AN-NUUR
Na.168 Jamadul Akhir 1419, Septembe 24 - Oktoba 1, 1998

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita

 

THE REGISTERED TRUSTEES OF THE SOCIAL POLITICAL DEVELOPMENT TRUST (AFORD)

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 7

INATOKA TOLEO LILILOPITA

SEHEMU YA PILI

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA MIIKO YA VIONGOZI

133. Kutakuwa na Tume ya Haki za Binadamu.

Tume ya Haki za Binadamu wajumbe wake watachaguliwa na Bunge baada ya kupendekezwa na vyama vilivyosajiliwa rasmi kwa ajili ya kujishughulisha na Haki za Binadamu.

Mtu yeyote mwenye umri kati ya miaka 45 na 65, raia wa kuzaliwa mwenye mwenendo na tabia iliyojidhihirisha kuwa njema na kuigwa, atakuwa na sifa ya kuweza kuchaguliwa. Tume ya Haki za Binadamu itakuwa na wajumbe wasiopungua 3 na wasiozidi 5.

(1) Wajumbe wa Tume ya Haki za Binadamu watashika madaraka yao kwa kipindi cha miaka 5 lakin hawatafanya kazi mfululizo bali kipindi hadi kipindi.

(2) Wajumbe wa Tume ya Haki za Binadamu watamchagua kutoka miongoni mwao mwenyekiti katika mkutano wao wa kwanza.

(3) Tume ya Haki za Binadamu itakuwa na wajibu wa

(i) Kusimamia utekelezaji wa muswada wa Haki za Binadamu kama ilivyoidhinishwa katika Katiba hii.

(ii) Kufuatilia utekelezaji wa Haki za Binadamu kama vilivyoainishwa katika mkataba na makubaliano ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

(1) Tume ya Haki za Binadamu itawasilisha Bungeni taarifa yake kwa kila kipindi cha robo mwaka.

(2) (I) Serikali italazimika kutekeleza maazimio ya Tume ya Haki za Binadamu.

(i) Tume ya Haki za Binadamu itakuwa na mamlaka ya kutoa maagizo kwa watendaji serikalini na wa umma kwa ujumla.

(1) Iwapo Tume ya Haki za Binadamu itatoa uamuzi wake na uamuzi huo ukapuuzwa na serikali, mtu yeyote ambaye ataathirika kutokana na hali hiyo na au Tume yenyewe waweza kupeleka suala mahakamani kwa uamuzi.

(2) Tume ya Haki za Binadamu itatekeleza kazi na wajibu wa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi.

(3) Bunge litatunga sheria ambayo, pamoja na mambo mengine, itafafanua na kuweka wazi zaidi majukumu na wajibu wa Tume ya Haki za Binadamu na utekelezaji bora wa shughuli hizo.

(10) SEHEMU YA TATU

TUME YA UKWELI NA UPATANISHI

134. (1) Kutakuwa na Tume ya Ukweli na Upatanishi ambayo itakuwa na wajumbe 5 waliochaguliwa na Bunge kutokana na mapendekezo ya taasisi za dini na vyama vya kiraia.

(2) Mwenyekiti wa Tume ya Ukweli na Upatanishi atachaguliwa kutokana na miongoni mwa wajumbe katika mkutano wao wa kwanza.

(3) Wajumbe watakuwa madarakani kwa kipindi cha miaka 5, lakini waweza kuchaguliwa upya.

(4) Kazi ya Tume ya Ukweli na Upatanishi itakuwa kupokea na kuchunguza malalamiko ya vitendo vya serikali za tangu uhuru dhidi ya raia.

(5) Bila ya kuathiri kazi ya Tume ya Ukweli na Upatanishi iliyotajwa hapo juu, vitendo vyote vya serikali dhidi ya raia ambavyo vilitendwa kwa nia njema havitachunguzwa na Tume hii.

(6) Tume ya Ukweli na Upatanishi haitakuwa na uwezo wa kupeleka mahakamani jambo lolote lile litakalotokana na uchunguzi wa Tume hii.

SEHEMU YA NNE

MKUTANO WA KATIBA

135. (1) Kutakuwa na Mkutano wa Katiba katika kuunda Katiba ambao utakuwa chombo muhimu.

(2)Mkutano wa Katiba utakuwa na wajumbe kati ya 500 na 1,000. Nusu ya wajumbe watatoka katika vyama vya kiraia na kisiasa na nusu watatoka kwenye majimbo ya Uwakilishi.

(3) Wajumbe wa Mkutano wa Katiba watateuliwa na Bunge kutokana na mapendekezo ya vyombo vya dini, vyama vya siasa, vyama vya kiraia na majimbo ya uchaguzi. Hata hivyo uteuzi wa wajumbe utatilia maanani swala la jinsia, hivi kwamba kuwe angalau na mwanamke mmoja kutoka kila majimbo ya uchaguzi.

(4) Wajumbe wa Mkutano wa Katiba watakuwa na sifa zifuatazo:

(i)Umri wa miaka 18 au zaidi;

(ii) Elimu ya Kidato cha nne au zaidi.

(5) Mkutano wa Katiba utakuwa kwa kipindi kisichozidi siku 5.

(6) Tume ya Huduma za Bunge itakuwa ndiyo Sekretarieti ya Mkutano wa Katiba.

(7) Mkutano utakuwa na kazi zifuatazo:

Kuchambua na kuidhinisha mapendekezo ya Katiba kutoka Tume ya Katiba.

Kuchambua na kuidhinisha jinsi ya kuandaa Katiba pamoja na utekelezaji wa kura ya maoni kuhusu Katiba.

(8) Maamuzi ya Mkutano yatakuwa mapendekezo.

SURA YA TANO

KURA YA MAONI YA KATIBA

136. (1) Kura ya maoni ya Katiba ni njia mojawapo ya kuunda Katiba.

(2) Upigaji kura za maoni ya Katiba utatanguliwa na uandikishaji wa wapiga kura ambao wataorodheshwa kwenye daftari ya kudumu.

(3) Bunge litatunga sheria kuhusu upigaji wa kura za Maoni ya Katiba. Sheria hiyo itafafanua jinsi upigaji kura na maoni ya Katiba utakavyoendeshwa.

SEHEMU YA SITA

ARDHI (LAND)

136. (1) Ardhi ni mali ya wananchi.

(2) Bunge la Shirikisho litatunga sheria itakayofafanua umilikaji wa ardhi na kutenga Ardhi kwa matumizi ya umma na serikali.

SEHEMU YA SABA

TUME YA USAWA JINSIA

138. (1) Kutakuwa na tume ya Usawa wa Kijinsia yenye wajumbe wasiopungua watatu na wasiozidi watano watakaochaguliwa na Bunge kutokana na mapendekezo ya vyama vya kiraia na hiari vinavyoshughulikia maswala ya kijinsia.

(2) Tume ya Usawa wa Kijinsia itaratibu uendelezaji wa usawa wa kijinsia.

(3) Bunge litatunga sheria ya kufafanua kazi, majukumu, wajibu na muda wa kushika madaraka.

SURA YA NANE

TUME YA UTANGAZAJI

139. (1) Kutakuwa na Tume ya Utangazaji yenye wajumbe wasiopungua watano na wasiozidi kumi watakaoteuliwa na Rais na kuthibitishwa na Bunge.

(2) Tume ya Utangazaji itasimamia maswala ya utangazaji na mawasiliano.

(3)Bunge litatunga sheria itakayofafanua kazi, majukumu, wajibu na muda wa wajumbe kushika madaraka.

SURA YA TISA

BENKI KUU

140. (1) Kutakuwa na Benki Kuu itakayosimamia uchumi wa nchi.

(2) Benki Kuu itaongozwa na Gavana ambaye atateuliwa na Rais kutokana na mapendekezo ya Tume ya Uchumi wa Taifa na ambaye uteuzi wake utathibitishwa na Bunge la Shirikisho.

(3) Katika utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii na sheria iliyotungwa na Bunge Gavana hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya serikali. Lakini maelezo haya ya ibara hii hayataizuia mahakama kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuchunguza kama Gavana ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na sheria iliyotungwa na Bunge au sivyo.

(4) Gavana atashika madaraka kwa muda wa miaka mitano lakini muda huo unaweza kuongezwa.

(5) Bila ya kuathiri masharti mengine yaliyomo katika Katiba hii Gavana wa Benki Kuu atalazimika kuacha kazi yake (I) atakapotimiza umri wa miaka sitini na tano (ii) kushindwa kutekeleza kazi zake kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote au kwa sababu ya tabia au kwa kuvunja masharti ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

(6) Bunge litatunga sheria itakayofafanua utaratibu mwingine wowote wa namna ya kumwondoa Gavana kazini.

SEHEMU YA KUMI

TUME YA UCHUMI WA TAIFA

141. (1) Kutakuwa na Tume ya Uchumi wa Taifa.

(2) Tume ya Uchumi wa Taifa itakuwa na Wajumbe wasiopungua watatu na wasiozidi watano ambao watateuliwa na Rais na kuidhinishwa na Bunge kutoka kwenye orodha ya majina yatakayopendekezwa na Vyuo Vikuu, Vyama vya Wafanyabiashara, na Vyama vya Wachumi.

(3) Kazi za Tume zitakuwa ni kufuatilia maendeleo ya uchumi na kutoa ushauri juu ya hali na mwelekeo wa uchumi.

(4) Maoni na mapendekezo ya Tume hii yatawasilishwa Bungeni na kujadiliwa.

(5) Tume ya Uchumi wa Taifa itakuwa na Sekretarieti ya kudumu.

(6) Bunge litatunga sheria itakayofafanua majukumu, kazi, wajibu na muda wa kushika madaraka.

SEHEMU YA KUMI NA MOJA

MKURUGENZI WA MASHITAKA

142. (1) Kutakuwa na Mkurugenzi wa Mashitaka ambaye atateuliwa na Rais wa Shirikisho na uteuzi wake utaidhinishwa na Bunge.

(2) Mkurugenzi wa Mashitaka atakuwa na sifa za uzoefu wa kazi kwa miaka 15 au zaidi na atakuwa na umri usiopungua miaka 45.

(3) Masharti ya kazi ya Mkurugenzi wa Mashitaka yawe kama yale ya Mdhibiti Mkaguzi na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali.

(4) Ofisi itakuwa na madaraka kamili ya kumfikisha mtu yeyote mahakamani bila ya kuomba kibali kwa mujibu wa Katiba hii.

(5) Maamuzi ya Mkurugenzi kuhusu kutoshitakiwa au "Nolle Prosequi" yaweza kusahihishwa na Mahakama Kuu.

SEHEMU YA KUMI NA MBILI

TUME YA ULINZI

143. (1) Kutakuwa na Tume ya Ulinzi ambayo wajumbe wake watakuwa Rais, Waziri Mkuu wa Tanganyika na Waziri Mkuu wa Zanzibar, Mkuu wa Majeshi, Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Magereza pamoa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama.

SURA YA KUMI NA TATU

MENGINEYO

Maelezo ya Katiba

144. (1) Mtu yoyote mwenye dhamana ya mambo ya kazi iliyoanzishwa na Katiba hii (pamoja na yanayohusika kazi ya Waziri, naibu Waziri au Mbunge, isipokuwa ya madaraka ya Mbunge ambaye ni Mbunge kwa mujibu wa madaraka ya kazi yake, aweza kujiuzulu kwa kutoa taarifa iliyowekwa saini kwa mkono wake kwa kufuata masharti yafuatayo:-

(a) Iwapo mtu huyo aliteuliwa au alichaguliwa na mtu mmoja, basi taarifa hiyo ya kujiuzulu atawasilisha kwa mtu huyo aliyemteua au aliyemchagua, au iwapo aliteuliwa au alichaguliwa na kikao cha watu, basi taarifa hiyo ya kujiuzulu ataiwasilisha kwenye kikao hicho;

(b) iwapo mtu huyo ni Rais, basi taarifa hiyo ya kujiuzulu ataiwasilisha kwa Spika;

(c) iwapo mtu ni Spika au Naibu Spika wa Bunge, basi taarifa ya kujiuzulu ataiwasilisha kwenye Bunge; na

(d) iwapo mtu huyo ni Mbunge, basi taarifa hiyo ya kujiuzulu ataiwasilisha kwa Spika.

(2) Mtu aliyetoa taarifa ya kujiuzulu kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (1) ya ibara hii, atahesabiwa kuwa amejiuzulu tangu siku ile ambayo taarifa yake ya kujiuzulu itakapopokelewa na mtu yoyote aliyeruhusiwa kuipokea taarifa hiyo na mtu anayehusika au kikao kinachohusika, lakini kama taarifa hiyo ya kujiuzulu imeeleza kwamba mtu huyo atajiuzulu tangu siku nyingine baada ya taarifa hiyo kupokelewa na mtu anayehusika au kikao kinachohusika, basi mtu huyo atahesabiwa kuwa amejiuzulu tangu siku hiyo nyingine ya baadaye.

(3)Iwapo mtu yeyote mwenye dhamana ya kazi yoyote iliyoanzishwa na Katiba hii (pamoja na kazi ya Waziri, Naibu Waziri au Mbunge, isipokuwa Mbunge ambaye ni Mbunge kwa mujibu wa madaraka ya kazi yake) amejiuzulu, basi ikiwa anazo sifa zote zinazohitajika na kwa kila hali anastahili, aweza kuteuliwa au kuchaguliwa tena kushika madaraka ya kazi hiyo kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.

(4) Masharti yaliyomo katika ibara ndogo ya (3) ya ibara hii hayatamzuia mtu ambaye ni Rais kuchaguliwa tena kuwa Rais wakati bado ameshika madaraka ya kazi ya Rais.

(d) Maelezo kuhusu utaratibu wa kukabidhi madaraka ya kazi ya utumishi serikalini

145. (1)Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya Katiba hii kuhusu utaratibu wa kukabidhi madaraka ya kazi katika utumishi wa Serikali ya Shirikisho, ifahamike kuwa mtu yeyote mwenye mamlaka, kwa mujibu wa Katiba hii, ya kumteua au kumchagua mtu mwingine katika kushika madaraka ya kazi fulani anao pia uwezo wa kumteua au kumchagua Kaimu au mtu wa serikali ambaye atashikilia kwa muda na kutekeleza madaraka ya kazi hiyo:

Isipokuwa kwamba maelezo hayatatumika kwa madaraka ya kazi ya Waziri, Naibu Waziri, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama ya Shirikisho au Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi.

(2)Kanuni zifuatazo zitatumika pia kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya Katiba hii kuhusu utaratibu wa kukabidhiana madaraka ya kazi katika utumishi wa serikali ya Shirikisho, yaani:

Iwapo kuna mtu mwenye madaraka ya kazi fulani aliyokabidhiwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na mtu huyo yupo likizoni na wakati huo huo anangojea kuacha kazi hiyo, basi anaweza kuteuliwa mtu mwingine na kukabidhiwa madaraka ya kazi hiyo, bila ya kujali kuwapo kwa yule mtu anayengojea kuacha kazi hiyo;

iwapo kuna watu wawili au zaidi ambao kwa wakati mmoja wote wanashika madaraka ya kazi fulani kutokana na uteuzi wao uliofanywa kwa mujibu wa Kanuni iliyoelekezwa katika aya ya (a) ya ibara hii ndogo, basi katika hali hiyo kukitokea haja ya kutekeleza shughuli yoyote inayohusika na madaraka ya kazi hiyo yule wa mwisho kuteuliwa ndiye atakayehesabiwa kuwa mtu pekee mwenye dhamana ya kazi hiyo;

iwapo mtu ameteuliwa, kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii, kuwa Kaimu au kushikilia madaraka ya kazi fulani wakati mtu maalum aliyeteuliwa kushika madaraka ya kazi hiyo anashindwa kutekeleza shughuli zinazohusika na kazi hiyo, basi haitaruhusiwa kufanya uchunguzi wowote au kutoa hoja yoyote juu ya uteuzi wa huyo Kaimu eti kwa sababu kwamba huyo mtu maalum aliyeteuliwa kushika madaraka ya kazi hiyo hakushindwa kutekeleza shughuli zinazohusika na kazi hiyo.

Ufafanuzi

146. (1) Katika Katiba hii, ila iwapo maelezo yahitaji vinginevyo

"amri ya jeshi" maana yake ni sheria au amri iliyotolewa kwa mujibu wa sheria, ya kusimamia nidhamu katika jeshi;

"askari" likitumika kuhusiana na jeshi lolote, maana yake ni pamoja na askari yeyote ambaye kwa mujibu wa amri ya jeshi hilo ni mtu anayewajibika kinidhamu;

Baraza la Wawakilishi maana yake ni Baraza la Kijiji/Mtaa, Kata, Wilaya na Mkoa katika Tanganyika na Zanzibar utakaotekeleza madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii.

Bunge maana yake Bunge la Shirikisho Bunge la Tanganyika na Bunge la Zanzibar.

"Chama cha siasa" maana yake ni chama cha Siasa kilichoandikishwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria ya Vyama vya Siasa;

"Jaji Mkuu" maana yake ni Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Tanganyika au Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar.

"Jeshi" maana yake ni lolote kati ya majeshi ya ulinzi na ni pamoja na jeshi lolote jingine lililoundwa kwa mujibu wa Katiba hii au kwa mujibu wa Sheria na linalotaliwa kwa amri ya jeshi;

"Jumuiya ya Madola" maana yake ni jumuiya ambayo wanachama wake ni Shirikisho na kila nchi ambayo inahusika na masharti ya ibara ya 7 ya sheria ya uraia, ya mwaka 1961;

"Kiapo" maana yake itabidi kifamike kwa maana ya kawaida ya neno hilo ni pamoja na tamko rasmi la namna yoyote linaloruhusiwa kisheria kutumiwa badala ya kiapo;

"Jiapo cha uaminifu" maana yake ni kiapo cha kuwa mwaminifu kwa nchi na kwa serikali ya Shirikisho;

"Maadili ya Kazi ya Jaji" maana yake ni masharti ya kimaadili yanayoongoza mwenendo wa watu wafanyao kazi ya Jaji au ya Hakimu;

"Madaraka ya kai katika utumishi wa serikali ya Shirikisho" maana yake itabidi ifahamike kwa mujibu wa maana ya kawaida ya maneno hayo ni pamoja na utumishi katika Majeshi ya Ulinzi na Shirikisho na katika Jeshi la Polisi au jeshi linginelo lililoundwa kwa mujibu wa sheria;

"Mahakama" maana yake ni mahakama yoyote yenye mamlaka katika Shirikisho isipokuwa mahakama iliyoundwa kwa amri ya jeshi;

"Mahakama Kuu" maana yake ni Mahakama Kuu ya Tanganyika au Mahakama Kuu ya Zanzibar'

"Mambo ya Shirikisho" maana yake ni mambo yote ya umma ambayo yametajwa na ibara ya 4 ya Katiba hii kuwa ni Mambo ya Shirikisho;

"Mamlaka ya nchi" ni pamoja na Serikali Bunge la Shirikisho, Serikali na Bunge la Tanganyika serikali na Bunge la Zanzibar pamoja na mabaraza ya wawakilishi ya kijiji/mtaa, kata, wilaya na mkoa;

"Mwanasheria Mkuu" maana yake ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Shirikisho;

"Rais wa Mahakama ya Rufani" maana yake ni Rais wa Mahakama ya Rufani aliyeteuliwa chini ya ibara ya 111 ya Katiba hii;

"Serikali" maana yake ni pamoja na serikali ya Shirikish, Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar, Halmashauri ya wilaya/mji pamoja na mabaraza ya wawakilishi na pia mtu yeyote anayetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya serikali, halmashauri au baraza la wawakilishi;

"Serikali za Mitaa" maana yake ni vyombo vya kiserikali vilivyoundwa kwa mujibu wa ibara ya 32 ya Katiba hii kwa madhumuni ya kutekeleza madaraka ya umma;

"Uchaguzi Mkuu" au "Uchaguzi unaofanywa na wananchi" maana yake ni uchaguzi wa Rais na uchaguzi wa Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi unaofanywa baada ya Bunge kuvunjwa;

"Waziri" maana yake ni mtu aliyekabidhiwa madaraka ya Uwaziri;

(2)Kanuni zifuatazo zitatumika kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya Katiba, yaani:-

Kila yanapotajwa madaraka ya Rais, ifahamike kuwa madaraka yanayohusika ni pamoja na mamlaka ya kutekeleza shughuli na kazi mbalimbali na vile vile wajibu wa kutekeleza shughuli na kazi mbalimbali kma Mkuu wa Serikali ya Shirikisho, na pia mamlaka mengine kama hayo au wajibu mwingine kama huo ikiwa imeelezwa katika Katiba hii au katika Sheria nyingine yoyote kwamba mamlaka hayo mengine ni ya Rais au kwamba wajibu huo mwingine ni wa Rais;

kila yanapotajwa madaraka ya kazi katika utumishi wa serikali, ifahamike kuwa kazi inayohusika ni kazi katika Utumishi wa Serikali ya Shirikisho isipokuwa kama imeelezwa vingine, na kila inapotajwa idara ya serikali ifahamike kuwa idara inayohusika ni idara ya serikali isipokuwa kama imeelezwa vingine;

iwapo kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii kuna jambo lolote linalotakiwa litekelezwe au lishughulikiwe na chama chochote cha siasa, basi, jambo hilo litatekelezwa au litashughulikiwa na chama hicho kwa mujbu wa utaratibu uliowekwa na chama hicho kwa ajili hiyo, an pia kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii au Sheria yoyote iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo;

(e) kwa madhumuni ya Katiba hii, mtu hatahesabiwa kuwa ana madaraka ya kazi katika utumishi wa serikali ya Shirikisho kwa sababu tu kwamba anapokea malipo ya uzeeni au malipo mengine ya aina hiyo kwa ajili ya utumishi wake wa zamani katika serikali ya Shirikisho;

(f) katika Katiba hii, ila iwapo maelezo yahitaji vingine, kila anapotajwa mwenye dhamana ya kazi fulani kwa kutaja madaraka ya kazi yake, ifahamike kuwa mtu anayehusika ni pamoja na mtu yeyote ambaye ni kaimu au aliyeteuliwa kwa njia halali kushikilia dhamana ya kazi hiyo;

(g) katika Katiba hii, kila yalipotajwa mamlaka ya kumwondoa mtu katika madaraka ya kazi katika utumishi wa serikali ifahamike kuwa mamlaka yanayohusika ni pamoja na mamlaka yaliyomteua kwa mujibu wa masharti ya sheria yoyote yanayomtaka mtu huyo au yanayomruhusu mtu huyo kustaafu.

(h) Isipokuwa kwamba meelezo ya kanuni hii yasifahamike kuwa yanampa mtu yeyote mamlaka ya kumtaka Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama Kuu au Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu astaafu.

(i) Katika Katiba hii, kila ilipotajwa au kufuta sheria nyingine, ifahamike kuwa sheria inayohusika ni pamoja na sheria ambayo inarekebisha sheria hiyo nyingine au ambayo inaendeleza kutumika kwa hiyo sheria nyingine, ama bila madadiliko au baada ya kubadilishwa au kurekebishwa, au sheria ambayo inaweka masharti mapya katika sheria nyingine.

Jina kamili la Katiba tarehe ya kuanza kutumika na matumizi ya Katiba hii

147. (1) Jina kamili la Katiba ni Katiba ya Shirikisho la Tanzania ya

(2) Katiba hii itaanza kutumika tarehe

(3) Katiba hii itatumika Tanganyika na vile vile Zanzibar.

NYONGEZA YA KWANZA

(Imetajwa katika ibara ya 4)

Mambo ya Shirikisho

Katiba ya Shirikisho la Tanzania.

1. Mambo ya Nchi za Nje.

2. Ulinzi na Usalama.

3. Polisi.

4. Mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari.

5. Uraia.

6. Uhamiaji.

7. Utumishi katika serikali ya Shirikisho.

8. Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi, mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania unaosimamiwa na idara ya Forodha.

9. Bandari,mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu.

10. Mambo yote yanayohusika na sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yote halali (pamoja na noti)' mabenki (pamoja na mabenki ya kuweka akiba) na shughuli zote za mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni.

11. Maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa yanayotokana na mafuta aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa, na gesi asilia.

12.Usafiri na usafirishaji wa anga.

13. Utafiti.

14. Takwimu.

15. Mahakama ya Rufani ya Shirikisho.

16. Uandikishaji vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana navyo.

17. Haki za Binadamu.

18. Mahakama ya Shirikisho.

19. Tume za Shirikisho.

20. NYONGEZA YA PILI

MAMBO YASIYO YA SHIRIKISHO

Polisi (State Police)

20. External Trade and Borrowing

21. Public Service of States

22. Industrial Licensing and Statistics

23. Higher Education

24. Ardhi.

25. National Examination Councils na mambo mengine yote ambayo hayakutajwa katika nyongeza ya kwanza ya Katiba hii.

23rd May, 1998 

Juu 
 

YALIYOMO  
 
TAHARIRI 
Iran ina agenda gani?

Mauaji,udhalilishaji Mwembechai: Wanawake Waislamu waandamana Tabora Na Mwandishi Wetu

BUCHA YA NYAMA YA NGURUWE KATIKATI YA WAISLAMU
Na Mwandishi Wetu

'Serikali ieleze hatua iliyochukua kuhusu mauaji Mwembechai'
Na Kassim Juma

Vijana wa Kiislamu wajiimarisha Bukoba
Na Nooh Mustafa, Bukoba

Sheikh Mzonge awataka Waislamu Moshi wasimamishe swala
Na Ashraf Yussuf, Moshi

TAMKO LA PAMOJA LA MISIKITI SABA YA MWANZA-KUPINGA OMBI LA BAKWATA KWA SERIKALI LA KUIFUTIA USAJILI WAKE

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 7

MAKALA: Baadhi ya Watanzania wangali wanaishi ‘Tanganyika’
Na Mwandishi Wetu

HOJA BINAFSI: Maendeleo ya Tanzania ni ndoto
Na Fatma Mussa

‘Musiwasingizie wake zenu maovu’
Na Habiba Swedi, Arusha

Wanafunzi Waislamu Songea wapata viongozi
Na Mwandishi Wetu, Songea

Kikundi cha wanawake wa Kiislamu Bi. Khadija – Dodoma
Na Abu Zuberi, Dodoma

Waahidi kutekeleza majukumu kwa jina la Allah
Na Habiba Swedi, Arusha

Arumeru wahitaji Da’awa
Na habiba Swedi, Arusha

Wanawake wa Kiislamu wazungumzia maendeleo yao

Kauli ya wanawake wa Kiislamu Iringa kuhusu kadhia ya Mwembechai

Uislamu ulivyoingia Zanzibar

Wanawake Singida walaani mauaji Mwembechai Wamchangia Mama Chuki 17,000/-
Na Mwandishi Wetu

Sekondari ya Kiislamu kujengwa Maere Tanga
Na Abu Abdullah, Tanga

Sheikh ahimiza Waislamu Lindi wafuate mafunzo ya Uislamu
Na Mohamed Mussa, Lindi

Sheikh Zuberi awataka Waislamu Dodoma kuimarisha Misikiti
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mafundisho ya Quran 
Dhikiri maana yake nini? - 2

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 
Matatizo ya tumbo yanayosababishwa na utumiaji wa maziwa

Matangazo 

 

 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org  

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita