|
Na. 054 Jumatano Juni 28 - Julai 4, 2000 |
|
|
|
|
|
S.L.P. 72045, Dar es Salaam Serikali isikilize kilio cha wapinzani na Waislamu Tukio la uchaguzi ni moja ya mambo yenye kuhitaji kutekelezwa kwa uadilifu wa hali ya juu sana. Madhara makubwa yanaweza kupatikana ikiwa haki haikutendeka. Kwa kufahamu hatari inayoweza kutokea iwapo haki haitatendeka nchi inayohusika huweka utaratibu wa mlalamikaji kukata rufaa mahakamani kupinga matokeo. Kadhalika, taifa linalohusika hulazimika kuwaalika watazamaji kutoka katika jumuiya ya kimataifa kuwa kama mashahidi kwamba uchaguzi ulikuwa ni wa haki na huru. Katika jamii yoyote ile hakuna dawa bora zaidi ya kuondoa tatizo kama kujua chanzo cha tatizo hilo na kukishughukilia chanzo hicho. Kujishughulisha na masuala mengine yasiyo asili ya tatizo ni kupoteza muda na rasilimali. Katika uchaguzi mkuu uliopita, Oktoba 1995, malalamiko mengi yalitolewa kwamba haki haikutendeka, na kesi kadhaa zilifunguliwa mahakamani. Kesi nyingi katika hizo zilionekana zinastahiki kusiklizwa; na hilo lilifanyika, hukumu zikatolewa, matokeo yakatenguliwa na walalamikiwa wakavuliwa ubunge. Kwa kuzingatia hali hiyo tulitaraji kuwa safari hii juhudi kubwa ingeelekezwa katika kuhakikisha kuwa yale yote yaliyopelekea matokeo kulalamikiwa yanadhibitiwa. Lakini tumeshitushwa na kushangazwa na taarifa zilizopatikana kwamba serikali imeazimia kupitisha sheria itakayomtaka mtu anayetoa pingamizi la matokeo ya uchaguzi awe na dhamana ya shilingi milioni tano. (Sh. 5,000,000.00.) Sababu ya kuwekwa kiwango hicho cha fedha kama dhamana imeelezwa kuwa ni kuwazuia watu kufungua kesi bila ya kuwa na ushahidi wa kutosha juu ya madai wanayoyafikisha mahakamani. Kwa vile katika uchaguzi uliopita kesi zilifunguliwa mahakamani, na walalamikiwa wakapatikana na kesi za kujibu, na miongoni mwao wakapatikana na hatia na hukumu zikatolewa dhidi yao, dai hili la kutaka kuwazuia walalamikaji wasifungue kesi mahakamani bila ushahidi maalum 'linapwaya'. Bila shaka ni muhimu kwa serikali na wale wote wanaotetea utaratibu huu mpya wakajiuliza: Je mlalamikaji asiye na uwezo wa kukusanya hizo milioni tano lakini ikawa ni kweli 'alichezewa rafu' na mgombea mwenzake aliyeshinda afanye nini ili apate haki yake? Je, hatuoni kuwa ipo hatari ya mdhulumiwa huyo na wote waliokuwa wakimuunga mkono kushindwa kuvumilia, kuona haki yao imepokonywa kwa sababu tu hawana mamilioni hayo ya shilingi.? Je, serikali imejiandaa vipi kukabiliana na waliodhulumiwa ambao wataamua kuchukua njia za 'vyovyote iwavyo na iwe' katika kuirudisha haki yao? Wakati tunakaribia uchaguzi wa mwaka huu, mwezi Oktoba, vyama vya upinzani, Askofu Kakobe na Waislam wametoa malalamiko yao dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi. Vyama vya upinzani na Askofu Kakobe wamedai kuwa tume hiyo haitatenda haki kwa kuwa haina wajumbe kutoka kambi ya upinzani. Kwa upande wa Waislam wamedai kuwa wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni Wakristo watupu, na zaidi ya asilimia 90 ya wasimamizi na wasaidizi wao ni Wakristo. Katika hali kama hiyo Waislam wanadai kuwa Wakristo watapendelewa katika uchaguzi mkuu. Lakini serikali imekuwa ikiyapuuza malalamiko hayo kwa kutoa kauli kwamba "kwa wapinzani demokrasia ni kushinda uchaguzi" na " serikali haina udini". Sisi tunasema hivi kauli kama hizi na kuweka kiwango cha dhamana kuwa shilingi milioni tano kwa Watanzania ambao wanatambulika duniani kuwa wao ni maskini, ni mambo yanayotupeleka kubaya. Kwa hiyo, tunaikumbusha serikali kusikiliza kilio cha vyama vya upinzani, Askofu Kakobe na Waislam. |
YALIYOMO
Tahariri
Kishindo cha CUF chaitikisa Dar Mamia warudisha kadi za CCM Kilwa Chama cha Mugabe chupuchupu Zimbabwe Wasikilizeni wananchi wasemavyo toka kwenye meli mbovu mkabala na Posta ya zamani CCM yakasirishwa kwa kuswaliwa Mtume (S.A.W.) Wanaomzomea Bilal waambiwa Oktoba watakula jeuri yao CCM wapoteza viti 18196; CUF yaongoza kuvinyakua Ushauri Nasaha
MAKALA
MIPASHO NASAHA
MAKALA
KALAMU YA MUANDISHI
MAKALA
Lishe
RIWAYA
- |
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza
hapa
Au
Andika barua kwa: nasaha1420@yahoo.com
|
|
|
|