|
AN-NUUR
|
| Uislamu ulivyoingia
Zanzibar
MTUME Muhammad (saw) alifariki mwaka wa 11 Hijiria kwa mwaka 632 wa Kikristo. Makhalifa Waongofu wanne walishika nafasi yake kuongoza umma wa Waislamu. Wakarithi mfumo wa uongozi uliounganisha shughuli za dini na dola. Wakati huo mataifa yaliyokuwa na nguvu kubwa ni dola ya Warumi kwa upande wa Magharibi na Wafursi (persia) kwa upande wa Mashariki. MTUME Muhammad (saw) aliwahi kuwapelekea risala viongozi wa madola hayo makubwa na mengineyo wakubali Uislamu, na raia wao wanaoamua kufuata Uislamu wasiwatese. Waliojibiza ukafiri, kuwaonea au kuwashambulia Waislamu walipambana na majeshi ya dola ya Kiislamu na watu wa nchi hizo mpya walipofikiwa na neema ya Uislamu na Waislamu wakakaribishwa vyema kama ni wakombozi kutokana na watawala wa zamani walivyowakandamiza. Mtume (saw) aliwacha dola ya Kiislamu imo vitani na Makhalifa waliendeleza mapambano hayo. Mbali na nchi zilizokuwa karibu na Makka na Madina, Uislamu ulienea Afrika ya Kaskazini. Nchi nyingine kama vile Iran, Afghanistan, India n.k. zikafikiwa na Uislamu. Katikati ya karne ya 7 A.D. Uislamu ulikuwa tayari umeshafika Ethiopia, Visiwa vya Mediterrean. Alipofariki Sayyidna Uthman bin Affan (ra) eneo la ardhi linalokaliwa na Waislamu lilikuwa na ukubwa ulio karibu sawa na Bara la Ulaya. Kisha Uislamu ukafika nchi za Ulaya kama vile Hispania, pia kwa upande wa Mashariki ya Mbali ukafika Uchina. Baada ya kumalizika kipindi cha Makhalifa Waongofu kulianza vurugu kubwa. Waislamu wenyewe kwa wenyewe walipigana. Watawala wa Bany Umayya walioshika dola wakayahamisha makao makuu ya dola ya Kiislamu kutoka Madina na kuyaweka Damascus (Syria) 661 AD. Utamaduni wa sehemu hiyo uliathiriwa sana na Uzungu chini ya dola ya Kirumi na ucha-Mungu haukuwa mkubwa kama Madina na nguvu za kuenea kwa Uislamu zilipungua ingawa hazikusita. Katika Makhalifa wa Bany Umayya aliyefanikiwa sana kurejesha ucha Mungu na uadilifu, yakafunguka katika dola ya Kiislamu maendeleo mbalimbali ya kiutamaduni kama katika fani ya viwanda na matibabu ni Umar bin Abdu Aziz (817-20 AD) ingawa muda wake ulikuwa mfupi. Miongoni mwa makundi yaliyozuka na kutofautiana katika kipindi cha Bany Umayya ni kundi dogo la Mashia ambao baadaye walitegemea wanazuoni tofauti na kulifanya kundi hilo la kisiasa kuwa pia ni madhehebu. Yalikuwepo makundi mengine, lakini wengi waliobaki na ambao walikubaliana na sera za Bany Abbas wakahamisha makao makuu Damascus na kuyaweka Iraq katika mji wa Baghdad, Madinat salaam. Matokeo ya migongano yote hiyo yakafanya dola ya Kiislamu kuanza kusambaratika, baadhi ya magavana wa majimbo wakajitangazia tawala zao, wakajiita majina mbalimbali kama Makhalfa, Masultani na Maimamu. Kwa mfano baadaye (karne ya 10 AD) miongoni mwa Mashia kundi la Fatimiyya lilipata nguvu na mali na kufanya Misri makao ya utawala wao. Kwa sababu ya Uislamu lugha ya Kiarabu ikaendea na kuwa muhimu kuliko lugha nyinginezo. Tumeona kuwa kipindi ambacho ujumbe wa Mtume Muhammad (saw) ulianza kuenea sana duniani ni pale waliposhika Makhalifa. Dola ya Kiislamu haikufika Afrika Mashariki. Imani iliyopo ni kuwa Uislamu uliletwa katika miji ya Mwambao wa Afrika kupitia misafara iliyokuwepo ya kibiashara na pia kutokana na athari za Waislamu waliotokea nchi za Uarabuni hapo zamani kwa kukimbia vurugu au wimbi la mabadiliko kama tulivyogusia. Waislamu hao wa mwanzo waliokimbia huko kufika kwao katika mwambao wa Afrika, kuenezwa katika hadithi kdhaa zinazotaja baadhi ya makundi, ingawa hakuna uhakika kama ni makundi hayo yaliyotajwa, mengineyo au yote kwa pamoja walihusika na kufikisha ujumbe wa Nabii Muhammad (saw) katika miji ya Waswahili. Hadithi moja inasema kuwa katika karne ya 7 AD wakati Sayyidna Umar bin Khattab (ra) ni Khalifa, alitoa ujumbe wa watu wa Syria kufika Mwambao wa Afrika ya Mashariki kutangaza Uislamu. Hadithi nyingine ni ya kundi la wakimbizi wakati wa Khalifa Abdul Malik Marwan (685 - 707 AD) ambaye alimtuma Gavana wake aliyekuwa Hijaz (na baadaye Iraq), al Hajjaj Ibn Yusuf kuingia Oman na kutuliza fujo iliyokuwepo katika nchi hiyo baadhi ya walioshindwa wakakimbilia Afrika ni Said na Suleiman wa kabila la Julanda ambao inasemekana hasa walitoka mji wa Kufa Haijulikani mji hasa waliofikia Mogadishu (Somalia), Malindi (Kenya) au wapi. Haijulikani kama athari za kuja kwao miji ya Waswahili zilisaidia kusilimisha wenyeji. Kuna kisa cha mfalme wa Qanbalu kilichoandikwa na Buzurg Ibn Shahriyah katika kitabu chake alichokiita "maajabu ya India". Qanbalu ulikuwa mji mmojawapo uliokuwepo zamani katika kisiwa kimoja Mwambao wa Afrika ya Mashariki kuanzia katikati ya karne ya 8 AD na ambao ulitembelewa sana katika karne ya 10 na majahazi kutoka Oman kwa shughuli za kibiashara. Kisa cha huyo mfalme wa Qanbalu ni kutekwa nyara katika nchi yake na wafanyabiashara ambao walikuwa Waislamu na kumuuza katika mji wa Baghdad. Huko akauzwa tena kwa mtu mwingine na kwenda Basra ambako alijifunza Uislamu. Akakimbia na kujiunga na msafara wa watu waliokuwa wakienda Makka kuhiji akiwa ni mchukuzi wao. Akafundishwa kuhiji na alipomaliza akafuata msafara ulioelekea Misri ambako alifuata ukingo wa mto Nile na hatimaye akafuata msafara ulioelekea Afrika Mashariki na kurejea katika ufalme wake akiwa Muislamu na akasilimisha watu wake. Ameeleza kuwa kabla yake yeye, hakupata mtu yeyote katika Biladi Zanj neema aliyofadhiliwa na Mwenyezi Mungu kujua dini ya haki, kufahamu kusali, kufunga, kuhiji na kujua haramu na halali. Kwa ushahidi wa maelezo ya mfalme huyo wa Qanbalu inaonyesha kuwa hadi kufikia 922 AD (mwanzoni mwa karne ya 10 AD) Uislamu ulikuwa bado haujafika katika miji yote yoyote ya Mwambao wa Afrika ya Mashariki. Amma mpaka sasa ushahidi madhubuti kuthibitisha kuwa Uislamu ulifika Afrika ya Mashariki mnamo karne ya 7 AD kama inavyoelezwa katika hadithi hizo haujaptikana. Lakini mtaalamu mmoja wa mambo ya kale (Aathari-l-Kadim) aliyefanya utafiti eneo moja la mji wa kale katika Mwambao linaloitwa Shanga, miongoni mwa visiwa vya Lamu, katika kufukua kwake sehemu yenye gofu la Msikiti aligundua kuwa mahala hapo hapo palikuwa na Misikiti kabla katika vipindi mbalimbali vilivyopita. Amedai kuwa jengo la awali ambalo lilijengwa kwa udongo mwisho wa karne ya 8 AD huenda lilikuwa ni Msikiti ambao utakuwa ndio wa mwanzo katika sehemu hiyo. Ushahidi kuwa majengo yaliyofuatia mahala hapo yalikuwa ni Misikiti. Jengo lililofuatia, pia ni la udongo ambalo lilionekana kuwa ni la karne ya 9 AD halina shaka kuwa lilikuwa Msikiti na mnamo karne ya 10 AD ufundi wa kujenga kwa mawe ulipoanza kwenye miji ya Mwambao, Msikiti wa wakati huo ukatiwa jiwe. Inaendelea toleo lijalo |
YALIYOMO
TAHARIRI Iran ina agenda gani? Mauaji,udhalilishaji Mwembechai: Wanawake
Waislamu waandamana Tabora Na Mwandishi Wetu 'Serikali ieleze hatua iliyochukua
kuhusu mauaji Mwembechai' ‘Musiwasingizie wake zenu maovu’
Barua za wasomaji
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org