|
AN-NUUR
|
| MAKALA
Baadhi ya Watanzania wangali wanaishi 'Tanganyika':
Na Mwandishi Wetu HARAKATI za ukombozi wa Tanganyika zilianza mara tu mkoloni wa kwanza (Mjerumani) alipoingia humu nchini. Kadri muda ulivyokwenda harakati hizi ziliongezeka zaidi miaka ya hamsini na hasa baada ya TAA kubadili jina kuwa TANU. Matunda ya harakati hizi yalipatikana mwaka 1961 ambapo Tanganyika ilipata uhuru wake. Ni dhahiri kuwa usiku ule wa Desemba 9, 1961 wakati ilipokuwa inashushwa bendera ya Muingereza na kupandishwa ile ya Tanganyika, kila aliyeshuhudia alikuwa na yakini kuwa ule ulikuwa ndio mwanzo wa maendeleo ya nchi yake. Maendeleo ambayo yangekuja kuonekana katika hali bora zaidi za kiuchumi kwa taifa na mtu mmoja mmoja, nyumba bora zaidi, kilimo cha kisasa zaidi, usafiri bora zaidi na juu ya hayo elimu bora zaidi na kwa wote. Mashahidi walikufa katika harakati zile nao wamekufa wanaamini vivyo hivyo. Uhuru wenye tafsiri tofauti na hii kuleta maendeleo na kuondoa ubaguzi bila shaka usingesherehekewa kama ilivyoonekana siku ile ya uhuru. Hakuna mtu yeyote aliyekuwa na mashaka siku ile ya uhuru juu ya uhusiano mkubwa uliokuwepo baina ya kuondoka kwa wakoloni, yaani kupata uhuru na kuondoka kwa ubaguzi wa maendeleo duni miongoni mwa watu wa nchi hii. Leo ninapoandika makala hii wengi wa wale waliokuwepo na wale waliokuja kuzaliwa nyuma, si ajabu wakawa na wakati mgumu zaidi endapo wataulizwa kubainisha uhusiano uliopo baina ya maendeleo duni na ubaguzi hapa nchini mwetu na kuondoka kwa wakoloni. Si ajabu leo mtu akaulizwa uhuru na ukoloni utachagua nini? Kisha akisema, subiri nifikirie! Baada ya uhuru mwaka 1961 viongozi wa nchi hii walifanya mengi kwa nia ya kuendeleza nchi hii. Baadhi ya hayo ni kama ifuatavyo: 1961 - Uhuru wa Tanganyika 1962- Jamhuri ya Tanganyika 1964 - Muungano (Tanganyika na Zanzibar) Tanzania 1967 - Azimio la Arusha 1971 - Madaraka mikoani Bila shaka U.P.E, vijiji vya ujamaa, maduka ya kaya, elimu bure, kutaifisha majumba, mashamba n.k. Kwa wakati ule nyimbo nyingi zilitungwa kupongeza kila hatua iliyochukuliwa. Kwa bahati nzuri miaka yote ya sitini na sabini iliwashuhudia Watanzania chini ya utamaduni wa kuheshimu na kuthamini sana viongozi wao, hivyo moyo wa uzalendo ulijitokeza wazi wazi. Hali hii ilijitokeza hasa pale wananchi walivyozitii hata amri ambazo bila shaka hata serikali iliona tabu kuzitekeleza, mfano kuanzishwa vijiji vya ujamaa, kutaifisha majumba na mashamba n.k. Tuliambiwa na tukaamini kuwa Tanzania haiwezi kuwa huru hadi Afrika yote iwe huru. Tulitumia kila tulichoweza kufikia lengo hili. FRELIMO, MPLA, ANC, SWAPO walifaidi sana msimamo wetu huu. Tuliambiwa Idd Amin ni nduli anayetumiwa na mabwana zake ili kuzorotesha harakati za ukombozi wa Afrika. Tulikubali hili watu walitoa mali na roho zao kuikomboa ardhi yetu na kumpa adhabu kidogo ndani ya mipaka ya nchi yake. Haya yalifanyika bila mtu yeyote kuhoji kwa vile wengi walidhani kufanya vile ni katika harakati zile zile za kutuletea maendeleo. Leo ni miaka 37 tangu tumepata uhuru, wale waliojaliwa umri na wale waliozaliwa nyuma tunalazimika kujiuliza ikiwa ndoto zetu juu ya faida za uhuru zilikuwa kweli. Watu wanaoishi mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi wanaweza zaidi kuona kile kinachozungumzwa katika makala hii. Hawa watakuwa ni wawakilishi wa wale wanaoishi sehemu tofauti kijiografia, lakini zenye kufanana katika hali za kimaisha. Kiusafiri itamchukua msafiri masaa takribani 24 kufika Lindi kutokea Dar es Salaam na masaa 29 kufika Mtwara au Masasi na zaidi ya masaa 32 kwenda Nachingwea kutokea Dar es Salaam. Muda huu haumaanishi umbali wa sehemu zenyewe bali aina ya barabara na mabasi yanayoelekea huko. Kivuko cha Mto Rufiji ambacho hufanya kazi kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 12 jioni kinaweza kumuongeza msafiri masaa hadi 12 ya safari yake endapo ataingia kivukoni dakika chache tu baada ya saa 12 jioni. Mwandishi wa makala hii alimshuhudia mama mmoja aliyekuwa akisafiri kutoka Masasi kuja Dar es Salaam kwa basi la Air Msae baada ya kusota masaa 14 safarini na akiwa bado hata kuukaribia mto Rufiji akiuliza kwa hasira "hivi kwa nini serikali isione umuhimu wa kujenga barabara hii kabla ya kujenga daraja la mto Rufiji"? Watu wengi waliokuwa karibu naye kweli hawakuona sababu kwa nini serikali inatoa kipaumbele katika ujenzi wa daraja badala ya kujenga barabara. Ukweli ni kuwa ujenzi wa barabara pia unaweza ukafanyika sambamba na ujenzi wa daraja kama wahusika wangeacha 'vunga' na siasa za ubabaishaji. Na kama kuna haja ya kimoja kisubiri mwenzake basi daraja lingesubiri. Si jambo rahisi mtu kuelewa ujenzi wa barabara kutoka Mnazi Mmoja mkoani Lindi hadi Nangurukuru umekwamishwa na nini. Pia si rahisi kuona sababu ya kutokuwepo ujenzi wa barabara kutoka Nangurukuru hadi Mtoni Rufiji mpaka leo hii. Cha kushangaza zaidi ni hali duni ya barabara kutoka Rufiji hadi Dar es Salaam ambapo mabasi huchukua zaidi ya masaa manne, muda ambao basi hilo hilo bila Luku itakaribia Same kutoka Dar es Salaam. Hali ya barabara ya Mtwara - Masasi pia ina dosari. Kipande cha barabara kati ya Mtama na Masasi kilichofukiwa na mafuriko ya mwaka 1991 bado hakijafukuliwa na madaraja bado kujengwa. Mtu anaweza kutafsiri hali ya maisha ya watu wa kusini kwa kutumia kigezo cha usafiri, hali duni ya nyumba za watu kama zinavyoonekana kuanzia Rufiji hadi Mtwara, mavazi yao na watoto wao n.k. Ni matarajio ya binadamu anayeishi kwa kupambana na maisha kumwona mwanaye akilala katika nyumba bora zaidi kuliko ile yake, akila chakula bora zaidi na kuvaa mavazi bora zaidi. Kwa kweli hali ni kinyume kabisa kwa wale wanaoishi kusini mwa nchi hii. Mjini Lindi kuna kila dalili zinazoashiria kufa kwa mji huo kwa vigezo vya majengo na barabara. Nyumba zinazoonekana ni za miaka ya arobaini, hamsini hadi sitini, hazijui rangi na hakuna tamaa kuwa endapo zitaanguka patajengwa nyingine. Msikiti uliopo kituo cha mabasi cha Lindi ni mfano tu wa majengo yanayoonekana kama mahame bado unatumika. Hali katika Mtwara ya kale yaani Mikindani na ile ya Mtwara Mjini hazipitani sana. Kuna kila dalili za kufa kwa mji si rahisi kuona nyumba yenye hadhi ya makao makuu ya mkoa inayojengwa hivi sasa. Majengo ya zamani katika mtaa wa Khan yanaashiria kudumaa kwa mji kunakoashiria kifo chake siku za usoni. Mjini Mtwara nilimwona dalali akiuza kitanda cha kamba. Sikuamini macho yangu kuwa bado kuna uwezekano wa kumpata mtu anayelalia kitanda kile pale mjini tarehe hizi za Septemba ya 1998. Nikiwa nimesimama kando ya duka moja katika mtaa wa maduka makubwa mjini hapo yaani mtaa wa Aga Khan niliwasikia watu wapatao watano wakijadili na sababu ya Watanzania kuwa wavivu. Niliamua kuwasikiliza japo sikuwaruhsu wafahamu kuwa nilikuwa ninawasikiliza. Mzee mmoja wa makamo aliyeonekana kama mtu wa kijiweni alitoa hoja zilizonisisimua na kunifanya niamini kuwa alikuwa ni afisa wa serikali ya ujamaa na kujitegemea aliyestaafu. Kimsingi haiba yake haiwezi kumtofautisha na mtu wa mtaani bali hoja zake zilimtofautisha. Yeye alidai kuwa uvivu wa Watanzania umeanzia kwenye vijiji vya ujamaa na utaifishaji mali za watu uliofuatia Azimio la Arusha . Anasema mtu anahamishwa kwenye eneo lake lililokaribu na mikorosho yake halafu anahamia mbali na shamba lake vipi tena aweze kurudi kulihudumia? Serikali inapoamua kuzuia umilikaji mali binafsi na kutilia mkazo mali kuwa ya wote, au ya mtu kufanya kazi tena kwa nia ya kujipatia mali inatoweka. Akaongeza kuwa watu waliokuwa na majumba yao wanaponyang'anywa kwanini wengine wasiogope kujenga? Kuhusu korosho ambalo ndiyo zao la biashara huko kusini, ni kweli miti yake imetapakaa kila mahali bali suala linalogomba ni upaliliaji. Baadhi ya sababu ni kulegalega kwa soko lake kiasi kwamba wananchi hawalioni zao hili kama mkombozi ukilinganisha na kahawa au pamba katika kanda nyinginezo hapa nchini. Mstaafu huyo wa serikali ya ujamaa alionyesha kuwa huenda zao la korosho limehujumiwa na Wahindi kama kulipiza kisasi kwa serikali ambayo ilitaifisha nyumba zao. Mstaafu huyo anadai kuwa India ndiyo iliyokuwa mnunuzi mkubwa wa korosho ya Tanzania. Pia alidai kuwa viwanda vya kubangulia korosho vilivyotapakaa kuanzia Kibaha, barabara ya Nyerere, Barabara ya Kilwa, Mtwara mjini, Masasi hadi Nachingwea vyenye uwezo wa kubangua karibia tani 100,000 kwa mwaka vilijengwa bila kuzingatia utafiti wa kitaalamu juu ya uwezo wetu wa uzalishaji. Si hivyo tu, lakini pia vilijengwa kwa mkopo, kiasi kwamba japo vingi havijafanyika kazi na kuwa vile vinavyofanyakazi vinafanya hivyo chini ya uwezo wake, bado tunadaiwa deni la watu. Alitimisha kwamba maamuzi ya kisiasa yaliyofanywa na viongozi wetu bila kuzingatia ushauri wa kitaalamu ndiyo sababu ya kukata tamaa kwa Watanzania na hivyo kuwa wavivu. Kadri unavyoweza kufikiria hali ya maisha ya watu wa kusini kwa kuwaona na kuiona kusini yenyewe ndivyo unavyoweza kushangaa nini kimetokea hata wakawa hapo walipo. Hata ukiambiwa labda ukagombee ubunge huenda ukashindwa ni ahadi au matumaini gani uwape watu hao. Utashangaa zaidi ukianza kufikiri kuwa watu hawa wamekuwa wakishiriki uchaguzi wa wabunge na Rais kama mara saba sasa tangu tupate uhuru, na hasa ukitaka kujua ikiwa wengi wao wanafahamu uhusiano uliopo baina ya kura zao na hali yao duni ya maisha. Kuna wakati ilisemekana kuwa baadhi ya wabunge wa kusini wanaona heri kujitenga na kujiunga na Msumbiji. Wale Watanzania wasiofahamu hali ya kusini wanaweza kudhania kuwa huenda hawa wabunge wamekosa uzalendo au wamekosa la kuongea bungeni. Hata mie nilidhani hivyo hivyo, lakini sasa nimeona mantiki ya tamko hilo. Kwanza wenzetu wa Msumbiji wanasababu ya kuwa masikini. Uhuru wao wote, wameishi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Lakini sisi tunajivunia amani na utulivu hali yetu shwari kabisa, "mwanga" wetu nani? Wako watu ambao tayari wameanza kushtuka. Wabunge waliodai kujiunga na Msumbuji ni mfano wa hao. Lakini pia wako wapiga kura walioanza kujua chanzo cha matatizo yao huko kusini. Wako wale ambao wanadhani hali yao ya maisha inatokana na kudura za Mungu. Kunakuwepo tatizo watu kuja na njia na mbinu mbalimbali za namna ya kutatua. Kwa wale wenye mtazamo wa kisiasa kama mimi huenda watu hawa wanahitaji msaada wa kisiasa, katika zama hizi za uwazi na ukweli ni vyema wakazifahamu haki zao za kiraia, wakajua kutofautisha kati ya mwananchi na raia. Wakijua hili ni rahisi kujua kuwa kura yao ndiyo itakayochagua aina ya maisha watakavyoishi miaka 37 ijayo. Baada ya hapo watampima muombaji kwa kile atakachowafanyia, watamtazama endapo hana uhusiano na hao waliowadumaza. Kwa wale walio katika madaraka njia hii huenda ikawa mbaya kwao endapo wananchi wakigundua kuwa ndiyo "wanga" wao la sivyo ni njia nzuri ya kutofautisha wanasiasa wa watu na wale wababaishaji. Ni wazi pia kuwa wako wananchi wa kusini ambao hawajui kuwa wanatabu kwa vile tu hawajawaona wenzao wenye afadhali. Pia wapo wanaojua wana taabu lakini hawajui wafanye nini. Chamsingi ni kwamba wote waliotegemea maisha ndani ya Tanzania yawe bora kuliko yale ya Tanganyika, hawakutegemea kuishi ndani ya "Tanganyika" hadi leo hii miaka 37 baada ya uhuru. Huenda wanajiuliza "Musa" wetu atazaliwa lini? Au huenda wanatamaa labda ndiye huyu. Ninachopenda kuwaambia ni kuwa maendeleo ya watu huletwa na wao. Uzeni kura zenu kwa maendeleo. |
YALIYOMO
TAHARIRI Iran ina agenda gani? Mauaji,udhalilishaji Mwembechai: Wanawake
Waislamu waandamana Tabora Na Mwandishi Wetu 'Serikali ieleze hatua iliyochukua
kuhusu mauaji Mwembechai' ‘Musiwasingizie wake zenu maovu’
Barua za wasomaji
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org