukipa kura zao chama tawala? Mheshimiwa Mrema, naye, tokea achukue fomu za kugombea urais, kwa tiketi ya chama chake cha TLP, amekuwa akisikika akilitajataja swala la Mwembechai na pia ukadhi. Anaelewa kuwa Waislamu wamekasirishwa na jinsi serikali ilivyolishungulikia swali hilo la Mwembe Chai. Anataka alitumie kama chambo cha kuwavua Waislamu wampigie kura yeye, katika uchaguzi ujao. Kuhusu swali hili, haijulikani kama Mheshimiwa Mrema amelifanyia tathmini ya kina au anabahatisha bahatisha tu. Ni kweli Waislamu wamekasirishwa sana, tena sana na namna hilo swali la Mwembe Chai lilivyoshughulikiwa. Na wengi wao wametamka, bila ya kificho, kuwa watakinyima kura zao chama tawala. Inaonekana Mheshimiwa Mrema anataka kuutumia mwanya huo ili ajizolee kura za chee. Lakini Waislamu wanauliza jee,Mheshimiwa huyo anaelewa Mtume Muhamad (s.a.w.) alivyosema? Wanasema kama hajui, basi wanampasha kuwa Mtume (s.a.w.) amesema, "Muumin hatafunwi mara mbili katika shimo moja." Waislamu hao wanahoji kama Mhe.Mrema anaona kuwa Waislamu hawataipigia kura CCM kwa sababu ya kushughulikia vibaya kadhia ya Mwembe Chai; jee yeye anadhani Waislamu wamekwisha sahau jinsi yeye mwenyewe alivyokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani alivyolishughulikia swali la mabucha ya nguruwe?Au anahisi kuwa Waislamu hawajui kuwa yeye ndiye aliyeutangazia umma kuwa serikali imekamata makontena hewa ya majambia bandarini yaliyoingizwa na Mujahidina? Jee! Siye yeye alipokwenda msikiti wa Mtoro kusikiliza malalamiko ya Waislamu akageuka na kusema kuwa huko hakuwaona Waislamu bali alikutana na WAHUNI na WAVUTA BANGI? Leo anawataka Waislamu hao hao wampigie kura? Mradi sababu za kukikosesha chama cha CCM kura, ni nyingi sana. Na kama tulivyokwisha tangulia kueleza hata CCM yenyewe imekwishalielewa hilo. Yasemekana hata yale mabadiliko ya 13 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyofanywa hivi karibuni, yalitokana na wasiwasi huo. Kabla ya kubadilishwa katiba ilikuwa mgombea wa kiti cha Urais ili ahesabike kuwa ameshinda ilibidi apate zaidi ya asilimia hamsini kwa zote. Lakini kwa vile CCM inachelea kuwa, safari hii,haitafikia asilimia hiyo, ndiyo ikabadilisha kifungu hicho, na kufanya mgombea wa kiti hicho ataweza kuwa mshindi kama atawashinda wagombea wengine kwa wingi wa kura tu, hata kama hajafikia asilimia hamsini.! Kwa hiyo kwa mujibu wa mabadiliko hayo yaliyofanywa, kwa haraka haraka, uwezekanao wa kuwa na Rais asiyekubalika na wengi ni mkubwa sana. Na Mheshimiwa Mrema, kwa kukataa kwake kuungana na kambi ya upinzani, kuweka mgombea mmoja tu wa kiti cha urais kwa kambi hiyo,kwa kiwango fulani kutachangia kupatikana kwa Rais huyo asiyekubalika. Jambo moja halina ubishi.Hakuna chama chochote, safari hii, kiwe ni cha upinzani au chama tawala, chenye uhakika, wa mia kwa mia, kupata ushindi wa chee. CCM ambayo katika uchaguzi uliopita wa mwaka 1995, iliibuka mshindi kwa kupata asilimia 61.8 inahisi katika uchaguzi ujao haitafikia hata asilimia hamsini; jee Mrema ambaye alipata asilimia 27.8tu ana uhakika gani wa kupata ushindi mwaka huu? Tokea lilipochomoza wazo la kuweka mgombea mmoja kwa kambi ya upinzani, Mheshimiwa Mrema amekuwa akisitasita kujiunga na umoja huo. Lakini kutokana na kauli zake si kwamba yeye anapinga umoja huo, au kwamba anapinga wazo la kuwa na mgombea mmoja; bali anachokipinga yeye ni kwamba umoja huo wa upinzani usimsimamishe mgombea mwingine yeyote isipokuwa yeye tu. Kama upinzani utamhakikishia kuwa yeye ndiye atakayesimamishwa basi yuko tayari kuungana nao. Hoja kubwa anayoitoa ni kuwa yeye anaungwa mkono na Watanzania wengi. Ni kweli hapo kale alikuwa ni gumzo la nyumbani. Kila mtu alikuwa MREMA! MREMA! MREMA! Lakini hiyo ilikuwa lini? Ni 1995! Mwaka huu mambo yamegeuka ghafla. Sasa ni Lipumba! LIPUMBA! LIPUMBA! Kama katika uchaguzi wa mwaka 1995 Lipumba aliambulia kura 418,973 tu kwa nchi nzima, walioshuhudia mapokezi yake juzi, wanasema, safari hii, katika hili jiji la Dar es Salaam, peke yake, ikiwa wale waliojitokeza kumpokea, watajiandikisha na kupiga kura,basi Profesa huyo ana uhakika wa kupata kura milioni moja au hata zaidi! Mbali mikoa mingine! Na kwa jinsi watu hao walivyoivumilia mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha, wakahiari wakae ndani ya maji, inadhihirisha wazi wazi jinsi watu hao walivyojizatiti kumwunga mkono Profesa Lipumba. Kuna kila sababu za kuamini kuwa watu hao hawafanyi mzaha. Wamepania, watajiandikisha na watampigia kura. Jee! Mheshimiwa Mrema anayeng'ang'ana kuwa yeye ndiye kipenzi cha Watanzania ameliona hilo? 'Mwenye macho haambiwi tazama'.Hivyo yeye mwenyewe haoni mahudhuriao ya watu wanaohudhuria mikutano yake ya hadhara na wale wanaohudhuria mikutano ya Profesa Lipumba? Asisahau Waswahili walivyosema. "Mla,mla leo, mla jana, kalani?" Basi bidhaa ya mwaka '47 haina soko leo! Ama ile kauli ya Mhe.Mrema kuwa viongozi wa vyama vya CHADEMA, CUF na UDP walikuwa wana mpango wa kutaka kumtapeli chini ya ule mpango wa umoja wa vyama vya upinzani, ni danganya toto! Ameuliza kama kweli viongozi hao wanataka umoja mbona Profesa Lipumba amekwisha chukua fomu ya kugombania Urais na mbona Mheshimiwa Cheyo naye, hivi karibuni, ameliaga Bunge kuwa anakwenda kugombea Urais? Swali linalohitaji Mheshimiwa Mrema ajiulize ni kuwa jee,hao waliochukua fomu hizo ndiyo wamekwisha kuwa wagombea rasmi? Pili, fomu hizo walizozichukua ni za Tume ya Taifa ya Uchaguzi au za nyama vyao? Inaonekana wale wanaompinga Mheshimiwa Mrema asigombee nafasi ya uongozi wa juu wa nchi hii ni kutokana labda na uwezo wake mdogo wa kuchambua mambo. Kina Lipumba na Makani na wengineo wamechukua fomu, siyo kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi bali kutoka katika vyama vyao, ili wapate ridhaa ya vyama vyao. Na yeye Mhe.Mrema ana haki ya kufanya hivyo, na kwa hakika, na yeye amekwisha chukua fomu kama hiyo,kutoka katika chama chake.Lakini kitendo hicho hakiwazuii wagombea hao pamoja na yeye Mhe. Mrema,kukutana pamoja na kuteua mgombea mmoja tu miongoni mwao. Sasa hiyo kauli ya kutaka kutapeliwa inatokea wapi? Mbali ya kupendwa na watu, nafasi ya Urais inahitaji na uwezo. Kama Mhehimiwa Mrema ana nia ya kuwatumikia Watanzania anaweza kufanya hivyo kwa kushirikiana na wapinzani wengine.Aidha awe tayari kuwatumikia katika nafasi yo yote atakayopewa si lazima awe Rais. Kwa nini hataki akakutana ana kwa ana, na viongozi wenziwe akaona watamteua yeye au hawamteui? Ana wasiwasi wa nini? Kuna kisa kimoja.Mtu mmoja alikuwa akiwaambia Waislamu wenzake kuwa yeye hujisikia vizuri anapo uhudumia msikiti. Lakini, kila wenziwe wakimfuata ili asaidie katika huduma za msikiti,yeye hutoa udhuru huu na ule. Kumbe yeye nia yake hasa si kuhudumia msikiti bali ni kutaka kuadhini. Ingawa ana sauti kali,lakini hajui kuadhini vizuri. Wenziwe wakamshitukia. Basi siku moja mzee mmoja aliamua kumwondolea uvivu akamwambia kuuhudumia msikiti si lazima kuadhini au kusalisha; hata kufagia msikiti nako ni kuuhudumia msikiti. Na kweli wakati wa Mtume (s.a.w.) mwanamke mmoja aliyekuwa akifagia msikiti alifariki. Masahaba hawakuona umuhimu wa kumpa habari Mtume (s.a.w.). Wakamzika kimya kimya. Kwa vile alikuwa hasalishi, haadhini anafagia tu, wakadhani alikuwa ni mtu mdogo tu.Lakini Mtume (s.a.w.) alipopata habari ya kifo chake alisikitika sana, akawalaumu masahaba wake kwa kutompasha habari. Akaomba aonyeshwa kaburi lake, na akaenda mwenyewe kumwombea dua huko huko kaburini. Basi inafaa na Mhe.Mrema ajue kuwatumikia wananchi si lazima awe Rais tu! |
YALIYOMO
Tahariri
Kishindo cha CUF chaitikisa Dar Mamia warudisha kadi za CCM Kilwa Chama cha Mugabe chupuchupu Zimbabwe Wasikilizeni wananchi wasemavyo toka kwenye meli mbovu mkabala na Posta ya zamani CCM yakasirishwa kwa kuswaliwa Mtume (S.A.W.) Wanaomzomea Bilal waambiwa Oktoba watakula jeuri yao CCM wapoteza viti 18196; CUF yaongoza kuvinyakua Ushauri Nasaha
MAKALA
MIPASHO NASAHA
MAKALA
KALAMU YA MUANDISHI
MAKALA
Lishe
RIWAYA
Pupe, Mziray wamlia ‘dip’ Shungu - |
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza
hapa
Au
Andika barua kwa: nasaha1420@yahoo.com
|
|
|
|