NASAHA
Na. 054 Jumatano Juni 28 - Julai 4, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA 

Uchaguzi wa Zimbabwe: Vita kati ya mabeberu na wapinga Ukoloni mamboleo

  • Pia ni fursa kwa wananchi kuelewa nguvu ya mbinu za propadanda za vyombo vya habari 


UCHAGUZI wa Zimbabwe uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kuchagua wagombea viti vya ubunge ni uchaguzi pekee katika eneo hili la Afrika unaofuatiliwa kwa nguvu na karibu zaidi na nchi za mataifa makubwa ya magharibi pamoja na vyombo vyao vya habari, redio, televisheni na magazeti. Iliyo mstari wa mbele mwa nchi hizo ni Uingereza na vyombo vyake vya habari vikiwemo vya BBC ambavyo vimekuwa vikimchambua Rais Mugabe wa Zimabwe na serikali yake kwa mtazamo wa kumuonesha kama ni mtu aliyeshindwa kuongoza nchi kwa kuitumbukiza nchi katika dimbwi na umasikini na rushwa. Mwandishi H. Mashaka anaelezea zaidi.
 

PROPAGANDA hizo za vyombo vya habari dhidi ya rais Mugabe ni sehemu ya mapambano ya kisiasa kati ya rais huyo na serikali ya Uingereza yaliyozuka na kupamba moto tangu Rais Mugabe alipotangaza azma ya serikali yake kuchukua mashamba makubwa yanayomilikiwa na walowezi wa Kizungu wenye asili ya Uingereza. 

Mgogoro huo wa kutaka kutaifisha mashamba hayo ya Wazungu umeambatana na historia ya nchi hiyo tangu ilipovamiwa na wakoloni wa Kiingereza, miaka mia moja na zaidi iliyopita, pamoja na historia ya mapambano ya silaha waliyolazimika kuyafanya wazalendo wa Zimbabwe katika ukombozi wa nchi yao hadi walipofanikiwa kujitawala mwaka 1980. 

Ili kuielewa vyema hali ya mgogoro huu wa sasa kati ya Mugabe na Uingereza inayoshabikiwa na mataifa mengine ya magharibi, hatuna budi kuitazama japo kwa ufupi historia ya sehemu kubwa ya ardhi ya Zimbabwe kugeuzwa mashamba ya walowezi. 

Zimbabwe, kama ilivyokuwa Afrika Kusini, ilikaliwa na Wazungu wengi ambao walimiliki ardhi yote yenye rutuba na njia kuu za uchumi wa nchi hiyo. 

Pamoja na mfumo wa kibaguzi uliokuwa ukiendeshwa na serikali ya Ukoloni wa Kiingereza iliyokuwa ikiitawala Zimbabwe, Waafrika wazalendo wa nchi hiyo hawakumiliki ardhi na wale waliokuwa wakiishi katika maenejo ya vijiji vya asili walijikuta wakiishi katika ardhi iliyokuwa imegawiwa na serikali hiyo ya Kikoloni na kumilikishwa kwa mlowezi wa Kizungu. Hivyo wenyeji hao wa Kiafrika waliokuwa katika ardhi hizo walijikuta wakihesabiwa kama wavamizi wanaostahili kufukuzwa au wapangaji wa muda wanaoruhusiwa kuishi humo kwa malipo ya kuchunga ng'ombe zilizokuwa zikimilikiwa na walowezi hao, au kufanya kazi nyinginezo kwa kuajiriwa na walowezi hao. 

Wenyeji wengi walijikuta katika mazingira hayo kwasababu ardhi walizogawana walowezi hao ni katika maelfu ya eka ya ardhi ya nchi nzima ukiondoa maeneo ya mapori ya hifadhi za wanyama, mito na mashamba machache ya serikali kwa ajili ya taasisi za utafiti wa kilimo na mifugo. 

Kutokana na ukubwa wa maeneo waliyogawana walowezi hao, hawakuweza kuyalima yote na hivyo mengine kubaki kama pori au vijiji vilivyokaliwa na wazalendo hao waliojikuta wapangaji katika ardhi zao za asili. 

Hivyo moja ya azma kubwa ya wazalendo wa Zimbabwe katika kuikomboa nchi yao ilikuwa siyo kujitawala tu kwa uhuru wa bendera bali pia kurudisha mikononi mwao milki ya ardhi yao ya asili. 

Kwa kulijua hilo, Wazungu walowezi wa Zimbabwe walipinga serikali yaUingereza kutoa uhuru wa nchi hiyo kwa Waafrika jambo ambalo liliwafanya wazalendo waamue kuingia msituni kuanzisha vita vya silaha dhidi ya walowezi na ukoloni wa Kiingereza. 

Nguvu za wazalendo zilipoelekea kuwapa ushindi Waafrika, walowezi walijitangazia uhuru wa nchi hiyo iliyokuwa ikiitwa Rhodesia mwaka 1965 chini ya uongozi wa Mlowezi Ian Smith. 

Hatua hiyo ya walowezi haikuwasaidia kitu, ingawa Uingereza ilionesha kigugumizi cha wazi kwa kutodhibiti mtawala ule uliotajwa kuwa ni wa uasi wa Wazungu walowezi ambao hawakutaka Waafrika wa nchi hiyo wajitawale. 

Walowezi walitumia utawala wao kukandamiza zaidi, kutesa na hata kuua Waafrika walijitokeza kuunga mkono harakati za ukombozi wa nchi yao. 

Na walowezi hao walipoanza kuzidiwa nguvu na wapigania uhuru wazalendo, Uingereza na baadhi ya mataifa ya magharibi yalijitokeza kwa kiini macho 'kuwalazimisha" walowezi kukubali kushirikiana na Waafrika katika utawala wao. Kwa mbinu hiyo ya kiini macho, walowezi walipanga taratibu za kuweka viongozi wa Kiafrika vibaraka ambao wangelilinda maslahi ya walowezi. Mmoja wa viongozi hao vibaraka alikuwa Askofu Abel Muzorewa aliyewekwa na walowezi kuchukua nafasi ya Waziri Mkuu. 

Hata hivyo, mbinu hiyo ya walowezi na Ukoloni wa Kiingereza ilipingwa na vyama vikuu vya wapiganaji wazalendo chini ya uongozi wa Bw. Robert Mugabe (ZANU) na Bw. Joshua Nkomo (ZAPU) ambao walizidisha mapambano ya silaha hadi Uingereza na washirika wake wa nchi za magharibi walipoingilia mapambano kunusuru walowezi wasing'olewe kwa mtutu wa bunduki kama ilivyotokea katika makoloni ya Ureno ambako mwaka 1975 Ureno ililazimika kuziachia ghafla Angola, Msumbuji, Guinea Bisau na Cape Verde hatua ambayo iliwakosesha mali walowezi wake. 

Hivyo, mwaka 1980 Uingereza ilikubali kutoa uhuru wa Zimbabwe kwa kuzungumza na uongozi wa vyama vya wazalendo vya ZANU na ZAPU. 

Katika mazungumzo hayo ambayo yalifanyika katika jengo la Lancaster, jengo maarufu kwa majadiliano ya kutoa uhuru wa makoloni ya Uingereza, iliundwa katiba ya Zimbabwe ambayo ilikuwa na kifungu kilichosema kuwa katiba isibadilishwe chochote mpaka baada ya miaka 10. 

Katiba hiyo pia ilitetea maslahi ya walowezi waliokuwa na mashamba makubwa yaliyotokana na kuporwa kwa ardhi kubwa ya Waafrika wa Zimbabwe. 

Baada ya kutimia miaka 10, yaani mnamo mwanzoni mwa miaka ya 1990, rais Mugabe alitangaza azma yake ya kubadili katiba ya nchi hiyo na kutwaa ardhi iliyokuwa imehodhiwa na walowezi ili kuigawa kwa Waafrika ambao takriban wote hawakuwa na ardhi yoyote. 

Azma hiyo ya rais Mugabe ilipingwa na walowezi kwa madai kuwa walikuwa na hati za kumiliki ardhi hiyo waliyopewa tangu enzi za ukoloni wa Muingereza. 

Mabishano kati ya Mugabe na walowezi kuhusu ardhi yaliyohusisha Uingereza yalipelekea Mugabe kuwataka Waingereza kuwafidia walowezi mashamba ambayo yeye hakuwa na budi ya kuwagawia Waafrika ambao waliyapigania. 

Uingereza badala ya kusema ndiyo au hapana, ilitumia mbinu ya kuzungusha suala hilo wakati wakati walowezi wakipanga mbinu za kuundoa uongozi wa rais Mugabe na chama chake madarakani katika uchauzi utakaofuata kwa kuwapa ufadhili wapinzani ambao wangelikuwa tayari kulinda maslahi ya walowezi. 

Hali hiyo ilijitokeza mapema mwaka huu pale rais Mugabe alipoitisha kura ya maoni ya kutaifisha mashamba ya walowezi kwa madhumuni ya kuwagawia ardhi wananchi wasiokuwa na mashamba. 

Walowezi walilivalia njuga zoezi hilo kwa hali na mali ambapo pia baadhi ya nchi za magharibi na vyombo vyao vya habari zilijitokeza kwa nguvu kuendesha propaganda dhidi ya rais Mugabe na serikali yake. 

Moja ya propaganda hizo ni lawama kwa rais Mugabe kuwanyima uhuru na haki za mashoga ambao nchi nyingi za Ulaya zimewapa uhuru wa kuoana wanaume kwa wanaume na wanawake kwa wanawake. 

Zimbabwe ilimhukumu kifungo Padri Banana aliyewahi kuwa rais wa nchi hiyo kwa kosa la kumlawiti mlinzi wake. 

Lakini kikubwa kilichojitokeza dhidi ya rais Mugabe ni msimamo wake kwa kujitokeza mapema kumuunga mkono rais Kabila wa Congo RDC kwa kumpelekea majeshi ya kuzuia Rwanda na Uganda kumuondoa Kabila madarakani na kuweka serikali chini ya uongozi wa waasi wanaokubalika na nchi hizo. 

Inasemekana kwamba ingawa jumuiya za Kimataifa na vyombo vikuu vya kimataifa kama UNO vinapinga vitendo vya nchi kuvamia nchi nyingine na kuiangusha serikali iliyopo madarakani, vitendo vya Rwanda na Uganda vinafumbiwa macho na mataifa makubwa ya magharibi ambayo yana sauti kubwa katika vyombo vya Kimataifa kwa kuwa nchi hizo zinakubalika vizuri na mataifa hayo yenye sifa na historia ubepari wa kibeberu wa kujinufaisha kwa maliasilia za nchi changa, yakiwemo madini na mazao wanayochukua kwa kujipangia soko na bei wazitakazo. 

Aidha, mataifa hayo ya kimagharibi yameelezwa kuwa ili kufanikisha azma zao hupendelea kuziunga mkono serikali zinazokubali masharti yao na kulinda maslahi yao mfumo ambao ni maarufu kwa jina la ukoloni mamboleo. 

Jambo la kuhuzunisha ni kwamba wanaokubali nchi zao kuwa chini ya ukoloni mambeleo huwa hawaandamwi kwa propaganda za kuwakosoa au kuwaponda hata kam aserikali zao zimejaa matatizo. 

Na kwa mtazamo huo huo, wale ambao wataonekana kupinga mtazamo huo, wataandamwa kwa propaganda za mashinikizo ya kushindwa kuongoza nchi zao, na kutuhumiwa kutokuwa na utawala wa kidemokrasia na kushindwa kuzuia kuenea kwa rushwa. 

Kwa kutumia mtazamo huo, vyombo vya habari ambavyo vinatumikia maslahi ya nchi za magharibi vipo katika nafasi kubwa ya kupotosha hisia za wananchi katika kuchukua maamuzi muhimu yakiwemo yale ya kuchagua viongozi na vyama vinavyofaa kutetea na kuendeleza maslahi ya wananchi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kwanza vyombo hivyo vina uwezo mkubwa wa hali na mali katika kufanikisha uenezi wa habari zake kwa muda wa saa 24 na kuwafikia wananchi popote walipo. 

Pili, katika muda huo wa saa 24 vina uwezo wa kurudia habari zao za propaganda kila baada ya robo saa, kiasi cha kuzifanya habari hizo ziwe za kawaida zinazojulikana na wengi na hivyo kuchukua sura ya ukweli. 

Tatu, kwa mtindo huo wa propaganda za kurudiwa-rudiwa, vyombo vingine vya habari pamoja na udhaifu wak ewa kihali na mali ambavyo vinaweza vikawa na habari za ukweli kutoka upande wa pili hushindwa kupata fursa ya kuwafikishia ukweli huo wananchi ili kuwawezesha kupima ukweli wa mambo na hivyo kuchukua uamuzi ulio sahihi. 

Kwa mfano, kwa mujibu wa propaganda zinazopigwa kwa kurudiwa mara kwa mara na vyombo vya habari vya BBC na CNN kuhusu dai la rushwa kuwa limekithiri sana Zimbabwe, mtu anaweza akadhani kuwa nchi hiyo ndiyo inayoongoza kwa rushwa Afrika. Lakini ukweli ni kwamba nchi zinazostahili kushikiwa bango hilo katika Afrika ni zile zilizoshika nafasi tatu za juu. Na katika hizo Zimbabwe haimo. Nchi hizo ni Nigeria, Cameroon na Tanzania. 

Mwezi uliopita, mtangazaji wa BBC alifanya mahojiano na rais wa Tanzania kuhusu suala la rushwa. Mtangazaji huyo alikuwa hodari wa kutoa fursa ya kuambiwa kuwa hatua madhubuti zinachukuliwa kuondoa rushwa nchini. Lakini mwandishi huyo hakuwa "jasiri" wa kuhoji japo ukweli wa madai kuwa rais alimchukua kiongozi mmoja wa juu wa chama tawala na kusafiri nae nje ya nchi wakati kiongozi huyo alikuwa mikononi mwa kikosi cha kuzuia rushwa nchini kwa mahojiano muhimu; na kwamba hatua hiyo ya rais ilisitisha kabisa zoezi hilo la kumhoji kiongozi huyo. 

Lakini mtu unaweza kusema kwa uhakika kwamba tukio hilo la kumuokoa mtu anahojiwa na na kikosi cha kuzuia rushwa lingelimuhusu rais Muabe, dunia nzima ingeliambiwa na lingelikuwa kigezo kikubwa cha utendaji mbovu wa serikali katika kampeni za uchaguzi. 

Wananchi hawanabudi kujifunza kuzielewa nguvu za propaganda za vyombo vya habari vya kimataifa vinavyomilikiwa na nchi za magharibi na jinsi vinavyotumika kujenga maslahi yao na ya nchi wapambe wanaokubaliana nao. 

Halikadhalika nchi hizi za magharibi na vyombo vyake vya habari ambao ni mahodari wa kumshikia mtu bango kwa kuvunja haki za binadamu huwaoni wakifanya hivyo kwa mauaji ya Mwembechai, tuhuma za watu kufukiwa wakiwa hai katika machimbo ya dhahabu Ulyankhulu au tuhuma za watu kuuawa msituni na askari wa wanyamapori au watu kuteswa na polisi na wengine kufia rumande pasipo kuwafanyia uchunguzi wa kisheria (inquest).

Wakati uchaguzi umekwisha Zimbabwe, Uganda nako zoezi la kura za maoni lilikuwa likianza kutafuta kama wananchi wanataka vyama vingi au la. Chama cha rais Musevenicha NRM ndicho kinachotawala na kuendesha shughuli za kisiasa Uganda. Lakini licha ya nchi za kimagharibi kushikia bango demokrasia ya vyama vingi na kutumika kama kigezo cha nchi kupata misaada na mikopo mbalimbali ikiwepo ya IMF, Museveni anapata kila kitu na wala halaumiwi kwa kuendeleza mfumo wa chama kimoja, na kuwanyima wananchi haki yao ya kibinadamu, kikatiba na ya kidemokrasia katika kujiundia vyama vya kisiasa na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa. 

Vyombo vya habari vya kimataifa tulivyovitaja haumshikii bango Museveni kwa kupeleka jeshi Uganda na kushindwa kuwalinda wananchi wake dhidi ya Kibwetere, wala havimlaumu kwa kutumia fedha nyingi kwa jeshi hilo wakati wananchi wanataabika kwa njaa Uganda. Lakini vyombo hivyo hivyo vinajua kutumia propaganda dhidi ya Mugabe kwa kuepeleka jeshi Kongo DRC! 

Kundi la Kikatoliki la Kanisa la Kibwetere lilipouwa watu zaidi ya elfu ilielezwa kuwa umasikini uliokithiri miongoni mwa wananchi wa Uganda ulichangia watu hao kuongamia mikononi mwa Kibwetere. Wakati huo huo Museveni amekuwa akitumia mabilioni ya fedha za wananchi wake kuyaweka majeshi yaUganda nchini Kongo DRC. 

Sijui kwa nini propaganda hizi za vyombo hivyo vya habari vya kimagharibi vimeweza kuwateka baadhi ya Watanzania wakiwemo wanasiasa wa chama tawala pamoja na baadhi ya vyombo vya habari nchini. Au ni katika harakati za wanasiasa hao kutafuta hifadhi na kujengwa na propaganda za vyombo hivyo vya kimagharibi? 

Wanasiasa hao bila shaka kwa kutaka kuponda hoja za wananchi walio wengi wanaosema kuwa Prof. Lipumba anafaa kuiongoza Tanzania kutokana na matatizo yaliyokithiri ya umasikini, maradhi na ujinga, kwa kuwa Profesa ana uwezo wa kielimu wa kuyatatua. Wanasiasa hao wa Chama tawala waliponda kwa kumtaja rais Mugabe ambae ni Musomi, kuwa eti usomi si kigezo bora kwa kuwa rais Mugabe ameshindwa kuiongoza Zimbabwe. 

Wanasiasa hao wa chama tawala wanasahau kwamba mwaka juzi katika wilaya moja ya Ulanga watu zaidi ya 40 walikufa kwa njaa nchini, wakati hakuna aliekufa njaa Zimbabwe. Sasa ni wapi wa kupigiwa mfano wa utawala mbovu Zimbabwe au Tanzania? 

Suala la watu zaidi ya 40 kufa njaa katika nchi ambavyo baadhi ya viongozi wake wengi wanatanua na kodi za wananchi kwa matumizi makubwa ya kupeleka familia zao "shopping' Afrika Kusini, wanatibiwa Ulaya na kusomesha watoto wao Marekani, si suala la kipuuzi. Lakini wananchi wasipoelewa mchezo wa baadhi ya vyombo vya habari vinavyotumika kuzima habari muhimu na kuibua zile zisizokuwa na maana, wanaweza wakadhani kuwa hali hiyo haihusiani na uongozi mbovu wa nchi husika. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Serikali isikilize kilio cha wapinzani na Waislamu

Kishindo cha CUF chaitikisa Dar

Mamia  warudisha kadi za CCM Kilwa

Chama cha Mugabe chupuchupu Zimbabwe

Wasikilizeni wananchi wasemavyo toka kwenye meli mbovu mkabala na Posta ya zamani

CCM yakasirishwa kwa kuswaliwa Mtume (S.A.W.)

Wanaomzomea Bilal waambiwa Oktoba watakula jeuri yao

CCM wapoteza viti 18196; CUF yaongoza kuvinyakua

Tambwe huyoo anakuja!

Ushauri Nasaha
Unapomdharau mama yako mbele ya rafiki yako...

MAKALA
Uchaguzi wa Zimbabwe: Vita kati ya mabeberu na wapinga Ukoloni mamboleo

MIPASHO NASAHA
Matonya wahi, pesa zinatoka sasa!

MAKALA
Vijembe kwa viongozi wa vyama vya upinzani, huduma kwa wananchi ziro

KALAMU YA MUANDISHI
Ukongwe hausaidii kubaki madarakani

MAKALA
Kuchanganya siasa na ushirikina

Habari za Kimataifa

Lishe
Faida za vyakula vya nyuzi nyuzi

RIWAYA
Dunia ndivyo ilivyo - 4

Barua

MASHAIRI

TANGAZO

MICHEZO

  • Mpambano wa watani wa jadi: U-CCM umeiponza Yanga wasema Simba
  • Wanamichezo wamshtukia Mkapa
  • Mabosi DRFA kujulikana leo

  • Pupe, Mziray wamlia ‘dip’ Shungu
    -



     
     

       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita