NASAHA
Na. 054 Jumatano Juni 28 - Julai 4, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Habari 

Wasikilizeni wananchi wasemavyo toka kwenye meli mbovu mkabala na Posta ya zamani 

  • 'Rais wetu aangalie wananchi wake wanavyoishi' 
KATIKA majahazi na meli mbovu zilizotelekezwa ufukweni mkabala na posta ya zamani, kuna wananchi kibao wanaoishi humo. Yumo Mama Ntilie na mwanae mchanga, wamo watoto wa mitaani, wamo vijana wenye nguvu kazi kati yao kijana Jumanne (Fundi Ujezi) na Toronto Canada (Mpaa samaki). 

Vijana hao walijitokeza katika TV Juni 23, 2000 na kufanya mahojiano na mtangazaji wa kipindi cha Jiji letu.Wakijibu mshangao wa wananchi kuishi humo, vijana hao walieleza kwamba ni vyema"rais wetu aangalie wananchi wake wanavyoishi." 

2. Toka soko la makumbusho Kinondoni "wataka wenzao wavunjiwe vibanda"

Waliopangishwa katika soko hilo jipya hawapati wateja. Hivyo wameshauri kuwa magenge kadhaa toka Mwananyamala hadi eneo jirani na soko hilo na ikiwezekana hata soko la Tandale yavunjwe ili wateja wapate kwenda kwenye soko hilo la makumbusho. Baadhi yao walionekana kusema haya kwenye TVJuni 23, 2000. 

Lakini wenzao nao wauza magenge waliopakaziwa kuvunjiwa walijibu mapigo wakati wakiongea na NASAHA. Walidai kwamba kwanza mbao za soko la makumbusho zilitolewa kwa upendeleo wa udini na ukabila. Pili, wao pia ni wananchi wanaostaili ya kujiajiri. Tatu wamesema kwamba kama hivyo ndivyo,serikali ya jiji pia ivunje kwanza vioski vyote vilivyoenea mji mzima ili wateja waende kwenye maduka rasmi yaliyopo jijini. 

3.Toka kijini Lulonzi picha ya ndege Kibaha

Kipindi kingine cha TV kiitwacho kulikoni? Kiliwatembelea wanakijiji wazee kwa umri na walio taabani kiafya kwa umaskini na njaa kutokana na kuishi maisha yasiyo na uhakika. 

Kijiji cha Lulonzi kipo eneo la ndani upande wa Picha ya Ndege, yaani mbali na barabara ya Morogoro! Shughuli kuu katika kijiji hicho ni kilimo. Mashamba yao ni madogo. Kilimo chao ni cha chakula kwa jembe dogo la mkono. 

Kwa mujibu wa mjumbe wa nyumba wa shina Bw.Yohani Joseph eneo lao halina maendeleo yoyote. "Bibi Shamba huwa anapita "alisema mjumbe huyo. Alieleza pia kwamba baadhi ya wanakijiji wanajaribu kutafuta mbolea na dawa kwa kilimo huishia kwenye usumbufu wa madeni ya vifaa hivyo kuliko mapato. 

Miongoni mwa wanakijiji wengine waliohojiwa ni wazee watatu. Mmoja kati yao alikuwa na mumewe mwenye umri wa miaka 80. Mwingine alikuwa bado katika majonzi ya kufiwa na mkewe aliyemzika kwa sanda ya mkopo ambao hajui namna atakavyoilipa. 

Wazee hao walitoa historia zao za maisha hadi kufikia walipokutwa. 

Yule mama na mumewe walieleza kuwa wao ni miongoni mwa waathirika wa kampeni za kuwahamisha wananchi wa mikoa ya Pwani toka kwenye vijiji vyao vya asili kwenda kwenye vijiji vya Ujamaa. 

Kwa mujibu wa historia ya kampeni ile propaganda za chama na serikali zilidai kuwapeleka wananchi kwenye vijiji vya ujamaa ili wapate kuishi na kufanyakazi kwa pamoja kurahisisha serikali kuwapelekea huduma muhimu za maji,shule, hospitali na umeme. Aidha propaganda hizo ziliwaahidi wananchi msaada wa kujengewa nyumba bora, msaada wa kitaalamu katika kilimo, kuwajengea barabara za kusafirisha mazao yao na kuwapatia soko zuri. 

Kinyume chake yote hayo hayakupatikana. Wananchi walivunjiwa nyumba zao, wengine wakachomewa mashamba yao na huko walikopelekwa hakuna walichopewa kama walivyoahidiwa. 

Hivyo mama yule na mumewe walieleza kuwa zahma hiyo ya kampeni za vijiji iliwakuta Rufiji na kutokana na matatizo yale ikabidi wahamie hapo Lulonzi mnamo mwaka 1968. 

Mwandishi aliwakuta wakipepeta vuna lao la mpunga ambalo halikujaa kikapo, kutokana na kishamba chao kuwa kidogo na hali ya matatizo ya mvua za mwaka huu. 

Vizee hivyo vilieleza kuwa vyenyewe vimeishajizoelea hali hiyo ya matatizo na kwamba huishia kubangaiza kwa kufanya kibarua cha kuwalimia wakubwa wenye mashamba mazuri. 

Mama huyo ambaye alionekana mkakamavu wa kujiamini na mweredi wa kujibu maswali kwa mantiki, alimjibu mtangazaji aliyetaka kujua kiwango chake cha elimu kwa kusema kuwa elimu ya kilimo kaipata toka kwa wazazi wake tangu akiwa mdogo na kwamba alikuwa na elimu ya kutosha kumuwezesha kuujua ubinadamu wake na imani yake. "Nimesoma; naijua sala yangu na ninaujua udhu wangu....." alisema namna huyo,nakuibua hisia za mama mmoja aliyekuwa akisikiliza mahojiano hayo ambaye alimuitikia kwa kusema "sawa kabisa, hao waliopeana visomo na madaraka wako wapi, wakati wananchi wanateseka na kushindwa kuwasaidia wazee wao." 

Bi kizee mwingine wa Lulanzi alisema kuwa pia na yeye watoto wake ni wenye maisha ya kubangaiza. Alisema kuwa watoto hao hawakuweza kusoma kwa kukosa ada, fedha za uniform na vifaa vinginevyo. Akimjibu mwandishi aliyetaka kujua endapo alijaribu kuomba msaada wa serikali kwa kusema: "Ah...msaada gani.... Hata mume wangu nilijaribu kumuambia ajitokeze,lakini ah wapi," alisema mama huyo akionesha kutokuwepo kwa msaada wowote kwa watu kama wao. 

Kuhusu kuwategemea watoto wake mama huyo alisema kuwa haoni haki ya kumtegemea mwanadamu mwenzie. "Yeye kaumbwa na ana roho kama mimi ni vipi ni mtegemee...", alisema mama huyo mzaliwa wa Bunju na aliyeishi Dares Salaam kabla ya kuhamia Lulanzi baada ya kufiwa na mumewe. 

Mzee aliyehuzunisha ni Mzee Mohamed Ali Mwalimu ambaye alisema kuwa yeye hakuweza kulima chochote kwa kuwa kwa muda wote alikuwa akimuuguza mkewe aliyefariki tarehe 23 na kuzikwa tarehe 25 Mei, 2000. Mzee huyo alinung'unika kwa huzuni kwamba kutokana na umasikini alio nao, hakuweza hata kumudu fedha za kununulia sanda na akalazimika kukopeshwa shs.10,600 kwa ajili ya sanda kiasi cha deni ambacho hajui atakipata wapi ili awalipe wanaomdai ambao alisema kuwa humkumbusha mara kwa mara. Mzee huyo anaishi katika kijibanda kibovu sawa na kidunda cha kuamia ndege alisema",naishi humo, sijui kitaniangukia lini", alisema mzee huyo huku akionesha kibanda chake kibovu ambacho kimechoka na kuonekana kinaelekea kulala upande. 

Pengine kauli za wazee hao wenye kuishi maisha ya taabani huko kijijini inaweza kujumuishwa na kauli ya mjumbe wao Bw. Yohani Joseph ambaye alisema:"Nyie wakubwa mnaopita huko (barabara ya Morogoro) mjue sisi huku hatuna maendeleo;hatuna usawa." 


CCM yakasirishwa kwa kuswaliwa Mtume (S.A.W.)

Na Mwandishi Wetu 

KATIKA hafla ya kuzindua shina moja la wakereketwawa CCM Mtoni, Temeke kiongozi wa serikali ya CCM, Bwa. Luteni Yusuf Makamba alitoa hutuba na kusimulia kisa kinacho muhusu Mtume Mohammad (s.a.w.). Kisa hicho kinahusu mtu aliyekuwa akiweka kinyesi mbele ya nyumba ya Mtume Mohammad wakati akipita njiani.

Wakati akisimulia kisa hicho, Bwa.Makamba kila alipomtaja Mtume Waislam waliokuwa katika tawi la CUF, mkabala na pale alipokuwa anahutubia, waliitikia kwa kusema, "swallah Llah Alay Wassalam." 

Imedaiwa kwamba kiitikio hicho kilielekea kumuudhi Bw. Makamba. 

Habari zilizopatikana kutoka kwa Waislam waliokuwepo katika tukio hilo zimedai kwamba polisi waliamrishwa kuwakamata Waislam waliokuwa wakitia kila utajo wa Mtume. 

Hata hivyo, imeelezwa kwamba polisi hao walielimishwa na kuelewa kwamba ni amri ya Mwenyezi Mungu kwa wanadamu na malaika kumswalia Mtume (S.A.W.). 

Hivyo, kila anapotajwa Mtume (s.a.w.) Waislam huifikia kwa kumswalia kwa maneno yaliyotajwa hap juu. 

Hatua hiyo ya kutishia kuwakamata Waislam kwa "kosa" hilo tena wakati huu wa mfungo sita, mwezi wa kuzaliwa Mtume, kimewasikitisha Waislam wengi pamoja na wale walioko katika chama hicho cha mapinduzi 

"Ama hakika chama hiki (CCM) hakitupendi Waislam, na kinaichukia dini yetu", alisema mzee mmoja wa makamo anaeishi eneo hilo maarufu la Mtoni Sokoni. 
Juu


Wanaomzomea Bilal waambiwa Oktoba watakula jeuri yao 

Na Mwandishi Wetu Zanzibar 

KUNA msuguano wa maneno ya chini kwa chini miongoni mwa baadhi ya wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar ambao waliwadhamini na kuwashabikia waliochukuwa fomu za chama hicho kugombea kiti cha Urais Zanzibar,katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Msuguano huo umejitokeza kati ya wale waliomuunga mkono Dr. Gharib Bilal na wale ambao hawakupenda kumuona anagombea. Ingawa Dk. Bilal aliongoza kura za maoni katika uteuzi wa awali uliofanyika Zanzibar akaanguka katika kura za uteuzi wa mwisho uliofanyika katika mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika baadaye huko Dodoma, ambapo Bw. Amani Karume alichaguliwa. 

Ingawa msuguano huo wa maneno haujajitokeza wazi wala kutamkwa kwa sauti kubwa hadharani, unaelekea kupamba moto katika mitaa mingi ya Unguja kati ya wale waliomuunga mkono Dk. Bilal na wale ambao hawakumtaka. 

Kundi lisilompenda Dk.Bilal ndilo linaloelezwa kuwa ndio chanzo cha msuguano huo ambao tayari umezaa malumbano ya chini kwa chini miongoni mwa pande hizo mbili za wafuasi wa chama hicho. Kundi hilo linadaiwa kuwa linasambaza maneno ya vijembe na mipasho dhidi ya kundi la Dk.Bilal kwamba eti kundi hilo (la Dk. Bilal)mara baada ya kuona mgombea wao kaongoza katika kura za maoni Zanzibar, liliandaa sare za kanga, vitenge, fulana na kofia zenye picha ya Dk. Bilal kwa ajili ya sherehe ya mapokezi ya mgombea wao atakapokuwa anarudi toka Dodoma, kwa imani kwamba mapendekezo ya Zanzibar yangeliheshimiwa. 

Kundi la Dk. Bilal linakanusha kuwa lilifanya maandalizi ya aina hiyo na linawashutumu wanachama wenzao hao kwamba wanaeneza uzushi wa kutaka kumdhalilisha aliye kuwa mgombea wao. 

Katika kujibu mapigo, kundi la Dk. Bilal nalo linadai kwamba Wazanzibari hao wanao "mzomea" Dk.Bilal kwa kushindwa na Karume wanatumiwa na watu wasiojali maslahi ya Zanzibar, na kwamba huenda watu hao pia si Wazanzibari. 

Wafuasi hao wa CCM waliomuunga mkono Dk.Bilal wanaeleza kwamba hao wenzao wanaoendesha propaganda za chuki dhidi ya aliyekuwa mgombea wao wanamponza Bw. Karume kwa kumfanya aonekane hakuteuliwa kugombea kwa maslahi ya watu wa Zanzibar bali kwa maslahi ya wale waliompa kura nyingi za maoni dhidi ya Dk.Bilal. 

Wazanzibari hao waliounga mkono uteuzi wa Dk.Bilal wanasema kwamba wao walitegemea baada ya uteuzi wa mwisho kufanyika huko Dodoma wangelisahau tofauti zao, hivyo wamesema kuwa madhali wenzao wameamua kuendeleza "ligi" hiyo iliyoanza kuchezwa Zanzibar, basi na wao wataimalizia katika mchezo wa fainali Oktoba mwaka huu, kwa kumteua Mzanzibari yeyote isipokuwa yule wanaemtumia kama kigezo cha kumzomea Dk. Bilal na kueneza uzushi usio na maana, dhidi ya kundi lao. 

Mmoja wa watu wanaodaiwa kuwa upande wa kundi la Dk.Bilal akitoa maoni yake kuhusu sakata hiyo kwa masharti ya kutotajwa jina lake, aliwashutumu watu wa kundi linalomchukia Dk. Bilal kuwa ni vibaraka wenye mawazo ya kutumiwa na watu wengine wakiwemo wale ambao walijitokeza kumuandama Dk.Salmin Amour pale baadhi ya wananchi wa Zanzibar walipotaka kupendekeza marekebisho ya katiba ili kuondoa mkomo wa vipindi vya uongozi wa nafasi ya rais Zanzibar. 

Bwana huyo wa makamo kiasi ambae alisema kuwa yeye aliwahi kushika uongozi wa siasa ngazi ya matawi kwa muda mrefu mjini Unguja alidai kuwa chuki dhidi ya kundi lao na Dk. Bilal zinatokana na "mzee" mmoja mwenye cheo cha juu katika serikali ya Muungano kushindwa kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo ya Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM baada ya kugundua kuwa asingepata kura za kutosha za maoni kutokana na kinachoelezwa kuwa ana mtazamo wa kutumikia maslahi yake binafsi na ya wale wanaotaka kuifanya Zanzibar mkoa katika mfumo wa Muungano wa Tanzania. 

"Hawa jamaa baada ya kuona mzee wao kakwama kuchukua fomu wakaanza kampeni zao za kumuangusha Dk. Bilal katika mkutano wa Dodoma", alisema bwana huyo na kuongeza kwa kudai kuwa huko Dodoma walifanikiwa kutokana na "sapoti" ya mzee huyo:, pasipo kufafanua sapoti hiyo ilifanyika vipi. 

Bwana mwingine ambae alikiri kuwepo upande wa kundi linalo wazomea waliomuunga mkono Dk. Bilal alitetea msimamo wao kwa kudai kuwa hawakupendelea upande wa Bilal kwa kuwa eti kujitokeza kwake kulidhoofisha kambi ya Mzee kwa sababu mzee alitaka Dk. Bilal awe "mpiga debe" wake. Bwana huyu alikiri pia kwamba mzee wao hakubaliki na wengi Zanzibar kwahiyo alitegemea nguvu za Ikulu ya Zanzibar kumpigia debe la kampeni ya kukubalika kwa viongozi na wananchi wengi wa visiwa hivyo. 

Mama mmoja mkazi wa Kwamtipura ambaye nae pia hakutaka jina lake litajwe kwa madai kuwa malumbano haya yalikuwa "nyeti" alililaumu kundi lililokuwa likimuunga mkono mzee kwa kuendeleza chuki zao dhidi ya kundi la Dk. Bilal badala ya kujishughulisha na kampeni za mgombea wa CCM aliyepitishwa Dodoma, ambazo alisema mama huyo, kuwa zinaelekea kupwaya kwa kulinganisha na za mgombea wa Chama cha Wananchi -CUF. 

Mama mwingine ambaye alielekea kuwemo upande uliomuunga mkono Dk.Bilal alionya kuwa madhali lile kundi la mzee linadhani kwamba limeshinda kwa kumuangusha Dk.Bilal, litajuta ifikapo siku ya uchaguzi Oktoba mwaka huu. 

"Siku hiyo watakula jeuri yao. Wasifikiri kuwa sisi ni wajinga wa kumchagua pandikizi wa mzee anaetaka kuifanya Zanzibar mkoa badala ya nchi iliyoingia mkataba na Tanganyika kuunda Tanzania", alisema mama huyo na kuongeza kuwa watafanya kampeni za nyumba kwa nyumba kuhakikisha kuwa anachaguliwa "Mzanzibari mwenye uchungu na Visiwa hivyo pasipo kujali chama atakacho." 
Juu


CCM wapoteza viti 18196 
CUF yaongoza kuvinyakua 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepoteza viti 18196 wakati wa uchaguzi wa viongozi wa serikali za vijiji,vitongoji na mitaa uliofanyika mwaka jana. Waziri wa Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa, Kingunge Ngombale-Mwiru amesema wakati akiwakilisha hotuba ya makadirio ya Wizara yake kwa mwaka 2000/2001 Bungeni Dodoma wiki iliyopita.

Mheshimiwa Ngombale alisema kuwa katika uchaguzi huo CCM iliongoza kwa kupata asilimia kubwa zaidi ikifuatiwa na Chama cha CUF na nafasi ya tatu ilishikwa na TLP.Vyama vingine vilivyoshiriki uchaguzi huo na kupata viti ni UDP,NCCR-Mageuzi, CHADEMA, UMD, TADEA,PONA, NLO,NRA na UPDP.Chama kinachoongozwa na Dk.Alex Chemponda kilishiriki lakini hakikuambulia hata kiti kimoja. 

Hata hivyo pamoja na CCM kuongoza katika chaguzi hizo kumekuwa ni malalamiko toka kwa viongozi wa vyama vya upinzani kuwa CCM imekuwa ikitoa shinikizo kwa waamuzi wa uchaguzi ili kufuta matokeo sehemu ambazo vyama vya upinzani vilipata ushindi. Viongozi hao wa upinzani walitoa mfano wa kufutwa kwa matokeo ya viti ambavyo CUF ilipata ushindi katika wilaya za Kinondoni na Temeke jijini Dar es Salaam na Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani. 
Juu


Tambwe huyoo anakuja! 

Na Mwandishi Wetu 

MGOMBEA wa ubunge katika jimbo la uchaguzi la Temeke Mhe. Richard Tambwa Hiza anaongoza katika kura za maoni jimboni humo.

Katika mkutano maalum wa jimbo uliofanyika katika ukumbi wa Super Stereo uliopo Temeke Mikoshoroshini Juni 24 Mhe. Tambwa alipata kura 222 kati ya 336 zilizopigwa Bi Zainab kura 44. 

Kwa matokeo hayo Mhe. Tambwe Hiza na Haji Maulid Haji majina yao yatapitishwa na kikao cha mkutano mkuu wailaya na kwenda kuchujwa kwenye kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama chake cha CUF, kinachotarajiwa kukaa kati ya tarehe 7 na 30 mwezi wa Julai. 

Kwa kuwaacha mbali wagmbea wenzake kwa tofuati kubwa ya kura hizo za maoni kunamfanya Mhe. Tambwe kuwa mgombea ubunge mtarajiwa katika jimbo hilo la Temeke kwa tikiti ya CUF. 

Bw.Richard Tambwe Hiza ambaye ni Mwenyekiti wa wilaya ya Temeke wa chama hicho amejizolea umaarufu mkubwa katika medani ya kisiasa kutokana na jitahada zake alizozifanya kukijenga chama hicho wilayani humo na maeneo mengine hapa nchini. 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mhe. Tambwe alisema sasa anaelekeza nguvu zake katika uchaguzi mkuu wa Oktoba na akawataka wananchi katika jimbo hilo lililo nyuma kimaendeleo kuupigia kura upinzani na kuwa ngangari katika kuzilinda kura hizo. 

Alisema kuwa uzoefu unaonesha kuwa wananchi huchagua upinzani, lakini chama tawala kwa kushirikiana na tume ya uchaguzi ambayo alidai sio huru huiba kura hizo na kuipa CCM ushindi. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Serikali isikilize kilio cha wapinzani na Waislamu

Kishindo cha CUF chaitikisa Dar

Mamia  warudisha kadi za CCM Kilwa

Chama cha Mugabe chupuchupu Zimbabwe

Wasikilizeni wananchi wasemavyo toka kwenye meli mbovu mkabala na Posta ya zamani

CCM yakasirishwa kwa kuswaliwa Mtume (S.A.W.)

Wanaomzomea Bilal waambiwa Oktoba watakula jeuri yao

CCM wapoteza viti 18196; CUF yaongoza kuvinyakua

Tambwe huyoo anakuja!

Ushauri Nasaha
Unapomdharau mama yako mbele ya rafiki yako...

MAKALA
Uchaguzi wa Zimbabwe: Vita kati ya mabeberu na wapinga Ukoloni mamboleo

MIPASHO NASAHA
Matonya wahi, pesa zinatoka sasa!

MAKALA
Vijembe kwa viongozi wa vyama vya upinzani, huduma kwa wananchi ziro

KALAMU YA MUANDISHI
Ukongwe hausaidii kubaki madarakani

MAKALA
Kuchanganya siasa na ushirikina

Habari za Kimataifa

Lishe
Faida za vyakula vya nyuzi nyuzi

RIWAYA
Dunia ndivyo ilivyo - 4

Barua

MASHAIRI

TANGAZO

MICHEZO

  • Mpambano wa watani wa jadi: U-CCM umeiponza Yanga wasema Simba
  • Wanamichezo wamshtukia Mkapa
  • Mabosi DRFA kujulikana leo

  • Pupe, Mziray wamlia ‘dip’ Shungu
    -



     
     

       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita